lf.bevel
MWANZO CHAMA SERA KATIBA TUUNGE MKONO UCHAGUZI TUWASILIANE

Sera ya Maendeleo ya Vijana Tanzania
SERA AU SIRI?

na
John J. Mnyika

Mwaka 1996 Tanzania ilipiga hatua katika sekta ya vijana kwa kupitisha toleo la kwanza la sera ya maendeleo ya vijana nchini. Miaka isiyopungua saba imepita hivyo kwa uhai wa sera yoyote marejeo ni suala lisilohitaji shinikizo kutekelezwa. Pengine ni kwa kusukumwa na uhalisi huu wa kiutendaji ndio maana serekali imeanzisha tena mchakato wa kufanyia marejeo sera hii. Siri ya kuanza kwa mchakato huu ilifichuliwa na waziri wa Kazi, maendeleo ya vijana na michezo - Profesa Juma Kapuya katika hotuba yake ya kufungua maadhimisho ya siku ya kimataifa ya vijana Agosti 12 mwaka 2003.

Mheshimiwa waziri alibainisha kwamba rasimu ya sera tayari imesogezwa mikononi mwa sekretariati ya baraza la mawaziri ikiongezewa 'mapishi' kabla ya kupitishwa, nanukuu, "wiki chache zijazo". Ingawa miezi lukuki imepita toka ahadi hiyo ilipotolewa si lengo la makala haya kuhoji kuchelewa kwa mchakato huu. Labda subiri-kwanza hii imetokana na 'kelele' zilizofuata zikihoji ni kwa kiasi gani vijana walishirikishwa katika mchakato wa kurejea (reviewing process) sera hii. Hayumkini serekali imeamua kutafakari tena haja ya kuwashirikisha vijana katika mchakato huu.

Itakumbukwa kwamba 'nenda-rudi' kama hii ilitokea mwaka 2000 wakati marejeo mengine yalipofanyika lakini yakafutikwa-futi huku wadadisi wa mambo wakihusisha uamuzi huu na joto la uchaguzi mkuu na hoja za asasi za vijana zikiratibiwa na asasi iliyofutwa ya NYF kuhusu rasimu ya marejeo hayo.

Kuandaliwa kwa warsha ya kujadili sera ya mandeleo ya vijana hivi karibuni ni ishara tosha kwamba mlango wa kutoa maoni umefunguliwa rasmi. Makala haya yanalengo la kuchambua masuala kadhaa kuhusu sera iliyopo na mchakato unaoendelea wa kurejea husika ili kuibua mjadala wa umma kuhusu sera ya vijana nchini.

Umuhimu wa sera ya vijana ni mkubwa hasa katika kipindi hiki ambacho vijana, wazazi, wadau mbalimbali na jamii kwa ujumla tunaishi na kuendesha harakati mbalimbali katika ulimwengu unaobadilisha teknolojia, mitindo, itikadi, tamaduni na mitazamo kwa kasi ya paa. Tanzania si kisiwa katika dunia hii tandawazi hivyo upepo wa mabadiliko haya umesambaza athari kadhaa mathalani kushuka kwa uchumi, kufifia kwa taratibu zilizowekwa za kuwalea vijana, kupotea kwa maadili mazuri miongoni mwa jamii pamoja na kushuka kwa heshima ya mwanadamu.

Hivyo sera ya vijana ni nyaraka muhimu inayotoa mwongozo kwa vijana na sekta zote zote zinazohusika na maendeleo ya vijana kubuni na kutekeleza mipango yenye kuwafanya vijana kuwa raia bora wenye moyo wa uzalendo na msukumo wa kimaendeleo.

Hakika ni vyema kuanza kuibua mjadala kwa kuanza kuchambua mapungufu ya sera ya maendeleo ya vijana iliyopo hivi sasa. Sera ambayo kwa kipindi kirefu imekuwa 'mwenza wa makabati' ya ofisi za serekali pamoja na asasi chache za vijana zilizoko mijini. Sera ambayo haiko kwenye duka la nyaraka na vitabu vya serekali. Sera ambayo haiko kwenye ofisi za asasi za vijana zilizo nyingi. Sera ambayo haiko katika maktaba za mashule na jumuia. Ni sera inayofikia ukingoni bila kuonwa sembuse kusomwa na vijana walio wengi na wadau waliotajwa ndani yake. Inashangaza kwamba pamoja na asasi za vijana pamoja na mashule kufahamika anuani zake, idara inayohusika imeshindwa kutuma kwa njia ya posta japo nakala moja ya sera kwa asasi na vikundi husika. Gharama ya zoezi hili ni sawa na warsha moja! Matokeo yake nakala lukuki zilizozalishwa kwa pesa za wahisani zinaendelea kupata vumbi katika makabati ya warasimu. Mola bariki wito alioutoa mheshimiwa Rais mwaka jana kuhusu mawasiliano kati ya watumishi wa serekali na umma ufanye maajabu katika mwaka huu!

Kosa kuu la kwanza sera inayotumika sasa ni katika kutoa tafsiri ya kijana ni nani. Sera 'imemeza' nzima nzima tafsiri ya kwamba kijana ni mtu mwenye umri wa kuanzia miaka 15 mpaka 24. Matokeo ya tafsiri hii ni sera nzima pamoja na programu mbalimbali nchini kumtazama kijana kama kiumbe mwenye mchango mdogo katika jamii. Upungufu huu umeviza upana wa masuala mbalimbali ambayo sera inapaswa kuyashughulikia kuhusu vijana. Kwa tafsri hii asasi zinazohusika zimetua jukumu la kuwalenga sehemu kubwa ya vijana. Umoja wa mataifa unakubali kwamba maana ya kijana inaweza kutofautiana kutokana na mila, desturi, hali na mahitaji ya jamii. Katika kurejea sera hii ni vyema umri wa ujana ukapanuliwa kutokana na mahitaji ya jamii yetu.

Katiba za asasi kadhaa za vijana mathalani YUNA na TYVA zinataja umri wa ujana mpaka miaka 30. Tafsiri hii ilipitishwa pia na mkutano wa kimataifa wa vijana ulioitishwa kuunda asasi ya Umoja wa mataifa ya vijana uliofanyika Hispania mwaka jana. Hata benki ya dunia katika mchakato wake wa kukusanya maoni kuhusu vijana ulitumia tafsiri hii. Lakini nia ya serekali ni kupandisha umri wa ujana mpaka 35. Haibainishwi uamuzi huu unapigiwa upatu kwa hoja zipi. Ama ni kuiga nchi nyingi za afrika ambazo zinatumia tafsiri hii au ni kupenyeza tafsiri ya Umoja wa vijana wa chama tawala! Sera haibainishi pia mgawanyo wa kiumri miongoni mwa vijana (15-24 na 25-35) kwa misingi ya utofauti wa kimahitaji. Hivyo mjadala mpana unahitajika katika suala hili. Zaidi ya kutumia tafsiri ya umri sera ilipaswa kutumia fursa hii kueleza tabia zinazowatofautisha vijana na makundi umri mengine. Vijana wana ari, maono, utayari, nguvu, shauku, uthubutu, vipaji na sifa nyingine kedekede.

Kwa kuchukua tafsiri ndogo ya umri sera imepotosha kwamba vijana ni asilimia ishirini na ushee ya taifa hili. Takwimu sahihi zinahitajika kwa mujibu wa tafsiri mpya na sensa ya hivi karibuni. Inapaswa kutambua kwamba watanzania chini ya miaka 35 ni zaidi ya asilimia 60 ya idadi ya watu nchini. Wakati Tanzania inapata Uhuru idadi ya wakazi ilikuwa takribani milioni tisa. Hii inaamaanisha kwamba sehemu kubwa ya watu 34.5 milioni walioko sasa ni kizazi cha baada ya Uhuru-kizazi cha vijana. Sera inapaswa itambue hili ili nafasi ya vijana katika taifa changa la Tanzania iwe bayana. Sera inapaswa kutambua kwa idadi na mahitaji kwamba vijana wako wa aina mbalimbali: maskini na matajiri, wakike na wakiume, waliokatika sekta rasmi na isiyo rasmi, waliooa na wasiooa, wenye ajira na waliojaa vijiweni, waliosoma na wasiosoma, wamijini na wavijijini. Sera inapaswa iwatambue vijana wenye ulemavu, wakulima nk.

Ukisoma jinsi sera ilivyochambua hali ya kiuchumi ya vijana nchini utamaizi jinsi dhana ya 'funika kombe mwanaharamu apite' inavyotumika. Sera imeshindwa kubainisha kwa takwimu umaskini ukiambatana na 'kansa' ya ukosefu wa ajira vinavyowatafuna vijana. Sera inashindwa kusema wazi kwamba vijana wa Tanzania ni walalahoi!. Sera haisemi kwamba asilimia kubwa ya vijana wa Tanzania hawamiliki njia kuu za kiuchumi kama ardhi na mitaji. Sera inawatazama vijana kama wafanyabiashara ndogondogo na wazalishaji mali wa dogo. Kwa mtazamo huu si ajabu kuona mipango ya serekali katika ngazi mbalimbali inalenga kutoa mikopo uchwara kwa vijana. Matokeo yake ni vijana wengi kutia mfukoni pesa hizi kiduchu na 'kutokomea'. Mpaka lini vijana wa Tanzania watendelea kutizamwa kama wamachinga? Sera inatoa uchambuzi tenge kwamba tegemeo pekee la vijana kiuchumi ni biashara na shughuli ndogo ndogo za uzalishaji na kushindwa kutambua mchango wa vijana kiuchumi katika sekta za huduma, michezo na burudani.

Sera imechambua kwa kifupi sana hali ya vijana kisiasa. Sera imeshindwa kukubaliana na ukweli kwamba siasa ndio msingi wa ushiriki na ushirikishwaji wa vijana kuchochea mabadiliko katika jamii. Tafsiri hapa ni kwamba kijana anatazamwa kama taifa la kesho.Kwa hali hii si ajabu kuona sera inalenga kumuandaa kijana kuwa kiongozi bora wa baadaye. Sera ilipaswa kubainisha kwamba kwa hali ilivyo vijana hawashiriki ipasavyo katika mchakato wa kisiasa. Vijana wanatumika kama vyombo vya kampeni. Kuna idadi ya vijana wachache sana katika vyombo vya maamuzi ukiwianisha na idadi ya vijana nchini. Mathalani wakati hakuna mbunge hata mmoja aliyechini ya miaka 27, kuna wabunge 17 tu wenye umri kati ya miaka 27 na 35. Sera iseme wazi kwamba hakuna chombo cha kuwawakilisha vijana nchini - Hakuna baraza la vijana nchini. Hivyo inapokuja suala la kuchagua wawakilishi wa vijana katika michakato mbalimbali mfumo wa 'mimi namjua' hutumika. Sera iseme kwamba bado kuna asasi za vijana chache na changa hususani katika maeneo ya vijijini. Uchambuzi katika sera ni utabibu wa majeraha ya kihistoria ni budi mgonjwa awe wazi kusema wapi panauma ama sivyo taifa litaumbuliwa kwa kilio kitakachotoka huko tuendapo!

Kiuchambuzi sera imejitutumua vyema kuchambua hali ya vijana kijamii utadhani ni sera ya malezi. Lakini sera haitaji mapungufu yaliyopo katika mifumo yetu ya ushauri nasaha na huduma kwa vijana waliothirika na madawa ya kulevya, UKIMWI, matatizo ya kifamilia na misongo mingine ya kijamii. Sera haitaji kabisa hali na wajibu wa vijana-wazazi ambao tayari wamezaa au wako katika maisha ya ndoa kwa ujumla. Katika kuchambua hali ya elimu na mafunzo kwa vijana mkazo umewekwa katika elimu ya msingi na elimu ya sekondari pekee. Sera imesheheni takwimu na kuepa kugusa matatizo ya msingi yanayowakabili vijana katika mchakato wa elimu mathalani kukosa ada, vifaa vya kusomea na matatizo ya kimitaala. Sera ilipaswa kusema wazi kwamba kuna mafunzo mathalani ya ujasiriamali ambayo hayapo vya kutosha katika mfumo wa elimu na hivyo kurudisha nyuma ari ya vijana kujiajiri.

Haki nyingi za vijana zimeachwa kuwa siri.Katika kuchambua haki za vijana sera imegusa haki tano zifuatazo: elimu, usawa, kuishi mahali popote, kufanya kazi na faragha. Hii inazua maswali mengi. Vigezo gani vimetumika kuchagua haki hizi pekee? Vipi kuhusu haki nyingine zilizoainishwa kwenye kanuni na wajibu katika katiba na mikataba ya kimataifa? Vipi kuhusu vijana kukamatwa kama wazururaji? Vipi kuhusu vijana kukosa chombo cha kuwaunganisha? Zipi haki za wachimbaji madini vijana? Vipi haki za wamachinga? Vipi haki za vijana vibarua? Vipi haki ya kupata taarifa kuhusu mambo yanayowahusu? Sera inaficha majibu na kufichua maswali!

Katika sera yoyote uchambuzi wa hali ilivyo ni mzizi,malengo ni shina, matawi huwa mipango, majani ni shughuli za kuleta maua ya mabadiliko. Hivyo uchambuzi finyu ulitolewa katika sera ya sasa ya vijana ni kiini cha mipango legelege kuhusu maendeleo ya vijana nchini. Kupinda kwa mwelekeo sera kinyume na uhalisi wa mambo kumesababisha kila mdau katika sekta ya vijana kwenda kivyake vyake. Si ajabu mambo kuwa shaghalabagala!

Ni mtanziko kwamba kurasa mbili na nusu tu ndio zimetumika kueleza malengo na mipango ya maendeleo ya vijana. Hapa ndipo mahali ambapo sera ilipaswa kutoa mwongozo wa kina kuhusu wapi kama taifa tunapeleka mustakabali wa vijana na kwa namna gani. Haitoshi kudondoa tu eti-mipango ya elimu na malezi, mipango ya barudani, mipango ya ujasiri nk. Sera inapaswa kutoa mwongozo kamilifu kuhusu mipango hii.

Sera imejaribu kutaja wadau mbalimbali na kueleza kwa kifupi jukumu la kila mmoja. Wadau zaidi wanahitaji kuongezwa kutokana na mazingira ya sasa.Inachekesha kwamba wizara ya sayansi teknolojia ilisahaulika kabisa miongoni mwa wadau zaidi ya 15 waliotajwa! Inasikitisha zaidi kwamba asasi na vikundi vya vijana na vijana kwa ujumla hawakuwekwa kama wadau katika utekelezaji wa sera huu. Mtazamo huu wa 'kaeni pale tuwafanyie kila kitu' hautajenga kamwe taifa lenye raia wenye kujituma na kujitegemea.

Sera imegutuka mwishoni na kutoa mwongozo wa kuundwa kwa baraza la maendeleo la vijana nchini huku muundo wake ukiwa ni suala linalokanganya. Kwanini liundwe na vyama na vikundi vya vijana? Kwa nini wanachama wa baraza hili wasiwe vijana mmoja mmoja kuanzia ngazi ya chini kama ilivyo kwa jirani zetu Uganda au kule Nigeria? Nini mamlaka kwa maneno mengine 'meno' ya baraza hili? Litaundwa na nani-bunge au vijana wenyewe?

Kiiini macho ni pale ambapo sera inaelekeza kuundwa kwa kamati za kirasimu za maendeleo ya vijana katika ngazi za mikoa na wilaya. Kamati hizi zimebakia serani kama siyo sirini isipokuwa kwa sehemu chache nchini. Kamati zilizochini ya uenyekiti wa wakuu wa mikoa na wakuu wa wilaya wajumbe wakiwemo wabunge na madiwani! Hapa ni mgongano mwingine kati ya matakwa ya kisiasa na hali halisi. Kwa namna yoyote kamati za vijana ziwepo katika muundo wa baraza. Hizi ni kamati wakilishi zitakazochaguliwa na vijana wenyewe. Kamati nyingine za kiutendaji zaweza kuundwa chini ya urasimu wa watawala kwa lengo la kusaidia utekelezaji wa mipango ya moja kwa moja ya mikoa na wilaya kuhusu vijana.

Marejeo ya sera yaweke bayana kwamba Baraza la Vijana nchini liatakuwa na dhima ya kufanya ufuatiliaji na tathmini kuhusu utekelezwaji wa sera ya vijana. Tuige mfano wa jirani zetu Afrika ya Kusini. Sera hii ya mwaka 1996 ya maendeleo ya vijana pamoja na kutoa jukumu la uratibu na usimamizi wa shughuli za maendeleo ya vijana kwa wizara inayoshughulikia sekta hii, haisemi chochote kuhusu nafasi na jukumu la idara ya vijana na maofisa wa maendeleo ya vijana waliopo nchini. Hekeya nyingine ya siri ya kisera!

Pamoja na kutaja haki za vijana nchini,sera ilipaswa kuwa na kipengele kinachozungumzia wajibu wa kijana wa kitanzania. Wajibu huu utatoa mwongozo wa kizalendo kwa vijana kama zilivyokuwa ahadi za mwa-TANU. Wajibu huu ni usuli wa vijana kujivunia ujana wao. Hii iende sambamba na sera kuwa na kipengele kinachoonyesha historia ya nafasi ya kijana katika Tanzania. Sera ieleze jinsi vijana walivyotoa mchango wa pekee katika maendeleo ya Taifa kuanzia harakarati za ukombozi mpaka vuguvugu la kuondoa unyonyaji. Wapo vijana waliofanya maajabu katika medani za michezo, sayansi nk. Wapo wengi. Utamaduni wa kuficha historia utawakosesha vijana urithi wenye kuchochea hamasa na ari ya kizalendo.

Katika kurejea sera kuongezwe kipengele cha hali inavyopaswa kuwa mara baada ya sehemu ya uchambuzi wa hali ilivyo. Hii ni sehemu ya ndoto na maono ya Taifa kuhusu maendeleo ya vijana Tanzania. Hii iandikwe kwa mujibu wa vipaumbele vya vijana. Utafiti unaonyesha vijana wanavipaumbele vifuatavyo: elimu, ajira, afya, nafasi katika vyombo vya kutoa maamuzi, vipaji kundelezwa, burudani/starehe na kuwa katika upendo hususani wa familia. Sera ya vijana inapaswa kuwa dira ya vijana nchini. Katika afya suala la afya ya uzazi kwa vijana lipewe msisitizo na kuwekewa kipengele mahususi.

Marejeo ya sera ni muhimu yafanyike kwa mujibu wa Tamko la Lisbon kuhusu sera za vijana, programu ya dunia ya maendeleo ya vijana kuanzia mwaka 2000 na kuendelea, mpango wa Braga wa maendeleo ya vijana, mkakati wa Dakar wa uwezeshaji wa vijana na mikataba mbalimbali ya kimataifa.

Mpaka sasa makala imechambua mapagufu ya sera iliyopo. Kwa kuwa kuna 'harufu' ya sera kufanyiwa marejeo ni vyema kuuchambua mchakato unaotumika sasa kurejea sera husika ili kuchochea ushiriki wa vijana na jamii kwa ujumla. Chini ya imani ya 'penye wengi hapa haribiki neno', sera ya sasa isingekuwa ilivyo kama vijana na jamii kwa ujumla wangehusishwa kikamilifu katika uundaji wa sera hiyo. Wakati wa wataalamu na warasimu wachache kujifungia vyumbani na kuundaa sera kwa siri umepita. Wakati wa vijana wachache kukusanywa bila uwakilishi mwafaka na kutamba katika mfumo huo kwamba vijana walishirikishwa usahaulike. Wakati wa rasimu ya sera kuwa 'hasimu' wa kufungiwa huku mjadala ukifanyika kwenye karatasi tupu usikubaliwe.

Ni wakati wa uwazi, ukweli na ushirikishwaji. Ni zama za maendeleo shirikishi-mwenye hamu ya maji na nia ya kuyatafuta ni yule mwenye kiu! Hivyo mikutano ya kukusanya maoni kuhusu sera ya vijana ifanyike mpaka vijijini. Sera hii ni ya vijana wote! Mijadala ifanywe kwenye vyombo vya habari. Wanaoandika waandike, wanaosema waseme. Katika mchakato huu mamlaka inayohusika iwe na mdomo mdogo, masikio makubwa na macho makubwa! Rasimu ya marejeo iwekwe kwenye tovoti ya taifa na kusambazwa kwa njia mbalimbali ili maoni zaidi yaweze kutolewa. Baadaye uitishwe mkutano wa vijana wa kitaifa kuhusu sera ya maendeleo ya vijana kupitisha. Baraza la mawaziri libaki na jukumu la kuidhinisha sera husika pekee. Mara baada ya kuundwa kwa baraza la vijana jukumu la kurejea sera ya vijana nchini libaki kwa baraza hilo kama ilivyo katika nchi mbalimbali.

Haikuwa shabaha ya makala haya kuibua fursa chache zilizomo katika sera ya sasa labda makala mengine.Lakini yatosha kusema kwamba pamoja na mapungufu ya kisera tuliyoyaona kama wadau mbalimbali wangetimiza wajibu wao kama ilivyoainishwa kwenye sera hiyo 'vijana wangekuwa vijana'! Sera hii ni kielelezo cha nia-siasa ya kiserekali yakuboresha mustakabali wa vijana nchini.

Hiyo ndio sera yetu ya vijana nchini na mchakato unavyoendelea sasa. Sera siri, mchakato mkato!! Zamu yako kutoa hoja.


 
lf.curl lf.curl2 rt.curl2 rt.curl