lf.bevel
MWANZO CHAMA SERA KATIBA TUUNGE MKONO UCHAGUZI TUWASILIANE

25 Aprili 2007

Elimu kwetu ni mahitaji au matakwa?

na
Kitila A. K. Mkumbo

NI aibu kwamba Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kimefungwa kwa mara nyingine tena kwa sababu ya mgomo wa wanafunzi.

Sote tunalazimika kuendelea kutafakari sababu na namna ya kumaliza migomo ya wanafunzi katika vyuo vyetu.

Tukitafakari sababu za migomo hii, ni muhimu pia tujiulize swali; ‘hivi elimu kwetu ni mahitaji au matakwa?’

Kabla sijajaribu kujibu swali hili, kwanza nieleze maana ya dhana ya mahitaji na matakwa kama nitakavyoitumia katika makala haya.

Mahitaji ni mambo ambayo ni ya lazima kuwepo na bila kwayo, taifa haliwezi kuwa kamili.

Mahitaji hayawezi kutekelezwa na mtu mmoja mmoja, bali yanachangiwa na jamii nzima kupitia serikali.

Elimu, afya, barabara, maji na huduma zingine muhimu kama hizi, ni baadhi ya mahitaji muhimu ya kijamii.

Matakwa yanajumuisha mambo yote ambayo yawepo ama yasiwepo, hayawezi kutukwamisha kuendelea kuishi kama jamii na kama taifa.

Kwa mfano, mtu kutaka kumiliki gari lake binafsi inaweza ikawa ni muhimu kwake, lakini si lazima maana jamii yetu na kama taifa haliwezi kuathirika kwa watu kushindwa kumiliki magari binafsi.

Kwa hivyo, matakwa ni mambo ambayo yanaweza kuwa muhimu kwa mtu mmoja mmoja, lakini si ya lazima kwa jamii au taifa.

Kazi ya serikali si kutekeleza matakwa binafsi ya mtu mmoja mmoja, bali kuhakikisha mahitaji ya kijamii yanapatikana kwa wote.

Chanzo cha migomo isiyokwisha katika vyuo vyetu vikuu, ni pale serikali ilipoamua kuifanya elimu ya juu kuwa matakwa ya mtu binafsi badala ya mahitaji ya kijamii.

Sera ya uchangiaji wa gharama za elimu ya juu si sera ya CCM. Hii ni sera waliokopa kutoka Benki ya Dunia na Shirika la Fedha la Kimataifa.

Serikali ya CCM walikubali ushauri wa kijinga wa mashirka haya, kwamba si muhimu kwa nchi maskini kama Tanzania kuwekeza katika elimu ya juu.

Wakati mashirika haya yakitushauri sisi kuacha kuwekeza katika elimu ya juu, serikali za huko kwao zimejiwekea utaratibu wa kuhakikisha kuwa hakuna mtu anayeshindwa kusoma chuo kikuu kwa sababu ya kukosa pesa.

Ndio shida nyingine ya serikali yetu, ipo tayari kukubali kila takataka ya ushauri kutoka nje na kukataa kila busara ya ushauri wa wataalamu wake.

Wataalamu wetu walipinga sana uamuzi wa serikali wa kuacha kugharamia elimu ya juu, lakini serikali iliamua kubeba ushauri wa mashirika ya kimataifa.

Sasa kama alivyotuasa Mwalimu Nyerere, madamu CCM walikubali ushauri huu wa kijinga, ni wazi kuwa aliyemjinga hapa si haya mashirika!

Sasa tuyaangalie kwa undani kidogo matatizo yaliyosababisha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kufungwa.

Katika kutekeleza sera ya uchangiaji wa gharama za elimu ya juu, serikali kupitia Bunge letu, iliunda Bodi ya Mikopo, lengo lake likiwa kuwakopesha wanafunzi wanaochaguliwa kusoma katika vyuo vya elimu ya juu ili waweze kujiunga na kuendelea na masomo yao bila kikwazo cha kifedha.

Ilitarajiwa kwamba, serikali yetu kwa kuwa ina mkono mrefu, ingetengeneza utaratibu wa kuweza kutambua mahitaji ya kila anayeomba mkopo ili kila mwanafunzi apate mkopo kutokana na mahitaji yake. Hili limeshindikana hadi leo.

Ilitarajiwa pia kwamba serikali ingetengeneza utaratibu thabiti wa kuwawezesha wale wote waliopata hii mikopo wairudishe ili iweze kuwasaidia watu wengine. Hili nalo limeshindikana. Badala yake Serikali ya CCM imekuwa ikibadilisha taratibu za mikopo kila kukicha.

Kibaya zaidi ni kwamba mabadikiko yenyewe yanafanywa kwa njia ya matamko tena nje ya Bunge.

Tangu Serikali ya Kikwete iingie madarakani, imeshabadilisha taratibu za mikopo angalau mara tatu. Kwanza, mara baada ya Rais Kikwete kuunda baraza lake la mawaziri, Waziri wa Elimu ya Juu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Peter Msolla aliibuka na tamko lililotushangaza wengi; kwamba kuanzia mwaka wa masomo 2006/2007, serikali ingetoa mikopo kwa wanafunzi waliochaguliwa kusoma katika vyuo vya umma tu!

Hakuishia hapo, muda mfupi baadaye, Profesa Msolla akaibuka na tamko kwamba, watakaopata mikopo ni wale waliopata daraja la I (kwa wanaume) na la II (wanawake) katika mitihani ya kidato cha sita.

Uamuzi huu nao uliozomewa na kila mtu isipokuwa aliye kada wa CCM. Pengine tamko la ajabu kabisa kutolewa na utawala wa Rais Kikwete ni hili lililosababisha vijana wetu kugoma.

Serikali imeamua kwamba wazazi wa wanafunzi wanaosoma katika vyuo vikuu, watachangia asilimia 40 ya gharama zote za masomo.

Kuna watu wengi hawaelewi maana ya asilimia 40 ya gharama za chuo kikuu. Na kama kawaida ya Serikali ya CCM, wametoa tamko hili bila kufanya uchanganuzi halisi wa gharama zenyewe.

Kwa kutumia mfano wa gharama za kusoma katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (Mlimani), nitajaribu kudodosa hizi gharama kwa kifupi kabisa ili msomaji upate picha kamili na uweze kuamua kama Watanzania wanaweza kweli kulipia hiyo asilimia 40 ya gharama za elimu ya juu au la.

Kwa mujibu wa mwongozo (prospectus) wa Chuo Kikuu cha Dar cha Dar es Salaam kwa mwaka 2005/2006 (uk.37), kuna aina kuu sita za gharama za mwanafunzi wa shahada ya kwanza.

Gharama kubwa kabisa ni ada ambayo hutofautiana kufuatana na aina ya shahada.

Kwa mujibu wa mwongozo huu, ada ya chini kabisa ni ile inayotozwa katika vitivo vya elimu, sanaa na sayansi ya jamii na uhandisi ambayo ni sh 600,000 kwa mwaka.

Gharama zingine na mahesabu yake katika mabano ni chakula (472,500), vitabu (80,000/mwaka), maandikio (60,000/mwaka), matibabu (100,000/mwaka) na mazoezi kwa vitendo (6,000/siku).

Ukifanya mahesabu utaona kuwa gharama yote kwa mwaka bila kujumlisha gharama ya malazi kwa mwanafunzi anayesoma aina ya shahada zilizotajwa hapo juu ni sh 1,564,500.

Asilimia 40 ya gharama hii ni sh 625,800. Kwa hiyo gharama ya chini kabisa ambayo serikali inataka mzazi wa mwanafunzi anayesoma chuo kikuu achangie ni sh 625,800 kwa mwaka.

Kwa mujibu wa ripoti ya serikali ya hali ya umaskini na maendeleo ya watu ya mwaka 2005, kipato cha wastani kwa Mtanzania ni sh 9,900 katika siku 28 (mwezi).

Kwa kiwango hiki na kwa mujibu wa viwango vya kimataifa vya kupima umaskini, asilimia 57.5 ya Watanzania ni maskini wa kutupa. Hii inamaanisha kwamba, pato la wastani la Mtanzania kwa mwaka ni sh 118,800. Sasa tujiulize, serikali inaposema wazazi walipie asilimia 40 ya gharama za kusoma chuo kikuu (zaidi ya sh 625,800) inawalenga Watanzania gani?

Kwa takwimu hizi, zaidi ya asilimia 50 ya Watanzania hata kama wangeamua kuacha kula na kuvaa kwa mwaka mmoja, wasingeweza kumudu hata asilimia 10 ya gharama za kumsomesha mtoto wao mmoja katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Kuna madai yanayotolewa mara kwa mara na serikali kuwa, haina uwezo wa kuwalipia wanafunzi wote wanaojiunga na elimu ya juu nchini.

Bahati mbaya, viongozi wetu huwa hawatuelezi gharama zenyewe ni kiasi gani na uwezo wa serikali ni kiasi gani.

Nimejaribu pia kudodosa hili ili tupime kama kweli madai ya serikali ni ya kweli au inajaribu kukwepa majukumu yake.

Kwa mujibu wa hotuba ya Waziri wa Elimu ya Juu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Peter Msolla aliyoitoa katika mkutano wa Benki ya Dunia hivi karibuni, hadi kufikia Desemba 2006, Tanzania ilikuwa na jumla ya vyuo vikuu vya umma vipatavyo 11 na vyuo vikuu binafsi 19. Jumla kuna vyuo vikuu 30.

Idadi ya wanafunzi katika vyuo vikuu vya umma ilikuwa 35,821 na katika vyuo vikuu binafsi ilikuwa 5,275. Jumla ya wanafunzi katika vyuo vikuu vya umma na binafsi ilikuwa 41,096.

Kwa mujibu wa taarifa ya Profesa Msolla aliyoitoa bungeni katika kikao kilichomalizika hivi karibuni, Bodi ya Mikopo ilikuwa inahitaji sh bilioni 140 kwa ajili ya mikopo ya wanafunzi.

Hata hivyo, ilipatiwa sh bilioni 63.5 na baadaye wakaongezewa sh bilioni 47.8. Hii inamaanisha Bodi ya Mikopo ilipatiwa jumla ya sh bilioni 111.3 kwa ajili ya kutoa mikopo kwa wanafunzi kwa asilimia 100.

Kwa hivyo, kwa hesabu ya idadi ya wanafunzi iliyotajwa hapo juu, na kama serikali ingeamua kukopesha wanafunzi wote walio katika vyuo vya umma na binafsi, kila mwanafunzi alistahili kupata sh 2,708,292.78, kiasi ambacho ni kikubwa kuliko kiwango cha chini cha kusoma katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ambacho ni sh 1,564,500.

Kwa mahesabu ya hapo juu, mambo manne ni bayana. Mosi, kwa hali ya umaskini tuliyo nayo, wazazi wengi wa Kitanzania hawawezi kumudu gharama za watoto wao kusoma chuo kikuu.

Pili, serikali ina uwezo wa kulipia gharama za elimu ya juu kupitia Bodi ya Mikopo bila kutetereka.

Tatu, serikali iliipa Bodi ya Mikopo pesa za kuwapatia wanafunzi mikopo na kubakiwa na akiba ya kutosha.

Nne, kuna uwezekano mkubwa kuwa pesa za mikopo kwa ajili ya wanafunzi zinatumika vibaya kiasi kwamba haziwafikii walengwa.

Serikali bado ina nafasi ya kuboresha utoaji wa mikopo kwa ajili ya wanafunzi wa elimu ya juu.

Mimi nashauri mambo matano muhimu ya kuzingatia. Kwanza, pamoja na umaskini wetu, wapo wenzetu japokuwa ni wachache wenye uwezo wa kuwalipia watoto wao elimu ya chuo kikuu hata kwa zaidi ya asilimia 100.

Hivyo serikali ifanye uchambuzi kwa kutumia ripoti zake za hali ya umaskini nchini kuainisha wale wenye uwezo.

Pili, serikali itengeneze haraka utaratibu wa kisheria na endelevu wa kuwawezesha wale waliokopa pesa za kusoma chuo kikuu waanze kurudisha.

Tatu, Bodi ya Mikopo iimarishwe na ijitegemee. Ni aibu kusikia kwamba bodi imewahi kugawa pesa hata kwa baadhi ya wanafunzi waliokwisha kumaliza chuo.

Nne, serikali ianzishe udhamini ili kuweza kutambua na kuendeleza vipaji miongoni mwa vijana wenye uwezo maalumu, hasa katika nyanja ya sayansi na teknolojia.

Tano, serikali ianzishe kodi ya hiari ili kujenga moyo wa kujitolea miongoni mwa jamii. Hii kodi ya hiari itumike kukuza mfuko wa elimu ya juu.

Wenye kulipa kodi ya hiari ndio wawe wanapata msamaha wa kodi. Ujumbe wangu ni kuwa, elimu ya juu ni mahitaji ya kijamii na wala si matakwa ya mtu mmoja mmoja, lazima sote tuigharamie kama jamii na kama taifa.

Lazima tuendelee kuikemea Serikali ya Kikwete kwa tabia yake ya kutumia pato dogo la taifa kutekeleza matakwa binafsi ya viongozi badala ya mahitaji muhimu ya taifa kama elimu ya juu.

Tuendelee kumkumbusha Kikwete kuwa, kuendelea kuwa na mawaziri lukuki, kununua magari ya kifahari na safari zake lundo nje ya nchi, ni matakwa yake binafsi na si mahitaji ya taifa letu.

Nimalizie makala yangu kwa kuwashangaa viongozi wa vyama vya CUF, TLP na NCCR. Wiki iliyopita walikaririwa pamoja na mambo mengine, wakimtaka Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Rwekaza Mkandala ajiuzulu kwa kufunga chuo.

Huu ni mwendelezo wa wanasiasa wetu wa kutaka kupata umaarufu kwa bei rahisi na ni ukurupukaji wa kisiasa.

Wasichoelewa viongozi wa vyama hivi ni kwamba, matatizo yanayoikabili sekta ya elimu nchini ni makubwa na magumu kuliko yanavyoonekana, wala suluhu yake haiwezi kuwa majibu rahisi ya kuwataka viongozi wa chuo wajiuzulu.

Wao walipaswa kutupatia mbadala wa sera ya elimu ya juu dhidi ya hii ya CCM iliyoshindwa.

Wasichokielewa pia viongozi hawa ni kuwa, hata kama Makamu Mkuu wa Chuo cha Dar es Salaam angekuwa na makosa ya kumfanya ajiuzulu, wao hawawezi kuwa wadau wa kwanza wenye uhalali unaoshikika wa kumtaka ajiuzulu.

Kama walivyosema wanafunzi wenyewe, tatizo hapa si Profesa Mkandala, “tatizo ni hii serikali ya kishikaji ya Kikwete.”

 
lf.curl lf.curl2 rt.curl2 rt.curl