HIVI karibuni, akiwa mkoani Mbeya katika majumuisho ya ziara yake ya vyuo vikuu, Waziri wa Sayansi, Teknolojia na Elimu ya Juu, Profesa Peter Msolla, alinukuliwa na vyombo vya habari akitoa vitisho kwa wanafunzi wa vyuo vikuu kwa madai kuwa wanafunzi wanaohusika na migomo katika vyuo vikuu wanajiandalia mikosi na kwamba hawatapata ajira baada ya masomo yao.
Prof. Msolla ametoa kauli hiyo huku kukiwa na vuguvugu la wanafunzi wa vyuo vya elimu ya juu kupinga taratibu za sasa za utoaji mikopo, kwa mujibu wa taratibu za sasa ambazo kimsingi zinakinzana na sheria halisi ya mikopo.
Pamoja na upungufu mwingine wa msingi ni kwamba wanafunzi wanalazimika kuchangia asilimia 40 ya gharama za masomo.
Na sasa vuguvugu hili huenda likasambaa zaidi wakati wowote kwani mpaka sasa kuna taarifa kuwa baadhi ya wanafunzi katika baadhi ya vyuo wanashinikizwa kuchangia pesa hizo ambazo ni kati ya sh laki tatu na zaidi ya laki tano ili waruhusiwe kuingia darasani sambamba na kupewa huduma nyingine za msingi.
Aidha, hivi karibuni, vyombo vya habari vimeandika kwamba wanafunzi wa Chuo cha Kilimo Sokoine (SUA) waliendesha mgomo na kuja wizarani kutaka kuonana na waziri kupinga utaratibu wa kuchangia asilimia 40 ya mkopo.
Pesa hizi ni takriban laki tano ambazo walipaswa kuzilipa kabla ya kuanza masomo.
Imeelezwa kuwa serikali imewataarifu kuwa wasaini mikataba na kuendelea na masomo. Uamuzi huu unaweza kutafsiriwa kuwa tayari serikali imewasaidia wanafunzi hawa kuendelea na masomo.
Lakini ukweli ni kuwa huu ni mtego. Ni wazi kwamba serikali ama inasubiri kipindi cha karibu na mitihani ndipo iwabane wanafunzi kwa kuwataka kulipa hiyo asilimia 40 au inaweza kuwaruhusu wafanye mitihani na pindi watakapokwenda likizo ikatoa maelekezo kuwa wasiolipa wasirejee mpaka watakapopata pesa za kulipa.
Huu ni mkakati wa ‘wagawe uwatawale’ (divide and rule), ambao serikali imekuwa ikiutumia mara kwa mara kuvunja mshikamano wa wanafunzi.
Na hii inathibitika kutokana na kauli ya Waziri wa Elimu ya Juu, Profesa Msolla ambaye amenukuliwa na gazeti la Uhuru la Januari 17 akisema kwamba serikali haina mpango wa kulipa hiyo asilimia 40 kwa kuwa wanafunzi walikwisha kusaini fomu za mikopo na kwamba sharti hilo lilikuwa sehemu ya mkataba.
Waziri anasahau fomu hizo zilishasainiwa na wanafunzi chini ya shinikizo la serikali pamoja na ahadi mbalimbali kwamba serikali iko mbioni kuandaa utaratibu mzuri zaidi.
Tunachotaka ni serikali kutoa tamko kwamba itahakikisha kwamba utaratibu huu unafutwa kwa kutenga pesa katika bajeti ya mwaka huu, zikiwamo za kulipia gharama za wanafunzi walioko masomoni hivi sasa.
Ni katika muktadha huo, tunapaswa kulijadili suala hili ili kuhakikisha serikali inafika mahala inakiri kuwa mikopo si hisani ni haki ya kila Mtanzania anayepata ufadhili wa chuo kikuu kwa mujibu wa sheria inayounda bodi ya mikopo. Na kwa mantiki hiyo, nasisitiza msimamo wangu katika misingi ifuatayo :
Migomo na maandamano
Kauli ya waziri ni kama vitisho ambavyo vilikuwapo hata wakati wa serikali ya mkoloni - kuwadhibiti wanafunzi wanao nyanyaswa na serikali yao, wasiisimamie haki yao kwa vigezo kwamba kufanya hivyo ni kujihatarishia mazingira ya ajira punde baada ya kumaliza masomo yao.
Tunapaswa kutambua kuwa nguvu ya umma ni hatua ya mwisho katika kuhakikisha umma unapata haki yake stahiki kutoka kwa serikali isiyojali. Migomo na maandamano ni hatua ya mwisho inayorejesha wadau katika meza ya majadiliano baada ya hatua za awali za majadiliano kutokuzaa matunda.
Maandamano na mashinikizo ya hali ya juu kutoka kwa wanafunzi wenyewe dhidi ya serikali ni mambo yasiyoepukika kama hatua ya mwisho, kwani serikali yetu imekuwa na tabia ya kutowatendea haki wanafunzi kila wanaponyanyaswa mpaka wanapoamua kusitisha masomo kwa migomo na maandamano.
Hivyo kwa kuwa serikali imejenga tabia ya kutowasikiliza wanafunzi wa elimu ya juu hadi wagome na kuandamana, na kwakuwa migomo na maandamano ni njia zinazoruhusiwa kwa mujibu wa mikataba ya kimataifa ya haki za binadamu, katiba ya nchi na sheria za taasisi mbalimbali ikiwamo vyuo vikuu kama moja ya njia ya kushinikiza haki kutendeka.
Hivyo si ajabu kwa wanafunzi wa elimu ya juu kufanya kila linalowezekana ikiwa ni hata kugoma na kuandamana kwa mujibu wa sheria ili kuhakikisha haki yao inapatikana, inalindwa na kuheshimiwa.
Ndiyo maana natoa rai kwa waziri kuacha vitisho, na badala yake ahakikishe wanafunzi wanapata haki yao kama kweli ni msomi mzalendo. Hakuna binadamu anayependa kugoma wala kuandamana. Serikali isiwaweke wanafunzi katika mazingira yanayowalazimisha kugoma na kuandamana.
Haiingii akilini kwa mwanafunzi kutishwa kuwa asigome na wala kuandamana, kwa madai kuwa kufanya hivyo kunahatarisha ajira yake hapo baadaye, wakati ukweli ni kwamba mwanafunzi asipogoma hatapata mkopo, na asipopata mkopo atafukuzwa chuo, hatamaliza chuo. Sasa kama hatapata mkopo na kushindwa kumaliza chuo, ni ajira gani ambayo Msolla anasema wanafunzi wanahatarisha ?
Upungufu wa sera ya mikopo
Utaratibu wa sasa wa mikopo una upungufu wa aina mbalimbali za kimsingi, ambao unaleta mkanganyiko wa hali ya juu katika taifa hili, na zaidi unatishia mustakabali wa elimu hiyo kwa wanafunzi wa Kitanzania wanaotoka familia maskini.
Mosi; dhana ya uchangiaji wa gharama za elimu ya juu imegeuzwa kuwa mfumo wa kufanya elimu ya juu nchini kuwa bidhaa inayouzwa badala ya huduma (service). Dhana nzima ya uchangiaji gharama za masomo ya elimu ya juu imepotoshwa. Kwa mujibu wa sera ya serikali, mwanafunzi anatakiwa kuchangia asilimia 40 na serikali kumchangia asilimia 60 ya mkopo wote.
Lakini kinachotokea ni kwamba, wanafunzi wanapewa mkopo wa asilimia 60 (huu ni mkopo si mchango, kwani watalipa), na baadaye mwanafunzi anatakiwa kujilipia mwenyewe asilimia 40 ya gharama zinazobaki.
Hivi katika muktadha huu, serikali inawezaje kusema kuwa inawachangia wanafunzi kusoma elimu ya juu ? Hii ni cost sharing ya namna gani ?. Kilichopo hapa ni mwanafunzi kujilipia asilimia 100 za gharama za masomo yake (total cost bearing).
Pili; dhana ya kutoa mkopo kwa wanafunzi waliofaulu kwa daraja la kwanza wavulana, na la kwanza na la pili wasichana, ina upungufu wa msingi. Kwanza inapingana na sheria ya mkopo kuwa kila atakayekidhi vigezo vya mkopo ikiwa na maana ya kupata usajili wa chuo na kuhakikisha kuwa hana uwezo wa kujisomesha, atapatiwa mkopo.
Kinachozungumzwa hapa ni kufikia viwango vya kusajiliwa/kudahiliwa chuoni na si utaratibu wa madaraja kama ulivyoelezwa hapo juu.
Baada ya upinzani kutoa msukumo katika suala hili, serikali ilirudi nyuma kidogo na kuamua kutoa mkopo kwa baadhi ya wanafunzi wa daraja la pili wavulana na la tatu wasichana ambao wengi wao walijiunga na ualimu.
Hii ni kwa mujibu wa kauli ya Rais kuwa pamoja na serikali kuwaruhusu baadhi ya wanafunzi wa daraja la pili wavulana, na la tatu wasichana, lakini bado vigezo vilivyowekwa katika fani mbalimbali ni kikwazo kwa wanafunzi hawa kujiunga na vyuo husika. (Mathalani katika fani za udaktari na uhandisi).
Vigezo vilivyowekwa vilizingatia uhaba wa fursa zilizopo kwa msingi wa ni kiwango gani serikali imepanga kutoa mkopo katika fani fulani. Kwa mantiki hiyo, serikali inapotoa tamko kuwa imewaruhusu wanafunzi wa daraja la pili wavulana na la tatu wasichana katika fani chache, bila kuhakikisha vigezo vinabadilishwa, ni sawa na kutoa haki ambayo haipo. Ni kuwafanyia ‘usanii’ vijana wetu.
Ni vyema Rais atambue hilo, lakini pia atafiti kuhusu ukweli wa kauli yake kuwa serikali inasomesha wanafunzi waliofaulu vizuri kabisa kwa madai kuwa serikali haiwezi kuwekeza kwa wanafunzi wasio na uwezo.
Nasema hivyo kwa sababu kuu mbili:
Kwa upande mmoja, kuna wanafunzi wengi wanaofaulu kwa kiwango cha chini kutokana na mazingira ya shule wanazosomea, mifano dhahiri ni shule za serikali na zile za umoja wa wazazi wa CCM.
Shule hizi nyingi hazina walimu wala vifaa, mwanafunzi anayepata daraja la tatu au la pili katika shule za aina hii anao uwezo mkubwa wa kujifunza kuliko wanafunzi wengi wanaosoma katika shule za kimataifa, seminari na baadhi ya shule za sekondari chache za serikali ambazo zinafaulisha vizuri.
Kwa upande mwingine, kauli hii imekuwa ikithibitishwa na maprofesa wanaofundisha vyuo vikuu kwa kubainisha wazi kuwa wanafunzi wengi wanaofanya vibaya vyuo vikuu ni wale wanaotoka shule zenye majina makubwa, ambao waliingia kwa alama za juu.
Kwa maana hiyo basi, hoja ya Rais kumchukulia kila mvulana aliyepata daraja la pili na kila msichana aliyepata daraja la tatu hawezi kufanya vizuri sana, ina upungufu huo wa msingi.
Tatu; dhana ya kwamba waliopata daraja pili wavulana, na la tatu wasichana kuwa ndio wenye uwezo wa chini kitaaluma, na kwa hiyo wataenda ualimu, ni kielelezo kuwa serikali yetu inaamini ualimu ndiyo taaluma isiyohitaji utaalamu sana, na hivyo haihitaji watu wenye uwezo mkubwa. Kitu ambacho kimewahi kurudisha nyuma maendeleo ya taaluma nchini kwa miaka kadhaa sasa.
Nne; mwisho lakini kubwa zaidi, ni kwamba chama tawala CCM katika ahadi zake wakati wa kampeni, iliahidi kuhakikisha inawapatia mkopo wanafunzi 30,000 kwa mwaka.
Hata hivyo waliofaulu kwa kiwango cha daraja la kwanza mpaka la tatu ni wanafuzi 21,000 tu. Hivyo kama serikali ingekuwa inatekeleza ahadi zake, wanafunzi wote wangepata udhamini wa chuo kikuu. Hata hivyo zaidi ya nusu ya hao, ambao walikidhi vigezo vya mkopo hawakupata mkopo.
Serikali ieleze ni wanafunzi wangapi walistahili mkopo kwa mujibu wa sheria lakini wamekosa na sasa inaandaa utaratibu gani kuhakikisha waliokosa mwaka 2006 watapewa haki yao mwaka 2007, na kwamba mwaka 2007 kosa halijirudii na kwamba ahadi ya Rais itatekelezwa.
Ili serikali iweze kutekeleza ahadi yake inapaswa kutenga si chini ya sh bilioni 195 kwenye bajeti ya mwaka huu kwa ajili ya mikopo.
Hii inawezekana, kwani kama tunaweza kutenga sh bilioni 272 katika miradi yenye utata kama mkataba wa Richmond, inashindwaje kusikiliza matakwa ya wananchi ya kufanya suala la elimu kuwa kipaumbele ?
Kama mfanyabiashara mmoja wa Kitanzania anaweza kutuhumiwa kupata shilingi bilioni 15 ambayo ni sawa na milioni elfu 15 kama ‘hongo ya asilimia 30’ kwenye ununuzi wa rada, tunaweza kweli kusema hatuna pesa za kusomesha wanafunzi elfu 15 wanaohitaji takriban shilingi milioni moja kwa mwaka ?
Mwandishi wa makala hii ni mwanaharakati na mwanasiasa kijana, anayepatikana kupitia simu: 0754 694 553 ; mnyika@chadema.net www.chadema.net/blogu/mnyika/