KUNA kanuni kuu tatu katika ufundishaji, ambazo kila mwalimu mwenye kufuata kanuni za ualimu huzifuata pindi anapoingia darasani kufundisha.
Kwanza, mwalimu atawaambia wanafunzi wake kile ambacho anataka kuwaambia katika siku hiyo. Pili, atawaambia kile ambacho alisema atawaambia. Tatu, anapomaliza kufundisha somo, atawaambia tena wanafunzi wake kile alichowaambia.
Kwa wanasiasa walio waadilifu, kuna kanuni tatu pia. Kwanza, mwanasiasa atawaambia wananchi wake kile ambacho amepanga kufanya na kwa nini anafikiri ni muhimu kufanya hicho kitu. Pili, atafanya kile alichowaambia wananchi wake kwamba atakifanya. Tatu, akishakukifanya, atawaambia kwamba amefanya kile alichofanya na kuonyesha mazao au matunda ya yale aliyoyafanya.
Kuna kanuni nyingine ya mafanikio kwa kiongozi wa siasa. Ili kiongozi wa siasa afanikiwe anahitaji awe na nia nzuri na uwezo.
Ukiwa na nia tu bila uwezo haisaidii. Vile vile, ukiwa na uwezo bila nia, hiyo pia haisaidii; utakwama.
Ni wazi, kwa mfano, Rais mstaafu Benjamin Mkapa alikuwa na uwezo, lakini hakuwa na nia ya kuwaendeleza Watanzania.
Yeye nia yake ilikuwa ni kuwafurahisha wakubwa wa kimataifa na nafsi yake mwenyewe.
Ndiyo maana alizomewa nchini, lakini akashangiliwa nje ya nchi na wakubwa wa ubepari. Ndiyo maana aliamua kununua ndege na rada za anasa, huku mawaziri wake wakiwaambia walio na njaa wawe tayari kula majani!
Nimekuwa nikifuatilia kauli na matendo ya Rais Jakaya Kikwete tangu wakati wa kampeni ndani ya CCM hadi kwenye kampeni za uchaguzi mkuu na sasa akiwa ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Kama ilivyo kwa Watanzania wengi, nimepata kumsikiliza Kikwete kupitia redio, televisheni na kumsoma kwenye magazeti.
Nimebahatika pia kumsikiliza ana kwa ana mara mbili alipofanya ziara nchini Uingereza. Katika mara zote hizi, nimeshindwa kumuweka Kikwete katika makundi niliyoyataja hapo juu.
Lazima nikiri mapema kabisa kuwa, rais wetu amejaliwa ucheshi na haiba ya hali ya juu. Ukimuona utafurahi na ukimsikiliza lazima ucheke! Lakini, ukijiweka kama mwanafunzi na ukamweka Kikwete kwenye mizani ya ualimu, basi ujue ni wazi kabisa kwamba yeye hafuati kanuni za ualimu.
Hii ni kwa sababu utashtukia amemaliza kufundisha bila kujua alianzaje na amemalizaje! Hata hivyo sitaki kumlaumu kwa kutokufuata hizi kanuni za ualimu maana yeye kitaaluma si mwalimu; kwa hiyo ni kumuonea kama tutatarajia naye afanye kama wafanyavyo walimu wanaofuata maadili na taaluma yao!
Tatizo langu kubwa ambalo ndilo chimbuko la makala hii, ni kauli na matendo ya Rais Kikwete kama mwanasiasa.
Kila anaposimama kuzungumza, amekuwa akiibuka na kauli zinazokinzana.
Zaidi ya yote, haelekei kwamba yale anayoyafanya yanafanana na yale ayasemayo.
Kuna kila dalili kuwa katika urais wake, Kikwete atasema yale asiyoyatenda na atatenda yale asiyoyafanya.
Ni wazi pia kuwa Rais Kikwete hataweza kutekeleza ahadi lukuki alizozitoa katika kampeni zake za uchaguzi wa mwaka 2005.
Kisicho dhahiri ni sababu za Rais Kikwete kushindwa kutekeleza ahadi zake. Ni kwamba, hana nia, lakini ana uwezo? Au nia anayo, lakini hana uwezo? Au vyote hana? Nitatoa mifano michache kuthibitisha hisia zangu.
Moja ya ahadi kubwa alizotoa Kikwete wakati wa kampeni za uchaguzi wa mwaka 2005 na hata baada ya kuapishwa kuwa rais, ni kupitia upya mikataba ya madini.
Ahadi hii ilikuwa ni jibu kwa kilio cha muda mrefu kilichopuuzwa na utawala wa Rais Mkapa, kuhusu uporwaji wa madini unaofanywa na kampuni za madini katika migodi mbalimbali nchini.
Kikwete aliahidi kuwa serikali yake ingeipitia mikataba yote ya madini ili hatimaye sisi nasi tuanze kufaidika na madini yanayochimbwa katika migodi yetu.
Akasema kuwa yeye alikuwa anataka ‘win-win situation’, yaani kila upande ushinde, kampuni na sisi wenye madini; kwa kuwa kampuni zina nyenzo za kuchimba madini, lakini madini haya yapo katika ardhi yetu, kwa hivyo ni kwetu.
Pamoja na onyo la Profesa Ibrahim Lipumba kuwa, Kikwete alikuwa ni mtu wa mzaha, haamanishi anachokisema, bado Watanzania walio wengi walimwamini, wakamchagua, tena kwa kura nyingi.
Sasa Kikwete baada ya kukabidhwa nyenzo ya kupitia mikataba, amebadili kauli.
Akijibu swali la Mtanzania mmoja jijini London katika moja ya ziara zake nyingi, Kikwete kwa ujasiri mkubwa na bila aibu ya kusutwa na maneno yake ya nyuma, alisema kuwa, kwa hali halisi ilivyo katika mikataba ile, “that is the best we can get”, akimaanisha kuwa tunachopata ndiyo stahili yetu!
Akasema pia kuwa, mikataba ya madini ambayo Tanzania imeingia, ni kwa mujibu wa sheria za kimataifa na yeye kwa kuwa anahangaika kuvutia wawekezaji, asingekuwa tayari kugeuka jiwe.
Kikwete akasema kuwa anachofanya sasa ni kuwaomba hawa wenye kampuni wafupishe muda wa kutokulipa kodi ili waanze kulipa mapema zaidi kuliko ilivyoanishwa kwenye mkataba.
Alihitimisha jibu lake kwa kusema kuwa, wakati akifanya jitihada za kuwashawishi wenye kampuni kuanza kulipa kodi ya serikali, itabidi Watanzania tuendelee kuvumilia na ana imani kuwa hili litafanikiwa kufikia mwaka 2010!
Ukimsoma vizuri Kikwete katika maelezo yake, ni kama vile ndiyo kwanza alikuwa anaielewa mikataba ya madini baada ya kuwa rais.
Na kwa mtu ambaye hakuwa Mtanzania na ndiyo ilikuwa mara ya kwanza kumsikiliza katika mkutano ule, angefikiri kuwa rais anayezungumza, alishinda urais akitokea chama cha upinzani!
Ingebidi uwe na ushawishi wa aina yake ili mtu huyo akuamini kuwa anayezungumza mambo hayo alikuwa waziri mwandamizi katika wizara mbalimbali za serikali zilizopita kwa zaidi ya miaka kumi na tano, tena nyingine zikihusika moja kwa moja na mikataba ya nishati na madini!
Nilizidi kushikwa na butwaa zaidi baada ya kusoma mazungumzo ya rais na mwenyeji wake nchini Norway.
Pamoja na mambo mengine, kule Rais Kikwete aliibuka na kauli mpya ya aina yake kuhusu mikataba ya madini.
Akasema kuwa tatizo la mikataba mibovu lilisababishwa na ukosefu wa wataalamu wenye uwezo wa kujadili mikataba!
Hii ni kauli mpya kabisa ambayo rais hakuwahi kuitoa kabla; kauli ambayo inaibua maswali mengi kuliko majibu.
Kwanza, iweje nchi hii katika miaka 45 ya uhuru isiwe na wataalamu wa kuelewa mikataba? Iweje nchi hii yenye idara kubwa sana ya Jiolojia pale Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (Mlimani) na yenye wizara nzima inayohusu madini, isiwe na wataalamu wa kuelewa mikataba?
Inawezekanaje rais ateue kamati ya kupitia upya mikataba ya madini wakati akijua kabisa kuwa hakuna Mtanzania mwenye uwezo wa kujua hiyo mikataba yenyewe? Au ndiyo tuseme moja ya mang’amuzi ya kamati ile ni kuwa hatuna wataalamu wa kuelewa mikataba, wakiwemo wajumbe wa hiyo kamati?
Kwa maoni yangu, rais katudhalilisha. Tatizo la mikataba haliwezi likawa limesababishwa na ukosefu wa wataalamu.
Limesababishwa na kukosekana nia safi ya kusimamia mali zetu asili. Limetokana pia na mwendelezo wa Serikali ya CCM ya kusimamia maslahi ya watu binafsi na wachache badala ya umma.
Ni ubinafsi wa Serikali ya CCM ndio umewafanya waifiche mikataba isijulikane hata kwa Bunge ambalo limejaa wabunge wa CCM!
Ni vigumu kuelewa inakuwaje serikali hii inawaamini madalali wa kigeni kujadili mikataba kwa niaba yetu, lakini haiwezi kuwaamini wabunge waliochaguliwa na wananchi angalau waione tu mikataba hiyo, tena wabunge kutoka chama kinachotawala! Hii inaweza kutokea Tanzania tu!
Ahadi nyingine ambayo Rais Kikwete amekuwa akiitamka kwa sauti kubwa kuwa, ataitekeleza kwa dhati na kwa moyo mkunjufu, ni ujenzi wa demokrasia.
Amekuwa akirudia kila mara, kwa mfano, kuwa hana nia ya kuvidhoofisha vyama vya upinzani na kwamba atazingatia utawala wa sheria na haki za binadamu na kudumisha uhuru wa watu kutoa maoni yao.
Hata hivyo, ukiangalia matendo ya serikali yake tangu aingie madarakani, ni rahisi kung’amua kuwa ayasemayo Rais Kikwete siyo anayoyatenda.
Kwa mfano, kwa mara ya pili Mahakama Kuu imeharamisha sheria inayozuia wagombea binafsi.
Lakini Rais Kikwete, katika vikao vya Kamati Kuu na Halmashauri Kuu ya CCM akaweka msimamo wa kupinga hukumu ya Mahakama Kuu katika Mahakama ya Rufaa.
Na kweli, miezi kadhaa baada ya hukumu, tumeona Mwanasheria Mkuu wa Serikali - naamini kwa maelekezo na shinikizo kutoka CCM - akifungua rufaa hiyo katika Mahakama ya Rufaa.
Sasa haiingii akilini kwa rais aliyeahidi na anayehimiza ujenzi wa demokrasia kuendelea kung’ang’ania sheria ambayo inapingana na katiba ya nchi na ambayo ilipingwa vikali na hata mwasisi wa chama kilichomweka madarakani, Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere.
Ni serikali ya Kikwete pia ambayo imebuni mtindo mpya wa kuwarubuni viongozi wa upinzani kwa kuwaahidi kuwapa madaraka pindi wahamiapo CCM.
Anachokifanya Kikwete na serikali yake, ni kuwaonyesha wananchi kwamba upinzani haufai kiasi kwamba hata viongozi wao wanawakimbia.
Ni aibu kwamba Kikwete na CCM wanajaribu kujenga uhalali na ufuasi wa chama chao kwa kujaribu kubomoa upinzani badala ya kutekeleza yale waliyoyaahidi katika uchaguzi uliowaweka madarakani!
Sasa yote haya yananifanya nijiulize hivi, Rais Kikwete unataka tuamini uyasemayo au uyatendayo? Pili, Rais Kikwete una nia na uwezo wa kuyafanya uliyoahidi?
Kikwete ukitaka uache alama chanya katika utawala wako, fanya kama usemavyo. Kama kweli unataka kukuza demokrasia katika nchi yetu, onyesha hili kwa vitendo.
Ruhusu wabunge wetu wajadili mikataba yenye maslahi ya taifa kabla ya kutiwa saini.
Ruhusu mjadala mpana wa mapungufu ya katiba yetu na muungano wetu. Tekeleza hukumu ya Mahakama Kuu kuhusu mgombea binafsi.
Vinginevyo, utaingia katika historia ya viongozi wanaohubiri wasiyoyaamini.