Napenda kuungana na wote waliompongeza waziri wa elimu na mafunzo ya ufundi, Magreth Sitta (MB) na serekali kwa ujumla kwa uamuzi wa kubatilisha mabadiliko ya elimu ya msingi na sekondari yaliyofanywa mwaka 2004 yaliyosababisha kufutwa na kuunganishwa kwa baadhi ya masomo. Namshukuru Sitta na serekali kwa kurejesha mitaala ya zamani inayotenganisha masomo mbalimbali katika ngazi hizo za elimu.
Katika kutangaza uamuzi huo sababu kuu mbili zimetolewa:Mosi, wadau kutoridhiwa na mabadiliko hayo; Pili,mabadiliko na changamoto mbalimbali ambavyo vimetokea hivi sasa kijamii na kiuchumi.
Nakubaliana na sababu ya kwanza kwani wananchi, wanafunzi, wazazi na waalimu kupitia Chama cha Waalimu Tanzania (CWT) wakati huo wewe ukiwa kiongozi wake walipinga hoja hiyo. Pia wadau wengine wakiwemo Chama cha Mameneja na Wamiliki wa shule na vyuo binafsi (Tamangsco), vyombo vingi vya habari na vyama vya siasa walipinga uamuzi huu. Wapo pia watu binafsi waliochambua kwa kina madhara ya mabadiliko hayo wakati huo mathalani Mzee Yusufu Halimoja. Lakini serekali ya wakati huo haikutaka kusikiliza!. Nakumbuka waziri wa wakati huo ambaye sasa ni waziri wa Kilimo, Joseph Mungai alitetea uamuzi huo bungeni kuwa umetokana na wataalamu ambao umehusisha pia maoni ya wadau. Mungai pia alitetea kwamba uamuzi huo umetokana na mabadiliko na changamoto mbalimbali mathalani mfumo wa soko huria, mahitaji ya sayansi na teknolojia na ajira katika sekta mbalimbali.
Nimeshangaa waziri na serekali kutumia hoja hizi hizi za mabadiliko na changamoto kama sababu ya msingi wa kutengua mabadiliko ya awali. Haiyumkiniki kwamba kutoka mwaka 2004 serekali iliposema mabadiliko na changamoto hizi zimetokea leo baada ya miaka isiyofika miwili mabadiliko na changamoto hizi zimetokea tena safari hii kinyume cha yale ya mwanzoni. Ndio maana sitaki kujilazimisha kuikubali sababu ya pili labda niambiwe ililenga ‘kufunika kombe’. Kama hoja ya pili ingekuwa na uzito ni wazi serekali isingetumia lugha ya ‘kutengua mabadiliko’ bali ingesema ‘kufanya mabadiliko’.
Kwa kuwa mabadiliko na changamoto hizi za kijamii na kiuchumi havitokei kwa muda mfupi ni wazi kuwa vilishatokea wakati serekali inafanya mabadiliko ya mitaala mwaka 2004. Kwa mantiki hiyo ni lazima kukiri kuwa mabadiliko ya wakati huo yalifanyika bila kuzingatia hali halisi. Katika hali kama hiyo ni wazi wataalam waliotajwa hawakuzingatia maoni na hali halisi na hatimaye kumdanganya waziri na serekali, kama kweli ulikuwa msimamo wa wataalam huru. Katika serekali inayoelezwa kuendeleza uwajibikaji kwa ‘ari mpya, kasi mpya, na nguvu mpya’ ni lazima kuchukua hatua za ziada ili kuleta mabadiliko ya kweli na uhuru wa kweli. Lakini hatua hizi zisiishie kwa wataalam tu-hata wanasiasa walioongoza mchakato huu. Sote tunajua kuwa sehemu ya msingi ya wajibu wa wanasiasa wakiwemo Mawaziri ni kusikiliza maoni ya wananchi. Hivyo kwa kuwa wananchi na wadau wengine walisema,tena walisema sahihi lakini hawakusikilizwa uwajibikaji ama uwajibishwaji haupaswi kuepukwa!
Vipo vyama vya siasa ambavyo vilitekeleza wajibu huu. Mathalani CHADEMA ilisikia kilio cha wadau na kuweka masomo yaliyorejeshwa kama sehemu ya sera yake ya elimu toka wakati huo na ulipofika uchaguzi mkuu 2005 ilitamka bayana katika ilani yake kuwa ingebatilisha uamuzi huo na kurejesha masomo yaliyofutwa na mgombea wake wa urais wakati huo-Freeman Mbowe kuipigia debe sana ajenda hii. CCM kwa upande wake haikuwa na suala hili katika ilani yake lakini Rais Jakaya Kikwete ametamka hadharani kwamba hili ni moja ya suala ambalo kila alipopita wakati wa kampeni wananchi walimwomba alishughulikie. Alisikiliza wananchi na wadau na mara baada ya kuingia katika utawala alitangaza nia ya kutengua mabadiliko haya alipotembelea wizara ya elimu na mafunzo. Huku ndiko kutimiza wajibu wa uanasiasa!
Pamoja na waziri Sitta na serekali kuchukua hatua ambazo zitasadia sakata kama hili lisitokee wakati mwingine namuomba pia atoe ufafanuzi kuhusu masuala yafuatayo ambayo kimsingi yalipaswa kuulizwa bungeni hoja husika ilipowasilishwa: Mosi,ni wanafunzi wangapi ambao wameathirika na mabadiliko haya ya kizungumkuti? Serekali inampango gani wakuwaongezea au kuwapitisha katika programu maalum ili kuwawezesha kupata stadi na ufahamu wa kukabiliana na changamoto zilizotajwa ambazo wamezikosa? Pili: ni hasara kiasi gani imepatikana kutokana na mabadiliko yaliyofanywa mathalani idadi ya vitabu vya kiada na ziada ambavyo tayari vilishachapwa? Ni makampuni yapi binafsi yatapata hasara hii?, serekali inaweza kupata hasara kiasi gani kutokana na fidia inayoweza kutokana na madai ya na makampuni ya vitabu ambayo yalikuwa na mikataba na serekali katika kuzalisha vitabu ambavyo vitapaswa kuwekwa pembeni kutokana na mabadiliko yaliyofanyika?Tatu, wakati mabadiliko haya yanapingwa serekali ilishutumiwa kuwa mabadiliko yalishinikizwa kutokana na ufisadi hususani kwa lengo la kuzalisha tenda,serekali ya wakati huo ilikaa kimya-Je,ukimya huu ulimaanisha ‘ndio’?
Nategemea masuala haya yatatolewa ufafanuzi wa wazi na serekali pamoja na kuwa yameulizwa na mwananchi wa kawaida. Asante waziri Sitta, usisite kuchukua hatua.
John J. Mnyika
kazi wa Jimbo la Ubungo
0744 694 553
mnyika@chadema.net