lf.bevel
MWANZO CHAMA SERA KATIBA TUUNGE MKONO UCHAGUZI TUWASILIANE

2 Mei 2007

Tutaendelea kuita koleo kijiko kikubwa hadi lini?

na
Kitila A. K. Mkumbo

KUNA tamaduni na imani zingine ifike mahala Watanzania tuziache. Imani kwamba mkubwa akikosea haambiwa amekosea ni imani mbovu na potofu. Kwamba mkubwa haambiwi ‘amechafua hewa’ bali shetani mbaya amepita, ni utamaduni uliopitwa na wakati.

Ukweli ni kwamba kila mtu ‘huchafua hewa’. Dawa ya kuepuka aibu ya kuambiwa na watoto ‘umechafua hewa’ ni ‘kutokuchafua hewa’ mbele yao. Vinginevyo, uwe tayari kukabiliana na aibu ya kuchekwa na kuzomewa.

Utamaduni wetu wa kutowaambia ukweli wakubwa zetu, ni mbaya kwa sababu unazaa ukondoo. Unaua udadisi. Unaleta uvivu wa kufikiri. Unaleta woga. Unazaa taifa la ‘ndio mzee’.

Kibaya zaidi, unazaa viongozi wasio makini, wenye kiburi na wababaishaji, maana wanajua hakuna atakayewauliza. Ni huu utamaduni wa ‘ndio mzee’ uliotufikisha kusaini mikataba ya ajabu na aibu ya IPTL, City Water, Richmond na mingine.

Ni utamaduni huu uliotufanya tubambikiziwe bei ya rada hata wajanja wakachota sh bilioni 12 sisi tukiwa tunawakodolea macho.

Watanzania ni mahodari wa kusema pembeni. Hata kama ni kazini, kiongozi akiitisha mkutano kujadili jambo ama watakaa kimya au watamsifia kwa kusema kila kitu kinakwenda vizuri. Lakini wakitoka nje ya kikao, wanakuwa wa kwanza kulalamika na wakati mwingine kukwamisha hata utakelezaji wa yale yaliyokubaliwa katika vikao.

Ni utamaduni huu wa ‘ndio mzee’ uliowafanya vijana wetu wa chuo kikuu washindwe kumkabili Rais Jakaya Kikwete walipokutana naye pale Diamond Jubilee mapema mwaka huu. Vijana wetu wa chuo kikuu wangekuwa wadadisi wa mambo, wangemkabili Rais Kikwete awaambie hiyo ahadi yake ya “matatizo yenu nimeyasikia, yatashughulikiwa” ingetekelezwa lini na kwa vipi. Badala yake, vijana wetu wakaendekeza ‘u-ndio mzee’.

Ndio maana wakati mwingine inakuwa vigumu hata kuwahurumia vijana wetu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kwa kufukuzwa chuoni baada ya kugoma. Kama wangeitumia vizuri nafasi ya kukutana na Rais Kikwete, pengine wasingelazimika kugoma na chuo kufungwa.

Wao badala ya kujiandaa kumkabili Rais Kikwete kwa hoja, wakajiandaa kwa kupiga pasi magwanda na kofia za CCM. Badala ya kuandaa risala ya kisomi, wakaandaa risala ya kumsifia Kikwete na CCM yake.

Naye kama kawaida yake, akawapa tabasamu zito kisha akawaahidi, “matatizo yenu nimeyasikia, yatashughulikiwa”; baada ya hapo akawagawia magwanda na kadi za CCM nao wakaitikia, kigumu Chama Cha Mapinduzi!

Lakini vijana hao hao baadaye walipokaa pembeni, wakaiita serikali ya Rais Kikwete “serikali ya kishikaji”. Yaani serikali waliyoishangilia miezi miwili iliyopita, ghafla imekuwa serikali ya “kishikaji”? Huo ndio ninaouita unafiki, umbea na ubabaishaji.

Habari kwamba serikali imeyapa magazeti ya Tanzania Daima na Mwana Halisi onyo kwa kutumia lugha ya matusi, ni juhudi zingine za Serikali ya CCM za kutaka kuzima moyo na ari ya udadisi iliyoanza kuibuka miongoni mwa baadhi ya Watanzania.

Bahati mbaya, serikali haikuwa bayana sana na sababu zake za kutoa hili onyo. Hata hivyo, ukisoma kwa makini taarifa ya serikali si vigumu kujua kuwa onyo lake lilisababishwa na mfululizo wa makala zinazoikosoa Serikali ya Rais Kikwete, ambazo zimekuwa zikichapwa katika magazeti haya mawili.

Katika taarifa yake, serikali imesema imeyapa onyo magazeti haya kwa sababu yamejijengea “tabia ya kuchapisha kauli za matusi”.

Serikali imesema katika taarifa yake kuwa, “haitavumilia hata kidogo tabia hii ya kuchapisha kauli za matusi dhidi ya viongozi na watendaji wakuu wa serikali, hususan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama”.

Bila shaka yeyote, ile taarifa ya serikali ilikuwa inarejea makala ya Freeman Mbowe katika moja ya tafakuri zake, inayotoka kila siku ya Jumatano. Katika waraka wake wa nne kwa Rais Kikwete, Mbowe pamoja na hoja zingine, alionyesha hofu yake kuwa, kuna hatari tuendako rais wetu akaanza kuonekana mwongo, na kwamba sifa ya uongo si nzuri kwa rais.

Kusema kweli alichofanya Mbowe ni kuita koleo, koleo badala ya kijiko kikubwa. Alichosema Mbowe ndiyo hicho wanachosema Watanzania kwenye mabaraza, vijiwe na nyama choma. Tofauti ya Mbowe na watu wengine ni kuwa, yeye amekuwa na ujasiri wa kuyasema mambo haya hadharani.

Maneno uongo na uzushi, si mapya katika lugha ya Kiswahili na wala maana yake haiwezi kuwa matusi kama anavyotaka Mpenda tuamini. Wala huhitaji kamusi ya Kiswahili kujua maana ya maneno haya. Kusema uongo maana yake ni kusema kitu ambacho si cha kweli. Kuzusha ni kusema kitu ambacho hakipo.

Walichotakiwa kufanya serikali, ni kumtoa wasiwasi Mbowe na Watanzania wengine kuwa, rais hajawahi kusema kitu ambacho si kweli na ambacho hakipo na wala hatarajii kufanya hivyo.

Kuyatisha magazeti haiondoi ukweli katika kile alichokisema Mbowe. Kwa kuwasaidia serikali niwakumbushe tu kuwa, rais amewahi kusema kitu ambacho si cha kweli (hakusema uongo!) si mara moja. Kwa mfano, mwaka jana kupitia mkutano wake na wazee wa Mwanza, pamoja na mambo mengine, aliitangazia dunia nzima kwamba wananchi wa Mwanza hawali mapanki. Lakini ukweli wa mambo ulivyokuwa wakati huo na ulivyo sasa ni kuwa, wananchi wa Mwanza wanakula mapanki ama kwa kupenda au kwa kulazimika kwa kuwa hawana uwezo wa kumudu bei ya minofu ya samaki.

Mfano wa pili. Mwezi Februari mwaka huu, rais akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, alisema kuwa shirika lililotuuzia rada kwa bei ya kitapeli la BAE Systems la Uingereza, linamilikiwa kwa asilimia 100 na Serikali ya Uingereza.

Rais alilisema hili alipokuwa anaeleza haja ya Serikali ya Uingereza kuilipa Tanzania kiasi cha ziada kilichozidi katika manunuzi ya rada. Kwa maneno yake mwenyewe, rais alisema kuwa: “Tutafungua madai rasmi, maana (BAE Systems) ni shirika la Serikali ya Uingereza asilimia 100 hana ubia na mtu. Ni shirika lao la silaha wenye kiasi kikubwa cha hisa ni serikali.”

Lakini ukweli wa mambo, kama ilivyokuja kuthibitishwa baadaye na ubalozi wa Uingereza jijini Dar es Salaam, ni kuwa BAE Systems haimilikiwi na Serikali ya Uingereza kwa asilimia 100.

Mfano wa tatu. Akizungumza na wanafunzi wa vyuo vikuu jijini Dar es Salaam mapema mwaka huu, rais alisema kuwa hakuna mwanafunzi atakayefukuzwa chuo kwa kushindwa kulipa asilimia 40 ya gharama za masomo vyuoni.

Lakini hadi niandikapo makala haya, sharti moja la wanafunzi waliogoma kuruhusiwa kurejea masomoni ni kulipa hiyo asilimia 40!

Sasa kwa mifano hii na mingine, serikali ilitaka Mbowe ambaye ni mwenyekiti wa chama cha upinzani asemeje? CCM waache uvivu. Wajibu hoja za Mbowe kwa hoja.

Tatizo la Serikali ya CCM ni kama baba fukara. Baba fukara siku akipata nafasi ya kununua nepi, anataka watoto na nyumba nzima wamsifu. Lakini sote tunajua kuwa, baba anayetaka sifa kwa kumnunulia mtoto wake nepi, ni uzumbukuku, maana kununua nepi ni wajibu wake wa kila siku.

Ajabu ya baba fukara ni kwamba, siku akishindwa kununua nepi hataki aulizwe, anakuwa mkali kwamba ni ukosefu wa adabu na ni matusi!

CCM walichekelea sana pale walipokuwa wanamwagiwa sifa na magazeti kila kukicha hadi Rais Kikwete akakerwa na hizo sifa. Sasa leo hii wanashindwa kununua nepi, hawataki kuulizwa, wanasema ni matusi!

Ni kweli kabisa ni aibu rais kuambiwa mwongo; lakini si kosa wala dhambi kama kweli hakusema kweli. Tunatambua na kuheshimu sana mamlaka na hadhi ya kikatiba ya rais kama taasisi, lakini hii haina maana kuwa tutakuwa vipofu wa kuyaona mabaya na mazuri ya yule atakayekuwa amekalia kiti cha taasisi hii. Dawa ya kuepuka adha ya kuambiwa mwongo ni kusema ukweli.

Kama kitu huna uhakika nacho, huna haja ya kukisema. Ikitokea umejikwaa ukasema jambo ambalo si la kweli au halipo, unajitutumua, unalisahihisha na kuomba msamaha. Huu ndio uungwana wa demokrasia ya vyama vingi.

Tunahitaji pia kuwashauri washauri wa Rais Kikwete kwamba, waache kuendekeza ukada. Wafanye kazi zao za kitaaluma kama walivyosomea. Kazi yao ni pamoja na kuhakikisha kuwa kila anachokisema rais wetu kina kila chembe ya ukweli.

Laiti wataalamu wetu wangekuwa wanamwambia rais wetu ukweli, Mbowe asingepata nguvu za kuandika yale aliyoyaandika, maana angekuwa hana ushahidi. Shida ya wataalamu wetu na wanasiasa waliopo katika Serikali ya CCM ni kuthamini zaidi ukada na kuwa watiifu zaidi kwa CCM kuliko taaluma zao.

Wataalamu wetu kwa kuendekeza ukada, wapo tayari kutetea yasiyowezekana kutetewa na kuhalalisha yasiyohalalishika. Inashangaza kuona, kwa mfano, profesa mzima anaithamini zaidi nafasi yake ya kisiasa aliyoipata kwa kampeni za mwezi mmoja kuliko uprofesa wake aliousomea kwa miaka nenda rudi!

Viongozi wetu wajue kuwa, katika karne ya leo hawawezi kuuficha udhaifu wao wa kifalsafa, kisera na kiutendaji kwa kuvitisha, kuvifungia na hata kuvifuta vyombo huru vya habari.

Kama hawaamini hili, wajifunze kutoka Zimbabwe. Rais Robert Mugabe wa Zimbabwe amevipiga marufuku vyombo vyote huru vya habari nchini mwake. Lakini ni katika kipindi hiki ambacho tumeweza kujua udhaifu wa kutisha wa Rais Mugabe kuliko kipindi kingine chochote.

Watanzania inabidi tujue kwamba, viongozi wetu hawawezi kujibadilisha wenyewe. Tukiendelea na nidhamu yetu ya woga ya kutowaambia viongozi wetu ukweli wanapokosea, hawawezi kujirekekisha. Viongozi pia wanaweza kukosea. Wakikosea tusisite kuwaambia bila visingizio. Tuanze kuita koleo, koleo na wala si kijiko kikubwa!

 
lf.curl lf.curl2 rt.curl2 rt.curl