Wiki iliyopita, vyombo vya habari na mazungumzo ya kawaida mitaani na kwenye mitandao ya kompyuta yalitawaliwa na habari za Rais Jakaya Kikwete kumwachisha kazi aliyekuwa Gavana wa Benki Kuu, Daudi Ballali.
Vyombo vingi vya habari na wananchi kwa ujumla wameonekana kufurahishwa sana na uamuzi “mzito” aliouchukua Rais Kikwete wa kutengua ugavana wa Ballali. Angalau magazeti mawili yalibeba tahariri mahsusi zenye kumpongeza Rais Kikwete kwa kumfukuza kazi Ballali.
Gazeti la Tanzania Daima, kwa mfano, katika tahariri yake ya Januari 10, 2008 lilikuwa na kichwa cha habari kilichosema: “Hongera Rais Kikwete”. Nalo gazeti la Mwananchi katika tahariri yake ya Januari 12, 2008 lilimsifu Rais Kikwete kwa kichwa cha habari kisemacho “Hapa Kikwete umeanza kufanya kweli”. Wananchi pia katika mikoa mbalimbali wameripotiwa wakimsifu Rais Kikwete kwa uamuzi wake wa kumfukuza kazi Gavana Ballali.
Nimekuwa nikitafakari uamuzi wa Rais Kikwete wa kumuachisha kazi Ballali na kujiuliza kama kweli Rais Kikwete anastahili au kustahiki sifa anazomwagiwa. Niseme wazi mwanzoni kabisa kuwa natilia shaka sana sifa ambazo Rais Kikwete anapewa; na niseme pia kwamba kwa maoni yangu tunamshangilia Kikwete kwa mafanikio hewa.
Kuna mambo kadhaa nimezingatia katika kutilia shaka sifa anazopewa Kikwete. Kwanza, sote tunatambua kwamba Ballali alishaandika barua ya kujiuzulu kazi ya ugavana kwa sababu za kiafya. Hata hivyo, kabla ya Ballali kuondoka kwenda Marekani kwa kile kilichoelezwa alikwenda kutibiwa, kulikuwa na wito kutoka kila kona ya nchi ukimtaka Rais Kikwete amuachishe kazi Ballali ili apishe uchunguzi wa tuhuma lukuki zilizokuwa zinamkabili.
Rais Kikwete alishindwa kumuachisha kazi Ballali. Sasa kitendo cha Rais Kikwete kumuachisha kazi mtu ambaye tunaelezwa yupo mahututi na ambaye alikwishajiuzulu kazi yake hiyo, ni kitendo cha woga na kinathibitisha kwa mara nyingine kuwa rais wetu hana uwezo wa kufanya maamuzi magumu. Alichofanya Rais Kikwete ni sawa na mkulima aliyekuwa anajaribu kukata mbuyu kwa kutumia wembe na akashindwa kwa miezi kadhaa, leo mbuyu unaangushwa na upepo mkali, yeye anakimbia kutangaza kuwa ndiye aliyeuangusha!
Sababu yangu ya pili ya kutilia shaka nia ya Kikwete ya kumuachisha kazi Ballali, ni kitendo cha serikali kujaribu kuficha au kuzikana habari za Ballali kujiuzulu, kilichoambatana na kuficha ugonjwa wake na mahali anapotibiwa huko Marekani.
Bahati mbaya waliyonayo Kikwete na wenzake serikalini ni kwamba hawana uwezo wa kuficha habari katika karne ya leo. Sasa wao walificha habari za barua ya Ballali ya kujiuzulu, lakini ikapatikana katika mtandao na vivyo hivyo pamoja na kukataa kutaja ugonjwa na mahali anapotibiwa Ballali, watu wamejua maana kuna Watanzania lukuki wanaishi aliko Ballali na kuna wengine wanatibiwa naye katika hospitali moja.
Matukio haya ya serikali yananifanya nikubaliane na wale wanaosema kwamba Kikwete kamtoa Ballali kafara ili aonekane kwamba ameanza kushughulikia ufisadi katika serikali yake. Mbinu hii si ngeni ndani ya CCM. Rais Mkapa naye aliitumia katika kujaribu kuonyesha kwamba ana nia ya dhati ya kupambana na rushwa alipoingia madarakani, kwa kumtoa kafara aliyekuwa Waziri machachari wa Ujenzi katika serikali ya mzee Ali Hassan Mwinyi, Nalaila Kiula.
Lakini sote tunatambua kuwa hiyo yote ilikuwa danganya toto, kwani baada ya Kiula, mambo yaliendelea kama kawaida na rushwa ikapamba moto na mwisho wa siku Rais Mkapa akageuka kuwa mtetezi mkubwa wa matendo ya rushwa katika serikali yake.
Tofauti ya kafara hizi mbili, ya Kikwete na Mkapa, ni kwamba Kikwete ameamua kumtoa kafara mtu ambaye anajua hana uwezo tena wa kujitetea kutokana na matatizo ya afya aliyonayo na ukweli kwamba yupo nje ya nchi.
Jambo la tatu nililozingatia katika shaka yangu juu ya sifa anazomiminiwa Kikwete, ni ukweli kwamba tuhuma za ubadhirifu wa Benki Kuu ziliwahusisha vigogo zaidi ya kumi na moja, wengi wao wakiwa ni wanasiasa waandamizi katika CCM na serikali yake. Sasa najiuliza ni nini hatima ya wale waliotuhumiwa wakiwemo mawaziri wa Kikwete?
Vilevile, viongozi wa juu sana katika serikali hii wakiongozwa na mzee asiyekubali kuzeeka, Kingunge Ngambale Mwiru si tu kwamba walikanusha na kudharau tuhuma zilizotolewa na Dk. Willibrod Slaa, lakini pia walijaribu, japokuwa bila mafanikio, kuwafanya wananchi waamini kwamba Dk. Slaa na wenzake katika upinzani ni waongo na wazushi. Sasa mimi nilitarajia kwamba waandishi wa habari badala ya kukimbilia kummiminia sifa Rais Kikwete, wangewauliza akina Kingunge ni nani mzushi kati yao na Dk. Slaa?
Jambo la nne na muhimu zaidi ni kwamba, mpaka hapo Rais Kikwete hajagusa kiini cha tuhuma za ubadhirifu wa Benki Kuu. Kiini cha ubadhirifu huu ni madai kwamba pesa zilizochotwa Benki Kuu ndizo hizo zilizotumika kuendesha kampeni kubwa na za kukufuru zilizomwezesha Rais Kikwete kuchaguliwa kwa asilimia themanini.
Ushahidi wa madai haya umeshaanza kujitokeza kutokana na ukweli kwamba takribani kampuni zote zinazoelezwa kuhusika na utafunaji wa mabilioni ya Benki Kuu, zilisajiliwa katika kipindi cha kuelekea uchaguzi mkuu wa 2005. Ndio kusema kampuni hizi zilitumika kama njia ya kupitisha haya mabilioni kwenda kwenye kampeni za CCM.
Hapa pia ndio unaweza kuelewa ni kwa nini Rais Kikwete alikuwa hana uwezo wa kumuachisha kazi Ballali akiwa mzima wa afya na akiwa nchini. Ni wazi kwamba Ballali ana siri nzito juu ya haya mabilioni na yeye kama zilivyo zile kampuni za kitapeli, alitumika tu kama mfereji wa kupitisha haya mabilioni kwenda kwa wahusika ambao ndio hao vigogo wa CCM.
Katika hali ya kawaida, zile kampuni zisingekuwa na sifa ya kupata tenda kubwa kama zile ambazo zimeonyeshwa katika ripoti ya EPA, kwa kuzingatia kuwa zilikuwa hazina uzoefu wowote wa kazi zilizoomba kuzifanya kutokana na uchanga wao.
Mwisho kabisa, kitendo cha Rais Kikwete kuwaagiza wakuu wa vyombo vya dola kuwachukulia hatua wale wote waliotajwa katika ripoti ya uchunguzi wa EPA, kinaacha maswali mengi zaidi kuliko majibu. Sasa najiuliza ina maana hawa wanaopaswa kuwa walinda sheria wasingechukua hatua zozote kuwahusu wale waliotuhumiwa kama wasingeagizwa na rais?
Naendelea kujiuliza tena, ina maana wakuu wetu wa vyombo vya dola hawana uwezo wa kuwachukulia hatua wakubwa wanaovunja sheria bila kuagizwa? Hii kwa mbali inaanza kunipa jibu ni kwa nini kuna watu wana kesi za mauaji wanaendelea kukaa nje miaka wakati mtu anayekamatwa kwa kufanya maandamano ya amani kesi yake hukimbizwa harakaharaka. Kama hivi ndivyo, basi safari yetu ya ujenzi wa utawala wa sheria bado ni ndefu mno madamu tunaendelea kutawaliwa na CCM.
Hili la ubadhirifu wa BoT na kusuasua kwa Rais Kikwete kuchukua maamuzi mazito litukumbushe kwa mara nyingine kuwa CCM ya leo haina nia wala uwezo wa kupambana na rushwa. Yote hii ni kwa sababu CCM yenyewe kama chama haiwezi kusimama bila rushwa. Sote tunatambua kabisa kwamba viongozi wengi katika CCM hawachaguliki tena pasipo rushwa na wengi wao wanaendelea kubaki katika uongozi wa kisiasa si kwa lengo la utumishi kwa umma, bali wanautumia uongozi kama njia rahisi na ya haraka ya kujipatia utajiri na heshima katika jamii.
Kikubwa zaidi, tunapaswa kujiuliza nia na uwezo wa Rais Kikwete kuchukua maamuzi mazito kama ya kupambana na ubadhirifu wa aina ya BoT. Bahati mbaya Rais Kikwete hana historia ya kufanya maamuzi mazito katika maisha yake ya kisiasa na wengine hatujashangaa kwa nini amekuwa akisuasua katika kufanya maamuzi mengi.
Bahati aliyekuwa nayo Kikwete kabla ya kuwa rais ni kwamba, alikaa karibu miaka kumi katika Wizara ya Mambo ya Nje, wizara ambayo, katika nchi maskini kama ya kwetu, kwa kawaida utendaji wa kila siku wa waziri haugusi moja kwa moja maisha ya Mtanzania wa kawaida. Hii ni wizara salama na kichaka kizuri cha kuficha udhaifu wa mwanasiasa.
Mara nyingi tumekuwa tukimsifu Rais Kikwete kwa mambo ambayo kwa kweli ni wajibu wake wa kawaida na ambayo anakuwa ameyafanya kwa kiwango cha chini ya matarajio. Mbaya zaidi ni kwamba, hata taasisi za kisomi kama REDET nazo zinajikuta katika mtindo huu. Kwa mfano, walipotoa tafsiri ya utafiti wao wa hivi karibuni kwamba Rais Kikwete anakubalika zaidi kuliko baraza lake ni wazi kwamba walikuwa wanamdanganya.
Walimdanganya kwa sababu sote tunatambua kuwa huwezi kusema wewe ni mrefu kuliko wengine wakati wote waliokuzunguka ni wafupi kuliko nyasi. Ukweli ni kwamba kama tunaamini Baraza la Mawaziri la Kikwete ni dhaifu, tunachosema hapa ni kwamba serikali ya Kikwete ni dhaifu. Sasa haiwezekani Kikwete aongoze serikali ambayo ni dhaifu halafu yeye asiwe dhaifu!
Sasa hii tabia ambayo inaanza kumzoesha au tayari imeshamzoesha vibaya Rais Kikwete ya kumpa sifa kwa mafanikio hewa haimsaidii yeye wala haiwezi kukidhi hamu yetu ya kuona ubadhirifu katika sekta ya umma unakoma. Ni muhimu basi waandishi wa habari na sisi wananchi kwa ujumla tubadilike tuanze kumwambia rais wetu ukweli.
Tunapomsifu Rais Kikwete kwa kuwa amesema anakasirishwa na kuhuzunishwa sana na ufisadi na kwa kuwa amewatoa kafara watu kama akina Ballali ambao ni wagonjwa na walishajiuzulu kazi zao, tunashangilia mafanikio hewa.