KWA takriban wiki mbili sasa, nchi yetu imeendelea kugubikwa na habari kuhusu mkutano wa Halmashauri Kuu ya CCM, uliofanyika Butiama, mkoani Mara.
Katika kipindi chote cha mkutano huu wa CCM, waandishi wengi muhimu walivihama vituo vyao vya kazi Dar es Salaam wakaenda Butiama, kiasi cha kuwashangaza hata wenye mkutano. CCM walikaririwa kupitia Ofisa Habari na Mawasiliano wa chama hicho, Gabriel Athumani, wakiwashangaa waandishi kujazana Butiama kwa ajili ya mkutano wao bila hata kualikwa!
Katika kutafuta habari zilizoandikwa kuhusu mkutano wa CCM Butiama kupitia mtandao maarufu wa Google, nilikutana na vichwa vya habari 38 - vyote vikiwa na habari kuhusu mkutano huu na ambavyo viliandikwa na waandishi wa habari wa Tanzania.
Hizi ni zile ambazo hazijumlishi taarifa za redio, televisheni na magazeti ambayo hayapo katika mtandao wa intaneti.
Miongoni mwa habari na makala nilizosoma kuhusu mkutano huo ni zile zilizobeba vichwa vya habari vifuatavyo: “Butiama: kivumbi kutimka”; “Butiama kuitikisa CCM”; “CCM yafanya maamuzi magumu kwa nchi” na “Mkutano wa Halmashauri Kuu CCM na masuala magumu ya nchi”.
Katika kusoma habari na makala kuhusu mkutano huo, niligundua kwamba waandishi wa habari na wananchi kwa ujumla walikuwa na matumaini makubwa sana kuhusu kile ambacho kingejiri kutoka Butiama. Hiyo ndio sababu iliyowapeleka waandishi kwenye mkutano huo.
Uchambuzi nilioufanya kuhusu habari na makala zilizohusu mkutano huu unaonyesha kwamba waandishi na wananchi kwa ujumla walitarajia angalau mambo mawili yatokee.
Kwanza, kwamba CCM wangepitisha azimio la kuundwa kwa serikali ya mseto huko Zanzibar kama walivyofanya wenzao wa CUF. Bahati mbaya miongoni mwa waliotarajia hili ni pamoja na viongozi wa CUF akiwamo Maalim Seif Shariff Hamad.
Nasema ni bahati mbaya kwa CUF kutarajia hili kwa sababu inaonyesha kwamba pamoja na Maalim Seif kukaa na CCM kwa miaka yote hiyo, bado hajawajua.
Jambo la pili lililotarajiwa kama nilivyoelewa kupitia makala hizo, ni kwamba hatimaye majambazi wa fedha za walipa kodi pale BoT wangeshugulikiwa kikamilifu.
Hili nalo lilikuwa tarajio la kimiujiza kwa sababu kama nilivyopata kusema katika makala zangu huko nyuma, ni sawa na kumtegemea jambazi akuibie halafu ajikamate mwenyewe!
Tumejikuta mateka wa CCM kisiasa, baadhi yetu kwa kujua na baadhi yetu kwa kutokujua. Umateka wetu unajitambulisha na kujithibitisha kwa njia nyingi.
Njia mojawapo ni kitendo chetu cha kuendelea kuweka matumaini na matarajio kwa CCM kwamba ndicho chama kinachoweza kutatua matatizo yetu pamoja na kushindwa kufanya hivyo kwa miaka yote kilichokaa madarakani.
Umateka wetu unatia huruma na wakati mwingine hasira kwa sababu tunawatarajia CCM watengeneze na kurekebisha kitu walichokiharibu wenyewe.
Kwa hiyo, kwa mfano, tunajua kwamba waliofanya ufisadi wa fedha za Benki Kuu ni baadhi ya viongozi wa CCM, lakini bado sote tulitarajia kwamba wangekaa Butiama wapange mikakati ya kujikamata badala ya namna ya kujificha na kutuziba midomo tusiwahoji.
Ni wazi katika hili CCM wamekuwa washindi, maana wameweza kufunika kombe mwanaharamu apite na sisi tumebaki tumeduwaa, hatujui kinachoendelea.
Katika kujipa matumaini juu ya uwezo na uzuri wa CCM na hivyo kuhalalisha umateka wetu, tumekuwa tukiamini kwamba tatizo la CCM ni watu wachache tu wenye kutumia madaraka yao vibaya.
Kwa hiyo, kwa kufuata mantiki hii, kwa mfano, tukakubaliana na ghilba kwamba Edward Lowassa ni hatari kwa nchi yetu lakini si CCM wala Kikwete. Tena waandishi wa habari wakaandika makala lukuki wakishangilia uamuzi wa Lowassa kujiuzulu na wengine wakaenda mbali hata kutaka CCM wamfukuze uanachama.
Kitu cha kusikitisha ni kwamba kwetu sisi ubaya wa kiongozi huonekana pale anapokuwa ametoka madarakani. Nasema hili kwa sababu ni waandishi na wanazuoni hao hao, waliomkandia Lowassa baada ya kutoka madarakani, ambao walikuwa wanamsifu na kutukumbusha mara kwa mara kuhusu uimara wake kama kiongozi alipokuwa Waziri Mkuu.
Mbaya zaidi ni waandishi hawa hawa na sisi wananchi tuliokubali kutumiwa kumnyamazisha, ama kwa kujua au kutokujua, Lowassa asiseme yale aliyokuwa nayo moyoni na kusahau kwamba uhuru wa kusema ni pamoja na kumpa nafasi mtu aseme hata yale usiyoyataka au yanayokuumiza.
Bado tunakumbuka pia jinsi waandishi walivyokuwa hawaishi kuupamba utawala wa Mkapa, lakini leo ni hao hao ambao hawasiti kutukumbusha jinsi Rais wetu huyu mstaafu alivyoifilisi nchi.
Yote haya unaweza kuyatolea muhtasari kwa maneno mawili tu ya Kiswahili; nayo ni unafiki na woga.
Tunachokisahau na ambacho sitaacha kukikumbusha katika makala zangu, ni ukweli kwamba kinachosababisha mtu awe mwovu ni mazingira ya uovu ambayo yametengenezwa na mfumo wa uovu.
Kwa maneno mengine hakuna kinasaba (gene) cha uovu na kwamba hakuna mtu anayezaliwa akiwa mwovu. Hili si jambo ninaloliongea kwa hisia; ni jambo ambalo limefanyiwa utafiti na kuna makala za kitafiti lukuki zimeandikwa katika majarida maarufu duniani zikithibitisha hivyo.
Ndiyo kusema wanaotenda uovu katika CCM hawakuzaliwa waovu; uovu wao unasabishwa na mazingira waliyomo ambayo ni chama chao.
Ninachosema hapa ni kwamba tofauti na imani kwamba kuna viongozi wanaoichafua CCM, ni CCM ambayo imekuwa ikiwachafua watu waliokuwa “watakatifu” kuliko utakatifu wenyewe. Sote tulio watu wazima tunayo mifano ya wana CCM ambao walikuwa “watakatifu” sana tu lakini wakageuka kuwa mafisadi wa ajabu mara walipoamua kujiingiza katika CCM.
Hahitaji akili nyingi sana kujua kwamba ukiingia kwenye jalala la uchafu lazima utachafuka. Kutarajia kwamba utaingia kwenye jalala la uchafu kisha utoke ukiwa msafi ni kutarajia muujiza kuliko muujiza wenyewe.
Kwa hiyo, kuendelea kufikiri kwamba tutafanikiwa kwa kuwatoa baadhi ya viongozi wa CCM tunaofikiri ni mafisadi na kuiacha CCM madarakani ni kutafuta majibu mepesi kwa maswali magumu na ni kukwepa wajibu wetu wa msingi kama raia.
Jambo la pili linalothibitisha umateka wetu kwa CCM ni jinsi tulivyokuwa tukiutathmini utendaji wa Rais Kikwete. Tumejikuta tukimtathmini Rais wetu kwa mujibu wa maneno anayoyasema majukwaani badala ya yale anayoyatenda katika kutekeleza wajibu wake wa urais.
Kwa hiyo, kwa mfano, tukajikuta tunamsifu sana Rais wetu kwa kusema kuwa ana nia ya dhati ya kuumaliza mgogoro wa Zanzibar. Tukamsifu sana pia pale aliposema kwamba atawashughulikia wala rushwa wakubwa na tayari majina yao anayo. Tukaendelea kummwagia sifa kwa kutuahidi angemaliza tatizo la dawa za kulevya, tena akawapa na onyo wafanyabiashara wa mihadarati kuwa alikuwa na majina yao wote.
Mwisho wa yote, sote tukajikuta tunapumua kama vile tumetua mzigo mzito pale tulipoahidiwa na Rais wetu kabla na baada ya kuingia Ikulu, angehakikisha kila Mtanzania anapata maisha bora. Swali la kujiuliza ni kuwa ni yapi kati ya mengi aliyoyasema ameweza kuyafanya hadi sasa anapokaribia kumaliza miaka mitatu katika urais wake?
Sina tatizo na rais wetu kuwaahidi wananchi wake mambo makubwa na mazuri. Tatizo langu ni sisi wananchi kumsifu rais wetu kwa yale anayoyasema badala ya yale anayoyatenda.
Katika kusomasoma kwangu wasifu (biography) za viongozi maarufu wa kisiasa duniani, sijaona mahala ambapo kiongozi amesifiwa kwa yale aliyoyasema. Kote nilikosoma nimeona viongozi wamesifiwa kwa yale waliyoyatenda walipokuwa madarakani.
Ni Tanzania pekee ambako kiongozi anasifiwa kwa kuahidi kuwashughulikia wala rushwa na majambazi akiwa katika jukwaa la siasa na kuambiwa huyu ni “kiboko” hata kama hatafanya hivyo katika uongozi wake wote.
Wanasaikolojia wa siasa wanaamini kwamba kiongozi mahiri ni yule mwenye kuweza kufanya maamuzi magumu kuhusu jamii yake na asiyeogopa kukosea katika kuchukua maamuzi.
Pengine hili la kushindwa kwa Rais wetu kuumaliza mgogoro wa Zanzibar na kususua kwake katika kupambana na ufisadi, kama alivyoahidi mwenyewe bila kulazimishwa, litatusaidia kuanza kutambua uwezo halisi wa kiuongozi wa Rais wetu.
Kilichowazi ni kwamba hawezi kufanya maamuzi magumu na anaogopa kufanya makosa katika uongozi wake. Na kwa kuogopa huku anajikuta hafanyi chochote cha maana katika utawala wake.
Kwa kiasi kikubwa, kuogopa kukosea kunakoonyeshwa na Rais wetu kumesababishwa na sisi wananchi kuendelea kumpa sifa hata kwa mambo ambayo hastahili.
Hivyo lazima aogope kukosea na asite kuchukua maamuzi mazito kwa vile anajua kufanya hivyo atazipoteza sifa ambazo tumekwishamzoesha.
Vivile ni matumaini yangu kwamba kwa matukio ya CCM kama ya huko Butiama, yatasaidia wananchi kuanza kuelewa kwamba CCM haijawahi kubadilika.
Walichofanya CCM katika kukaa kwake madarakani kwa takriban nusu karne sasa, ukijumlisha na miaka ya TANU, ni kujibadilisha rangi kama afanyavyo kinyonga kwa lengo la kujificha asitambuliwe. Kwa maneno mengine ujio wa Kikwete haujafanya CCM ibadilike kama wengi wetu tulivyoaminishwa, bali ilikuwa njia nyingine ya kuendelea kutushikilia mateka.
Ambacho kimekuwa kikifanyika nikiazima msemo wa kale, ni kwamba CCM wamekuwa wakibadilisha chupa pekee lakini wameendelea kutunywesha mataputapu hayo kila siku na kama kawaida.
Ni aina ya matukio niliyoyaanisha hapo juu ambayo yamenifanya nifikie hitimisho kwamba Watanzania tulio wengi tumejikuta katika umateka wa kisiasa chini ya CCM.
Vinginevyo, utaelezaje kwamba leo hii pamoja na CCM kufanya kila aina ya uharibifu katika nchi yetu, lakini bado wananchi wanaendelea kukiamini na kukichagua kama tulivyoona huko Kiteto?
Utaelezaje kwamba leo hii pamoja na CCM kuwadanganya Watanzania kwa miaka yote iliyokaa madarakani, bado kuna waandishi wanaweza wakahama vituo vyao vya kazi na kujaza makala kwenye magazeti yetu wakitabiri mambo makubwa kutokea kwenye mkutano wa CCM?
Pengine swali kubwa zaidi ni kwa nini Watanzania wanaendelea kuonyesha “mapenzi” makubwa kiasi hiki kwa CCM wakati huu tukiwa katika mfumo wa vyama vingi?
Na ni kwa nini wananchi hawataki kuachana na CCM na kuchagua chama kingine? Kuna wanazuoni na waandishi wengi ambao hutoa jibu rahisi kwa swali hili kwamba Watanzania hawajapata chama mbadala ndio maana wanaendelea kuichagua CCM! Hii ni hoja dhaifu kwa maana halisi ya neno dhaifu na ni mwendelezo wa tabia za waandishi na wasomi wa Tanzania kutoa majibu rahisi kwa maswali magumu.
Jibu la namna hii nalifananisha na mfungwa aliyefungwa maisha na akakaa gerezani karibu nusu ya maisha yake na ghafla akapata msamaha wa Rais wa kutoka gerezani, lakini akagoma kutoka.
Anapoulizwa sababu za kukataa kutoka gerezani anasema kwamba alikwishazoea maisha ya gerezani na haamini tena kama atayamudu tena maisha ya uraiani!
Kwa hiyo, swali linalonijia mara kwa mara ninaposoma hoja za wanazuoni wetu ni hili: Je, madai kwamba vyama vya upinzani bado havina uwezo wa kutawala ni ya kweli ama ni hisia tu katika kuhalalisha kuendelea kushikiliwa kwetu mateka na CCM? Hili ni jambo ambalo nitalijadili katika makala zangu zijazo.