lf.bevel
MWANZO CHAMA SERA KATIBA TUUNGE MKONO UCHAGUZI TUWASILIANE

Oktoba 2005

Mbowe amejenga hoja, Ameeleweka, Tumpe Kura

na
Kitila A. K. Mkumbo
Dar es Salaam

Wataalamu wa saikolojia ya siasa (political psychology) hugawa wapiga kura katika makundi makubwa manne. Kundi la kwanza linajumuisha wale watu wanaomchagua mgombea kwa kuwa mgombea huyo anatoka nao chama kimoja. Hawa kwao hoja au haiba ya mgombea sio muhimu; muhimu kwao ni kwamba mgombea ni kada mwenzao. Kundi hili sio kubwa maana wengi wao ni makada wa vyama ambao kawaida sio wengi. Kundi la pili ni lile ambalo linamchagua mgombea kwa kufuata sera za chama chake na hoja za mgombea mwenyewe. Watu katika kundi hili huwa makini kusikiliza sera za chama na hoja za mgombea kwa jinsi ambavyo zitaboresha maisha ya wapiga kura binafsi, jamii, na Taifa kwa ujumla. Uwingi au uchache wa kundi hili unategemea umakini wa wanajamii, kiwango cha elimu miongoni mwa wapiga kura, na jinsi ambavyo wanaona uongozi wa kisiasa una athari katika maisha yao ya kila siku. Kwa maoni yangu kundi hili limeongezeka sana katika uchaguzi wa mwaka huu. Kundi la tatu linajumuisha wapiga kura ambao wanaangalia haiba ya wagombea na vinjonjo vinavyoambatana na kampeni zao. Hawa wanavutiwa na mambo kama sura ya mgombea, sare, burudani za ngoma, nyimbo, na dansi, umahiri katika matangazo na mambo kama hayo. Kwa kundi hili sera na hoja sio vitu vya msingi katika kuamua nani apigiwe kura. Kwa maoni yangu kundi hili katika uchaguzi huu limepungua sana. Kundi la nne linajumuisha watu ambao hupiga kura kwa mazoea. Hawa ni watu ambao kwao sera, hoja, au aina ya kampeni sio muhimu. Watu hawa watapiga kura kwa mgombea atokaye katika chama ambacho kimezoeleka kuchaguliwa. Hawa hawajihangaisha kusikiliza kampeni wala kufuatilia sera za vyama na hoja za wagombea kwa kuwa walishaamua kwa mujibu wa mazoea. Utasikia mara kwa mara wakisema mgombea fulani anajihangaisha bure, hawezi kupita kwa sababu mgombea fulani alishapita. Kundi hili pia linazidi kusinyaa kadri ambavyo watu wanaendelea kuuzoea na kuukubali mfumo wa vyama vingi.

Mimi ni miongoni mwa watanzania waliofuatilia kampeni za vyama na wagombea tangu kipenga kilipopulizwa na tume ya uchaguzi tarehe 21 Agosi 2005, na bahati nzuri sijasafari nje ya nchi tangu wakati huo. Nimepata nafasi pia ya kuhudhuria mikutano kadhaa ya kampeni za vyama na wagombea wao wa urais, hasa vyama vya CHADEMA, CUF, na CCM. Nimeshawishika kabisa kuwa kampeni za mgombea urais kupitia CHADEMA Freeman Mbowe zimetawaliwa na uibuaji wa hoja za msingi zinazohusu mustakabali wa nchi yetu sasa na miaka mingi ijayo. Katika makala hii nitachanganua baadhi ya hoja ambazo mgombea huyu ameziibua na kuwashawishi watanzania wenzangu wamchagua Freeman Mbowe na CHADEMA.

Msingi wa sera za CHADEMA na hoja za mgombea urais wake zimejengwa katika falsafa ya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere inayohusu vigezo vya maendeleo. Katika falsafa hii Mwalimu alitaja vitu vinne vinavyohitajika katika kuleta maendeleo ambavyo ni watu, ardhi, siasa safi na uongozi bora. Kuhusu watu, Mbowe anasema nchi yetu ina watu wa kutosha tena wenye nguvu na afya njema, akili, na vipaji lukuki. Wakati Mwalimu anatoa tamka hili Tanganyika (wakati huo) ilikuwa na watu wasiofikia milioni sita. Leo tupo watu karibu milioni thelathini na tano. Kuhusu ardhi, Mbowe anasema tunayo ardhi ya kutosha yenye ukubwa wa eneo lisilopungua kilomita za mraba 940,000. Ardhi hii imejaa kila aina ya raslimali kuanzia madini ya kila aina (almasi, dhahabu, Tanzanite, rubi, n.k.); wanyama, milima, misitu hadi maziwa, mito, mabonde, na rutuba yenye kustawisha kila aina ya mazao ya chakula na biashara. Mbowe anasema tatizo la nchi yetu ni kukosekana kwa siasa safi na kuongozwa na viongozi wasiopenda mabadiliko tena wenye fikra zilizoganda. Na hapa ndipo anapokuna watu wengi walio makini; walio katika lile kundi la pili ambalo nimelifafanua hapo awali.

Katika kutibu tatizo la kukosekana siasa safi, CHADEMA na Mbowe wamependekeza mfumo mpya wa utawala wenye kufuata kanda au majimbo badala wa sasa wa kugawanya nchi katika mikoa na wilaya. Katika mfumo mpya, nchi itagawanya katika kanda nane za utawala; kila kanda ikiwa na mamlaka kamili ya uongozi na umilikaji na uendelezwaji wa raslimali zilizopo katika eneo husika ikiwemo kukusanya mapato yatokanayo na hizo raslimali. Serikali kuu itachukua sehemu tu ya mapato kwa ajili ya shughuli za utawala katika ngazi ya Taifa na kusaidia maendeleo katika zile kanda ambazo raslimali zilizopo hazikidhi haja ya maendeleo katika eneo husika. Mfumu huu ndio unaotumika katika nchi nyingi duniani zenye ukubwa kama wa Tanzania. Hoja ingine ya Mbowe katika mfumo mpya ni kukomesha nafasi za kuteuliwa za wakuu wa mikoa na wilaya. Hoja yake ni kwamba wilaya nyingi hapa nchini zina majimbo ya uchaguzi zaidi ya moja. Kila jimbo lina mbunge na madiwani kadhaa. Isitoshe kila wilaya ina mkurugenzi wa halmashauri. Bahati mbaya sana hawa wakuu wa wilaya na mikoa wa kuteuliwa wana madaraka makubwa kuliko wabunge waliochaguliwa na wananchi. Kimsingi hawa hawana kazi za msingi zaidiya kutumika kuminya demokrasia na kutisha watu wenye mawazo tofauti na watawala na kwa kweli ni mzigo usio wa lazima kwa serikali.

Kuhusu tiba ya uongozi, Mbowe anasema ni muhimu tukumbuke tulipotoka. Nchi hii ilikuwa na misngi mitatu mikubwa nayo ni: uwezo wa kuamua mambo yetu wenyewe, heshima na usawa kwa binadamu wote, na amani na umoja. Sasa hivi hatuna uwezo tena wa kuamua mambo yetu wenyewe. Sera za nchi zinatungwa na wakubwa wa Benki ya Dunia na Shirika la Fedha la Kimataifa. Mikakati ya kuondoa umaskini inabuniwa na akina de Soto. Tumekuwa mabingwa wa kuibuka na misamiati kama wanamuziki wa bongo fleva; mara mkukuta mara mkurabita. Mbowe anasema lazima turudishe heshima ya nchi ya kujiamulia mambo yake yenyewe ambao ndio msingi wa uhuru wetu. Kwa sababu ya kuukubali mfumo wa vyama vingi kwa shingo upande, sasa tunatengana kwa minanjili ya vyama vya siasa; wewe CUF, mimi CHADEMA, yule CCM. Matokeo yake tunabomoana na kulibomoa taifa pia. Mbowe anasema UTAIFA kwanza vyama baadaye. Mbowe pia anahimiza maadili katika uongozi wa nchi. Anasema sio vizuri kuendelea kudanganya wananchi kuwa nchi ipo katika mfumo wa siasa ya ujamaa na kujitengema wakati kila tufanyalo ni la kubariki ubepari na ubeberu. Viongozi wa CCM wanapiga ngoma ya ujamaa na kucheza kibebari. Mbaya zaidi uongo hu umetaasisiwa (institutionalized) katika katiba ya nchi. Huku ni kukosa ujasiri wa kusimamia wanachokiamini na kukitenda.

Kwa maoni yangu Mbowe amejenga hoja ya msingi na ameeleweka. Ameibua hoja za Mwalimu Nyerere amabazo CCM walishazitupa siku nyingi. Amepania kulijenga Taifa la watu wenye kupendana na kutanguliza utaifa wao badala ya vyama na nafsi zao. Hakuna mgombea mwingine anayehubiri haya zaidi ya Mbowe. Wagombea wengine wameamua kujikita katika kumjadili Mbowe na Helikopta badala ya sera za vyama vyao. Wameonyesha udhaifu mkubwa wa kufikiri na kujenga hoja, wanaegemea zaidi kwenye haiba na mbwembwe za kampeni kwa minajili ya dansi na mabango. Watanzania sasa hivi wameamuka; wanataka kusikia sera na hoja. Na hawaamini tena kuwa mfumu wa vyama ni uadui. Chama sasa hivi hakibebi mtu ila mtu anakibeba chama kwa uwezo wake wa kujenga hoja; hiyo ndio siasa safi. Ndio maana mimi kura yangu nitampa MBOWE Freeman mwana wa CHADEMA! Wewe je?

 
lf.curl lf.curl2 rt.curl2 rt.curl