lf.bevel
MWANZO CHAMA SERA KATIBA TUUNGE MKONO UCHAGUZI TUWASILIANE
banner

28 Novemba 2007

Kamati ya Madini ikajifunze kwa Hugo Chavez, Venezuela

na
Kitila A. K. Mkumbo

TANGU Rais Kikwete aunde Kamati ya Madini, kumejitokeza mjadala juu ya umuhimu wa kamati hiyo na uhalali wa baadhi ya wajumbe wanaoiunda.

Mjadala huu kwa kiasi kikubwa umesababishwa na kuongozwa na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).

Msingi mkuu wa mjadala huu, ni ushiriki wa Mhe Kabwe Zitto katika kamati hii.

Wapo wanachama wa CHADEMA kwa nia nzuri walipinga kushiriki kwa Zitto katika kamati hii kwa kuona kuwa kuteuliwa kwake ni janja ya Rais Jakaya Kikwete na Chama cha Mapinduzi (CCM) katika kujaribu kumziba mdomo baada ya kuinyima usingizi CCM na serikali yake kwa muda sasa.

Kwa haraka haraka, ni rahisi kuona mantiki ya wale waliokuwa wanapinga ushiriki wa Zitto katika kamati hii. Hata hivyo, kwa wale wafuatiliaji wa mafundisho ya Kikristo (pengine na Uislamu pia), watakubaliana nami kuwa majaribu katika imani si dhambi, dhambi ni kukubali kuangushwa na majaribu. Mtu jasiri haogopi kujaribiwa, bali hujazatiti kuhakikisha kuwa anashinda majaribu ya dhambi.

Hivyo, kama Rais Kikwete amemuwekea Zitto mtego wa kisiasa, kinachotakiwa ni yeye kugundua mtego huo na kuutegua bila kunasa. Hawezi kuugundua wala kuutegua mtego huo kwa kuukimbia. Tunashukuru kwamba busara imetawala kikao cha kamati kuu ya CHADEMA, ambacho kiliamua kwa usahihi kabisa kuwa Zitto aendelee kushiriki katika kamati.

Naamini Kamati Kuu ya CHADEMA ilimpa tahadhari za kutosha Zitto ili kuhakikisha kuwa anashinda majaribu yoyote yatakayojikeza katika mchakato wa shughuli za kamati hii.

Kuna mambo mawili muhimu ya kujifunza kutokana na sakata lililotokea katika uundwaji wa Kamati ya Madini.

Kwanza, Watanzania sasa wameanza kuuchukulia upinzani kwa umakini mkubwa kuliko wakati mwingine wowote tangu mfumo wa vyama vingi uanze hapa nchini. Kwa muda mrefu, chama pekee ambacho mikutano ya vikao vyake ilikuwa inakuwa ni habari kubwa katika vyombo vya habari na mazungumzo ya kawaida, kilikuwa ni CCM.

Kwamba karibu wiki nzima iliyopita kurasa za mbele za magazeti karibu yote isipokuwa yale ya CCM, zilitawaliwa na habari za kikao cha Kamati Kuu ya CHADEMA, ni hatua nyingine muhimu katika kukubalika kwa upinzani hapa nchini.

Pili, kama kweli Rais Kikwete aliunda Kamati ya Madini kama njia ya kutuliza lengo lake hilo, litatimia. Jambo lililo bayana ni kuwa wananchi walio wengi wameipa uzito mkubwa na wana matarajio makubwa sana na kamati hii.

Huu ni ujumbe pia kwa Mwenyekiti wa Kamati, Mark Bomani, kwamba wananchi wanatarajia kamati iibue maswali na majibu ya maana yanayohusu sekta ya madini ili hatimaye taifa hili lianze kufaidika na rasilimali zake.

Kwa kuwa swala la ushiriki wa Zitto kwenye kamati limeshatolewa majibu na CHADEMA, tunataraji sasa kamati itaanza kazi yake bila bughudha. Tukiwatakia kila la heri katika kazi hii, tunawajibika pia kuwashauri pale tunapoona inafaa. Nami kupitia makala haya, napenda kuishauri kamati hii ya Bomani ikajifunze kwa Hugo Chavez.

Labda kwa wale wasiomjua Chavez, nitamweleza kidogo na kufafanua kwa nini nafikiri kamati hii ya Bomani inaweza kufaidika katika kazi zake kwa kwenda kujifunza kwake.

Chavez ni Rais wa Venezuela aliyechaguliwa kwa mara ya kwanza mwaka 1998. Alichaguliwa tena mwaka 2000 na 2006. Venezuela ni moja ya nchi duniani zenye kuzalisha mafuta kwa wingi, lakini kabla ya Chavez kuwa rais, mafuta haya yalikuwa yanawafaidisha watu wachache, wakiwemo viongozi wa serikali na kampuni za kigeni.

Katikati ya utajiri wa mafuta, wananchi wa Venezuela walikuwa ni maskini wa kutupa, jambo ambalo lilizusha hasira kubwa miongoni mwa jamii na hii ndiyo ikawa turufu ya kampeni za Chavez.

Kwa hivyo kampeni za uchaguzi za Chavez zilikuwa na ajenda moja, nayo ni kuhakikisha kuwa Venezuela inatumia utajiri wa mafuta kwa kutokomeza umaskini, maradhi na magonjwa miongoni mwa wananchi wake badala ya kufaidisha kampuni za wazungu kutoka Ulaya na Amerika. Chavez alitunza na kutekeleza ahadi yake baada ya kuchaguliwa kuwa rais chini ya falsafa ya demokrasia ya kijamaa (democratic socialism).

Hivyo, kazi ya kwanza aliyoifanya Rais Chavez mara baada ya kuapishwa ni kubadili sera na sheria ya uvunaji wa mafuta kwa kuipa serikali kwa niaba ya wananchi asilimia kubwa ya umiliki wa visima vya mafuta badala ya kampuni binafsi ambazo nyingi zilikuwa za nchi za magharibi.

Mabadiliko ya sera na sheria za mafuta nchini Venezuela, ndio ikawa mwanzo wa neema kwa wananchi wa nchi hiyo na mwanzo pia wa ugomvi kati ya Chavez na mataifa ya magharibi, yakiongozwa na Marekani.

Matokeo ya falsafa na sera za Chavez ni kwamba, kipato cha wananchi wa Venezuela kimeongezeka kwa asilimia 130, asilimia 91 ya wananchi wanapata maji yaliyo safi na salama na kila mwananchi anapata huduma za afya zilizo bora kwa kiwango cha kimataifa bure.

Wakati anaingia madarakani kulikuwa na madaktari wapatao 1,628, lakini sasa kuna madaktari 19,571 ikiwa ni ongezeko la zaidi ya mara kumi katika kipindi cha chini ya miaka kumi! Utajiri wa mafuta ambao ulikuwa unawafaidisha wachache, sasa unawafaidisha wananchi wote wa Venezuela, ambayo ni malipo ya kura zao walizompigia Chavez mwaka 1998.

Mafanikio makubwa ya Chavez wa Venezuela hayakuwafurahisha wakubwa wa duniani. Marekani imeongoza nchi za magharibi kupinga utawala wa Chavez kwa nguvu zote. Mataifa haya yamefadhili kupinduliwa kwa Chavez mara mbili, na safari zote hizi yameshindwa, si kwa nguvu za jeshi la Venezuela, bali kwa nguvu za wananchi wa nchi hiyo.

Upinzani wa Marekani na mataifa mengine ya magharibi unatokana na uamuzi wa Chavez kutumia utajiri wa mafuta kwa ajili ya wananchi wake badala ya kampuni zao za kibepari. Kimsingi Chavez amekuwa mpinzani mkubwa wa falsafa ya utandawizi na ubeberu (imperialism), mambo ambayo viongozi wetu wamekuwa wakiyatetea kwa nguvu zao zote.

Ninaamini Kamati ya Madini kama wapo makini wana jambo la kujifunza kutoka Venezuela, nalo ni hili, ni kwa namna gani Chavez aliweza kushinda nguvu ya ubeberu hata akaweza kurudisha utajiri wa mafuta mikononi mwa wananchi.

Tunaomba Kamati ya Madini kama wapo “serious” na kazi hii waliyopewa, wakajifunza ya Venezuela, kuna kitu wanaweza kujifunza ambacho kinaweza kikawa jawabu kwa kitendawili cha madini hapa kwetu.

Tunatarajia watupe jibu la namna ambavyo nchi yetu inaweza kujikwamua na minyororo ya mabeberu ili kuirudisha ardhi ya madini mikononi mwetu mapema iwezekanavyo kabla madini yenyewe hayajaisha kabisa.

Rais Kikwete pia ana jambo la kujifunza kwa Chavez. Kwanza, Rais Kikwete na Chavez wana mambo mengi yanayofanana. Kikwete kama alivyo Chavez, alianzia kazi kama afisa wa jeshi kabla ya kuingia katika siasa. Vilevile, kama ilivyokuwa kwa Chavez aliyeingia madarakani kwa turufu ya kuhakikisha Venezuela inafaidika na mafuta ya nchi hiyo, Kikwete naye aliingia madarakani kwa turufu ya kuwa angehakikisha nchi inafaidika na madini. Cha muhimu zaidi, falsafa za chama cha Chavez na cha Kikwete katika maandishi zinafanana, yaani ujamaa na vyama vyao wote wawili vinajiita vya kimapinduzi.

Zipo pia tofauti za wazi. Kwanza, wakati Chavez anatekeleza kwa vitendo yale aliyoaidi na yaliyomo katika nyaraka za chama chake, Rais Kikwete bado amebaki mwenye maneno mengi na vitendo haba na haelekei kama atafanikiwa kutekeleza ahadi yake ya kuhakikisha nchi inafaidika na madini.

Pengine kuunda Kamati ya Madini, ni hatua muhimu ya kujaribu kutekeleza nia yake kabla ya uchaguzi wa 2010 ambapo itabidi atupe hesabu za utekelezaji wa ahadi zake.

Pili, wakati Rais Chavez ni mpinzani mkubwa wa sera za Marekani, Rais Kikwete ametokea kuwa kipenzi kikubwa cha Marekani na nchi zingine za magharibi na sera zake zote!

Kama kweli Rais Kikwete ana nia ya kutekeleza ahadi zake, hasa ya kuhakikisha madini na rasilimali zinaifaidisha nchi, itapidi aangalie tena kupendwa na kuwapenda hawa wakubwa wa dunia.

Namkumbusha maneno ya mwanazuoni maarufu wa Kimarekani, Profesa Noam Chomsky, ambaye katika kitabu chake cha ‘Imperial ambitions’, anaonya kuwa ukiona Marekani inamsifia kiongozi wa nchi yeyote inayoendelea, ujue kuwa kiongozi huyo hatekelezi wajibu wake katika nchi yake sawasawa!

Chomsky anaonya kuwa, viongozi wengi wa dunia ya tatu waliopendwa sana na mataifa ya magharibi na hasa Marekani, walishindwa kutekeleza majukumu yao katika nchi zao na mwisho wa yote waligeuka kuwa maadui wakubwa wa wapiga kura wao.

Rais Kikwete itabidi afike mahala achague, ama awe ni rafiki mkubwa wa Marekani na washirika wake au awe rafiki wa wananchi wake. Kwa hakika hawezi kupata vyote viwili kwa kuwa malengo yao hayafanani. Uchaguzi ni wake.

Kama kawaida yangu, namalizia makala haya kwa kutoa ujumbe kwa wananchi wenzangu. Ukombozi wanaoupata wananchi wa Venezuela chini ya kiongozi wao mahiri, Chavez, umetokana na kura zao. Kama kweli tunakerwa na kuchoshwa na yanayoendelea katika utawala wa CCM, tujue kuwa hakuna wa kutukomboa na madhila haya isipokuwa kura zetu.

Historia inatuonyesha kuwa, hakuna sehemu hapa duniani ambako walipata mabadiliko ya kweli ya kiuchumi na kimaisha kwa ujumla bila mabadiliko ya kweli katika nyanja ya siasa.

Kwa hivyo tujiweke tayari kufanya mabadiliko makubwa na ya kweli katika siasa za nchi yetu ifikapo mwaka 2010 na mengine yote yataongezewa.

 
lf.curl lf.curl2 rt.curl2 rt.curl