lf.bevel
MWANZO CHAMA SERA KATIBA TUUNGE MKONO UCHAGUZI TUWASILIANE

Makamba huu ni Undumilakuwili

Imeandikwa John J. Mnyika, Mkurugenzi wa Vijana wa CHADEMA

Mhariri, hivi karibuni Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Luteni Yusuph Makamba, ametoa kauli iliyoripotiwa na vyombo mbalimbali vya habari kwamba wanasiasa wanaodai takrima ni rushwa ni wanafiki. Bw Makamba amesema wanasiasa hao ni wanafiki kwa kuwa hata vitabu vya dini vinaeleza bayana kuwa, takrima si rushwa. Alitoa kauli hiyo wakati wa harambee ya kuchangia Shule ya Sekondari ya Charis iliyopo wilayani Tarime.

Nilikuwa mmoja wa wanasiasa tuliompongeza kwa dhati Makamba kwa kuzindua kitabu alichokindika cha kupiga vita rushwa kwa kutumia mafundisho na mausia ya dini.

Kama mmoja wa wanasiasa ambao tumekuwa tukisisitiza kwamba takrima ni rushwa ningependa kusema kwamba nimekerwa na kauli ya Mheshimiwa Makamba ambayo ni ya kinafiki na inadhihirisha undumilakuwili wa wanasiasa.

Quran tukufu inaruhusu takrima pale ambapo inatolewa na mwenyeji kumkirimu mgeni wake. Hata Mtume S.A.W alikirimiwa mara nyingi na wampendao. Hii ndio tasfiri sahihi ya takrima kwa mujibu pia wa kamusi ya Kiswahili na utamaduni wa Mwafrika. Lakini hii sio takrima wanasiasa tunayoizungumzia inayofanywa na wanasiasa walaghai kipindi cha uchaguzi.

Napenda kuchukua fursa hii kusisitiza tena kwamba takrima wakati wa uchaguzi ni rushwa yenye kulenga kuwaghilibu wapiga kura. Inachefua kwamba badala ya takrima (kwa maana ya kamusi) kutolewa na mwenyeji tunachokiona kwenye chaguzi ni wageni (wagombea na maswahiba wao) ndio wako mstari wa mbele kutoa takrima kwa wenyeji (wapiga kura). Hii kwa tafsiri yoyote ile ni rushwa-kupata kisichokustahili kwa namna isiyostahili.

Quran Tukufu Surah ya pili Al-Baqarah aya 188 inasema usile kwa mali ya mwingine bila ya haki wala usitoe hongo kwa mtawala. Nayo Biblia Tukufu inatamka "Nawe usipokee rushwa, kwani hiyo rushwa huwapofusha macho hao waonao, na kuyapotoa maneno ya wenye haki (Kut:23:8). Si wanasiasa tu, hata viongozi wetu wa dini wameibuka kwa wingi na kutahadharisha kwamba takrima wakati wa uchaguzi ni rushwa. Kama wanasiasa wanaosema hivi ni wanafiki basi Makamba anasema viongozi wa dini nao ni wanafiki. Huku ni kukosa nidhamu kwa viongozi wetu wa dini hivyo ni vyema Makamba akaomba radhi.

Hayati Edward Moringe Sokoine alituasa kwamba "ni uongozi mbovu au duni unaoogopa kuamua au kutekeleza mambo yaliyokwisha kuamuliwa". CCM, chama cha kina Makamba, kilishaamua katika chaguzi zake za ndani kwamba takrima ni mwiko-Makamba kuipigia upatu nje ni unafiki!


 
lf.curl lf.curl2 rt.curl2 rt.curl