lf.bevel
MWANZO CHAMA SERA KATIBA TUUNGE MKONO UCHAGUZI TUWASILIANE
banner

20 Februari 2008

Kuanguka kwa Lowassa tucheke au tuchekelee?

na
Kitila A. K. Mkumbo

KAMA ilivyotarajiwa, kujiuzulu (wengine wanasema kususa) kwa Edward Lowassa kuwa Waziri Mkuu kulikofuatiwa na kuvunjwa kwa Baraza la Mawaziri, kumepokelewa kwa hisia mchanganyiko.

Ni wazi kuwa wananchi walio wengi wameonekana kufurahishwa kwa kuondoka Lowassa katika kiti cha uwaziri mkuu. Sasa ni jukumu lake kujiuliza kulikoni watu wafurahie kuondoka kwa kiongozi wao waliokuwa wanampenda?

Lowassa na washirika wake akiwemo Rais Jakaya Kikwete, itabidi pia wajiulize, inawezekanaje wananchi wafurahie kuanguka kwa kiongozi wao aliyekuwa anapaisha uchumi wa Tanzania?

Pengine ni mtihani mkubwa zaidi kwa Waziri Mkuu mpya, Mizengo Pinda, kwani kama Waswahili wasemavyo, ukiona mwenzako ananyolewa wewe tia maji nywele zako.

Ni fundisho pia kwa viongozi wengine wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), wanaodhani wamezaliwa na madaraka kuwa, ipo siku nao itabidi waondoke ama kwa kususa kama alivyofanya Lowassa au kwa kufukuzwa na waliowapa madaraka, yaani wananchi. Leo tunashangilia Lowassa kuanguka, ipo siku tutashangilia kuanguka kwa CCM!

Bila shaka kuanguka kwa Lowassa ni jambo la kuchekelea sana. Hata hivyo, siamini kwamba hili ni jambo linalopaswa kutufanya tucheke. Nitaeleza. Tunastahili kuchekelea kuondoka kwa Lowassa kwa sababu mbili kubwa.

Sababu ya kwanza ni kitendo chenyewe cha kujiuzulu. Kujiuzulu kwa Lowassa katika nafasi ya uwaziri mkuu ni tukio kubwa na la kiheshima si tu katika nchi yetu, bali pia katika bara la Afrika kwa ujumla.

Heshima hii inatokana na ukweli kwamba, kujiuzulu uwaziri, achilia mbali uwaziri mkuu, si jambo linalotarajiwa kutokea miongoni mwa wanasiasa waliopo madarakani katika bara letu hili.

Ndiyo maana basi, habari za kujiuzulu kwa Lowassa zilikuwa kubwa karibu katika vyombo vyote vya habari katika nchi za Afrika. Binafsi nilizipata nikiwa jijini Abuja nchini Nigeria, nilipokwenda kuhudhuria mkutano.

Habari za kujiuzulu kwa Lowassa ni kati ya habari zilizopewa uzito wa juu katika taarifa ya habari ya Televisheni ya Taifa ya Nigeria siku hiyo. Hata wajumbe wenzangu katika mkutano walionitambua kuwa natokea Tanzania, hawakusita kunizonga kutaka kujua kilichotokea nchini mwangu hadi kusababisha Waziri Mkuu ajiuzulu.

Kikubwa kilichowashangaza, hasa wakazi wa Nigeria, ni kitendo cha waziri mkuu kujiuzulu katika nchi ya Kiafrika kwa madai ya kuhusika na rushwa au ubadhirifu wa mali ya umma.

Ni wazi basi kuwa, kwa kiwango cha Afrika, tukio la kujiuzulu kwa waziri mkuu ni jambo zito na ambalo kwa kiasi fulani limetutofautisha na mataifa mengine barani Afrika.

Hakuna shaka pia kwamba tukio hili limetusogeza hatua moja mbele katika shauku yetu ya kushamirisha utawala bora na demokrasia katika nchi yetu.

Sababu ya pili ya kuchekelea kuanguka kwa Lowassa, ni tabia zake binafsi kama binadamu na kiongozi wa watu.

Hakuna shaka kwa wale wanaomjua Lowassa vizuri, huyu ni mtu mwenye uwezo mkubwa kiakili na kiutendaji, tena aliyejaliwa kipaji kikubwa katika nyanja za uongozi, ikiwemo uwezo wa kushawishi kwa njia ya lugha yenye mantiki na umbile la kiutawala wakati wote anapoongea na adhira.

Bahati mbaya sifa za Lowassa haziishi hapo. Huyu pia ni mtu mwenye udhaifu wa kuwa na kiburi na dharau za kutisha. Ni kiburi na dharau vilivyomfanya ajione yeye na kauli zake kuwa ni sheria ya nchi kiasi kwamba alifikia hatua ya kufukuza watu kazi kupitia majukwaa ya kisiasa, bila hata kufanya utafiti wowote kujua ukweli wa mambo kabla ya kuchukua hatua.

Kwa utaratibu huu, ni wazi kuwa Lowassa alijijengea maadui wengi zaidi kuliko marafiki ndani na nje ya serikali aliyokuwa anaiongoza. Haishangazi basi kwamba kuanguka kwake kulipokelewa kwa shangwe na wananchi wa kila rika wakiwemo waliokuwa wafanyakazi chini yake katika serikali kuu na katika ngazi ya mikoa na wilaya.

Pengine udhaifu mkubwa zaidi wa Lowassa na ambao ndio hasa sababu za kuanguka kwake ni taswira aliyojijengea kwa muda mrefu miongoni mwa Watazania kwamba ni mtu aliyetumia madaraka yake vibaya kwa kujilimbizia mali.

Taswira hii iliimarika zaidi pale Mwalimu Nyerere, alipoiweka wazi na hatimaye kumkwamisha Lowassa kugombea urais katika uchaguzi wa mwaka 1995.

Naamini ni taswira hii iliyowafanya mashahidi wengi katika tume ya Dk. Harrison Mwakyembe, kumhusisha Lowassa na kashfa ya Richmond na hatimaye tume hiyo kufikia maamuzi ya kumweka katikati ya kashfa hiyo bila hata kumhoji.

Hapa niungane na wale wachache wanaohoji uhalali wa tume ya Dk. Mwakyembe, kufikia hitimisho kubwa la kumuweka Lowassa katikati ya kashfa ya Richmond bila hata ya kupata maelezo yake.

Ukiacha misingi ya kawaida ya kisheria ambayo Dk. Mwakyembe anaielewa vizuri zaidi yangu, kitendo cha kufikia hitimisho walilofikia tume kuhusu Lowassa, bila kumhoji kama mhusika mkuu, ni uvunjifu wa maadili ya msingi ya kitafiti.

Tume pia inarahisisha mambo pale inapojaribu kuhalalisha kutomhoji Lowassa kwa sababu kuwa hakujikoteza kama walivyofanya mashahidi wengine. Tume wanajidanganya wenyewe wanapotaka tuamini kwamba uzito aliokuwa nao Lowassa kama waziri mkuu, ulikuwa sawa na mwananchi mwingine yeyote aliyejitokeza kutoa ushahidi.

Kwa hiyo, pamoja na kuisifu tume kwa kazi nzuri waliyoifanya, hili la kutomhoji Lowassa litabaki kuwa doa katika taarifa yao.

Sasa nieleze ni kwa nini naamini kwamba kuanguka kwa Lowassa na wenzake si jambo la kutufanya tucheke au tufurahi. Tungestahili kucheka na kufurahi kama kujiuzulu huku na kuundwa kwa Baraza la Mawaziri jipya kungekuwa ni hatua za mwanzo katika kutokomeza wimbi la ufisadi ambalo linazidi kushamiri katika utawala wa CCM.

Lakini ukweli ni kwamba malengo waliyokuwa nayo watawala katika kujiuzulu kwa Lowassa na hatimaye kuvunja Baraza la Mawaziri hayashabihiani na yale ambayo inaelekea wananchi wanayo.

Wakati wananchi wakielekea kuamini kwamba Serikali ya Rais Kikwete sasa imeamua kupambana na ufisadi kwa vitendo, kuna kila dalili kwamba hatua zilizofanyika hivi karibuni zililenga katika kujisafisha katika macho ya wananchi na hasa jumuiya ya kimataifa na wafadhili.

Sote tunakumbuka kwamba hivi karibuni wafadhili walionyesha waziwazi kukerwa na wimbi kubwa la ufujaji wa fedha za umma kunakofanywa na utawala wa CCM kiasi cha kutishia kusimamisha misaada yao kwa serikali.

Hili ndilo hasa jambo ambalo utawala wa CCM huliogopa kuliko kelele za wapinzani na wananchi kwa ujumla kwa sababu serikali yetu haina ubavu wa kujiendesha pasipo misaada ya Wazungu.

Kama nilivyopata kusema katika makala zilizotangulia, na ninarudia tena kuwa, ufisadi hautakwisha katika nchi yetu kwa kukata matawi badala ya mti na kung’oa mizizi ya ufisadi au kwa kuwatoa samaki wachache wanaoonekana kuoza zaidi kuliko wengine badala ya kusafisha maji yanayoozesha hao samaki.

Ukweli ni kwamba, tatizo la ufisadi katika nchi yetu ni la kimfumo zaidi kuliko hali inayosababishwa na watu wachache kama akina Lowassa. Madamu ni CCM hii hii inaendelea kutawala, itabidi tuendelee kubaki nao na kuuzoea ufisadi kama sehemu ya maisha yetu ya kisiasa.

Kitu ambacho bado wengi kinatupa shida kuelewa ni kwamba, ufisadi ni silaha muhimu sana ya CCM kuendelea kubaki madarakani. Ndio kusema kuwataka CCM watokomeza ufisadi ni sawa na kuwataka waukate mti walioukalia jambo lisilowezekana.

Katika hali ya kawaida, kama kweli Rais Kikwete angekuwa hata na chembe ya kuchukia wabadhirifu na kupenda usafi katika siasa, isingewezekana amteue Lowassa kuwa Waziri Mkuu katika serikali yake kutokana na historia yake huko nyuma.

Kwa kumteua Lowassa kuwa waziri mkuu, Rais Kikwete alijua kwamba alikuwa anaanza utawala wake na doa kubwa la kukumbatia ubadhirifu na ufisadi.

Vilevile, baada ya kujiuzulu kwake, asingehuzunishwa na kusikitishwa na kujiuzulu kwa Lowassa.

Zaidi ya yote, kama Rais Kikwete angekuwa kweli ameguswa na matatizo ya ubadhirifu na ufisadi katika serikali yake, baada ya kuvunja baraza lake la mawaziri, asingethubutu kuwarudisha mawaziri ambao majina yao yamesambaa kila kona ya nchi kuwa ni mafisadi.

Kwa hiyo ni wazi kuwa hatua ya kujiuzulu kwa Lowassa na kuvunjwa kwa Baraza la Mawaziri, ni mazingaombwe yenye lengo la kutupofusha na kuuwezesha mfumo wa ufisadi kujipanga upya ili tuwasahau kwa muda huku wakiendelea na biashara kama kawaida.

Kikubwa zaidi, Rais Kikwete anajua vizuri sana kuwa mpaka sasa serikali yake haijatekeleza majukumu ya msingi wala kukidhi kiu na matarajio ya wananchi aliyoyachochea mwenyewe wakati wa kampeni zake mwaka 2005.

Kwa hiyo, anajua hana cha kuwauzia Watanzania ifikapo mwaka 2010 zaidi ya kubandika mabango makubwa kila kona ya nchi na kugawa kofia na kanga kwa vijana na kina mama kama ilivyo desturi ya wanasiasa hao.

Kikwete anajua mambo yote haya yanahitaji pesa nyingi ambazo binafsi hana na itabidi azipate kupitia mawakala wa ufisadi kama ilivyokuwa katika uchaguzi uliopita.

Kwa sababu hizi, ni muhimu sana Watanzania tusififishe hasira zetu juu ya mafisadi, lazima tuziendeleze ili angalau kuwatisha wakati tukisubiri kufanya mabadiliko ya kweli katika chaguzi zijazo, lakini tuanzie Kiteto.

Nimalizie kwa kukiri kwamba, hili la kujiuzulu kwa Lowassa na hatimaye kuvunjwa kwa Baraza la Mawaziri limemhuisha Rais Kikwete kisiasa. Ni jambo ambalo angalau litamuwezesha kusifiwa na vyombo vya habari na wananchi kama alivyozoea.

Hata hivyo, jambo hili pia linatutia moyo sisi wenye shauku ya kuona mabadiliko makubwa katika utawala wa nchi yetu. Hii ni kwa sababu wakati tukiendelea kuimarisha nguvu ya upinzani nchini mwetu, tumepata faraja kuona kuwa kumbe CCM inaweza kuanguka kwa uzito wake yenyewe bila hata kusubiri nguvu kubwa kutoka nje.

Hili ni jambo linalotufanya wapenda mabadiliko tuchekelee, lakini halitoshi kutufanya tuanze kucheka!

 
lf.curl lf.curl2 rt.curl2 rt.curl