Niko jiji la Washington-Marekani, nimetembelea maeneo mbalimbali. Masuala niliyoyaona na kuyasikia ni mengi, nitayaeleza katika makala zingine. Nafika katika mnara wa kumbukumbu ya Mwanasayansi Albert Einstein, navutiwa na kauli zake kadhaa zilizoandikwa lakini moja inanichota zaidi na kunikumbusha nyumbani. Ni kauli nzito, “kila mtu ana haki ya kuutafuta ukweli lakini akishaupata ana wajibu wa kuutoa huo ukweli”. Nakumbuka, wapo watu walioishi maneno haya nchini kwetu. Ukisoma kitabu cha uongozi wetu na hatma ya Tanzania cha hayati baba wa Taifa utakubaliana nami. Kwenye kitabu hicho Nyerere ameeleza hatua kwa hatua jinsi alivyoutafuta ukweli kuhusu hatma ya Tanzania, alipoupata akauweka wazi. Kwa maandishi yake akatamka ‘our country is rotten to the core’. Kwa tafsiri yangu, nchi yetu imeoza mpaka kitovuni. Mwalimu akaelezea jinsi ufisadi na kutowajibika kulivyoshamiri na kutishia hatma ya Taifa. Aliamua ukweli utafanye huru, na kweli ukatufanya huru japo kwa muda ule mfupi.
Ushujaa huu wa Mwalimu Nyerere unanisukuma kuutafuta ukweli, nazunguka maeneo kadhaa, naupata ukweli, narejea hotelini nafika na kuanza kuandika. Lakini si kuhusu uongozi. Ni kuhusu “vihiyo”. Vihiyo wetu na hatma ya Tanzania. Nimepata haki ya kuupata ukweli, makala hii inatimiza wajibu wa kuutoa!
Vihiyo! Ni wakina nani? Kamusi niliyonayo hainipi tafsiri ya neno hili. Lakini kumbukumbu zinaniambia Mwaka 1996 aliyekuwa Mbunge wa jimbo la Temeke kupitia CCM Bw. Ramadhani Kihiyo, alibainika kughushi vyeti vya elimu, katika Mahakama Kuu ya Tanzania, mahakama ikatengua matokeo ya uchaguzi. Baada ya sakata hili kila aliyegushi vyeti akaitwa “Kihiyo”, wakati mwingine hata asiyesoma naye akaitwa “kihiyo”. Neno likashika kasi likazoeleka. Leo nikisema “Vihiyo” yatosha kueleweka kuwa ni wote wenye kujitambulisha kuwa na kiwango cha elimu wasichonacho. Hawa wako katika makundi mawili. Kundi la kwanza ni wale ambao wanaghushi vyeti kwa kuandika au kusema wamesoma chuo fulani kumbe hawajawahi kabisa kusoma katika chuo hicho. Hawa si sehemu ya makala hii. Hawa ni wajibu wa raia wema kuwataja, kutoa ushahidi na hatua zikachukuliwa. Hawa ni rahisi sana kwa vyombo vya dola kuwabaini. Kundi la pili ni vihiyo wanaotumia teknolojia. Wanatumia vyuo ambavyo vipo lakini havina hadhi ya vyuo. Ni mitambo kuzalisha vyeti. Hivyo wanashirikiana na vyuo hivi kughushi. Vyuo ambavyo havitambuliki kisheria, kimazingira wala kitaaluma. Hawa nawajadili katika makala hii. Kwa kuwa mkono wa dola unaweza kushindwa kuwabaini kama ukweli hautawekwa bayana.
Ukweli kuhusu vihiyo wetu na hatma ya Tanzania naupata ughaibuni? Ndio!. Niko nje, lakini Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEKNOHAMA) imefanya dunia kuwa kiganja. Upaswa kuwa mjanja tu kujua nini kinaendelea. Hivi karibuni nilitembelea tovuti na kukuta habari kwamba kuna kashfa ndani ya Bunge letu tukufu. Kwamba kuna sakata la baadhi ya wabunge kutuhumiwa kughushi vyeti. Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Bwana Samwel Sitta alizungumzia sakata la skendo linalowakabili wabunge wanaotuhumiwa kufoji vyeti vya elimu kuonyesha kitabu kimepanda kumbe siyo. Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano Bw. Samwel Sitta amekiri tuhuma hizo kuwepo lakini akasema suala zima hivi sasa liko mikononi mwa vyombo vya dola. Spika Sitta amesema baada ya kupata tuhuma hizo, aliyaripoti majina hayo kwa vyombo vya dola, ikiwemo polisi, kwa ajili ya uchunguzi zaidi. Hata hivyo, Bw.Sitta alitahadharisha kwamba idadi ya wabunge hao ni ndogo, hivyo jambo hilo lisikuzwe na kuonekana kana kwamba bunge lote ni linahusika. Aidha, Bw. Sitta alikataa kutaja majina ya wabunge hao, kwa madai kwamba bado ni watuhumiwa, na hatua yoyote ya kutaja majina yao inaweza kuvuruga uchunguzi. Aidha akasema hajaweka mipaka ya muda wa uchunguzi huo, ili kuvipa uhuru vyombo husika vifanye kazi kwa misingi ya maadili ya kazi zao. Aidha alipoulizwa ni hatua gani za kisheria ambazo watachukuliwa wabunge hao, iwapo watabainika kughushi vyeti vya elimu, Bw. Sitta akasema ni mapema kutaja hukumu hiyo. Lakini akasema ikishabainika hivyo, suala hilo litakuwa limegusa zaidi sheria za nchi kuliko hata Bunge.
Amebainisha kwamba mbunge mmoja kati ya hao, alilalamikiwa zaidi na mtu ambaye alimshinda katika kinyang’anyiro cha uchaguzi mkuu mwaka jana. Habari nzito hii!
Nikatafakari! Nikakumbuka kauli kauli nyingine, hii ilitolewa na Waziri wa Sayansi Teknolojia na Elimu ya Juu, Profesa Msolla, kwamba serikali itawashughulikia wote wenye vyeti vya kughushi.Nikimnukuu, "Kuna hili suala la mtu kuwa na fedha na kuuziwa digrii...anatakiwa kusema anahitaji cheti cha aina gani na kwa daraja gani kisha akiwasilisha hundi anatumiwa digrii yake. Watu wa aina hii lazima hatua zichukuliwe ili kuwabaini na tuwachukulie hatua," Hii aliitoa mwanzoni mwaka, katika mkutano wake wa kwanza kabisa na watendaji wa wizara yake. Miezi kadhaa imepita mpaka naondoka nyumbani sijamsikia tena Waziri akizungumzia suala hili. Pengine kauli ya Sitta ni fukuto la hekaheka za Profesa Msolla. Lakini nachelea kuamini hiyo kwa Spika ameweka bayana kwamba uamuzi wake wa kuchunguza umetokana na barua ambazo ameandikiwa na raia wema kuhusu suala hili. Nami nachukua fursa hii kama raia mwema kuchangia masuala kadhaa kwa uwazi kuhusu sakata hili.
Baada ya shutuma hizi kwa waheshimiwa wabunge wetu, nikaamua kutembelea tovuti ya bunge letu tukufu kupata japo hisia za kashfa hii. Kitu kimoja kilinivuta kuwa mdadisi zaidi, nakuta karibu asilimia kumi ya wabunge wamepata shahada na wengine udaktari hivi karibuni. Hii ni habari njema kwa Taifa!. Kinachonivutia, wengi wamesoma katika vyuo vitatu vinavyofanana- Washington International University, Pacific Western University na Commonwealth Open University. Cha pekee zaidi wamehitimu na wengine udaktari kwa muda mfupi. Jina la chuo kimojawapo linavuta wasi wasi wangu zaidi kuliko mengine. Nalikumbuka hilo kwa kuwa mwanzoni mwa mwaka huu lilizua mjadala katika uchaguzi nchini Uingereza. Katika uchaguzi huo, mgombea wa Torries katika jimbo la Elmwood Transcorna, Bi. Linda West aliitwa “Kihiyo”. Alishambuliwa kwa kujiita Daktari wa Falsafa wakati hana hadhi hiyo na kwamba chuo unachokisema hakitambuliki. Yeye mwenyewe akaibuka na kukiri kuwa chuo hicho hakitambuliwi na mabaraza ya ithibati lakini kimempa shahada ya udaktari. Hivyo hajaghushi!
Heeh! Kumbe wabunge wetu ambao wengine ni mawaziri na manaibu nao wamesoma kwenye chuo hicho. Napata shauku. Natandaa zaidi. Natembelea tovuti ya chuo chetu kikuu kimojawapo. Haah! Nakuta wahadhiri kadhaa wamepata shahada zao za udaktari katika vyuo hivi. Naendelea na udadisi zaidi. Mama yangu, nakuta rais mmojawapo katika eneo la maziwa makuu naye amepata shahada yake katika vyuo hivi. Nashusha pumzi!
Naendelea naendelea na udadisi zaidi. Natembelea tovuti za vyuo hii. Nakuta mambo ya kuvutia. Vigezo vya kila mtu kuweza kupata shahada; moja, mbili, tatu-kiasi chako unachotaka kupata. Kadiri ya uwezo wako wa kutuma maombi, kulipa ada na kupeleka nyaraka wanazohitaji.
Kimoja kinasema. Udaktari wa falsafa unaweza kupatikana kwa mwaka mmoja ilimradi mwanafunzi popote pale alipo awasilishe dhana (thesis) ya kuelezea ufahamu wake wa somo analotaka apewe udaktari. Kingine kinaeleza, “hatutasema katika shahada yako kwamba umechukua shahada yako kwa kujifunza ukiwa mbali (distance learning)”. Chuo kinajiuliza swali- “Vyeti wa chuo chenu ni halisi?Kina jibu chenyewe-Ndio, vimethibitishwa na mawakili (notary). Hiki kinajivunia kwa kutoa shahada ya udaktari kwa bei nafuu kabisa, dola elfu nne na ushee. Kingine kinajitangaza, “pata udaktari wa falsafa bila kukaa darasani”. Kimoja kimeandika kabisa, hakuna vigezo vyovyote (no entry requirement) kama uanataka kuingia shahada ya kwanza. Duh!, najiuliza kwa utaratibu huu kwa nini serikali isitoe ruzuku kidogo kwa kila mwananchi, watu wengi wakapata shahada za kutosha, wengine wakajiajiri, wengine wakaajiriwa katika nafasi zinazohitaji wataalamu na wengine wakasambazwa kote ulimwenguni kama wataalamu na kuijaza nchi mapesa ya kigeni? Ndio Mzee!
Kwa hatua hii naamua kuachana na udadisi. Naamua kufanya uchunguzi wa haraka. Naanza na mtandao. Dunia ya utandawazi! Kwanza nakuta vyuo vyenye kutambulika na kuheshimika duniani shahada zinatolewa kwa miaka kadhaa, udaktari ndio usiseme!. Tena kwa gharama kubwa, hata vyuo vya Tanzania. Nakuta vyuo vimethibitishwa na mabaraza ya ithabati. Hata nyumbani Tanzania, chuo kikuu lazima kithibitishwe na baraza la Taifa la ithabati(National Accreditation Council). Na baadhi ya wahitimu toka nje ya nchi hupaswa kupeleka vyeti vyao kwenye baraza kama wametoka katika vyuo visivyozoeleka ili vyeti viweze kutambuliwa hadhi yake. Nakuta kimoja kimetoa onyo kwa maandishi madogo kwamba vyeti vyake havijathibitishwa na baraza la ithabati la nchi kilichomo. Nakuta kingine kinatamka kabisa kuwa vyeti vyake vinakubaliwa na baadhi ya waajiri lakini hakiwezi kukuhakikishia kuwa mwajiri wako atakubali cheti hicho. Maajabu!
Naamua kufanya uchunguzi wa ziada. Niko Washington, na chuo kimojawapo kinaitwa Washington International University (WIU). Naamua kuzunguka. Nafika George Washington University. Wanakana kwamba sio wenyewe, na wanaweka wazi kuwa hakuna chuo kinachoitwa hivyo hapa katika mji mkuu wa Marekani. Naamua kwenda kwenye mamlaka zinazohusika na elimu-nakutana na ukweli unaosisimua. Chuo hiki hakitambuliwi na baraza lolote la ithabati, sio Marekani tu hata nchi nyingine kama Canada na Uingereza. Chuo hiki kimepigwa marufuku majimbo mbalimbali mathalani Hawaii na Oregon huku Marekani na nchini Australia. Chuo kina wahadhiri wawili tu wenye shahada za udaktari. Chuo hakina mazingira ya chuo (campus), kinafanyia kazi zake nje katika kakisiwa kadogo maeneo ya Carribean. Chuo hiki kilishtakiwa na kuhukumiwa Hawii kikaamua kufunga taasisi yake na kuhamishia ofisi yake Pennyslvania. Kwa uchambuzi wowote, chuo hiki ni kinu cha diploma(diploma mill). Ni chuo cha kutoa shahada ‘vihiyo’.
Nikarejea na kuanza kutafakari kuhusu “vihiyo” na hatma ya Tanzania. Nini hatma ya mwanachuo anayefundishwa na mhadhiri kihiyo? Jibu liko kwenye sayansi ya kompyuta-GIGO (Garbage Inn, Garbage Out). Takataka Ikiingia, Takataka Itatoka!, Taifa la vihiyo. Taifa linapata hasara kiasi gani pale ambapo mishahara inalipwa kwa watu ambao viwango vyao haviwafanyi wastahili kulipwa mishahara wanayolipwa? Ikumbukwe kuwa baadhi ya mishahara inalipwa kulingana na kiwango cha elimu. Wananchi wa baadhi ya majimbo wanapata faida gani kwa kuongozwa na viongozi ambao hawakuwastahili? Naambiwa wapo waliojinadi katika kampeni kwamba wachaguliwe kwa kuwa wamesoma zaidi yaw engine, ya kwamba wana udaktari wa falsafa. Pengine hata kasi ya Rais wetu Kikwete inapunguzwa na mambo kama haya. Nakumbuka pamoja na kusema kwamba hakuwapanga mawaziri kutokana na taaluma zao kwa kuwa uwaziri hausomewi, JK amekuwa akisisitiza sana kwamba ana matumaini kubwa na safu yake kwani imejaa wasomi kuzidi yeye, tena wengine wana udaktari wa falsafa. Kubwa kuliko yote, inakuwaje pale ambapo wengine wanashahada kama hizi katika masuala yanayogusa uhai wa binadamu. Nakumbuka mjadala wa Bi. Linda West, kule uingereza ulikuwa mkali zaidi kwani kitaaluma alikuwa nesi na akajipatia udaktari wa falsafa katika utawala wa afya! Tunaowakina Linda wangapi katika taasisi zetu nyeti?
Kwa vyovyote haya maneno ni makali, yanaumiza na kuchoma roho na pengine hata kuniogopesha. Lakini tusionane maadui, hatma ya Taifa iko mashakani katika hili. Ni kama kwenda peponi, sote tunapenda kwenda hata sasa hivi. Lakini kwa nini tunaogopa kufa wakati ndio njia pekee ya kwenda peponi. Naamini waliosoma katika vyuo hivi wanapaswa kuwa wakwanza kujitokeza kupinga. Ama kama hanauona ukweli huu wawe wa kwanza kujitokeza kukiri tatizo hili kwa maslahi ya Taifa. Na kutangaza wazi kwamba pengine walitapeliwa na vyuo vya jamii hiyo. Na kuomba umma usiwaite tena kwamba ni madaktari au kwamba wasitambuliwa kuwa wanashahada za ngazi ambazo wamezipata katika vyuo vya jamii hii. Nilisema mwazoni. Ukweli utatufanya huru.
Hili lisipofanyika mamlaka zinazohusika zichukue hatua. Naamini Profesa Msolla sasa umepata mahali pa ziada kwa kuanzia. Sikubalini na mheshimiwa Spika. Sio suala la vyombo vya dola. Ofisi yake kama mwajiri inawajibu wa kufanya uchunguzi wa ndani kabla na ikiwezekana kutoa taarifa kwa umma hata kabla ya kuwasilisha mashtaka kwa vyombo vya dola. Ofisi ya bunge inapaswa kuiitisha vyeti halisi vya wabunge, ikivitilia shaka ndio inaweza kuvitoa kwa vyombo vya dola. Lakini hii ni kwa vihiyo wa kundi la kwanza. Hili kundi la pili nililolitaja halihitaji hatua hii. Maana ni wazi vyeti wanavyo, tena vizuri sana. Vyenye nembo za kila namna. Hata ukiwasiliana na vyuo vya jamii hiyo watakwambia hawa ni walikuwa wanafunzi wetu. Wanao utaalamu wa kuwalinda wateja wao. Hapa ofisi ya spika ishirikiane na baraza la ithabati la Taifa (NAC). Tamko litolewe kama vyuo hivi viko katika orodha ya vyuo vilivyopitishwa. Kama hakuna serikali ifanye mchakato wa kuvipima kwamba kwa utaratibu wao huu niliotaja kama vinakidhi hadhi ya kuwa vyuo vikuu kama kama itathibitika ndio nitakuwa wa kwanza kuomba radhi kwa usumbufu wowote uliowapata wote waliosoma katika vyuo hivi na nitafuta makala yangu yote sentensi kwa sentensi na neno kwa neno. Lakini nitafanya hivyo kwa serikali ya nchi yetu pekee sitafanya hivyo kwa Marekani, Uingereza, Australia na nchi nyingine ambazo zimekataa kuvitambua vyeti toka katika vyuo vya jamii hiyo ambavyo viko vingi kote duniani. Mwanafalsafa, mwanafasihi na gwiji wa magwiji wa lugha ya Kiswahili hayati Shaaban Robert katika moja ya vitabu vyake aliwahi kunasihi hivi, ninamnukuu "Msema kweli hukimbiwa na marafiki zake nikipatwa na ajali kama hiyo sitawaonea wivu wale wanaodumu na marafiki zao siku zote. Siwezi kuikana kweli kwa kuchelea upweke wa kitambo na kujinyima ushirika wa milele unaotarajiwa kutokea baada ya kushindwa kwa uongo". Maneno haya yawe chagizo kwako na kwangu wakati tukiendelea kutafakari kuhusu “Vihiyo” na hatma ya Tanzania.
Mwandishi wa makala hii ni Mkurugenzi wa Vijana CHADEMA kwa sasa yuko ziarani na anapatikana kupitia mnyika@yahoo.com na www.chadema.net/blogu/mnyika/