lf.bevel
MWANZO CHAMA SERA KATIBA TUUNGE MKONO UCHAGUZI TUWASILIANE
banner

21 Novemba 2007

Sumaye na CCM wametushtua

na
Kitila A. K. Mkumbo

TAKRIBAN wiki mbili zilizopita Chama Cha Mapinduzi (CCM) kilikamilisha uchaguzi wa ndani wa chama hicho. Kuna matukio mengi yaliyojiri katika uchaguzi yatakayoendelea kuumiza vichwa vya wanazuoni na wafuatiliaji wa mambo ya siasa kwa muda mrefu ujao.

Tukio moja la aina yake ni ukweli kwamba CCM imeendelea kuwa chama pekee katika ulimwengu wa demokrasia bado kinachoendelea kuchagua viongozi wake kwa mtindo wa kikomunisti wa kura ya ndiyo au hapana.

Haiyumkini pia kwamba wajumbe wa Halmashauri Kuu ya chama hiki ambao wote ni watu wazima, tena wenye upeo wa juu kabisa wa kuelewa mambo, wanakaa siku mbili kwenye kikao kwa ajili ya kubariki majina ya wajumbe wa Kamati Kuu wote walioteuliwa na mtu mmoja.

Ndiyo maana watu wengine wanaoamini katika mambo ya uchawi wanasema hawa wenzetu katika CCM ‘wamepigwa juju’; vinginevyo ni vigumu katika akili ya kawaida kukubaliana na mambo yanayoendelea katika CCM hasa mtindo wa kuchagua viongozi.

Hata hivyo makala yangu hii haina lengo la kujadili mchakato wa uchaguzi katika CCM. Hili nawaachia wenye chama hicho. Ninachotaka kujadili leo ni kung’atuka kwa Mzee John Malecela kutoka katika uongozi wa CCM na jinsi alivyoshindwa kutumia nafasi yake katika CCM kukamilisha utabiri mmojawapo wa Mwalimu Myerere.

Labda niseme tu hapa kuwa sina uhakika kama Mzee Malacela aling’atuka au Mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya Kikwete, hakumtaka aendelee kuwa makamu mwenyekiti wa chama hicho.

Nasema hivi kwa sababu hatujawahi kumsikia Mzee Malecela akitangaza kwamba alikuwa na mpango wa kuachia madaraka aliyokuwa nayo. Tulichoshuhudia ni kutokumuona Malecela katika orodha mpya ya vigogo wa CCM. Hata hivyo ili tumsaidie Malecela kupumzika kwa amani baada ya utumishi wa miaka mingi, ngoja tujifanye kwamba aliomba kung’anuka mwenyewe pamoja na kwamba chama chake kilikuwa bado kinamuhitaji!

Mwalimu Nyerere katika uhai wake alitabiri mambo mengi. Moja ya utabiri unaokumbukwa na kusubiriwa sana utimie ni ule unaohusu kugawanyika kwa CCM. Mwalimu Nyerere aliamini kwamba upinzani wa kweli hapa nchini ungepatikana kutoka ndani ya CCM.

Kwamba CCM ingegawanyika katika makundi mawili; kundi moja lingekuwa ni CCM ya sasa yenye kukumbatia ubepari uchwara unaongozwa kwa kiasi kikubwa na viongozi wa chama hicho na serikali.

Kundi la pili lingekuwa ni CCM asili yenye wanachama wa aina ya Makwaia wa Kuhenga ambayo ingebaki na misingi iliyokianzisha chama hiki ya Ujamaa na Kujitegemea. Bahati mbaya Mwalimu Nyerere alifariki bila kuona utabiri wake huu ukitimia.

Swali la kujiuliza sasa ni kwa nini utabiri huu wa Mwalimu hadi leo umeshindikana kutimia tofauti na tabiri zake nyingi zingine? Inawezekana kuna sababu nyingi. Kwangu mimi sababu moja ya msingi ni kukosekana kwa ujasiri miongoni mwa wana CCM wasiokubaliana na mambo yanavyoendelea katika CCM ya leo.

Sina shaka kabisa katika moyo wangu kuwa kama kuna mtu aliyepaswa kusababisha utabiri wa Mwalimu Nyerere utimie kwa maana ya CCM kuvunjika vipande viwili ni Mzee John Malecela. Nitaeleze mlolongo wa matukio matatu yanayomhusu mzee Malecela katika kujenga hoja yangu hii.

Mapema Desemba 1994, Rais Ali Hassan Mwinyi alibadilisha baraza lake la mawaziri. Katika mabadiliko hayo alimtoa Mzee Malecela katika nafasi ya uwaziri mkuu. Sababu za msingi za kumtoa Malecela katika nafasi ya uwaziri mkuu ilikuwa ni kile kilichoelezwa kushindwa kwake kuzuia hoja ya kuundwa kwa serikali tatu iliyoanzishwa na kikundi cha wabunge kilichojulikana kama G55.

Kimsingi shinikizo la kumtoa Malecela kwenye nafasi yake lilitoka kwa Mwalimu Nyerere kwa madai kwamba Malecela akiwa kama waziri mkuu na Katibu Mkuu wa CCM wakati huo, Marehemu Horace Kolimba, walimshauri vibaya Rais Mwinyi kuhusu suala la kuanzishwa kwa serikali tatu katika Jamhuri ya Muungano kinyume na sera ya CCM. Malecela alionyesha ukomavu wa hali ya juu wa kisiasa akakubali yaishe na akaendelea kubaki ndani ya CCM.

Haikuishia hapo. Katika uchaguzi wa kwanza wa vyama vingi wa mwaka 1995, Mzee Malecela ni miongoni mwa watu 13 waliochukua fomu kugombea urais kupitia CCM. Malecela alikuwa ni mmoja wa wagombea waliokuwa na nguvu na waliotarajiwa kutoa ushindani mkali na hata kushinda nafasi ya kugombea kupitia CCM na hatimaye kushinda urais.

Hata hivyo, katika mazingira ambayo hadi leo hatujawahi kuelezwa, jina la Malecela liliondolewa na halikupelekwa katika vikao vya CCM kwa ajili ya utaratibu wa kawaida. Minong’ono iliyopo ni kwamba jina la Malecela liliondolewa kwa maelekezo ya Mwalimu Nyerere aliyetamka wazi wazi kabisa kuwa “kama jina la John lipo, nitarudisha kadi ya CCM!” Hivyo Mzee Malecela alikosa nafasi ya kugombea kupitia CCM si kwa sababu ya kushindwa katika uchaguzi wa ndani ya CCM, bali kwa sababu hakutakiwa na baadhi ya viongozi katika chama chao.

Pigo la mwisho kwa Malecela lilikuja kumpata mwaka 2005. Safari hii tena ‘mzee wa watu’ alichukua fomu akija na mtindo maarufu wa kampeni uliojulikana kwa jina la tingatinga. Malecela alifanya kampeni nzuri na ya kistaarabu kabisa ikilinganishwa na wagombea wengine. Alionekana kuwa na wafuasi wa kutosha kiasi cha kupata ushindi wa kuwa mgombea kupitia CCM.

Kwa mshangao wa wafuasi wake ndani ya CCM na wafuatiliaji wa mambo ya siasa Tanzania, jina la Malecela liliondolewa na wala halikufikishwa katika vikao halali vya chama hicho ili lijadiliwe na hatimaye kupigiwa kura kama ilivyokuwa kwa wagombea wengine.

Kuna tetesi kwamba Mzee Malecela alikata rufaa ambayo hata hivyo haikusikilizwa! Tukumbuke kwamba haya yote yakimpata mzee wetu huyu alikuwa ni Makamu wa Mwenyekiti wa CCM. Mwisho wa yote, Malecela alikubali yaishe na akaendelea kubaki kuwa makamu wa mwenyekiti wa CCM. Hata hivyo, safari hii angalau alichukua hatua kidogo kwa kujiuzulu ukamanda wa Umoja wa Vijana wa CCM. Lakini hili ni tukio ambalo halikuwa na athari zozote kisiasa kwa CCM na nchi kwa ujumla.

Nimetoa mlolongo wa matukio yote haya ya kisiasa yanayomhusu Malecela katika kujenga hoja yangu kuwa Malecela alikuwa ni mfungwa wa kisiasa katika CCM. Kwa kweli alikuwa ni Messiah asiyetakiwa. Kwa hali ya kisiasa aliyokuwa nayo Malecela ndani ya CCM, ndiye hasa aliyepaswa na pengine ambaye Mwalimu Nyerere alimtarajia akamilishe utabiri wake wa kugawanyika kwa CCM.

Ni muhimu kukumbusha hapa kuwa pamoja na matatizo yote aliyokuwa nayo Mzee Malecela katika maisha yake ya kisiasa, hajawahi kuhusishwa na ufisadi au ubadhirifu wowote wa mali ya umma wala kuwa na utajiri wa kutilia shaka kama ilivyo kwa viongozi wengi katika CCM.

Na hii ndiyo hasa iliyokuwa sifa ya kiongozi wa CCM ya awali iliyotokana na TANU. Kwa hivyo, sina shaka kwamba Mwalimu Nyerere alimfanyia vituko vya kisiasa mzee mwenzake si kwa lengo baya au kwamba alikuwa hampendi, bali alitaka atoke katika CCM hii ya leo ya mabepari uchwara ili aiongoze ile CCM ya asili ya akina Makwaia wa Kuhenga.

Ni bahati mbaya kwamba Mzee Malecela ameondoka katika uongozi wa kisiasa bila kutekeleza hili ama kwa kuipenda mno CCM kuliko maendeleo ya kweli ya demokrasia nchini au kwa kukosa ujasiri wa kisiasa.

Wapo wanasiasa wengi wa aina ya Malecela katika CCM wanaoishi maisha yasiyo ya kwao. Naamini wapo wana CCM wanaotamani nchi yetu ipige hatua ya kweli katika demokrasia na maendeleo. Wapo wana CCM ambao msimamo wao kiitikadi, kifalsafa na kisera unagongana na ule wa chama chao cha CCM.

Hawa ni wale wana CCM ambao dhamira zao za ndani zinawasuta kwa kutoridhishwa na mwenendo wa mambo katika CCM na uongozi wa nchi, lakini wanaendelea kubaki katika chama hiki wakiamini katika dhana ya kuwa utawala wa mfalme huangushwa na wana wa mfalme.

Hawa ni wanasiasa ambao wamebaki CCM kimwili lakini kisaikolojia, kihisia na kiakili walikwishakuhama. Wanabaki CCM kwa kukosa ujasiri na kuthamini zaidi miili yao kuliko utu, utashi, imani na wito wa mioyo yao, na kwa kubaki kwao CCM wanaendelea kukwamisha ahadi ya Mwalimu Nyerere kama ilivyokuwa kwa Malecela.

Huo ndio ninaoita ufungwa wa kisiasa bila kujua, na ninaandika makala hii kuwasihi wana CCM wa namna hii kujinasua na kifungo walichomo na kuchukua hatua ya kijasiri kujiunga na vyama vya upinzani. Malecela naye bado ana nafasi katika hili kwa kuwashawishi na kuwaonyesha njia vijana wake aliowaacha katika CCM watoke ili wajiunge na majemedari wenzao katika vyama upinzani kuijenga demokrasia na kuleta mabadadiliko ya kweli hapa nchini.

Wana CCM wanaoitakia mema nchi yetu watakuwa wanajidanganya kufikiri kuwa uchumi wa soko huria unaoongozwa na msingi wa ushindani katika biashara, utafanikiwa bila kuwa na ushindani wa dhati katika nyanja ya siasa. Tunahitaji ushindani katika sekta ya kisiasa ili uweze kuchochea ushindani katika nyanja zingine. Ushindani wa kisiasa hauwezi kupatikana kama wanasiasa walio wengi katika nchi yetu wataendelea kubaki katika chama kimoja tu cha siasa ambacho ni CCM.

Niwahimizapo wana CCM kukiasi chama chao ninajua changamoto na hofu zinazowakabili katika kufikia uamuzi huu. Ninaamini kuna wana CCM wengi ambao wangependa kukihama chama chao na kujiunga na vyama vya upinzani, lakini wanatatizwa na mambo mengi yakiwemo hofu ya kupoteza kazi na umaarufu walio nao. Wapo pia ambao wamekuwa wakisema kuwa sio kazi rahisi kuitoa CCM madarakani kwa sababu CCM imekuwa sehemu ya maisha ya watanzania kwa muda mrefu.

Jibu langu kwa wote hawa ni kuwa mafanikio ya mwanasiasa makini hayapimwi kwa kufanya mambo rahisi. Mafanikio ya mwanasiasa hupimwa kwa kufanikisha mambo makubwa katika jamii ambayo yalikuwa yanaonekana katika macho ya wengi kuwa hayawezekani kama vile kuing’oa CCM madarakani.

Ipo dhana pia miongoni mwa wanasiasa wa Tanzania kuwa uasi wa vyama ni jambo baya na la aibu linaonesha usaliti. Hii ni dhana ya kweli tu pale ambapo uasi wa chama umetokana na ushawishi wa rushwa ya fedha au madaraka. Mimi binafsi siwaungi mkono wanasiasa wa aina ya akina Richard ‘Tambwe’ Hiza, Thomas Ngawaiya na Saidi Akwilombe ambao wamekuwa wakirudi CCM baada ya kupata umaarufu katika vyama vya upinzani.

Siwaungi mkono hawa kwa sababu wao wamekuwa wakivitumia vyama vya upinzani kama malisho ya kujinawirisha ili kukuza soko lao la kisiasa katika CCM, na kuna kila dalili kuwa uasi wa vyama vyao ulitokana na ushawishi wa rushwa ya fedha na/au madaraka.

Uasi wa vyama ninaoutetea mimi ni ule unaotokana na msimamo wa kisiasa uliojengwa katika misingi ya kiitikadi, kifalsafa na kisera. Uasi wa vyama unaotokana na misingi hii ni jambo la kawaida katika nchi zilizokomaa kidemokrasia. Mifano ya uasi wa vyama vya siasa katika nchi hizi ni mingi. Mwasisi wa uasi wa vyama vya siasa duniani ni aliyekuwa Waziri Mkuu wa Uingereza, Sir Winston Leonard Spencer Churchill (1874-1965).

Churchill alianza siasa akiwa mbunge wa chama cha kihafidhina (Conservatives) mwaka 1901, akaasi na kuhamia chama cha maliberali mwaka 1904 na kisha akakiasi tena chama cha maliberali na kurudi chama cha Conservatives mwaka 1925. Alibaki na chama hicho hadi alipopata uwaziri mkuu mwaka 1940.

Ipo mifano mingine. Mwaka 1993 Kiongozi wa Liberal Democratic Party (LDP) cha Japan alikiasi chama chake na kuanzisha chama kipya cha Shinseito kilichoshinda uchaguzi na kumaliza utawala wa miaka 38 wa chama cha LDP.

Mwaka 1967 Rais wa Chama cha National Congress cha India (INC), Indira Gandhi, alikihama chama chake na kuanzisha INC mpya ambayo ilikuja kuungana na chama cha Janata Party na kushinda uchaguzi wa mwaka 1977. Mifano ipo mingi hata hapa barani Afrika ikiwamo majirani zetu Kenya, Malawi, Zambia, Zimbabwe, n.k. Kimsingi siasa ya vyama vingi duniani imejengwa kwa wanasiasa kuhama kutoka chama kimoja kwenda kingine.

Kama nilivyosema awali katika makala hii wanasiasa wengi katika CCM ni wafungwa wa kisiasa kwa kuishi maisha yasiyo yao, kiimani, kiitikadi, kisera na kimsimamo. Wapo wengine ambao kuna kila dalili kwamba hawatakiwa na chama hicho lakini wanaendelea kung’ang’ania kwa kuthamini zaidi miili yao kuliko utu, utashi, imani na wito wao kisiasa. Maisha ya namna hii sio ya mwanasiasa; maisha ya kinafiki ni maisha ya mtu anayefanya kibarua maana yeye anachojali ni mshahara wake na sio kile anachokifanya.

Hamna kitu cha ajabu katika siasa kama kufanya jambo ambalo huliamini na hukubaliani nalo, lakini ukasahindwa kuchukua hatua kwa sababu tu ya kukosa ujasiri. Ujasiri wa kufanya maamuzi magumu ndiyo silaha kubwa ya mwanasiasa yeyote aliye makini. Nami nawasihi wana CCM walio makini katika siasa, kuwa na ujasiri wa kujiunga na vyama vya upinzani ili tujenge demokrasia ya kweli ya vyama vingi na tuweze kuleta mabadiliko ya kweli katika nchi yetu. Hii ndiyo iliyokuwa ndoto ya Mwalimu Nyerere na watekelezaji wake alitarajia watoke CCM. Wana CCM nimewakumbusheni msije mkasema tulisahau au hatukuambiwa.

 
lf.curl lf.curl2 rt.curl2 rt.curl