Nawashukuru wananchi wa Jimbo la Ubungo na watanzania kwa ujumla walioniunga mkono kwa hali na mali. Wapo walionipa kura, wapo walionichangia, wapo waliozunguka huko na huko kwa hiyari-kwa wote nasema asante. Nguvu yenu haijapotea bure. Mmechangia katika mchakato wa demokrasia na maendeleo. Nashukuru kuwa kampeni zangu zimeendeshwa kwa nguvu ya wananchi kama ambavyo Nyerere na wengine waliendesha kampeni za kudai uhuru.
Natamka kuwa kugombea kwangu kumekuwa na mafanikio makubwa na kuna mengi ambayo wanasiasa wanaochipukia wanaweza kujifunza kutokana na kugombea kwangu za jimbo la Ubungo. Ya pekee ya kujifunza ni kwamba siasa na uongozi si haki ya tabaka fulani katika jamii ila ni wajibu wa watanzania wote wenye vipaji, fursa au uwezo wa uongozi. Kupitia kampeni zangu nimedhihirisha kuwa vijana ama wananasiasa wa kizazi kipya wanao uwezo kabisa wa kushika mamlaka katika nchi hii. Imedhihirika pia hata bila ya rushwa na takrima upo uwezekano wa mgombea kukubalika katika jamii. Pia imeonyesha wazi kuwa pamoja na elimu duni yao ya uraia bado wanapiga kura wakisikiliza hoja huamua kupenda zaidi sera na ajenda kuliko matusi na malumbano. Yapo matokeo ya papo kwa papo yaliyotokana na kugombea kwangu mathalani katika kata moja shamba la Kijiji lililouzwa kinyemela lilirudishwa kwa wananchi baada ya kutangaza kulishikia bango suala hili, wananchi wamepata taarifa kuhusu baadhi ya fursa ambazo walikuwa hawazifahamu na tatizo la maji jimbo la Ubungo limepata sura mpya inayoleta matumaini ya utatuzi.
Mchakato wa uchaguzi katika hatua za awali ulikwenda vizuri pamoja na mapungufu madogo madogo. Lakini hatua za mwisho za zilikuwa na mapungufu makubwa kama ambavyo ripoti ambayo naiwasilisha kwenu inavyoainisha. Lakini kwa ufupi ni kuwa kulikuwa na matatizo katika mpangilio wa vituo na hivyo vituo vingine kuleta hisia kuwa ni ‘vituo hewa’ na ukiukwaji wa hali ya juu wa taratibu za jumlisha na kutangaza matokeo unaoacha maswali mengi kuhusu ‘nini kilichokuwa kinafichwa’. Kimsingi ni kazi ya sheria chini ya mahakama kuamua kuhusu shutuma hizi. Lakini mtiririko wa yaliyotokea unaonyesha:
Mosi, msimamizi alijumlisha matokeo peke yake bila mawakala wa vyama hali inayoleta hisia kuwa matokeo ‘yalipikwa’; Pili; msimamizi aliruka hatua ya kisheria ya kutangaza kwa sauti matokeo ya kituo hadi kituo hali inayoleta hisia ya kwamba matokeo yalifichwa ili uhalali wa vituo na kura usihojiwe kama ilivyotokea katika kura za rais. Kwa vyovyote vile, mimi kama mgombea nitakiomba chama changu tuchukue hatua za kisheria - ni muhimu zikawa hatua za kitaasisi kutokana na gharama na urasimu ulioko katika sekta ya mahakama.
Kwa upande mwingine zipo hisia za ‘mikakati ya kisayansi’ ambayo imefanyika Jimbo la Ubungo kama ilivyo katika majimbo mengine katika uchaguzi wa mwaka huu. Ni wajibu wa wadau wa demokrasia kote nchini kufanya utafiti wa kina wa nini haswa kilitendeka. ‘Mikakati hii ya kisayansi’ inatiliwa shaka kwani wananchi wa Jimbo la Ubungo wanaamini kwamba matokeo hayawasilishi ridhaa yao. Kwa vyovyote vile matokeo ya mwaka huu ni funzo kwa wapenda demokrasia kwamba uhuru wa vyombo vya uchaguzi na uthabiti wa sheria ni mihimili muhimu katika uchaguzi. Katika mazingira ya sasa ambapo chama tawala ni chama dola uchaguzi huru na haki ni kama ‘ngamia kupenya katika tundu la sindano’. Hivyo, suala la msingi kwa vyama na wadau wengine wote na haswa wananchi kupitia nguvu ya umma kutaka katiba mpya na tume huru ya uchaguzi.
Pamoja na yote hayo bado viongozi waliochaguliwa ndio viongozi halali kwa mujibu wa sheria labda sheria hizo hizo ziamue vinginevyo wakati mwingineo. Hivyo rai yangu ni kuwa wapewe ushirikiano unaostahili. Uchaguzi umekwisha, sasa wazalendo wote tushirikiane kuleta demokrasia na maendeleo katika jimbo letu na nchi yetu. Kwa upande wangu nitafurahi kama mgombea aliyeshinda atachota mawazo kutoka katika sera zangu na kujifunza kutoka mengi yaliyosemwa ama kufanywa na wagombea wengine. Kwa upande mwingine wananchi wa Jimbo la Ubungo wawe huru kunitumia kwa namna yoyote itakayofaa kwa jina lolote litakalostahili. Nawaahidi tutakuwa pamoja katika kipindi chote na sehemu ya ahadi nilizozitoa jukwaani ambazo zinawezekana kutekelezwa bila ya mimi kuwa mbunge nitafanya hivyo. Wakati huohuo, kama kijana nitaendelea kujiendeleza kielimu, kiuchumi, kijamii na kisiasa.