lf.bevel
MWANZO CHAMA SERA KATIBA TUUNGE MKONO UCHAGUZI TUWASILIANE
banner

6 Juni 2007

Wapinzani tafuteni kwanza itikadi na falsafa inayofanana

na
Kitila A. K. Mkumbo

KATIKA makala yangu ya Mei 23, mwaka 2005, nilianza kujadili hatua muhimu ambazo naamini upinzani unapaswa kuzipitia katika kuleta mabadiliko kwa maana ya kuing’oa CCM madarakani.

Nilihitimisha makala hiyo kwa hoja kwamba, hatua ya kwanza kabisa ni kwa upinzani kuonyesha kuwa wao ni njia salama kwa safari yetu ya kupambana na maadui umaskini, maradhi na ujinga kuliko CCM.

Leo naendelea kwa kujadili umuhimu wa kujipambanua kiitikadi, kifalsafa na kisera.

Ninaamini itikadi na falsafa ni nguzo muhimu katika shughuli za kisiasa na ndizo zinatofautisha chama cha siasa na taasisi zingine katika jamii kama vile asasi zisizo za kiserikali (AZISE).

Chama cha siasa kisichokuwa na itikadi na falsafa inazokiongoza, ni sawa na AZISE na kinakosa sifa muhimu katika kufanya kazi ya siasa.

Katika kujipambanua kiitikadi na kifalsafa, ni muhimu kwa upinzani kuchukua hatua ya kuwaelimisha wananchi wa kawaida ukweli kwamba kuna itikadi mbalimbali za kisiasa na pengine bora zaidi kuliko itikadi ya ujamaa na kujitegemea.

Hii ni hatua muhimu kwa sababu tangu nchi yetu ipate uhuru mwaka 1961, wananchi walio wengi hawajawahi kupata nafasi ya kujua uzuri wa itikadi zingine za kisiasa zaidi ya ile ya ujamaa na kujitegemea.

Hatua ya kujipambanua kiitikadi na kifalsafa kwa upinzani, haitakuwa rahisi kwa sababu ni hatua ambayo itakumbana na vikwazo vya baadhi ya wasomi wetu, na hasa wale wanaoitwa kuwa wamebobea katika mambo ya siasa.

Ugumu wa kujitambulisha kwa itikadi kando ya ujamaa, unatokana na ukweli kwamba, wasomi wetu wengi ni waathirika wa mfumo wetu dhaifu wa elimu na elimu ya siasa za Kivukoni.

Wasomi wengi wa Tanzania wamepitia katika mfumo wa elimu ambao ni elekezi, usiotoa nafasi ya kujitegemea kifikra.

Hawa ni watu walifundishwa na kuzoeshwa kufikiri njia moja na si nyingine, na hasa kufikiri vile wanavyofikiri viongozi waliopo madarakani.

Kwa hiyo, linapokuja swala la itikadi, wasomi wetu wengi walifundishwa kufikiri kwamba duniani kuna itikadi moja tu bora inayoitwa ujamaa.

Wale waliokwenda Kivukoni ndio kabisa wakapewa na mbinu za namna ya kuiuza itikadi ya ujamaa na namna ya kuziponda itikadi zingine kwa umahiri na mbwembwe za kila aina.

Lakini ukweli ni kwamba, kuna itikadi nyingi ambazo pengine ni bora na zimeleta mafanikio makubwa sehemu zingine duniani kuliko itikadi ya ujamaa.

Si rahisi kuainisha itikadi zote katika makala moja gazetini.

Kwa hiyo katika makala haya, najaribu kudodosa tu baadhi ya itikadi kwa lengo la kuonyesha kuwa kila itikadi ina mapungufu na mazuri yake.

Andrew Heywood ni mwanazuoni wa sayansi ya siasa katika nyanja ya itikadi za kisiasa (political ideologies).

Yeye amezigawa itikadi za kisiasa katika makundi makuu matatu.

Kundi la kwanza ni kundi la itikadi za mrengo wa kushoto na mrengo wa kati kushoto, zikijumuisha itikadi za ukomunisti, ujamaa na demokrasia jamii.

Kundi la pili ni la mrengo wa kulia wenye kujumuisha itikadi za uhafidhina (conservatism) na ufashisti (fascism) na kundi la tatu ni la mrengo wa kati lenye kubeba itikadi ya uliberali.

Nitazitolea ufafanuzi itikadi za ujamaa, demokrasia jamii, uliberali na uhafidhina, ambazo kwa kiasi kikubwa ndizo zinavuma duniani kwa sasa.

Msingi wa itikadi ya ujamaa ni usawa; itikadi hii inaongozwa na imani katika kumiliki njia kuu za uzalishaji, usambazaji na ugawaji kwa pamoja kwa lengo la kufikia jamii yenye haki na usawa.

Ili kufikia lengo hili, waumini wa itikadi hii wanaamini katika kuwa na serikali kubwa na yenye nguvu ambayo inadhibiti uzalishaji, usambazaji na ugawaji wa mali na huduma zote katika jamii.

Kwa asili yake, serikali inayofuata itikadi ya kijamaa hudhibiti uhuru wa mtu binafsi na ni vigumu kwa serikali za kijamaa kuepuka udikteta.

Ndiyo maana nchi nyingi zilizoamua kufuata mfumo wa kijamaa ziliishia kuwa na mfumo wa chama kimoja cha siasa kwa sababu hazikuwa tayari kukabiliana na ushindani wa kisiasa. Uhalisia wa dhana ya ujamaa uliyumba baada ya kusambaratika kwa taifa la Urusi.

Kuna nchi chache sana duniani ambazo bado zinafuata mfumo wa kijamaa zikiwemo Cuba, Korea ya Kaskazini na kwa kiasi fulani China.

Hapa nchini kwetu, Mwalimu Nyerere alijitahidi kujenga ujamaa katika misingi ya Kiafrika.

Hata hivyo, katika chama chake cha TANU na baadaye CCM, pengine ni yeye pekee na makomredi wenzake wachache waliokuwa wakiamini katika dhana ya ujamaa.

Kwa hiyo, kimsingi CCM ya kijamaa ilitelekezwa baada ya Mwalimu Nyerere kufariki.

Kilichobaki katika CCM baada ya Nyerere, ni mkusanyiko wa watu wanaohangaika kupata ushindi wa kishindo bila kuongozwa na itikadi na falsafa yeyote ya kisiasa wala malengo ya muda mrefu ya nchi.

Itikadi ya pili na inayofanana kidogo na ujamaa ni ya mrengo wa kati kushoto (centre left) inayojulikana kama demokrasia jamii (social democracy).

Dhana ya demokrasia jamii inafanana na dhana ya ujamaa kwa kuamini katika jamii iliyojengwa katika usawa.

Hata hivyo, waumini wa demokrasia jamii hawaamini katika serikali kumiliki kila kitu kwa nia ya kuleta usawa. Wana demokrasia jamii wanaamini katika uchumi mchanganyiko (mixed economy); kwamba kuna mambo serikali inapaswa kuyafanya na kuna mambo mengi sekta binafsi ndiyo inayostahili kuyafanya.

Kwa hiyo, itikadi ya demokrasia jamii imejengwa katika dhana inayojulikana kwa Kiingereza kama principled public-private partnership, yaani ushirikiano kati ya serikali na sekta binafsi katika uzalishaji, usambazaji na ugawaji wa mali na huduma za kijamii katika nchi.

Itikadi ya tatu ni uhafidhina (Conservatism). Hii ni itikadi iliyojengwa katika dhana ya ubepari ambao ni mfumo wa kiuchumi wa soko huria ambapo serikali haitarajiwi iingilie shughuli za kiuchumi.

Waumini wa itikadi hii hawaamini katika jamii iliyo sawa; wao wanaamini katika kutoa nafasi kwa kila mtu kujishughulisha katika kujitafutia mali kadiri awezavyo, madamu kufanya hivyo hakumdhuru mtu mwingine. Waumini wa itikadi ya uhafidhina wanaamini pia kwamba watu katika jamii hawawezi kufanana, kwa hiyo haiwezekani jamii ikawa na usawa au ukamilifu.

Itikadi ya nne ni ya uliberali. Neno uliberali (liberalism) limetokana na maneno mawili ya Kiingereza ya ‘liberal’ likiwa na maana ya ‘enye mtazamo usiojifunga’, na ‘liberate’ likiwa na maana ya ‘achia uhuru, komboa’. Waumini wa dhana ya uliberali wanaamini kwamba si kazi ya serikali kuamua namna gani watu waishi au watende madamu matendo yao hayaingilii uhuru wa watu wengine kutenda wanavyotaka.

Hata hivyo, ili kulinda uhuru na heshima ya kila binadamu katika jamii, waumini wa uliberali wanaamini katika sheria na utawala bora wakizingatia dhana ya John Locke kuwa “pasipo na sheria hakuna uhuru”.

Uliberali unafanana na demokrasia jamii katika umilikaji na uendesha wa uchumi, kwa kuamini katika dhana ya uchumi mchanganyiko (mixed economy) wenye kuratibiwa, lakini bila kuingiliwa na serikali.

Kwa hiyo, uliberali kama ilivyo demokrasia ya jamii haukumbatii uchumi hodhi kama ulivyo ujamaa wala uchumi wa soko huria kama ilivyo itikadi ya kihafidhina yenye kufuata misingi ya kibepari.

Baada ya ufafanuzi wa itikadi za kisiasa, turejee maandishi ya Prince Bagenda katika makala yake iliyochapwa katika gazeti hili toleo la Mei 9, 2007. Akielezea itikadi ya kiliberali pamoja na hoja zingine, Prince Bagenda anasema hivi: “Katika makala hii, moja kwa moja natangaza kutetea na kutangaza itikadi ya mrengo wa kati na sera za soko huria kama itikadi katika nchi maskini ni usaliti wa hali ya juu na unapaswa kupingwa waziwazi na wapenda maendeleo wowote, popote ulipo.”

Bagenda anaendelea kusema katika makala yake kuwa: “Hakuna wakati wowote ambapo itikadi ya kiliberali imekuwa ni itikadi ya ukombozi.”

Hakuna shaka kwamba kwa kiwango cha Tanzania, Prince Bagenda ni msomi aliyebobea katika uchambuzi wa mambo ya siasa.

Hata hivyo, kupitia makala yake hii, amedhihirisha kuathirika kwake na mfumo wetu wa elimu na siasa za Kivukoni.

Bagenda anaposema kuwa kutetea dhana ya uliberali ni usaliti, anataka watu wote wawe na mtazamo wa itikadi kama wake na tuichukie dhana ya uliberali kwa kuwa tu tunaishi katika nchi maskini.

Nimshauri Bagenda kuwa, ana haki ya kuamini anachokiamini, ikiwemo haki ya kutoipenda na hata kuichukia itikadi ya uliberali.

Lakini hana haki ya kulazimisha sisi wengine wote katika nchi hii tuuchukie uliberali kama yeye, na tena hana haki kabisa ya kuwaita wale wanaopenda na kutetea uliberali kuwa ni wanafiki.

Zaidi ya yote, Bagenda hana haki ya kupotosha maana na malengo ya dhana ya uliberali.

Ni wazi makala ya Prince Bagenda si tu kwamba ililenga kupotosha maana ya dhana ya uliberali, bali pia ilijengwa katika minajili ya usomi wa siasa za Kivukoni, zenye kulazimisha watu wote wawe na mtizamo mmoja katika kufikiri na kuona namna ya kutatua matatizo yanayoikabili jamii yetu.

Ushauri wangu kwa vyama vya upinzani ni kuwa na msimamo wa kiitikadi na kukataa kuyumbishwa na wasomi wa siasa za Kivukoni, wenye mtazamo wa Bagenda.

Kitu cha msingi ni kuhakikisha kuwa itikadi yoyote ambayo upinzani unaamua kuifuata, wanaifafanua vizuri kwa jamii kama dhana na kama falsafa na dira ya sera zao za maendeleo kwa nchi yetu.

Nashauri pia kuwa, wakati huu ambapo vyama vya CUF, CHADEMA, TLP na NCCR vipo katika harakati za kuungana, mazungumzo yao yajikite zaidi katika kutafuta na kukubaliana kuwa na itikadi na falsafa moja, ambayo ndiyo itakuwa dira ya sera zao.

Kama alivyowahi kuasa marehemu Kwame Nkrumah kuwa, utafuteni kwanza ufalme wa kisiasa na mambo mengine yatafuata, nami nawaasa wapinzani kuwa, tafuteni kwanza itikadi na falsafa inayofanana, mambo mengine yatajipa yenyewe.

 
lf.curl lf.curl2 rt.curl2 rt.curl