lf.bevel
MWANZO CHAMA SERA KATIBA TUUNGE MKONO UCHAGUZI TUWASILIANE
banner

2 Juni 2006

CHADEMA imebeba Utume wa kizazi kipya

na
Mwanaidi Abdalah

Mwanazuoni Franz Fanon anasema “ Kila kizazi nje ya vikwazo mbali mbali mbali lazima kitambue utume wake na ni aidha kiutekeleze au kiutelekeze”. Msemo huo ni maarafu sana katika duru za harakati za vijana Tanzania.

Unatumiwa mara kwa mara na waraharakati vijana na hata wanasiasa wa kizazi kipya katika kusisitiza juhudi za vijana katika kulitumikia taifa lao. Kwa siku za karibuni, msemo huu umekuwa ukiendelea kusikika zaidi katika duru za Chama kinachokuwa kila uchao, Chama cha Demokrasia na Maendeleo kwa kifupi CHADEMA. Hii ni kutokana na CHEDEMA kusheheni wanasiasa wapya, wanasiasa wenye mtazmo mpya, wanasiasa wa kizazi kipya.

Huwa inasisitizwa kwamba, kizazi cha kina Nyerere na wenzake kilikuwa ni kizazi cha uhuru. Utume wake ulikuwa ni kulikwamua taifa taifa toka kwenye makucha ya ukoloni.

Nyerere na wenzake walibeba jukumu hili kwenye mabega yao na hatimae kulipatia taifa uhuru. Kizazi kipya nacho nje ya ukoloni mambo leo kina jukumu la kuliondoa taifa katika makucha ya umaskini, ambapo sehemu kubwa ya umaskini huu ni wa kijitakia.

Makala haya yanafafanua ni kwanini CHADEMA inaendelea kuvutia wanaharakati wengi vijana kwa kulinganisha na Chama Tawala, chama cha mapinduzi, yaani CCM.

Tofauti na vyama vingine vya upinzani. CHADEMA ni tokeo la kukuwa kitaasisi na juhudi za wanachama wake katika kujiendeleza. Baadhi ya vyama vya upinzani viliibuka na kupata umaarufu miaka ya tisini kutokana na wanasiasa mbalimbali maarufu kuhama kutoka CCM na kujiunga na kambi ya upinzani. Umaarufu wa wanasiasa hawa uliambukiza umaarufu wa baadhi ya vyama vya upinzani.

Hivyo ukuaji wa ghafla wa vyama hivi haukuwa ni tokeo la vyama kukua kitaasisi na kimkakati. Ulikuwa ni mlipuko, umaarufu wake ulitokana na umaarufu wa watu binafsi na si ukuaji wa kitaasi na uwezo wa kubuni sera mbadala. Ulikuwa ni mlipuko,ukuaji wa puto ambao ulikuja kupasuka kutokana na wanasiasa hawa kushuka umaarufu na migogoro katika vyama husika.

Hali kadhalika CCM, umaarufu wake na nguvu zake umejengeka kihistoria na kuendelea kufaidika na matumizi mabaya ya dola, katiba dhaifu isiokidhi matakwa na mahitaji ya kidemokrasia tuliyo nayo sasa pamoja na tume dhaifu ya uchaguzi.

Nguvu hizi ni za mda, si za kudumu. Kadri ambavyo kizazi kipya kinavyozidi kuchukua nafasi yake katika duru za uongozi, iwe serekalini, CCM au vyama vya upinzani, na kadri mwamko wa watanzania unavyoongezeka juu ya demokrasia na utawala bora, nguvu za CCM ambazo ni katiba na tume dahifu ya uchaguzi zitatoweka. Kizazi kipya chenye kiu ya mabadiliko hakitakuwa na simile katika mambo haya, Ni hili si suala la itikadi ni kukidhi mahitaji ya muda tulio nao.

Kinyume na hali hii, Ukuaji wa CHADEMA umekuwa wa kitaasi zaidi na uwezo wake wa kujenga sera murua. Itakumbukwa hata baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Nyerere aliwahi kutamka hadharini akisifia ubora wa sera mbadala za CHADEMA. Pamoja na hayo, wanasiasa mahiri wa CHADEMA wanaofamika na kupendwa, umaarufu wao umetokana na juhudi za kujendeleza binafsi wakiwa ndani ya CHADEMA.

Hapa unaweza kuchululia mfano wa MwenyekitI wa Taifa wa CHADEMA, Freaman Aikaeli Mbowe, ama Mtu huru kama mashabiki wake wanavyopenda kumuita. Umaarufu wake wa kisiasa hakutokana na yeye kuwa mwanaCCM aliehama, bali jitihada binafsi na kukomaa kwa dhamira yake katika kuleta mabadiliko nchini. Sasa amejitokeza kama mwanasiasa mwenye mvuto na mwenye uwezo mkubwa sana wa kujenga hoja.

Inaaminika, katika wanasiasa waliopo nchini kipindi hiki, hakuna anaemkaribia mtu huru katika kujenga hoja kwa mvuto wa hali ya juu. Ndio maana hata wasikilizaji wa CLOUDS FM katika kipindi cha “power breakfast” kinachoongzwa na watangazaji mahiri wa kizazi kipya, Fina Mango na Masoud Kipanya, walimpigia kura nyingi Mtu Huru na hivyo kuongoza kati ya wanasiasa wenye mvuto akimuacha waziri mkuu Edward Lowassa aliye shika nafasi ya pili nyuma ya Mbowe.

Pamoja na Mbowe, wapo wanasiasa vijana kama Zito Kabwe, mbunge machachari wa Kigoma Kaskazini na John Mnyika aliepoteza jimbo la ubungo kwa mizengwe. Wanasiasa hawa ni alama muhimo za CHADEMA. Ni kiashirio cha uwekezaji wa CHADEMA. Mheshimiwa Kabwe alijiunga na CHADEMA akiwa na umri wa miaka 16! Amekuwa pamoja na CHADEMA.

Watu hawa hawakwenda na umaarufu wao CHADEMA, chama kimekuwa kutokana na ubunifu na juhudi za wanachama wake, Tofauti na CCM ambayo inajitambia dola, umaarufu wa kihistoria na Katiba dhaifu.

Hata kisera, CHADEMA imeweza kuja na sera ya kipeke ya majimbo, amabayo inaendelea kuchokoza mijadala katika duru za kisiasa Tanzania. Hali hii, inazidi kujenga mvuto kwa wanasiasa wa kizazi kipya. Wanataka kujihusisha na sera mbadala na ukuaji wa chama. Hi ndio sumaku ya kwanza ya CHADEMA kwa wanasiasa wa kizazi kipya.

Sababu ya pili, ni kiu ya mabadiliko ya kizazi kipya. Wanaharakati wengi vijana wanahusisha moja kwa moja umaskini wa sasa wa Tanzania na CCM. Kwa mtazamo wa wanaharakati wengi vijana,umaskini wa sasa ni tokeo la udahaifu wa kisera wa CCM na uwezo mdogo wa kudhibiti ufisadi.

Kushindwa kuwa na ufumbuzi wa kudumu juu ya mahitaji ya wanafunzi wa elimu ya juu ni utambi wa CCM kujiunguza yenyewe. Matokeo yake wanafunzi wengi wa elimu ya juu sasa wanaitazama CHADEMA kama eneo la kinabii, ndipo watakapo bebea utume wao. Ndio maana wanaharakati Kama John Mrema alie kuwa waziri mkuu wa DARUSO sasa ni moja ya injini muhimu za CHADEMA.

CCM kwa kutambua inazidi kupoteza mvuto wake kwa wanazuuoni ilikurupuka kuilaamu CHADEMA kwamba ipo nyuma ya mgomo wa chuo kikuu. Ukweli ni kuwa, mgomo ule halali ni tokeo la sera mbovu za CCM, ni harakati halali za kudai na kutetea sera zinazojali watu maskini. Kundelea kushindwa kutimiza mahitaji ya wanafunzi wa elimu ya juu ni uwekezaji mwingine wa rasilimali watu kwa CHADEMA.

Wapo ambao wataendelea na harakati hata baada ya kumaliza vyuo, hawa hawatapenda kuona wadogo zao na watoto wao kutaabika kama walivyo wao, watakwenda kujiunga na CHADEMA kama jukwaa la kuwaandalia “makazi” mema, mazingira mazuri ya kitaalumu wadogo na watoto zao.

Sabube ya tatu ni ugumu wa vijana kukatiza katika duru za uongozi katika chama cha mapinduzi. Kwa vijana wabichi chini ya miaka 30 ni vigumu kuweza kupata nafasi ya kuweza kupata fursa kutoa mchango wao kulitumikia taifa lao katika chama cha mapinzduzi. Kwa CCM, vijana wana jukumu la upambe kwa chama. Wamewekwa pembeni. CCM imeshindwa kutumia ubunifu na utayari wa vijana.

Katika kuhalalisha kuwaweka benchi vijana, CCM iliamua kuutangazia umma mwaka 2005 kwamba mgombea wake urais mwenye umri wa miaka 55 ni kijana. Baada ya wanaharakati wa vijana kuja juu walikuja kusema ni kijana kimtazamo. Kauli kama hizi zililenga kuwatumia vijana, kuwapoza!

Vijana wa kizazi kipya hawezi kukatiza ndani ya CCM, iwe nafasi za NEC, uongozi wa chama au kupata fursa za kuwa wagombea katika ngazi za ubunge, udiwani na hata serekali za mitaa.

Kwenye vinyang’anyiro vya uchaguzi wa CCM, utalazimika kuwa mtoa rushwa,mchawi,na bingwa wa majungu, pengine uwe na mtandao wa kuyapika. Pamoja na hayo, mgombea kijana atalazimika kukabiliana na mawazo mgando na ya ukale yaliopo ndani ya CCM, ataambiawa bado, anawahi nini. Ushahidi ni kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka 2005. Chama cha mapinduzi hakiweza kusimamisha walau mgombea mmoja mwenye umri chini ya miaka 30 katika uchaguzi wa majimbo.

Isitoshe, hata kama utakuwa kijana, ili upite, ubini wako utalazimika kuwa na majina kama:Kikwete, Malecela, Mongela, Mwinyi, Makamba na mengine yenye kurandana hayo, maana CCM ina wenyewe. Mazingira haya yanaonekana kuwa hatarishi kwa wanasiasa wa kizazi kipya. Badala ya kutumia nguvu na muda mwingi kujipendekeza kwa vigogo na kuyakabili majungu ya hapa na pale wameamua kugeukia chama mbadala, CHADEMA.

CHADEMA inatambua na kutumia vizuri wanasiasa wa kizazi kipya. Unapo iangalia CHADEMA ya leo kwa uhakika kabisa unaona uhakika wa chama hicho kuwa na uongozi imara siku za usoni. Ndio maana mara nyingi unakuta kijana mdogo kama John John Mnyika anapewa fursa ya kukaimu nafasi ya ukatibu mkuu wa chama, nafasi nyeti na juu katika chama chochote. Vijana wanapata fursa ya moja kwa moja kushiriki katika siasa na kulitumikia taifa lao.

Mtu anaweza kusema haya yanawezekana na yanatokea kwa kuwa CHADEMA ni chama kidogo, ya kwamba kina watu wachache. Ukweli ni kwamba, hiki ni kivutio kwa wanaharakati vijana, ni mfano wa kweli wa kuona “mashujaa” wao wakishika nafasi za juu katika vyama vikubwa vya siasa nchini. Wanapata hakikisho la utume wao, maono yao na mahitaji yao yakiwakiliswa katika ukamilifu wake.

Ndio maana, vijana wengi sasa wanavutika kwenda CHADEMA, kwetu sisi wanaharakati wa kizazi kipya, tunatafsiri CHADEMA kama eneo la utume ya kwamba, kama TANU ilivyobeba utume wa kizazi cha uhuru dhidi ya ukoloni ndivyo ilivyo kwa CHADEMA dhidi ya Umaskini, utume wa kizazi kipya. Halikuwa jambo la ajali kwa CHADEMA kujizindua upya na kubeba kauli mbiu ya “Tumaini Jipya”. CHADEMA inatambua nguvu zake zilipo ni chama kinacho angalia mbele zaidi, ni suala la muda tu kabla ya CHADEMA hakija shika nafasi stahili katika siasa za Tanzania.

Mkutano waliofanya CHADEMA na wanavyuo huko Morogoro ni mfano halisi wa chama cha kizazi kipya. Katika mkutano ule wa CHADEMA na wanavyo katika kujadili mustakabili wa elimu na Taifa kwa ujumla uliofanyika katika ukumbi wa shule ya sekondari ya Forest Morogoro, CHADEMA ilipeleka kikosi cha wanasiasa na wanaharakati wa vijana.

Baada ya Dr Slaa kuwa ameondoka, jukwaa lilibaki kwa kina John Myika, Zitto Kabwe, David Kafulila, John Mrema na wengine. Ilikuwa vijana kuzungumza na vijana wenzao. Unapoangalia taswira hii,unaona namna ambavyo CHADEMA inapika viongozi wabadaye ki matendo, watu wanajifunza wakiwa kazini.

Jamii inapata fursa adimu ya kuwajua, kufahamu mambo wanayoyasimamia, kuwakosoa na kuwajenga. Miaka ijayo wapambanaji hawa watakuwa zao na tokeo la kweli la matakwa ya jamii. Unaweza kujua CCM itakuwa na hali gani hapo badae kuweza kukabiliana na watu kama Zitto Kabwe, Halima Mdee, John Mnyka na wengine wengi ambao katika umri mdogo watakuwa wana uzoefu na uwezo mkubwa kiuongozi. Kwa msemo wa kijuweni tunasema patakuwa hapatoshi.

Pamoja na hayo, CHADEMA inaendelea kuvuna wanaharakati vijana kutokana na kuwa na mabingwa wa kweli wa harakati za vijana. Pamoja na sera zake makini, uwepo wa wanaharakati vijana ambao bado wanaendelea kufanya kazi na asasi mbali mbali za vijana ni sumaku tosha na yenye mvuto kwa vijana wanaharakati.

Wanasiasa hawa vijana walikuwa wanachama na viongozi wa asasi za vijana na taasisi za vyuoni. Uamuzi wa wanaharakati hawa kujiunga na CHADEMA kunaendelea kuwavutia “wapambanaji” wenzao, kwa maana wanajihisi salama kufanya kazi na watu ambao wanawafahamu vizuri na wana malengo sawa na wao.

Unaweza kuchukua mifano hii michache. John Mnyika ni mwanaharakati wa siku nyingi. Anafahamika kila kona ya nchi kutokana na historia yake ya utetezi wa maendeleo ya vijana. Mnyika alikuwa mmoja wa maafisa wa asasi iliyovuma sana iliyojulikana kama National Youth Forum (NYF), amabayo badae ilikuja kufutwa na serekali. Pia ni katibu mkuu mwanzilishi wa asasi makini ya vijana ijulikanayo kama TYVA (Tanzania Youth Vision Assocition) pia hujulikana kama Dira ya Vijana. Baadae alijiuzulu uongozi wa TYVA akiwa kama mwennyekiti na kujiunga na CHADEMA ambapo aliteuliwa kuwa mkurugenzi wa taifa wa kuregenzi ya vijana ya Taifa.

Bwana Mnyika pia amekuwa kiongozi na mwanachama wa asasi ya vijana wa umoja wa matifa (Youth of United Nations Associtions-YUNA) pia amekuwa mjumbe wa asasi mbalimbali za vijana zikiwamo zile za kanisa katoliki. Matokeo yake, Mnyika ameweza kuwa na mtandao mkubwa uliotapakaa nchi nzima. Haikushangaza, Wakati wa wa uchaguzi wa wa jimbo la ubungo, kambi ya Mnyika ilisheheni vijana wasomi toka vyuo karibu vyote vikubwa nchini. Nakumbuka mawakala wa Mnyika katika uchaguzi mkuu uliopita kwa kiasi kikubwa walitoka Chuo Kikuu cha Dar-es-salaam, Chuo cha Kilimo SUA, chuo kikuu cha mzumbe na chuo cha uhasibu Arusha.

Pia walikuwepo wanaharakati wengi vijana wengine wakitokea mikoa ya Mbeya, Kigoma, Kilimanjaro, Mara, Morogoro na Mwanza. Kischojulikana na wengi, uchaguzi wa jimbo la Ubungo ulikuwa ni mwanzo wa safari ndefu ya vijana kuingia katika siasa. Mnyika alichukuliwa kama mwakilishi wa vijana dhidi ya utamaduni mkongwe.

Kama alivyo Mnyika, Zitto Kabwe ni mwanaharakati kijana mashauri sana. Alikuwa ni kiongozi wa NYF kabla ya kufutwa kwake, ni mwanachama wa TYVA na la zaidi alikuwa katibu mkuu wa serekali ya wanafunzi chuo kikuu cha Dar-es-salaam-DARUSO, sasa cheo hicho kimebadilishwa na kuwa waziri mkuu. Alipokuwa chouni alikuwa mwiba mkali juu ya maamuzi ya ovyo na sera mbovu za serekali juu ya elimu wa juu.

Misimamo yake isiyotetereka ilimtia matatizoni na uongozi wa chuo na hivyo kusimamishwa mara kwa mara.Kwa vyovyote vile, kwa wanaharakati wengi vijana, Zitto ni shujaa. Ushindi wake katika katika uchaguzi mkuu wa jimbo la kigoma Kaskazini umendelea kuhamasiha na kuibua matumaini kwa vijana wengi. Hoja nzito anazowasilisha bungeni zinawasisimua vijana wengi na hivyo kujihisi kuwa na wajibu kwenda kuongeza sauti mbadala katika bunge baada ya uchaguzi mkuu wa 2010.

Pamoja na Zitto na Mnyika, kuna John Mrema alie kuwa waziri mkuu wa serekali ya wanafunzi chuo kikuu cha Dar-es-salaam(DARUSO) mika miwili iliyopita na Mheshimiwa Halima Mdee ambae alikuwa mmoja wa mawaziri wa serekali ya wanafunzi kipindi cha kina zito. Hadithi ya Halima Mdee ni ya kusisimua zaidi kwani alikuwa ni mfanyakazi wa serikali kabla ya kuteuliwa na CHADEMA kwenye viti maalum.

Halima Mdee ni nyota nyingine ambayo inasimama kama taa kuwamulika vijana waliopo serekali na kwenye makupuni binafsi. Kwamba vijana kwa nafasi zao iwe serekalini au kwenye makampuni binafsi wanaweza kuendelea kukitumikia chama. Ndio maana hii leo CHADEMA inajivunia wanaharakati wake waliopo serekalini na kwenye makumpuni binafsi. Vijana hawa wanaharakati ni hazina kwa CHADEMA na Taifa. Aina ya vijana hii wenye kujituma na kulitumika taifa inakosekana katika chama cha mapinduzi.

Tofauti nyingine ya vyama hivi viwili ni mtazamo wanachama vijana wanaojiunga na vyama hivi viwili. Vijana wengi wanaojiunga na CCM ni wale wanaotaka mafanikio ya haraka. Ni wasaka vyeo. Ukiwa ni mtoto wa kigogo au mfanya biashara unakuwa na nafasi nzuri ya kukatiza katika duru za uongozi wa CCM. Uwezo wa mtu na dhamira ya uongozi si mambo muhimu katika CCM.

Tofauti na CCM, Uwezo na dhamira ya kweli ni nguzo muhimu kwa kijana kuweza kupenya katika duru za uongozi wa CHADEMA. Matokeo yake, vijana wengi makini wanapenda kujihusisha na CHADEMA kutokana na umakini wake Kwa maanaa huko ndiko kuliko na kipimo cha kweli cha uwezo wao wa kiuongozi.

Mwisho CCM inajichongea kwa vijana kwamba kitatawala miaka mia. Kauli kama hizi zinavutia zaidi wanaharakati kwenda upande wa pili. Kwa maana CCM kinaonekana ni eneo la majigambo ambao wanaamini wanahodhi fikra za watanzania. Moja ya sifa za vijana ni utayari wao wa kuchukua “risk” na kupenda kufanya yale ambao wengine wanaamini hayawezekani. Kwa kwenda CCM, vijana hawatapata chanagamoto za kutosha. Hivyo CHADEMa ni eneo ambalo wanakidhi kiu yao ya asili ya uanaharakati.

Ndio maana wakati CCM inaendeleza mikakati ya Kizamani ya “kuvuna” wanachama wasio na misimamo kwenye mikutano yao ikumuhushisha mwenyekiti wake wa kitaifa, CHADEMA wamejikita kufanya mikakati ya kisayansi ya ujenzi wa chama kama CHADEMA ni Msingi wenye lengo la kuimarisha chama katika ngazi ya chini kabisa ya jamii pamoja na mikutano ya na wanavyuo ikilenga kuelezea sera zake na kuvuna rasilimali watu.

Pamoja na hayo CHADEMA wapo mstari wa mbele kwa kutumia mitandao na ujumbe katika simu za mkokoni katika kufanya kazi ya uenezi wa chama. Haya yanafanyika kutokana na ubunifu wa hali ya juu wenye mtazamo wa kizazi kipya. Ipo mijadala mizito inayofanyika katika Tovuti ya jambo forum. Huko ni CHADEMA pekee ambayo inachangia vizuri mijadala mbalimbali ikiwemo kupokea changamoto mbalimbali juu ya uendeshaji wake. Hata mwenyekiti wake amewahi kuchangia mijadala inayofanyika katika jambo forum jambo ambalo linazidi kukusimika chama katika mioyo ya wanaharakati wa kizazi kipya.

Kwa misingi hii wanaharakati wengi vijana wataendelea kuiona CHADEMA kama eneo muhimu la mapambano yao ya kisiasa. Kuiondoa CCM madarakani na kuweka sera mbadala katika kuwatua watanzania mzigo wa umaskini ni changamoto ya kipekee ambayo vijana wengi wanadhamiria kuikabili kila uchao. David Kafulila, mwandishi hodari hupenda kusema “ CCM works with a clock while CHADEMA Works with a compass” yaani CCM inafanya kazi kwa kutumia saa wakati CHADEMA inafanya kazi kwa kutumia dira. Hakika, hakuna kulala mpaka kieleweke.

Mwanaidi Abdalah ni mwanaharakati kijana na mwanachama wa CHADEMA. Kwa sasa ni mwanafunzi katika chuo kikuu cha Dar-es Salaam.

Wasiliana nae kupitia: mwanaidia@yahoo.com

 
lf.curl lf.curl2 rt.curl2 rt.curl