LEO najadili matukio mawili makubwa ya kisiasa ambayo yamejitokeza katika wiki ya mwisho ya mwezi Agosti 2007.
Kwanza, ninajadili mantiki ya kauli ya Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye, ya kwamba alikuwa hajui chanzo halisi cha umaskini wa Tanzania hadi alipokwenda kusoma shahada ya pili katika Chuo Kikuu cha Havard nchini Marekani.
Pili, ninajadili maana na athari za kuzagaa kwa rushwa na kuibiana kwa kura katika uchaguzi unaoendelea ndani ya chama tawala, Chama Cha Mapinduzi (CCM). Nitaanza na kauli ya Sumaye.
Nianze kwa kukumbusha jambo la wazi kuwa Frederick Sumaye alikuwa waziri mkuu katika Serikali ya Awamu ya Tatu chini ya Rais Benjamini Mkapa, kwa kipindi cha miaka kumi.
Ni waziri mkuu aliyekaa madarakani kwa muda mrefu zaidi kuliko wote tangu nchi yetu ipate uhuru. Kwa nafasi aliyokuwa nayo, Sumaye ndiye aliyekuwa kiongozi wa Serikali bungeni.
Kwa nafasi yake hiyo pia Sumaye alikuwa mjumbe wa Kamati Kuu pamoja na vikao vingine vyote muhimu vya kitaifa kupitia CCM.
Kamati Kuu ya CCM ndicho kikao chenye dhamana kubwa kabisa ya kutunga, kupitisha na kusimamia sera zinazotumika kuendesha nchi hii.
Kwa hiyo tathmini ya Sumaye kuhusu Serikali ya Awamu iliyopita ndiyo hasa tathmini ya fikra na utendaji wa serikali ya CCM!
Hebu turejee tena maneno ya Sumaye. Katika mahojiano yaliyochapishwa katika Gazeti la Sunday Citizen la tarehe 26 Agosti 2007, Sumaye, pamoja na mambo mengine, alikaririwa akisema kuwa, ninamnukuu, “Nilikuwa kipofu kwa nini umaskini ulikuwa hauishi Tanzania na Afrika kwa ujumla, lakini sasa naweza kuelewa sababu za mateso yetu.”
Sumaye aliendelea kusema kuwa: “Wakati wa uongozi wangu, nilikuwa nashangaa kwa nini, pamoja na juhudi zote ambazo tulizifanya katika serikali pamoja na misaada kutoka kwa wafadhili, bado nchi yetu iliendelea kuwa maskini na hali ya maisha ya watu wetu iliendelea kuwa mbaya, lakini sasa naweza kuelewa tatizo ni nini hasa.”
Katika mang’amuzi yake Sumaye anasema amegundua kuwa bila kuwawezesha wananchi kiuchumi ili waweze kushindana kibiashara ndani na nje ya nchi, kamwe hatutaweza kuumaliza umaskini.
Sumaye alieleza pia kile Gazeti la Sunday Citizen lilikiita kutoa siri, kuwa haifai kusafirisha mali ghafi; badala yake ni muhimu sana kusafirisha bidhaa zilizotengenezwa hapahapa nchini.
Kwa maana nyingine, Sumaye alikuwa anaongelea umuhimu wa kuwa na viwanda vya ndani na kwamba bila kuwa na viwanda haiwezekani kupata maendeleo ya maana ya kiuchumi.
Kwa maneno mengine ambacho Sumaye amegundua kwa kuchelewa sana ni kuwa maendeleo ya kweli yanapatikana kwa uzalishaji badala ya uchuuzi wa bidhaa za watu wengine kama ilivyo sasa.
Kuna mambo mawali ya kujadili katika huu ung’amuzi wa waziri wetu mkuu mstaafu. Kwanza kile ambacho Sumaye anakiita ni ung’amuzi kutoka Chuo Kikuu maarufu cha Harvard ndicho hicho ambacho wataalamu wa uchumi, wanazuoni na wanaharakati wa mambo ya jamii wa nchini mwetu wamekuwa wakikisema miaka nenda rudi pasipokusikilizwa na kina Sumaye na viongozi wenzake.
Sumaye ametuthibitishia kwa mara nyingine kuwa viongozi wetu bado hawajiamini na hawawaamini wataalamu wao wa ndani na wanasikia tu pale wanapoambiwa jambo na Wazungu.
Sumaye hakuhitaji kwenda hadi Harvard ili kujua jambo rahisi linalofundishwa katika somo la Uchumi kidato cha tano na sita kuwa uzalishaji wa mali ndio msingi wa kukua kwa uchumi na kumaliza umaskini badala ya uchuuzi wa bidhaa za nje ambao yeye na viongozi wenzake waliubebea mbeleko.
Laiti Sumaye angekuwa ameenda Harvard kabla hajawa waziri mkuu na baadaye akaja akaupata uwaziri mkuu, pengine tusingeuza viwanda vichache ambavyo Mwalimu Nyerere aliviacha.
Jambo la pili ambalo linaibuka kutokana na kauli ya Sumaye ni ukweli kwamba uwezo wa kifikra wa Sumaye ni kiwakilishi cha uwezo wa viongozi wa serikali ya CCM.
Kama nilivyosema awali, Sumaye alikuwa mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM na kwa hivyo muono aliotueleza ni muono wa Kamati Kuu ya CCM na CCM kwa ujumla.
Ndio kusema nchi hii imeongozwa kwa miaka kumi na viongozi ambao walikuwa hawajui wanachokifanya walipokuwa madarakani!
Sote tunatambua kuwa hatua ya kwanza ya kutatua tatizo ni kugundua chanzo cha tatizo. Hata daktari hawezi kuanza kumtibu mgonjwa kabla kwanza hajajua chanzo cha ugonjwa wenyewe.
Sasa kama kina Sumaye walikuwa hawajui chanzo cha umaskini wa nchi yetu, maana yake walikuwa wanatibu ugonjwa ambao walikuwa hawaujui!
Ndiyo kusema kuwa kama ingekuwa ni safari Watanzania tumejikuta tumepanda basi ambalo haliendi tunakoelekea. Kama tungekuwa tunakwenda Dodoma, tumejikuta tumo katika basi linalokwenda Mtwara; kwa hakika hatutafika Dodoma kamwe!
Pengine kibaya zaidi ni ukweli kwamba uongozi wetu wa sasa uliingia madarakani bila ajenda. Hii inatokana na ukweli kwamba wao walisema watayaendeleza yaleyale waliyokuwa wakifanya kina Sumaye kwa kasi mpya! Ndiyo kusema hawa nao wanajaribu kutibu ugonjwa wasiojua chanzo chake!
Haishangazi basi kwamba tunashuhudia mambo yakifanyika katika utawala huu bila kujua hasa falsafa yake ni nini. Kwa mfano, kwa sasa kuna kile kinachoitwa “mabilioni ya Kikwete” ambapo mapesa mengi yanagawiwa kwa wananchi huko mikoani.
Cha kujiuliza, hivi walioibuka na utaratibu huu wametumia falsafa gani hasa ya kiuchumi? Hivi ni nchi gani hapa duniani iliweza kumaliza umaskini kwa kuwagawia wananchi wake pesa?
Jambo la pili ambalo linafanana kimaudhui na kauli ya Sumaye ni vituko vya uchaguzi wa CCM. Katika uchaguzi unaoendelea tumeshuhudia kuzagaa kwa rushwa, kuibiana kura na kuchomekeana wapiga kura bandia kunakofanywa na wagombea wa nafasi mbalimbali na wafuasi wao.
Hili la rushwa katika uchaguzi wa CCM linatafsiri kubwa mbili. Mosi, CCM hawajiamini tena; kwamba wagombea hawana njia nyingine ya kuwashawishi wanachama wenzao wawachague isipokuwa kwa kutumia pesa. Na wanachama nao hawaoni cha maana ambacho wagombea watawafanyia zaidi ya kujinufaisha wao binafsi na madaraka wanayoyapata, hivyo wanaona wana haki ya kuuza kura zao.
Pili, pengine sasa wale ambao wamekuwa wakikataa kwamba CCM hushinda uchaguzi kwa rushwa na wizi wa kura wataanza kuelewa.
Kwa miaka mingi tangu mfumo wa vyama vingi uanze, wapinzani wamekuwa wakilalamika kwamba CCM wamekuwa wakiiba kura kwa kusaidiwa na Tume ya Uchaguzi dhaifu na iliyojaa makada wa CCM.
Hata hivyo kuna watu ambao wamekuwa wakibisha sana juu ya jambo hili. Sasa cha kujiuliza kama CCM wanaibiana kura wao kwa wao katika kutafuta uongozi wa kuwa kada wa chama hicho, inawezekanaje wawe waaminifu katika uchaguzi unaohusu madaraka ya dola?
Kama CCM leo wanapandikiziana wapiga kura bandia, inawezekanaje wale wanaopata nafasi ya kuingia katika serikali na kusimamia chaguzi za kupata viongozi wa dola wawe waaminifu?
Tukumbuke kwamba maadam CCM ndiyo chama tawala, hawa viongozi wanaochaguliwa kwa rushwa ndio haohao wanakwenda kuwa viongozi wa serikali.
Sasa cha kujiuliza hapa ni kuwa kama mtu amepata uongozi wa CCM kwa kununua, inawezekanaje akwepe kununua uongozi wa serikali na kama Mwalimu Nyerere alivyowahi kuuliza, atakapoupata huo uongozi kwa kununua, atarudisha hizo pesa?
Kama hao viongozi wa CCM hawawezi kudhibiti rushwa katika chama chao, watawezaje kudhibiti rushwa katika serikali?
Nihitimishe kwa kusema kwamba kama bado tunaamini kuwa umaskini ni adui mkubwa wa nchi yetu, kufuatia kauli ya Sumaye kwamba wao katika CCM walikuwa hawajui chanzo cha umaskini hadi alipokwenda kusoma Harvard, basi tukubaliane kuwa CCM wamepoteza uwezo, sifa na uhalali wa kuongoza vita dhidi ya umaskini.
Kwa kauli ya Sumaye, ni wazi kuwa hiki ni chama cha watu wenye uchu wa kushika madaraka ya dola lakini wasiojua wayafanyie nini hayo madaraka!
Vilevile tunaona kwamba CCM wamezoea mno kuiba kiasi kwamba wakikosa wa kumuibia wanaamua kuibiana wao kwa wao; yaani hii ni sawa na majambazi wanapoibiana zana za uhalifu ili majambazi wengine wakose zana hizo huku majambazi washindi wakibaki na zana na uwezo wa kuendeleza uhalifu!
Hii inaonyesha wazi kuwa CCM wamepoteza uwezo na sifa za kusimamia ujenzi wa demokrasia na utawala bora hapa nchini kwetu na umefika wakati sasa wa kuwanyang’anya dhamana ya kuongoza serikali. Hili ni jambo linalowezekana kama tukiamua; CCM si dini yetu na kuachana nayo si dhambi hata kidogo!