MWISHONI mwa wiki iliyopita, Chama Cha Mapinduzi (CCM) kiliandaa mkutano ulioitwa wa wanavyuo vya elimu ya juu, kama sehemu ya maadhimisho ya miaka 30 ya chama hicho katika Ukumbi wa Diamond Jubilee, Dar es Salaam.
Mgeni rasmi katika mkutano huo alikuwa Mwenyekiti wa chama hicho taifa ambaye pia ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete.
Ni haki ya CCM kuamua itakavyo, lakini nimeshangazwa na uamuzi wa chama hicho, badala ya kutumia maadhimisho hayo kutafakari na kutoa majibu kwa umma kuhusu mwelekeo wao, ikiwemo hatma ya Azimio la Arusha, imetumia tukio hilo kueneza propaganda zifuatazo:
Mosi, chama hicho kimetumia siku hiyo kueleza kwamba kimepokea wanachama wengi kutoka vyuo vikuu.
Hata taarifa za chama hicho zimejichanganya kuhusu idadi ya waliopokelewa. Wakati baadhi zikisema wamepokelewa wanachama 2,500 baadhi zimesema jumla ya wanachama 10,000 walipokelewa, idadi ambayo hata wasingeweza kutosha katika ukumbi ambao mkutano umefanyikia.
Kwa upande mwingine, pamoja na kutuma mabasi katika vyuo mbalimbali na kuwashawishi wanafunzi wa vyuo vikuu, lakini bado idadi ya waliojitokeza ilikuwa ndogo.
Pili, CCM imeitumia siku hii kuendelea kutoa ahadi kwa wanafunzi bila kuweka bayana mazingira ya kutekekelezwa kwake.
Rais Kikwete amenukuliwa akisema, atalipatia ufumbuzi suala la wanafunzi kuchangia asilimia 40 na kwamba hakuna mwanafunzi atakayeshindwa kusoma kutokana na kutakiwa kulipia kiasi hicho.
Hizi ni propaganda za kisiasa kwa kuwa wakati rais anatamka maneno haya, tayari wapo wanafunzi wa vyuo mathalani, Tumaini ambao wamezuiwa kufanya mitihani na hivyo kushindwa kuendelea na masomo.
Rais Kikwete ameendelea kusema, suala hili linahitaji pesa na kwa sasa serikali haina uwezo wa fedha na kwamba suala hili linategemea bajeti.
Hizi ni propaganda za kisiasa, kwani tulitegemea Rais Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa chama kinachotawala, atoe mwelekeo kwamba serikali yake katika mwaka huu wa fedha ina mpango wa kuongeza kiasi cha fedha ili kukabiliana na mapungufu hayo.
Hatukubaliani na kauli ya CCM kwamba serikali haina fedha kwa ajili ya kutoa mikopo asilimia 100.
Kama Mtanzania mmoja anaweza kupata bilioni 12 kama asilimia 30 ya ununuzi wa rada, ni vipi serikali inasema haina pesa?
Kama tunaweza kuingia mkataba wenye utata wa Richmond, wenye thamani ya takribani sh bilioni 272 ambazo zingeweza kusomesha wanafunzi wote
wa vyuo vikuu kwa miaka miwili, ni vipi serikali inasema haina pesa? Kama serikali inaweza kusamehe kiwanda kimoja cha nguo kodi ya thamani ya takribani sh bilioni 40, vipi inasema haina fedha?
Kuna sababu gani ya wananchi kuendelea kutozwa kodi ya asilimia 20 ya ongezeko la thamani (VAT) kwa kila bidhaa wanayonunua kama serikali inashindwa kutoa huduma kwa raia wake?
Serikali itoe tamko kuhusu hatma ya wanafunzi na sekta nzima ya elimu ya juu nchini, hususani katika maeneo yafuatayo:
Moja; CCM iliahidi katika uchaguzi mkuu 2005 kwamba, kwa kila mwaka itadhamini wanavyuo 30,000.
Tuna imani wakati inatoa kauli hiyo, ilitafakari kwa kina uwezo wa serikali. Je, ni maandalizi gani ya kibajeti ambayo Bodi ya Mikopo pamoja na wizara inayohusika imeshaanza kufanya kufanikisha azma hii?
Mbili; sheria ya mikopo imetamka bayana kwamba, wanaopata udahili (admission) wana haki kisheria kupewa mkopo.
Hivyo basi, serikali inapaswa kufuta utaratibu iliouanzisha wa kutoa mikopo kwa daraja la kwanza wavulana, na daraja la kwanza na pili kwa wasichana pamoja na daraja la tatu kwa fani chache.
Nimeshangazwa na uamuzi wa serikali wa kutoa mapendekezo ya mabadiliko ya sheria ya Bodi ya Mikopo ili kuhalalisha uamuzi huu ambao iliufanya.
Serikali itoe tamko la sababu za mabadiliko inayotaka kuyafanya na hatua ambayo mchakato umefikia ili wadau mbalimbali waweze kutoa maoni.
Tatu; serikali inapaswa kutambua katika mfumo wa sasa tayari mwanafunzi wa elimu ya juu anajigharamia mwenyewe kwa asilimia 100 ya gharama ya elimu ya juu.
Hakuna sera ya uchangiaji wa elimu ya juu nchini. Hii ni kwa sababu pesa inayotoka serikalini ni mkopo ambao mwanafunzi analazimika kuilipa.
Je, serikali inataka kuwakosesha wananchi hata haki ya kukopa kutoka kwenye kodi yao wenyewe kwa kuwataka kutoa asilimia 40 ya gharama toka mifukoni mwao moja kwa moja?
Kama serikali inataka wananchi watoe wenyewe pesa mifukoni, basi ianze kwanza kuboresha uchumi, kuweka mazingira ya wananchi kupata kipato cha kutosha na kupunguza ukubwa wa kodi.
Nne, serikali imefikia wapi katika kukusanya madeni ya wahitimu waliokopeshwa na serikali miaka ya nyuma kama sheria ya Bodi ya Mikopo inavyohitaji?
Naamini kwamba, kama kuna sekta ambayo ina fursa ya kuwa na mfuko mkubwa wa kukopesha, basi ni sekta ya elimu ya juu.
Kwa mfano rahisi, kwa idadi ya wahitimu laki moja wa miaka kadhaa iliyopita, kila mhitimu akirejesha shilingi milioni moja tu katika gharama zote ambazo zimetumika kumsomesha, Bodi ya Elimu ya Juu itapata jumla ya shilingi bilioni 100 ambazo zinaweza kusomesha wanafunzi wengi.
Kama serikali imeshindwa kutumia kodi inayopatikana hivi sasa kusomesha wanafunzi, basi viongozi wa serikali waanze kulipa madeni wanayodaiwa ili zipatikane fedha za kusomesha wanavyuo waliopo hivi sasa.
Tano; serikali ilipitisha sheria ya kuzuia siasa vyuoni, lakini kinachofanywa na CCM kwa mara kadhaa; mwaka jana na mwaka huu, ni kufanya siasa vyuoni.
Je, serikali imeamua kuacha kuisimamia sheria hii?
Serikali itoe tamko rasmi kama imeruhusu siasa vyuoni ili na vyama vya upinzani navyo vifanye.
Rais Kikwete iga mfano wa Baba wa Taifa, hayati Mwalimu Nyerere, ambaye kila alipotaka kuzungumza na wasomi wa vyuo vikuu, alikuwa akiwafuata katika taasisi za elimu ya juu badala ya kuingia gharama ya kukodisha mabasi kuwabeba katika kumbi za mikutano.
Lakini pia nimesikitishwa na risala ya wanavyuo, kujikita zaidi kuzungumzia tatizo la mikopo na kuisifia serikali wakati taifa linakabiliwa na matatizo mbalimbali.
Tulitarajia jumuia ya wasomi ichambue kwa kina matatizo ya ufisadi katika mikataba na masuala mengine yanayotishia mustakabali wa taifa na kutoa ushauri makini kwa CCM ili miaka mitano ijayo wakati chama hiki kikiwa madarakani, kiweze kutekeleza ahadi zake.
Mwandishi wa makala hii ni mwanaharakati na mwanasiasa kijana, anayepatikana kupitia simu: 0754 694 553 ; mnyika@chadema.net www.chadema.net/blogu/mnyika/