lf.bevel
MWANZO CHAMA SERA KATIBA TUUNGE MKONO UCHAGUZI TUWASILIANE
banner

Waraka wa Kwanza wa Mbowe kwa Rais Mkapa

na
Freeman Aikaeli Mbowe


Ndiyo, Rais Benjamin William Mkapa amebakisha miaka miwili kung'atuka. Atang'atuka mwishoni mwa mwaka 2005 baada ya kuongoza jahazi la nchi hii kwa miaka kumi. Kung'atuka kwake ni matokeo ya Katiba ya nchi inayompa Rais vipindi viwili tu vya kuongoza.

Tunampongeza kwa kuonyesha mwelekeo wa kuheshimu katiba pamoja na baadhi ya wapambe bila aibu kuanza "kumfagilia" kuwa katiba inastahili kubadilishwa ili apate muda zaidi wa kutawala! Wapambe kama hawa ni hatari kwa Taifa hili kwani ukiangalia kwa kina, matamko ya aina hiyo yanalenga kuwahakikishia ulaji kama Mzee atabaki madarakani! Mtu apate ulaji kwa kazi anayofanyia nchi na si kwa upambe kwa kiongozi! Wapambe sasa waombe ridhaa ya wananchi kwani muda wa dezo nao uko ukingoni!

Mara nyingi wenye hofu ya kiongozi kumaliza muda wake ni wapambe kuliko kiongozi mwenyewe. Kama walivyofanya kila hila kuchoma wenzao ili wao waaminike na wapate ulaji, kundi hili hufanya kila hila kutaka kiongozi azidishe muda wake ili ulaji uendelezwe. Wengi wamekula kwa mgongo wa viongozi walioko madarakani. Hata kwa Rais wetu nina imani wako wengi wametumia jina lake "kujinoma" bila hata yeye kujua! Historia haifutiki na iko siku ukweli utajulikana!

Mengi yamefanyika chini ya utawala wa Mkapa. Yapo mazuri yaliyofanywa na utawala wake na yapo yanayochefua. Ukiwa kiongozi ni lazima ubebe msalaba wa wote walio chini yako hata kama wanayoyafanya huyajui.

Sio nia yangu leo kueleza yale "yote" yanayochefua chini ya utawala wa Rais Mkapa. Aidha, sio nia yangu kueleza yale mazuri yaliyofanywa na utawala wa Rais Mkapa. Wako wahusika wanaolipwa kwa kazi hiyo bila kuwasahau "wapambe."

Kusudio langu leo ni kumkumbusha Rais Mkapa kuwa muda wake wa kuacha kumbukumbu ya kujengewa mnara katika nchi hii unapita tena kwa kasi ya ajabu. Wenye ustaarabu na shukrani hujengea viongozi wao minara na "monuments" nyingine za kuwatukuza mara wamalizapo madaraka na zaidi wanapokuwa wameitwa mbele ya haki.

Aidha, ni lazima wawe wamemaliza madaraka hayo kwa ustaarabu na kuacha kumbukumbu ya mambo ambayo si ya kawaida yaliyofanyika wakati wa utawala wao! Wazungu huita "legacy" sijui kiswahili sanifu nisemeje! Rais Mkapa kafanya mengi lakini bado sina hakika ataacha "legacy" gani? Hilo nawaachia Watanzania wajadili!

Naam, ili kusudio langu litimie, nitamega mawili tu kati ya yale mengi yanayotia kichefuchefu chini ya Utawala wa Mhe. Rais Mkapa. Nitazungumzia rushwa kama doa jeusi katika Utawala wa Rais Mkapa na kisha nitazungumzia Katiba ya nchi kama karata ya mwisho ya Rais Mkapa kuenziwa ndani ya mipaka ya nchi hii. Nje ameshasifiwa!

Naamini Mhe. Rais atapokea ushauri huu kwa moyo wa imani akielewa nayasema haya kwa ukweli na uwazi kwa kuwa ni pamoja na kudumisha sera yake binafsi (siyo ya serikali yake) na pia naipenda nchi yangu na wote waliopo. Ninajua Rais wetu ana majukumu mazito ndani na nje ya nchi yetu. Ni pengine majukumu haya ndiyo mara kadhaa yamemfanya Mhe. Rais aonyeshe jazba ya kutisha hadharani. Natumaini hataniita "mpumbavu" kwani kwa upumbavu wetu huo huo kama Watanzania ndiyo tumempa nafasi ya kutuongoza, na hata tukiwa wapumbavu bado ni raia wake. Aidha, naamini wapambe na baadhi ya wasaidizi wake wa karibu hawataniita "mchochezi."

Nimesema Rais Mkapa kafanya mazuri na mabaya, ni binadamu! Pamoja na kutokujadili yale mazuri aliyofanya Rais Mkapa na Utawala wake, ni sahihi kusema kuwa mazuri tuyafanyayo binadamu kwa muda mrefu yanaweza kuchafuliwa kwa sekunde chache tu kama hatukuwa waangalifu na akatokea mwingine akafumbua watu macho.

Mara nyingi Waswahili husema "chungu hupasukia mlangoni baada ya safari ndefu". Hatutaki Rais wetu akapasulia chungu chake mlangoni baada ya safari yake ndefu. "Chungu cha Mkapa" kwa mantiki hii kina falsafa pana yenye vionjo vingi. Kama nilivyosema awali, leo nitaonja viwili: RUSHWA NA KATIBA

Rais Mkapa alipoingia madarakani mwaka 1995 aliwaahidi Watanzania mengi. Kubwa zaidi aliahidi kupambana na rushwa. Haraka na kwa mkwara mzito, aliunda tume ya Jaji Warioba mwaka 1996 na kuipa jukumu kubwa la pamoja na mambo mengine kuainisha vyanzo au mianya ya rushwa ndani ya mfumo wa Serikali na namna ya kuithibiti.

Kwa kutumia kodi ya Watanzania, wengi wao wakiwa maskini wa kutupa, Jaji Warioba na wenzake walifanya kazi waliyotumwa. Waliandika makabrasha mengi na makubwa na kuyawasilisha kwa aliyewatuma.

Miongoni mwa mapendekezo ya tume ya Jaji Warioba kwa Serikali ni pamoja na kuiongezea mgao wa bajeti idara ya mahakama ili iweze kukabiliana na kesi kwa haraka zaidi na hivyo kuziba mianya ya rushwa. Aidha, tume ilishauri vilevile viongozi waeleze mali zao na pia pawepo uwazi na uwajibikaji kama msingi wa utawala bora wa Serikali.

Watanzania kwa muda mrefu sana wamekuwa na shauku ya kuona "mavuno" yatokanayo na kodi yao iliyotumika kugharamia Tume ya Jaji Warioba. Bado wanasubiri!!

Nchi hii leo haihitaji kuziba mianya ya rushwa kama suala la msingi. La msingi ni kuchimbua kwanza visiki vya rushwa kwa kishindo kikuu. Baada ya hapo ndiyo suala la kuziba mianya lifuate. Mtu aliyelemaa na rushwa hata ukimpa kipato cha uhakika na ukajaribu kuziba mianya yake ya rushwa, bado hujatibu kwani sasa ataiba maadam kukwapua kwake ni hulka. Katika nchi yetu hawa wapo kibao na kuna hisia nzito kuwa kwa ukimya wa Rais Mkapa uwezekano wa watu hawa kuwa wanalelewa ni mkubwa.

Taarifa mbalimbali zimetolewa kuhusiana na ripoti ya tume hii. Aidha, maswali mbalimbali yameulizwa! Maswali ya muhimu zaidi ambayo pengine Watanzania wengi wanaogopa kuuliza ni pamoja na: Je? Rais alikuwa ana dhamira ya kweli ya kupambana na rushwa alipounda tume ya Warioba? Au ni nini kilimzima Rais wetu ghafla katika mkakati wake wa kupiga vita na kutokomeza rushwa?

Je? kwa misingi ya rushwa ya Tanzania ilivyo, ilihitaji kuunda tume kuchunguza kinachoeleweka? Je? hao wanaostahili kusimamia zoezi la kupiga rushwa vita mbona wengi wao wamepata nafasi hizo kwa rushwa? Hakika hapa tunadanganyana!

Tume ya Jaji Warioba ilishughulika zaidi na rushwa iliyofanywa enzi za Utawala wa Mzee wetu, Rais Mstaafu Alhaj Ali Hassan Mwinyi. Tangu kipindi hicho mpaka leo rushwa imeendelea ki-uhakika na kwa ki-sayansi zaidi chini ya utawala wa Rais Mkapa.

Rushwa imefichwa chini ya mwavuli wa "sera sahihi za CCM" zinazohubiri uwezeshaji Watanzania wakati kiukweli zinasaidia kuneemesha wageni. Sijui kama Rais atakayekuja naye ataunda tume yake kuchunguza "mianya ya rushwa na namna ya kuithibiti" chini ya utawala wa Rais Mkapa! Kuna msemo wa kiswahili usemao "zimwi likujualo halikuli likakwisha." Isingekuwa busara kwa Rais Mkapa "kumalizana" na wala rushwa wa awamu yake sasa kuepusha shari ya baadaye?

Kazi ya kudhibiti rushwa ni ngumu kama viongozi hususan Kiongozi Mkuu hana dhamira ya kweli. Kutokuwa na dhamira ya kweli kunaweza kusababishwa na kuonea haya na huruma watu wako wa karibu au kuogopa nani amhukumu nani! Mimi nachambua tu, sijui hali ikoje! Panapokuwepo na dhamira ya kweli, kazi hii ni rahisi sana na hakika wananchi wako tayari kusaidia.

Mara kadhaa, Wabunge wa upinzani tumeshauri Serikali iunde tume ya Bunge ya kuthibiti rushwa. Tume hii iongozwe na sisi wabunge wa upinzani! Serikali ya CCM inaogopa! Inaogopa nini kama inajiamini ni safi? Tupewe shughuli hiyo na tunakuhakikishia Mhe. Rais katika kipindi chako kilichobakia utatoka shujaa!!

Haihitaji shahada ya juu kujua chanzo cha kigugumizi hiki cha vita dhidi ya rushwa. Rushwa kuu nchi hii bado iko Serikalini ambako kumesheheni makada wa CCM sambamba na viongozi wao waandamizi! Rushwa iko kwenye vibali mbalimbali vinavyotolewa na taasisi mbalimbali zilizo za kiserikali!

Rushwa iko katika baadhi ya mikataba mbalimbali ya aibu ambayo serikali yetu inaingia wa wawekezaji mbalimbali! Rushwa iko katika zabuni za ununuzi wa vifaa mbalimbali Serikalini ikiwemo baadhi ya kandarasi! Rushwa iko ndani ya mahakama! Rushwa iko ndani ya Halmashauri za Wilaya, Miji na Jiji. Kibaya zaidi rushwa iko ndani ya CCM na hata Viongozi wakuu wa chama hicho wamekiri.

Kama imekuwa vigumu kuthibiti rushwa ndani ya CCM itawezekana vipi kwa hao hao wa CCM kuondoa au kusimamia zoezi la kuondoa Rushwa nchini?

Je? katika hali hii unahitaji tume ya nini? Rais kama Mwenyekiti anajua dhahiri kuwa uongozi ndani ya CCM hupatikana kwa rushwa ama hila! Kama chama chake kinalea wenye hila, wala na watoa rushwa, Rais anategemea vipi "askari wake wa miavuli" na makada wamsaidie zoezi hili ilhali wengi wao ndiyo chimbuko na shina la rushwa?

Serikali ya Rais Mkapa imekuwa na sifa kubwa ya kupata heshima ya kimataifa! Hata viongozi waandamizi wa CCM na Serikali yake wamekuwa wakibeza wanaotuita "wapinzani" kuwa tunashindwa kumsifia Rais wetu ilhali watu wa nje wanamsifia! Sina hakika na unyoofu wa sifa hizo!

Ni kwa nini watu wa nje wasisifie Serikali inayowapendelea wao kuliko wananchi wake? Ni kwa nini wasisheherekee wakati makampuni yao yananunua mashirika yetu ya umma kwa bei poa tena kwa usiri mkubwa? Kwa nini wasishangilie wakati wao sasa ndiyo wameshika mpini na kugeuza Taifa letu ombaomba na kila wanachokitaka wao lazima kiwe?

Wasipongeze vipi wakati wao sasa wanauza hata wanasesere na uchafu wote wanaotaka bila mizengwe? Wasisifu vipi wakati wao na familia zao wanaishi Tanzania kama peponi wakati Watanzania kwa maelfu wananyemelewa na mauti ya kipindupindu, ukimwi na njaa kila kukicha? Oh! Samahani, nimesahau kuwa viongozi wameshasema kuwa Watanzania ni wavivu na hata hawajui kuweka mazingira yao safi!!? Tumekwisha!!

Mazuri yanayofanywa na wenzetu hususan wa Afrika ya Mashariki tuyaige tena haraka. Rais Mkapa, askari wako wa miavuli na hata taasisi zako za rushwa msilaze damu! Fungueni macho angalieni wenzenu "walivyochuna" Kenya na Wananchi wanawasaidia. Haraka nendeni Kenya mkajifunze maana ya askari wa miavuli.

Wenzenu hata mwaka haujaisha, matumaini yanaonekana! Ninyi mpaka leo mnaninginia tu sijui mtatua wapi! Pengine Alaska kwani tangu mwondoke ni miaka mitatu sasa tunangoja mutue na kipya mlichobuni na sio kuelekezwa na Benki ya Dunia na wafadhili wengine.

Mara baada ya kuapishwa, Rais Mwai Kibaki aliahidi Wakenya kwamba angepambana na rushwa kikamilifu ndani ya nchi yake kama ambavyo alifanya Rais Mkapa miaka nane iliyopita. Kibaki hakuunda tume ya kumpa mambo ya kinadharia pengine kwa lengo la kuwahadaha Wakenya! Ameunda tume mbalimbali za kupambana na rushwa kikamilifu na kila Waziri wake ana maagizo na wajibu wa kupambana na rushwa ndani ya wizara yake!

Tayari matokeo ni mazuri na Wakenya wanaona kuwa Serikali yao mpya iko kazini. Huwezi kuamini lakini ndiyo ukweli wenyewe! Wananchi wa Kenya wenyewe ndiyo wanaoongoza mapambano dhidi ya askari wa usalama barabarani wanapodai rushwa!

Gari yeyote ikisimamishwa na askari leo Kenya, abiria wote hushuka na kumtaka askari aeleze shida yake bila kificho. Baada ya askari kadhaa kushindwa kueleza kinagaubaga ni nini wamesimamishia gari na kisa cha kumwita dereva pembeni, abiria katika matukio tofauti wamewapeleka polisi na kuwafungulia askari wa barabarani mashtaka ya kutaka rushwa. Huu ndiyo uzalendo. Watanzania wako tayari, Rais Mkapa wawekee mazingira, unachelewa.

Watanzania tumesikia tume iliyoundwa na Rais Kibaki inavyoshughulika na mahakama nchini Kenya. Tayari majaji zaidi ya 23 wameshajiuzulu. Wengine kwa kuogopa kuchunguzwa zaidi na wengine kwa kutaka yaishe mapema! Mahakimu na wanasheria nao wako njiani! Hongera Kibaki!

Waziri wa fedha naye hajalaza damu! Maofisa ugavi zaidi ya 2000 walioendekeza rushwa au mazingira yake katika shughuli za zabuni nao wamefungishwa virago! Waziri wa Mazingira na Misitu naye ametimua maofisa 810 ndani ya wizara yake kwa kuruhusu ukataji wa miti na uuzaji nje wa magogo ya asili yaliyosababisha uoto wa asili kuharibiwa nchini Kenya hadi kufikia asilimia 1.7 tu kati ya asilimia 10 inayokubalika na sheria za mazingira za kimataifa!

Tume mbalimbali zinachunguza uhujumu uchumi uliofanywa kwa viwango vya kutisha na viongozi waandamizi wa awamu iliyopita ya Mzee Moi. Wafanyabiashara wakubwa na wanafamilia za viongozi ambao walionekana kama "hawagusiki" huko nyuma leo baadhi ni mahabusu wakijibu mashtaka kadhaa ya kuiibia Jamhuri ya Kenya! Kwa mtaji huu kwanini mwananchi usiipende nchi yako na Serikali yake?

Leo Watanzania tunasemaje? Hivi kweli tuko serious? Watanzania tunasifika kwa porojo Afrika nzima. Vita dhidi ya rushwa ni kuchapisha mabango ya "RUSHWA NI ADUI WA HAKI", "THIS IS THE CORRUPTION FREE ZONE" nk. Nenda ofisi zote za Serikali utakutana na utani huu. Wengi walio ndani wanajua dhahiri kuwa yote hiyo ni danganya toto na rushwa ni mtindo mmoja!

Misitu ya asili nchi hii inakatwa kama vile nchi haina Serikali. Nenda Kilwa, Rufiji, Lindi, Mtwara, Ikwiriri na ukanda wote wa Kusini mwa Tanzania misitu ya asili inateketea kwa kuvunwa na wageni wa sampuli mbalimbali na hafukuzwi mtu kazi.

Maadam hizi ni zama za uwazi na ukweli, aidha maadam wote tunatakiwa kukubaliana na "utandawazi", na kwa kuwa tunaamini kuwa viongozi wa CCM na makada wao ndani ya Serikali na hata Mashirika ya Umma hawana uwezo wa kuongoza nchi barabara, na kwa kuwa watu wa nje ndiyo wenye uwezo wa kuendesha taasisi za Kitanzania, na kwa kuwa "wapinzani wa Tanzania ni Uchwara" isingekuwa muda muafaka sasa tubinafsishe Serikali yetu kwa NARC ya Kibaki?

Kama kila kitu tunawapa wageni kwa kutokujiamini wenyewe, kwa nini hata Serikali na Bunge tusiwape wageni? Kwani wanaoongoza Serikali na walio Bungeni si Watanzania hao hao "wasiokuwa na uwezo wa kuongoza chochote"? Si unajua tena, mkuki kwa nguruwe mtamu lakini kwa binadamu ni mchungu!

Sasa nizungumzie Katiba. Watanzania wengi wanasikia Katiba lakini hawajawahi kuiona hata kwa macho. Ukiachilia mbali wananchi wenye elimu ya msingi na wale wasiojua kusoma kabisa, wasomi wengi wa kati na hata wa juu katika nchi hii hawaijui katiba. Siongei uzushi bali nazungumza niliyoshuhudia sehemu zote nilizotembelea nchi hii. Cha kusikitisha zaidi, hata wengi wa hao viongozi wa Serikali sambamba na vyama vyao vya siasa hawaijui katiba ambayo baadhi wameapa kuilinda.

Leo sitazungumzia mapungufu ya katiba yetu ya sasa ambayo ni toleo la mwaka 1977 kama ilivyorekebishwa mwaka 2000. Nitazungumzia dhana nzima ya mabadiliko ya katiba kama njia mojawapo muhimu ya kulikomboa Taifa letu.

Kama tunaitakia mema nchi hii, tulione tatizo la katiba kama letu sote. Tusitafute mchawi, mshindi wala mshindwa. Aidha, tusijidanganye kuwa tutaendelea kufukia mapungufu ya katiba zaidi bila kuleta mtafaruku wa kiutawala.

Mojawapo ya njia endelevu ya kudumisha amani na mshikamano wa Kitaifa, ni kwa wananchi wake kwa pampja kurithia katiba inayoongoza nchi. Nyingi ya nchi ambazo zimepitia mitafaruku mbalimbali ya utawala na hivyo kukosa amani kwa kuwa na vita vya wenyewe kwa wenyewe viongozi wake walipuuza umuhimu wa kuwa na muafaka kuhusu katiba ya nchi.

Aidha, mgao usio sawa na haki na pato la Taifa umepelekea baadhi ya nchi kukumbwa na machafuko.

Mhe Rais Mkapa, napenda kwa moyo mkunjufu kukuhakikishia kuwa leo Tanzania ina ufa mkubwa kuliko siku zote baada ya Uhuru. Nchi hii sasa inahitaji busara kuliko siku zote kuivusha mwaka 2005 bila mpasuko. Laiti ungeweza kuvaa "mask" ukapita mitaani na vijijini ukasikia mwenyewe kauli za wananchi wako. Najua ni vigumu wasaidizi wako kukueleza ukweli. Tusikilize na sisi ambao tunapenda kukuambia ukweli na hali halisi. Angalia na upande mwingine wa shilingi ili baadaye usiseme hatukukuambia.

Tunashangaa kwa nini wewe na Serikali yako mnaogopa mabadiliko ya katiba kujadiliwa na Watanzania wote! Tunahitaji viongozi wa dini zote kuu washiriki, tunahitaji wanasheria wetu na wasomi wengine washiriki. Wafanyakazi na hata vyama vya hiari vishirikishwe. Wakulima na wafugaji nao washiriki.

Leo Serikali ya CCM isidanganyike! Kuna hoja nyingi na nzito za kujadili kuhusu Katiba ya nchi yetu. CCM isiteke nyara hoja ya katiba ya nchi na kuibinafsisha. Wana Uhuru wa kucheza na katiba ya chama chao wanavyotaka lakini katiba ya nchi inahitaji kuridhiwa na wigo mpana zaidi wa Watanzania.

Badala ya Rais Mkapa kuonyesha wasiwasi, huu ndiyo wakati wake muafaka wa kuhakikisha kuwa nchi anaiacha salama salmin. Badala ya kuhofia, hiki ndiyo kipindi muafaka cha kuacha nchi iliyoshikamana na watu wake wa kada zote kuridhiana kwa faida ya nchi.

Nafasi hii ya mabadilioko ya katiba ikitumiwa vizuri mbali na kujengea nchi hii heshima zaidi mbele ya jamii ya Kimataifa, itasaidia kujenga UMOJA wa KITAIFA, ARI YA UZALENDO na hatimaye kazi iliyobaki itakuwa kujenga uchumi wa nchi chini ya katiba iliyoridhiwa na wote.

Hivi karibuni, kulifanyika kongamano lililoandaliwa na REDET chini ya Prof. Rwekaza Mukandala. Kongamano hili lililofanyika mjini Dar Es Salaam katika hoteli ya Golden Tulip lilifanyika kwa siku mbili na lilihudhuriwa na watu kadhaa kutoka nyanja mbalimbali katika nchi yetu. Nasikitika sikuweza kuhudhuria kwani liligongana na Mkutano wa Bunge unaoendelea mjini Dodoma.

Mambo mengi mazuri yalijitokeza katika kongamano lile. Pamoja na nia njema waliyokuwa nayo waandaaji ni vyema wakajua kuwa kiu ya katiba nchini kwetu sasa ni kubwa mno na kamwe haifai kuichokoza kwa kongamano la siku mbili au tatu. Muda ulikuwa kidogo mno na badala ya kukata kiu, kongamano lile sasa limezua mjadala mkubwa miongoni mwa wananchi. Mjadala huu unatakiwa kufanyiwa kazi na Rais Mkapa kwani sababu anayo, uwezo anao lakini sina hakika kama nia anayo.

Taarifa ya utafiti wa REDET kuwa Watanzania walio wengi hawataki mabadiliko ya Katiba nayo imezua hisia tofauti. Ni vyema msingi wa mabadiliko yetu ukawa kutafuta muafaka mapema kuliko dhana ya nani mshindi katika zoezi hili la mabadiliko ya Katiba. Hivi kweli REDET wanataka kutuambia kuwa utafiti wao ulioshirikisha watu wasiozidi 1500 ndiyo unaweza kutoa mustakabali wa nchi yetu?

Bado tuna imani na REDET kwani imefanya mengi ya kusaidia nchi yetu lakini ingekuwa vyema wakawa makini zaidi na suala la Katiba ya nchi. CCM nao wana uwezo wa kutumia mabavu kama ilivyo kawaida yao kuona wana hati miliki ya nchi hii.

Kwa upande wa pili, Serikali ya CCM nayo imeonyesha nia yake ya kuweka kiraka kingine katika katiba yetu. Imetangaza kusudio lake la kuleta mapendekezo ya mabadiliko ya katiba katika kikao kijacho cha Bunge. Mapendekezo hayo ni yale wanayopenda wao! Balaa gani hii? Suala la katiba kwa kawaida si suala la nani ana dola. Msilichezee hili mtakujajuta siku si nyingi. Kubalini nusu shari kuliko shari kamili.

Tunaonya kuwa historia haifutiki na binadamu huhukumiwa kwa makosa yake aliyoyafanya makusudi hata kama enzi za utawala wake umepita. Mkapa kwepa wimbi hili.

Afrika ya Kusini baada ya kutokomeza siasa za kibaguzi, ilikaa chini na kuandika upya katiba yake. Leo ni nadra kusikia mtafaruku wa kikatba ndani ya nchi ile kwani makundi yote yaliyokuwa na uhasama wa muda mrefu yaliridhia katiba mpya.

Leo pamoja na historia yao chafu, tofauti kubwa za rangi, uwezo tofauti sana wa kiuchumi kati ya weusi na weupe, Afrika ya Kusini ni mojawapo ya nchi zenye umoja wa Kitaifa wa kiwango cha juu sana katika dunia.

Wenzetu wa Kenya nao! Pamoja na kuwa bado wanavutana kuhusu katiba yao, tayari wanaijadili kwa faida ya nchi yao. Kwa taarifa tu, mjadala wa katiba mpya kwa Kenya imeweza kupunguza kwa kiasi kikubwa tatizo la ukabila. Tatizo hili lilikuwa sugu nchini Kenya. Wote sasa wanaangalia mbele kwa kuwa na Kenya Moja yenye kuangalia maslahi na utashi wa wote bila kujali aliyeko madarakani. KANU nao wanashirikishwa. Maelfu ya Wakenya wanaendeleza mjadala wa katiba yao iliyofanyiwa kazi kwa muda mrefu tangu enzi za utawala wa Mzee Moi chini ya tume ya Prof. Ghai.

Sasa nimalizie na ndugu zangu Watanzania. Na hapa nazungumzia Watanzania wasomi, wafanyabiashara na wale wenye nafasi katika nchi hii. Sijali wanatoka chama gani! Kadhalika siwaachi viongozi wetu wa dini zote.

Kwao napenda kuwauliza maswali yafuatayo:

  1. Je mnawapenda ndugu zenu hususan wale wanaoishi vijijini?
  2. Mnategemea neema yenu mliyonayo leo itakuwepo kwa muda gani ilhali mmezungukwa na vinywa vyenye kiu na njaa?
  3. Mnategemea nani amezaliwa kuwafanyia kazi ya kubadilisha hatma ya nchi yenu?
  4. Kwa nini mmekuwa nchi ya kwanza kwa woga duniani?
  5. Je, mnajua msipoziba ufa mtajenga ukuta?
Nawauliza Watanzania maswali haya kwani tabia ya Watanzania ina asili ya kulaumu. Tunalaumu bila kujiuliza sisi tuna mchango gani katika kuokoa nchi yetu! Wasomi wa nchi hii nao wamebakia kuwa mabingwa wa semina, warsha na makongamano!

Aaah! Nina mengi ya kuzungumza, nisiharibu msaafu wangu wa kwanza kwa Mhe. Rais. Watanzania mkitaka, nitaongeza wa pili, wa tatu na kuendelea! Niombeeni Mungu nimalize salama.

Tujadili hatma ya nchi yetu!

lf.curl lf.curl2 rt.curl2 rt.curl