NITAENDELEA kukumbuka mambo mawili makubwa kuhusu Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2005.
Mosi, uchaguzi ule ulionyesha kwamba Watanzania walikuwa wamechoshwa na utawala wa Rais Benjamin Mkapa, na kwamba walikuwa wana hamu ya mabadiliko katika uongozi wa kisiasa wa nchi yetu.
Pili, uchaguzi ule ulionyesha pia kwamba Jakaya Mrisho Kikwete alikuwa anatosha. Kutosha kwa Kikwete kulithibitishwa na ukubwa wa ushindi wa kura alizopata katika uchaguzi huo.
Hakuna shaka kuwa ushindi wa Rais Kikwete ndani ya CCM na baadaye katika Uchaguzi Mkuu uliamsha matumaini mapya miongoni mwa Watanzania wa kada na jinsia zote.
Hata hivyo kuna kila dalili kuwa Kikwete aliyeanza urais wake kwa kuwapa watu matumaini makubwa atamaliza urais wake watu wakiwa wamekata tamaa na kunyong’onyea kuliko wakati mwingine wowote tangu nchi hii ipate uhuru.
Serikali ya Kikwete si tu kwamba inaelekea kushindwa kutekeleza ahadi zake, lakini pia inaelekea kushindwa hata kulinda yale mafanikio madogo yaliyopatikana wakati wa utawala wa Awamu ya Tatu wa Rais Mkapa.
Katika kipindi cha miezi 17 cha urais wa Kikwete, mfumuko wa bei umepanda, ukuaji wa uchumi umeshuka na thamani ya shilingi dhidi ya dola ya Marekani imezidi kuporomoka. Tukiachana na hivi vigezo vya kiuchumi, Watanzania walio wengi ni mashuhuda wa kuongezeka kwa ugumu wa maisha katika miezi 17 iliyopita.
Kama kawaida ya serikali ya CCM, huwa hawakosi sababu za kuhalalisha kushindwa kwao.
Wimbo maarufu sasa hivi wa kuhalalisha kushindwa kudhibiti mfumko wa bei na matatizo mengine ni ukame na mgawo wa umeme, kana kwamba nchi hii ndiyo imeanza leo kukabiliwa na matatizo haya.
Utawala wa Kikwete utatukumbusha kwa mara nyingine kuwa tatizo la nchi yetu si kukosa watu wenye uwezo wa kuongoza. Wale waliokuwa na imani kwamba matatizo ya nchi yetu hayatokani na CCM bali viongozi wabaya katika CCM na kwamba kwa kumchagua Kikwete nchi ilikuwa imepata mkombozi itabidi wafikiri upya.
Ukweli ni kwamba ni vigumu kwa mtu yeyote mwenye uwezo kufanikiwa kuleta mabadiliko katika nchi hii kwa kupitia CCM ya leo. Yote hii ni kwa sababu CCM ya leo haina ajenda ya muda mrefu kuhusu maendeleo ya Tanzania, CCM ya leo haina uwezo wa kufikiri zaidi ya kushinda uchaguzi mwingine. Hiki ni chama ambacho kimsingi kimeishiwa ‘steam’ na kinahitaji kupumzishwa haraka.
Kwa hiyo hamu yetu ya kupata mabadiliko ya kweli katika utawala wa nchi yetu haitakamilika kama tutaendelea kubadilisha sura za viongozi pekee huku tukiacha mfumo wa utawala ukibaki uleule.
Tulianza na Mwalimu Nyerere. Mafanikio ya uongozi wake hadi leo ni mfano wa kuigwa. Kipindi cha Ali Hassan Mwinyi na Benjamin Mkapa hawakufanikiwa sana kuleta mabadiliko ya uchumi, na sasa Jakaya Kikwete aliyebeba matarajio lukuki ya Watanzania kuondokana a umaskini.
Kinachohitajika sasa ni kuiweka CCM pembeni. Sababu ya kuiweka CCM pembeni tunayo. Sababu yenyewe ni ukweli kwamba Chama Cha Mapinduzi si tu kwamba kimeshindwa kupambana na vita ya kutokomeza ujinga, umaskini na maradhi, vita ambayo kilirithishwa na TANU, bali chenyewe kimebadilika kuwa sehemu na kiranja wa maadui hawa.
Hii inamaanisha kuwa hatua yoyote ya kujaribu kupambana na ujinga, maradhi na umaskini isiyohusisha kuindoa CCM madarakani imeshindwa kabla haijaanza.
Uwezo wa kuwashinda hawa maadui pamoja na CCM tunao. Uwezo wenyewe ni nguvu yetu ya kura wakati wa uchaguzi. Hata hivyo, ili kuweza kuing’oa CCM madarakani, tunahitaji jemadari wa kutuongoza.
Katika mfumo wetu wa siasa, hatuna jemadari mwingine isipokuwa vyama vya upinzani. Lakini vyama vya upinzani tutavikabidhi tu ujemadari wa kuongoza vita yetu dhidi ya ujinga, maradhi na umaskini pale vitakapoonyesha kuwa vyenyewe si sehemu ya adui, bali ni sehemu ya jawabu la matatizo yetu.
Vyama vya upinzani vinawajibika kuonyesha kuwa vyenyewe vikipewa nafasi ya kuongoza vitaweza kuihuisha na kuishinda vita iliyoanzishwa na TANU kwa kuwatokomeza hawa maadui watatu niliowataja.
Kwa maoni yangu, ili vyama vya upinzani vionekane kuwa ni sehemu ya jawabu na si sehemu ya adui na hatimaye viweze kuchagulika, vinahitaji kupitia hatua zifuatazo.
Hatua ya kwanza, wapinzani waonyeshe kuwa mbali ya kuwa waathirika, wao ni fursa.
Wataalamu wa saikolojia ya siasa (political psychologists) huvigawa vyama vya siasa katika makundi makuu manne. Kundi la kwanza ni la vyama vya siasa ambavyo vipo kisheria (de jure political parties) lakini havipo kihalisia.
Wataalamu hawa wa saikolojia ya siasa wanabainisha kuwa hivi ni vyama ambavyo ukiwauliza watu 100, si zaidi ya watu watano wanaoweza kuvitaja kwamba vipo.
Kwa kawaida hakuna mpiga kura ambaye hupenda kuvipigia kura vyama vilivyopo katika kundi hili kwa kujua kuwa kuvipigia vyama hivi ni sawa na kuipoteza hiyo kura. Bila shaka vyama vya namna hii tunavyo vingi katika nchi yetu.
Japokuwa kuna vyama zaidi ya 15 vilivyoandikishwa kisheria, ni wananchi wachache wanaoweza kuvitaja vyama zaidi ya vitano.
Kundi la pili ni vyama athirika. Hivi ni vile vyama ambavyo wapiga kura huviona kuwa ni sehemu ya kundi la watu wanaoonewa na kuathiriwa na mfumo wa utawala uliopo.
Hivi ni vile vyama ambavyo huvuta hisia na huruma ya wananchi. Kwa hiyo wananchi huhesabu vyama hivi kuwa ni sehemu ya waathirika, lakini si lazima wavione kuwa ni sehemu ya jawabu la matatizo yao!
Kundi la tatu ni vyama adui. Hivi ni vyama ambavyo kwa nje vinaonekana vina nia ya kupambana na matatizo yanayoikabili jamii. Lakini ukweli ni kwamba kwa ndani vyama hivi ni sehemu ya adui na pengine ndiye adui mwenyewe anayesababisha matatizo yanayoikabili jamii.
Hivi ni vyama ambavyo kwa kiasi kikubwa kuwapo kwake kunategemea nguvu ya dola na mali kuliko nguvu ya ushawishi katika umma.
Kundi la nne ni la vyama fursa. Hivi ni vyama ambavyo vinajipambanua kiitikadi, kifalsafa, kiuongozi na kimkakati kuwa ni vyama vyenye malengo thabiti ya kukabiliana na matatizo yanayoikabili jamii.
Kwa hivyo wananchi huviona vyama hivi kuwa ni fursa ya kutatua matatizo yao na hutumia nafasi ya uchaguzi kuvichagua ili vipate nafasi ya kutekeleza ajenda zao za kimaendeleo.
Kila mtu anaweza akavinyambulisha vyama vyetu vya siasa katika makundi hayo manne niliyoyataja hapo juu kwa kadiri uelewa na utashi wake unavyomtuma.
Kwa maoni yangu, vyama vyetu vya siasa tulivyo navyo vinaweza kuingia katika makundi matatu ya mwanzo. Wasiwasi wangu ni kwamba hatuna vyama vyenye kuingia katika kundi la nne.
Ni maoni yangu kwamba CCM ya leo imo katika kundi la tatu kwa maana kwamba chama hiki si sehemu ya majibu ya matatizo yetu, bali ni sehemu ya adui.
Mfano dhahiri unaothibitisha uadui wa CCM ni matumizi mabovu ya kodi zetu yanayofanywa na viongozi wa serikali ya CCM. Serikali ya CCM ipo tayari kufumbia macho upotevu wa shilingi bilioni 900, lakini wakati huohuo ikaona ugumu kuwalipia masomo wanafunzi wanaosoma vyuo vikuu kwa gharama isiyozidi shilingi bilioni 111.3!
Ni maoni yangu pia kwamba vyama vya upinzani vinaangukia katika kundi la pili, yaani waathirika. Vyama vya upinzani ninavyoviongelea hapa si zaidi ya vinne, ambavyo ni CUF, CHADEMA, TLP na NCCR-Mageuzi.
Vyama vingine vya upinzani vipo katika kundi la kwanza. Vyama hivi nilivyovitaja kwa kiasi kikubwa vimekwisha kufanikiwa kujitambulisha kama sehemu ya watu wanaoathriwa na utawala wa CCM, na hivyo vimefanikiwa kupata huruma ya wananchi walio wengi.
Hata hivyo vyama hivi havijafanikiwa kujitambulisha kama sehemu ya jawabu na fursa ya kutatua matatizo yaliyopo.
Hii ni kutokana na ukweli kwamba vyama vya upinzani havijawapa wananchi mbadala wa yale yanayofanywa na CCM. Viongozi wengi wa vyama vya upinzani bado wanalalamika badala ya kutueleza wanachotaka kufanya wakiwa madarakani.
Kwa mfano, katika mgogoro wa hivi karibuni wa wanafunzi wa vyuo vikuu, walichofanya wapinzani ni kuungana na wanafunzi kulalamika na kulaani maamuzi ya serikali.
Nilitarajia kwamba vyama vya upinzani vingekwenda mbali zaidi ya kulalamika na kulaani; vingetumia fursa ya mgomo huu kuwaeleza wananchi sera mbadala ya elimu ya juu.
Ili kuweza kuishinda CCM katika chaguzi za mbeleni, vyama vya upinzani lazima vipige hatua kutoka kuonekana kuwa ni vyama athirika au vyama hurumiwa kwenda katika hatua itakayovionyesha kuwa ni vyama fursa.
Ni muhimu kwa vyama vya upinzani kutambua kuwa wapiga kura walio wengi hawapendi kupigia kura mgombea anayeonekana kuwa ni mnyonge na anayehitaji huruma.
Wapiga kura hupenda kuchagua vyama na wagombea wanaoonekana wana nguvu za kukabiliana na matatizo yanayoikabili jamii.
Kwa maana nyingine, ingekuwa ni barabara, kila mtu anajua kwamba barabara ya CCM ni mbovu, ina mashimo na ni hatari kupita. Lakini je, kuna barabara mbadala ya kupita?
Vyama vya upinzani vinawajibika kuonyesha kwamba barabara yao ni salama zaidi kuliko ile ya CCM.