lf.bevel
MWANZO CHAMA SERA KATIBA TUUNGE MKONO UCHAGUZI TUWASILIANE

26 Mei 2007

Ushirikiano wa Upinzani na hekima ya Umoja ni Nguvu

na

John Mnyika

Nimesoma kupitia vyombo vya habari makala za Thomas Ngawaiya, Tabwe Hiza na Abdul Mtemvu kuhusu suala la ushirikiano ama kama wao walivyoita muungano wa vyama vya upinzani nchini. Kwa kiasi kikubwa makala zao kwa ujumla wake zimebeza ushirikiano ambao vyama vya upinzani nchini vimeanzisha. Aidha nimesoma kauli za Wenyeviti wa vyama vya DP na SAU kuhusu suala la ushirikiano wa vyama ya upinzani. Nao kwa nafasi yao wameponda ushirikiano huo. Aidha nimesoma makala za waandishi mbalimbali pamoja na barua za wasomaji ambao wamepongeza ushirikiano huu wa vyama vya upinzani. Si lengo langu katika makala ya leo kujibu hoja ambazo waandishi wameziibua. Lengo langu leo ni kuchambua tamko la ushirikiano ambalo vyama hivi vilisaini na sababu za ushirikiano wa vyama hivi. Wachina wanasema wanamsemo wa miaka mingi, kwamba usipofanya utafiti, usipokuwa na taarifa/takwimu, huna haki ya kusema. Naamini ambayo yameandikwa ndivyo sivyo kutokana na kukosekana kwa taarifa. Naweka wazi mambo haya mawili-tamko na sababu za ushirikiano ili watanzania wengi zaidi waweze kuchangia mjadala huu muhimu kwa mustakabali wa demokrasia na maendeleo nchini.

Tarehe 10 Mei 2007 viongozi wa vyama vya siasa vya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), The Civic United Front (CUF - Chama Cha Wananchi), National Convention for Costruction and Reform (NCCR-Mageuzi) na Tanzania Labour Party (TLP) walikutana Dar es salaam kusaini tamko la ushirikiano, nilikuwa mmoja wa mashuhuda.

Tamko hilo la vyama linaanza kwa kutambua masuala kadhaa ya msingi. Kwamba wananchi wa Tanzania wanahitaji mageuzi ya dhati ya kisiasa, kiuchumi, na kijamii. Kwamba mageuzi ya dhati hayawezi kupatikana bila kwanza vyama vya kisiasa vya upinzani kuunganisha nguvu zao na nguvu za umma ili kuundoa madarakani mfumo wa chama dola ambao umezuia demokrasia, umedidimiza haki na hali za kiuchumi na kijamii za wananchi wa Tanzania walio wengi na kuongeza ukandamizaji, rushwa na ufisadi wa watawala. Kwamba mfumo wa kikatiba na wa kisheria uliopo kwa sasa hautoi uhuru wa wazi wa vyama vya siasa kuungana na kuendesha shughuli za kisiasa kama mseto wa vyama vya siasa.

Wakizingatia masuala hayo viongozi walisaini tamko la kudhamiria kutekeleza vipengele kumi vya ushirikiano. Mosi, lengo letu kuu na la pamoja na la jumla ni kuunganisha nguvu zetu katika kukabiliana na mfumo wa chama dola uliopo sasa ambao umezuia kukua kwa demokrasia, ukiukwaji wa haki za msingi za raia, kuongezeka kwa ukandamizaji , rushwa, vitendo vya ufisadi na kuzorota kwa uchumi. Pili, vyama vyetu vitafanya kazi au kuendesha shughuli zake za kisiasa kwa pamoja na kushauriana katika masuala yote makuu ya kisiasa, ya kuichumi na ya kijamii katika Tanzania. Tatu, viongozi wakuu wa vyama vyetu watafanya mikutano ya hadhara ya pamoja na/au ya mmoja mmoja katika sehemu mbalimbali za nchi yetu na pamoja na shughuli nyingine, kwa nia ya kuelezea haja, umuhimu na ulazima wa kuunganisha nguvu zetu na za umma. Nne, vyama vyetu vitashirikiana katika masuala yote ya kisiasa ikiwa ni pamoja na kuwa na msimamo wa pamoja bungeni na/au katika vyombo vingine vya uwakilishi wa umma. Tano, vyama vyetu vitashirikiana na kuwa na msimamo wa pamoja katika jitihada za kuweka mfumo mpya wa kikatiba na kisheria ambao utaruhusu vyama vyetu kushirikiana na kuendesha shughuli za siasa kimseto. Sita, viongozi wakuu wa vyama vyetu watatoa maazimio na matamko ya pamoja kuhusiana na masuala mbalimbali ya kitaifa na kimataifa pale itakapohitajika. Saba, tutafanya jitihada zote kuelimisha viongozi wa vyama vyetu wa ngazi mbalimbali, wanachama wetu, na wananchi kwa ujumla juu ya haja na ulazima wa vyama vyetu kushirikiana katika nyanja mbalimbali kuanzia ngazi za chini kabisa hadi ngazi za kitaifa. Ili kulifanya jambo hili lifanikiwe na kujengewa misingi imara ya kukubalika na kutekelezwa kila Chama kitalifikisha suala hili katika vikao vyake vya kikatiba. Nane, tunaomba wanachama wetu, wananchi wa Tanzania na Jumuia ya kimataifa watuunge mkono ili tutimize malengo tuliojiwekea leo kwa faida ya Watanzania wote. Tisa, Chama chochote kingine cha upinzani kinaweza kukubaliwa kujiunga na ushirikiano huu kwa mujibu wa kanuni zitakazoandaliwa. Kumi, utekelezaji wa makubaliano haya utasimamiwa na kanuni ambazo zitapitishwa na viongozi wakuu wa vyama.

Tamko au makubaliano haya hayakuja hivi hivi. Ni matokeo ya sababu mbalimbali. Hivyo kama sehemu ya kuingia makubaliano hayo, sababu zilizofanya vyama hivi kuamua kuingia katika ushirikiano ziliwekwa bayana. Vyama vinne vya Upinzani Chadema, CUF, NCCR – Mageuzi na TLP viliainisha mambo yafuatayo kama msukumo na sababu za msingi za kuanzisha Mashirikiano.

Mara nyingi suala la mashirikiano ya vyama limekuwa likizungumziwa pindi uchaguzi unapowadia au kwenye matukio maalum na hivyo kufanyika katika hali ya kurashiarashia na isiyokuwa ya umakini wa kutosha na hivyo kutofaulu malengo yetu. Jambo hili likianzishwa hivi sasa utakuwa ni wakati muafaka kwani tunao muda wa kujiandaa na kujipanga (miaka 3) kabla ya Uchaguzi ujao.

Tangu 1992 mfumo wa vyama vingi ulipoanzishwa rasmi malengo makuu ya vyama vya Upinzani ya kuchukua dola au kuwa na sauti katika kuathiri (influence) maamuzi ya serikali iliyoko madarakani bado hayajawa na nguvu inayopasa hadi sasa. Na mbaya zadi, kadri muda unavyopita nguvu hiyo imekuwa ikionekana kitaswila kupungua.

Wapinzani kutoshirikiana kumekuwa kukiwafanya CCM WASHINDE KATIKA Chaguzi mbali mbali kirahisi kutokana na kutokuwepo kwa nguvu ya pamoja ya kukabiliana na hujuma za Chama Tawala wakati wa Uchaguzi.

Hali halisi imedhihirisha kuwa kadiri muda unavyopita CCM imeendelea kujiimarisha zaidi kupitia nguvu za mtandao haramu wa kidola na kuzidi kuvidhoofisha vyama vya upinzani na kuhakikisha taswira hiyo inaonekana hivyo kwa umma, ili visiheshimike, kutumainiwa wala kuaminika. Kwa kiasi kikubwa CCM imefanikiwa na inaendelea kufaulu kwa kasi katika jambo hili linalofanyika kwa njia zilizo chafu. Kwa Zanzibar ambako upinzani mkubwa na kushindwa kwa CCM kumekuwa dhahiri zaidi, CCM wameendelea kujenga na kutengeneza mazingira ya wazi ya kupora Ushindi kwa nguvu.

Kutokana na kutokuwa na mashirikiano ya pamoja, kauli na mipango ya kutufitinisha, kutuchonganisha, na kutuhujumu kama wapinzani imekuwa ikifanya kivyepesi na CCM na vyombo vyake vya dola kupitia kwenye vyama vyetu ka njia mbali mbali zisizoweza kugundulika kirahisi.

Watanzania walio wengi wamekuwa wakielezea wazi umuhimu wa upinzani kushirikiana na kujenga nguvu ya pamoja ya kulikabili “CHAMA DOLA CCM”. Wengi wanaona kuwa ushirikiano wa upinzani katika mazingira ya sasa ya kisiasa ndilo jibu pekee, na kutofanya hivyo ni kuzidi kuwakatisha tamaa na kuwachanganya wananchi hali itakayopelekea kuwafaya wasiwe na matumaini na upinzani.

Viongozi wetu wameona kuna haja ya kusoma alama za nyakati za mwenendo wa kisiasa. CCM wamekuwa wapesi kulitambua hilo na wamekuwa wakijibadilisha kama kinyonga kwa kutegemea upepo na mtizamo a kisasa na hali ya mazingira yaliyopo ili mradi wakidhi haja yao ya kuendelea kuwepo madarakani hata kama utawala wao hauna ufanisi wa tija. Mwenendo wa siasa za sasa zilivyo si vyema kuendelea kuendekeza na kutanguliza umimi bali tuangalie ni lipi la kutufanikishia njia tunayoihitaji sasa.

Vyama vya Upinzani vina rasilimali yenye ufahamu na kuaminika ya “RASILIMALI WATU” ambayo imesambaa bila utaratibu ulio mzuri na makini wa kuiratibu na kuitumia. Kugawanyika na kutawanyika kwa rasilimali hiyo muhimu kunaifanya isiwe thabiti (effective) pale ilipo na CCM kunufaika na hali hiyo.

Kutokana na kukosekana nguvu ya pamoja iliyo kubwa, upinzani umeshindwa kutoa msukumo wenye nguvu hata wakati wa kuwasilisha madai yenye msingi ambayo yangepaswa kusikilizwa na kufanyiwa kazi na Serikali. Mfano; madai ya Katiba Mpya, Tume Huru ya Uchaguzi matatizo ya sheria mbovu na utaratibu usioridhisha unaosimamia chaguzi, ukiukwaji wa haki za binadamu, tatizo la Zanzibar n.k.

Kutokana na kukosekana ushirikiano wa pamoja wa Vyama Vya Upinzani katika kuunganisha nguvu ya Umma kuwawajibisha Viongozi na Serikali iliyo madarakani kutekeleza ahadi lukuki ilizozitoa na inazoendelea kuzitoa pamoja na kushirikiana katika kukabiliana na rushwa, umaskini, ujinga na maradhi.

Baada ya kuweka wazi tamko na sababu za ushirikiano, naamini mjadala huu kuhusu ushirikiano wa vyama vya siasa nchini utaelekea zaidi katika kujenga kuliko kubomoa. Wahenga walisema, kidole kimoja hakivunji chama. Umoja ni Nguvu.


 
lf.curl lf.curl2 rt.curl2 rt.curl