WANASIASA wengi waliofanya mambo makubwa duniani, walianza kwa kuota ndoto. Kwa mfano, Martin Luther King Jr. aliwahi kuota kuwa siku moja watu weusi nchini Marekani watakuwa na haki sawa za kiraia na wataishi sambamba na raia wengine wenye ngozi nyeupe (rejea hotuba yake maarufu ya “I have a dream”).
Hakuishia kuota tu. Akachukua hatua ya kuanzisha harakati katika kutekeleza ndoto zake hizo. Japokuwa alifariki kabla weusi hawajapata haki kamili, lakini sote tunatambua mchango wa Martin Luther King Jr. katika kuwafikisha watu weusi hapo walipo sasa nchini Marekani.
Nelson Mandela naye aliwahi kuota kuwa siku moja ubaguzi wa rangi utaisha na kwamba watu wote wataishi kama binadamu walio na haki sawa nchini Afrika Kusini. Zaidi ya yote, Mandela aliota kuwa serikali ya kibaguzi ya Afrika Kusini itakuja kushindwa, tena kwa njia za kidemokrasia.
Mandela akaendesha harakati za miaka mingi kufikia hiyo ndoto yake. Yaliyobaki ni historia.
Wapo pia viongozi waliota ndoto zikabaki kuwa ndoto. Kwa mfano, Kwame Nkrumah aliwahi kuota kuwa nchi za Afrika zitaungana na kuwa nchi moja. Hata hivyo sote tunajua kuwa hii imebaki kuwa ndoto hadi unaposoma makala haya.
Leo najadili ndoto za Rais wetu Jakaya Kikwete za kuleta maisha bora kwa kila Mtanzania. Hata hivyo lazima nikiri mapema kabisa kuwa, sina uhakika juu ya ndoto ya rais wetu. Sina uhakika kama Kikwete aliota kuwa Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania au kumpatia kila Mtanzania maisha bora.
Kama Kikwete alikuwa na ndoto ya kuwa rais, ni wazi kuwa ndoto yake hii ilikwisha kutimia kwa kuchaguliwa kuwa rais, tena kwa kura za kishindo zilizompa ushindi wa asilimia 80.
Lakini kama Kikwete aliota kuwapatia Watanzania maisha bora na kwamba angeutumia urais kama nyenzo ya kutimiza ndoto yake hii, basi inabidi ajipange upya. Bila kujipanga upya ni wazi kuwa Kikwete hatoweza kuitekeleza ndoto yake. Hii ni kwa sababu miezi 15 baada ya kuchaguliwa kuwa rais, bado hakuna dalili zozote za maana, si tu za Watanzania kuanza kuona hayo maisha bora, bali hata jitihada zenyewe za kuelekea huko.
Wasiwasi wa kushindwa kwa Kikwete kutekeleza ndoto yake ya kumpatia kila Mtanzania maisha bora, umeonyeshwa pia na jarida maarufu duniani la The Economist.
Katika toleo lake la Machi 22, jarida la The Economist limesema lisiloweza kusemwa katika Tanzania ya sasa. Kwamba Serikali ya Rais Kikwete inaelekea kushindwa kutekeleza ahadi alizozitoa katika kampeni za uchaguzi.
Pengine sasa kina Kikwete na timu yake watasikia. Tuwashukuru gazeti la Tanzania Daima kwa kudodosa hatua kwa hatua yaliyoandikwa katika jarida la The Economics kwa Kiswahili, maana Watanzania wengi wakiwemo akina Makamba watakuwa wameisoma.
Lilichosema hili jarida ndicho kilekile ambacho Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe, amekuwa akikisema katika moja ya tafakuri zake. Mbowe amesema mara nyingi kuwa “nchi haiendi, Kikwete amekwama.”
Hata hivyo, nani angemsikia Mbowe wakati yeye ni mpinzani? Kwa tafsiri ya CCM, maneno ya Mbowe ni wivu, tena wa kijinga! Sitashangaa CCM wakikurupuka kulisuta hili jarida maana wao siku zote hutanguliza ukada mbele kuliko ukweli.
Tena CCM wasivyo na aibu wanaweza hata kuliambia hili jarida pilipili usizozila zakuwashiani. Lakini niwakumbushe CCM kuwa, ni jarida hili pia lililosifu mipango ya Kikwete ya kupambana na umaskini takribani miezi minne baada ya kuingia madarakani.
Walichofanya hili jarida ni kupima utekelezaji wa ile mipango iliyotolewa kwa mbwembwe. Hili jarida limegundua kuwa, ile mipango ni ‘hot air’. Ndiyo yale yale niliyosema katika makala yangu ya wiki jana kuwa, anachosema Kikwete sicho akifanyacho.
Sina haja ya kuthibitisha yale waliyoyasema jarida la The Economist. Lilodhahiri ni kuwa, Kikwete anaelekea kukwama kutekeleza ndoto yake ya kuwapatia Watanzania maisha bora.
Cha kujadili sasa ni kwa nini Kikwete anakwama na afanye nini katika kujikwamua? Hili hasa ndio lengo la makala yangu ya leo.
Tatizo la kwanza linalomkabili Kikwete ni ubovu wa gari analoendesha. Inawezekana Kikwete ni dereva hodari, hasa tukizingatia uzoefu alionao katika uongozi wa siasa, maana alishika karibu kila ngazi ya uongozi wa siasa kabla hajawa rais, kuanzia ukatibu wa wilaya hadi uwaziri uandamizi.
Lakini gari analoendesha Kikwete ni gari lililoharibika kwa kiwango ambacho haliwezi kukarabatika. Ni wazi CCM kama chama cha siasa, hakikujiandaa kukabiliana na siasa za ushindani kisera.
CCM ilizoea kutungiwa sera na Mwalimu Nyerere. Kila sera ya kuliongoza taifa hili kabla ya mfumo wa vyama vingi, ilibuniwa na kuasisiwa na Mwalimu Nyerere. Baada ya Nyerere kuachia uongozi na baadaye kufariki, CCM iliachwa mufilisi kiitikadi, kifalsafa na kisera.
Viongozi waliobaki CCM baada ya Nyerere, kazi yao kubwa imebaki kubuni mikakati ya namna ya kukibakisha hiki chama madarakani. Bahati mbaya mikakati yenyewe si ya kisera.
Ni mikakati ya usiku, ghiliba, uhuni na mazingaombwe ya kuwapofusha wapiga kura. Inasikitisha kuona kuwa, badala ya CCM ya leo kuwatumia wazee waliobaki katika chama hiki kuwa ni chemchemi ya busara ya kuibuka na sera zenye mvuto, inawatumia wazee hawa kama matingatinga ya kupanga mikakati ya kuwashinda wapinzani kwa kampeni za usiku na za kihuni za kitanda kwa kitanda, shuka kwa shuka.
Haishangazi basi falsafa na sera ya maana ya mwisho iliyowahi kutolewa na CCM ni Azimio la Arusha. Baada ya Azimio la Arusha, CCM haikuwahi kuibuka na sera ya maana ya kuikomboa nchi hii. Siasa ya ujamaa na kujitegemea imebaki kuwa wimbo wa kuwaridhisha wazee wachache katika chama hiki ambao bado wanapenda siasa ya ujamaa ili wasife na ugonjwa wa moyo.
Baada ya kushindwa kutekeleza Azimio la Arusha na siasa ya ujamaa na kujitegemea, CCM wamebaki na wimbo mmoja tu, amani na utulivu, kama hii nayo ni sera. Inabidi tuendelee kuwaelimisha CCM kuwa hii si sera wala itikadi. Amani na utulivu ni mazingira ya kutekeleza sera. Kama huna itikadi na sera, mazingira mazuri peke yake hayawezi kuleta maendeleo.
Ilitarajiwa kuwa Kikwete angetumia kukubalika kwake ndani na nje ya CCM kukisaidia chama chake kuibuka na falsafa na sera za maana na kwamba ingekuwa mwisho wa uhuni wa kampeni za kitanda kwa kitanda katika CCM. Lakini wapi. Wadadisi wa mambo wanasema hata ilani ya uchaguzi hakushiriki kuitunga! Ilani yenyewe ya CCM aliyobebeshwa kuihubiri ikajazwa shughuli za kufanya badala ya sera.
Kazi ya chama cha siasa si kuorodhesha shughuli za kufanya. Chama cha siasa ni itikadi, falsafa na sera, mambo ambayo CCM haina. Na wala kazi ya rais haiwezi kuwa kusimamia shughuli za kila siku kama kugawa viwanja kwa wamachinga, maana kuna watendaji chungu nzima wa kufanya hizo shughuli.
Haishangazi kwamba Kikwete ilibidi akatae kwenda kwenye mdahalo maana kule ilikuwa zijadiliwe sera na wala si shughuli za kufanya. Kwa hivyo CCM kama chama cha siasa kilikwisha kufa! Ndio maana nimesema Kikwete anaendesha gari bovu lisiloweza kutengenezeka.
Haijalishi yeye ni dereva bora kiasi, madamu amechagua kuendesha gari lililokufa, kamwe hatatufikisha kule alikoahidi kutupeleka.
Hata hivyo, Kikwete bado ana nafasi ya kutekeleza ndoto yake kama akijipanga upya. Inabidi afanye mambo kadhaa. Kwanza, akiri ama kimya kimya au waziwazi kuwa ilani ya uchaguzi ya CCM haina kitu.
Yeye hatokuwa rais wa kwanza kufanya hivi. Rais wa sasa wa Malawi, Bingu wa Mutharika, muda mfupi baada ya kuchaguliwa aligundua kuwa chama chake kilikuwa kinamkwamisha kutekeleza ajenda alizokuwa nazo, ikiwemo ya kupambana na rushwa. Akaachana nacho na akaanzisha chama chake kingine. Najua mazingira ya kisheria ya Malawi na ya kwetu yanatofautiana, lakini naonyesha tu kuwa inawezekana kwa Kikwete kujipanga upya bila kuitegemea CCM.
Hapa nyumbani pia Mkapa aliikana CCM muda mfupi tu baada ya kuchaguliwa. Alikiri mbele ya kadamnasi kuwa Ilani ya Uchaguzi ya CCM haitekelezeki! Kisha akatangaza upya kipaumbele cha serikali yake, pale alipohutubia wana jumuiya wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Februari 6 mwaka 1999.
Naikumbuka sana hii tarehe kwa sababu ni siku nilipopata bahati ya kuwa miongoni wa wajumbe walioratibu ziara ya Rais Mkapa, nikiwa Rais wa DARUSO, na ndio ilikuwa siku ya mwisho ya muhula wangu wa kuwa Rais wa Serikali ya Wanafunzi pale Mlimani.
Akitangaza kipaumbele cha serikali yake, Mkapa alisema angependa akumbukwe kwa jambo moja alilolisisitiza mara tatu kwa Kiingereza, economy, economy, economy! Pengine ni kweli kwamba tunamkumbuka zaidi Mkapa kwa kukuza uchumi, japokuwa ni kweli pia kuwa tunamkumbuka kwa kupenda matumizi ya anasa na kwamba ni rais ambaye hakupenda kusikia sauti nyingine isipokuwa sauti yake mwenyewe.
Kwa hiyo, Kikwete hana budi kuchagua kipaumbele chake sasa maana kwa wingi wa matatizo ambayo CCM imeshindwa kuyatatua kwa miaka nenda rudi, hatoweza kufanya kila kitu kwa miaka mitano ya uongozi wake.
Rais Kikwete afike mahala atambue kuwa ‘ari mpya, kasi mpya na nguvu mpya’ si sera wala ajenda. Nalisema hili kwa sababu imetokea kila mtu katika serikali yake anaimba kama kasuku hii kauli.
Nakumbuka nilihudhuria semina moja iliyoandaliwa na Kituo cha Uwekezaji kwa ajili ya Watanzania waishio Uingereza. Mwakilisha mada kutoka kituo hiki naye alianza kwa kuimba wimbo huohuo kama kasuku, “sasa hivi tunavutia wawekezaji kwa kasi mpya, ari mpya na nguvu mpya!”
Nilikutana pia na rafiki yangu ambaye ni mkuu wa wilaya moja hapa nchini, akitokea kwenye semina ya uongozi ya Ngurdoto. Katika kumdodosa walichofundishwa huko, ananiambia tena kwa uchangamfu kabisa; “kilichosisitizwa zaidi ni kufanya kazi kwa kasi mpya, ari mpya na nguvu mpya!”
Balozi wetu Uingereza naye kila tukikutana katika vikao vya Watanzania hasiti kutukumbusha; “jamani tushirikiane, hii ni awamu ya ari mpya, kasi mpya na nguvu mpya!” Yaani hii ari mpya ndio imekuwa ile kauli ya ‘uhuru na kazi’ enzi za TANU!
Akishakuchagua ajenda ya kufanya, itabidi Kikwete awe jasiri wa kuisimamia kikamilifu na akumbuke kuwa haiwezekani akamfurahisha kila mmoja ndani na nje ya serikali yake.
Na hatua ya kwanza ya ujasiri ni kuwaambia marafiki zake ukweli katika nyanja mbili. Mosi, kuwa pamoja na utamu wa safari za nje, basi zinatosha. Pili, awe na ujasiri pia wa kuwaambia ukweli marafiki zake katika baraza lake la mawaziri kuwa, mzigo aliobeba haubebeki kama wanataka kutekeleza yale waliyoyaota kwa ajili ya Tanzania.
Hivyo itabidi apunguze ukubwa wa baraza lake la mawaziri. Itakuwa ni vigumu kwa Kikwete kuwekeza pesa katika kuwahudumia wananchi huku akibeba mzigo mkubwa wa kuendesha serikali yake.
Duniani kote, mwelekeo sasa hivi ni kuwa na serikali ndogo. Sijui rais anapata raha gani kuwa na mawaziri 60, idadi ambayo ni kubwa kuliko idadi ya wakuu wa mikoa na makatibu tawala wa mikoa ikijumuishwa!
Kikwete lazima aamue, kubeba mzigo wa kuwahudumia wananchi au kuhudumia serikali yake!
Sisi jamii pia tuna wajibu wa kumsaidia Rais Kikwete. Kwanza, wasomi wetu inabidi watusaidie kumwambia rais na jamii ukweli wa mambo. Inasikitisha kwamba kipindi hiki ambacho ndio tuna idadi kubwa ya maprofesa katika nchi yetu, ndio kipindi hikihiki ambacho hatusikii hawa maprofesa wakisema chochote.
Baada ya akina Issa Shivji, Haroub Othman na Baregu kustaafu na Chachage kufariki, wasomi wetu wengine wako wapi? Mimi naamini Afrika na nchi yetu sasa hivi inahitaji zaidi sasa, kuliko kipindi kingine chochote, wasomi wa jamii (public intellectuals) badala ya wasomi wa madarasani pekee.
Kama wasomi wa Afrika hawawezi kuwanyooshea vidole viongozi wetu, nani afanye hivyo? Naamini silaha kubwa ya msomi ni kuona na kusema ukweli wote madamu ni ukweli.
Kwa nini wasomi wetu siku hizi wanachagua ukweli wa kusema? Tena wanachagua kusema ukweli unaowafurahisha wanasiasa waliopo madarakani tu? Kwa nini tusibiri The Economist ndio wamwambie Kikwete kuwa mambo hayaendi, wasomi wetu wako wapi?
Mwisho ni sisi wananchi. Inabidi tutambue kuwa kubadilisha dereva peke yake haitasaidia kuikamilisha safari yetu ya kutafuta maendeleo. Inawezekana ni kweli tunampenda sana dereva Kikwete, lakini ukweli ni kwamba dereva huyu anaendesha gari (CCM) lililokwisha kufa. Gari ni injini. Bodi peke yake hata kama inavutia kiasi gani bila injini haina maana.
Tukipata nafasi nyingine ya kubadilisha uongozi wa nchi yetu, tusibadilishe dereva pekee, tubadilishe na gari pia.