Nimepata bahati ya kusikiza mahojiano kati ya Rais Jakaya Kikwete, Waziri Mkuu-Edward Lowasan na Waziri wa Sayansi Teknolojia na Elimu ya Juu-Profesa Msolla na radio ya mtandaoni ya KLH News International kuhusu sakata la wanafunzi wa kitanzania waliokwama Ukraine. Kwa kuwa mahojiano haya yanaendelea kusikilizwa duniani kote kupitia www.mwanakijiji.podomatic.com naamini makala hii haitawekwa kapuni kwa kuwa tu inawahusu ‘wakubwa’ serikalini. Naandika makala hii kwa nia ya kujenga.
Waziri Mkuu yeye alikataa kuzungumza chochote na kusema kama ‘aachwe kwa kuwa anakula’, hata baada ya kuulizwa apewe muda ili apigiwe baadaye aliendelea kusisitiza kwamba ‘aachwe ale’! Ni ngumu lakini ndio ukweli. Rais Kikwete, yeye alijibu kiuongozi kwamba suala hili bado linapaswa kushughulikiwa na ngazi ya chini, yeye ni juu sana. Akasema mwandishi awasiliane na Msolla. Baada ya kuambiwa Msolla anakata simu. Rais alisisitiza kwamba suala bado liko juu kwake. Rais baada ya kuambiwa kwamba Mwenyekiti wa Bodi ya Mikopo aliahidi kwamba atashughulikia suala hilo, Rais ‘akapata pa kutokea’ akasisitiza kwamba mwandishi amtafute Nkono. Mwandishi aliporudi kwa Msolla, yeye aliendelea na tabia yake ya kukata simu! Huu ndio uwajibikaji wa awamu ya nne ya uongozi wetu. Ndio utendaji wa Ari, Kasi, na Nguvu Mpya.
Katika maisha yetu ya kawaida ya kila siku: Hivi ni mzazi gani ambaye akipigiwa simu, akiambiwa mwanae yuko ugenini-hana pa kulala, hana pakula; yuko anawaya waya kwenye mageti ya majirani- atajibu nakula! Ama atasema waulizwe ndugu wengine au ataka kabisa simu? Jibu unalo wewe, lakini litoe baada ya kusoma sakata hili la wanafunzi wa Kitanzania waliokwama Ukraine.
Nikukumbushe! Wanafunzi hawa wapatao 29 waliondoka nchini kuanza masomo nchini Ukraine katika mwaka wa masomo 2006/2007. Wanafunzi hawa walidahiliwa katika vyuo vya Ukraine katika mwaka wa masomo 2005/2006 lakini kutokana na kuchelewa kupatiwa mikopo na Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa vyuo Vikuu, waliahirisha kuanza masomo ili waanze mwaka 2006/2007 kwa maelewano na vyuo vilivyowadahili na serikali ya Tanzania.
Walipoondoka nchini mwaka 2006 kuanza masomo yao nchini Ukraine, wanafunzi hao walipata baraka zote za serikali kwa ahadi kwamba watatumiwa fedha zao za mikopo wakishaanza masomo nchini Ukraine. Taarifa zinazotolewa na wazazi wa wanafunzi hao, serikali haikutimiza ahadi yake ya kuwapelekea mikopo yao na haitaki kueleza kwa nini haijafanya hivyo.
Hii ndio hali waliyonayo hivi sasa! Wanaishi katika mazingira magumu ambayo yanatishia siyo tu usalama wao bali pia afya zao. Tayari wameshaitiwa vyombo vya usalama vya serikali ya Ukraine kuwachunguza.
Vyuo vyao vikuu viliwapa hadi tarehe 20 ya mwezi huu wa tano kama tarehe ya kufutwa chuoni. Hatua ya kufutiwa udahili wao itamaanisha kuwa wanafunzi hao hawana uhalali tena wa kuishi nchini Ukraine na hivyo watahesabiwa kuwa ni wahalifu ambao wanaweza kukamatwa na kufungwa kama watakuwa hawajalipia ada pamoja na madeni ya gharama za kujikimu walizokuwa wametumia kwa muda wote wakiwa wapo chini Ukraine.
Jitihada za wanafunzi hawa kuwasiliana na viongozi wa wizara zimekwama. Kila mara wanaishia kuzungushwa zungushwa na viongozi wa wizara hiyo akiwemo Waziri wa Wizara hiyo Prof. Msolla. Mwenyekiti wa Chama cha TLP Mhe Augustino Mrema alimuandikia Raisi Jakaya Kikwete kuhusu tatizo la wanafunzi hawa tangu tarehe 23/1/2007. Hii inamanisha kuwa Wizara hiyo hiyo imeshindwa kushughulikia matatizo ya wanafunzi hao. Habari zinazoanza kuja zinaonesha kuwa wanafunzi wengine walioko nje ya nchi wanaokabiliwa na matatizo yanayolingana au kukaribiana na yale ya Ukraine ni wale wanaosoma nchini Cuba, na Urusi. Je, Wizara na Bodi ya Mikopo wanayo sera za kibaguzi dhidi ya nchi zilizokuwa zikifuata siasa za kijamaa. Mbona hatujapata habari kama wanafunzi wanaosoma katika nchi za kibepari na hata wanaosoma nchi jirani kama vile Uganda na Kenya wanafanyiwa kama wanafunzi walio nchini Ukraine?
Jitihada za wazazi wa vijana hao kuwasiliana na viongozi wa Bodi ya Mikopo na wizara hazijazaa matunda kwa kuwa maofisa waliowahudumia hawakutoa ushirikiano wa kutosha. Jambo ambalo limejionesha wazi ni kuwa hakuna ofisa aliye tayari kusema wazi msimamo wa serikali na hivyo wazazi wamekuwa wakipigwa kama mpira kutoka ofisi moja hadi nyingine bila mafanikio yoyote.
Aidha habari zinasema kwamba Ubalozi wa Uingereza nchini Ukraine uliipa serikali ya Tanzania ufadhili wa kuwasaidia na kuwalipia vijana hao na kuwapa misaada mingine ya kibinadamu endapo tu serikali ya Tanzania itaandika barua ya kurudisha fedha hizo kwa serikali ya Uingereza. Serikali ya Tanzania haikuwapa jibu hadi leo hii. Matokeo ya haya ni kuwa wanafunzi hao 29 wamesimamishwa masomo, hawana chakula wala fedha za kulipia pango katika nyakati hizi za majira ya baridi. Imewalazimu wanafunzi hao kujisalimisha ubalozi wa Uingereza kule mjini Kiev, kwa vile Tanzania haina Ubalozi nchini Ukraine kwa takribani zaidi ya siku kumi na nne sasa wakiomba “yala saidia maskini” ili wasaidiwe.
Habari zilizopo sasa ni kuwa wanafunzi hao wamepewa hadi Jumanne tarehe 29 mwezi huu kulipa fedha wanazodaiwa vyuoni au watanyang’anywa hati zao za kusafiria na kasha kufukuzwa kwenye mabweni wanamoishi. Wanafunzi hawa hawaruhusiwi kurejea Tanzania kwa vile wanadaiwa na vyuo vyao. Hali ni mbaya mno kwa wanafunzi hawa kiasi kwamba ipo haja ya kufikiriia hatua za dharura za kuokoa maisha ya raia wenzetu.
Ni wazi kuwa Dhamana ya Wizara ya Elimu ya Juu, Sayansi na tekinolojia imekabidhiwa pasipo. Mheshimiwa Profesa Msolla hafai kushikilia wadhifa wake wa uwaziri, hamsaidii Rais Jakaya Kikwete ila anambomoa. Ni hatari kuwa na waziri wa elimu ambaye kazi yake ni kugombana na wanafunzi badala ya kwaongoza. Wazazi wa wanafunzi hao wametoa nyaraka zinazoonesha kuwa Wizara ilitoa baraka zake kwa wanafunzi hawa kuondoka nchini kwa ahadi kuwa itawakopesha fedha za kugharamia masomo yao huko waendako.
Pia serikali ilitoa ahadi kuwa inazo fedha za kutosha kutoa mikopo kwa kila mwanafunzi aliyedahiliwa. Hatuoni kwa nini serikali inakwepa wajibu wake wa kutenda uungwana kwa kutekeleza ahadi zake. Ikiwa serikali imeshindwa kuongoza, basi ni vyema ama ijiuzulu yote au ikiwa ni tatizo la Profesa Msolla pekee, basi mheshimiwa huyu aombwe kupisha nafasi hiyo ipewe anayeimudu. Tunatamka wazi kuwa Profesa Msolla ajiuzulu haraka kwani hajaiangamiza serikali nzima ya Rais Jakaya Kikwete.
Rai yangu kwako! Kwa kuwa hali ya wanafunzi kule Ukraine ni mbaya, tunalione jambo hili kuwa ni janga linalohitaji misaada ya kibinadamu. Wakati jambo hili linatafutiwa ufumbuzi lazima tuchukue hatua za kuokoa maisha ya watanzania wenzetu. Hapa natarajia mashirika yanayohusika na haki za binadamu yataangalia swala hili kwani vijana wale wanaishi kwenye mazingira magumu sana na hili linahatarisha hata mustakabali wa maisha yao kwani huenda wengine wakapatwa na matatizo ya kiakili na kuamua kufanya jambo lolote ambalo nlitayahatarisha maisha yao.
Elimu ni zaidi ya chakula kwa mwanadamu wa dunia ya leo. Ni wakati wa wale wanaoenzi misingi ya Rais ya awamu ya kwanza ya kuweka mbele elimu zaidi ya gharama yoyote. Ni fursa ya kumkumbuka kwa vitendo haya Edward Moringe Sokoine kwa kuutumikia umma wakati wowote. Ni wakati wa kila raia anayeguswa kuwaokoa vijana hawa 29 aunge mkono harambee hii. Serikali ikiwakana, wewe je?