lf.bevel
MWANZO CHAMA SERA KATIBA TUUNGE MKONO UCHAGUZI TUWASILIANE
banner

Waraka wa Tatu wa Mbowe kwa Rais Mkapa

na
Freeman Aikaeli Mbowe


Nikisema nachanganyikiwa, mnaniambia Oh Mbowe kaza roho na ongeza mapambano ya hoja! Sawa, pamoja na kushukuru kwa kupewa moyo haipingi ukweli wa hoja kuwa Tanzania ni nchi yenye wanasiasa ambao wengi wao wamejaa unafiki, ubinafsi, chuki, wivu na mbaya zaidi upofu wa fikra.

Wanasiasa wa Tanzania tumegeuza wananchi wetu tena wale masikini ambao ni zaidi ya asilimia 90 kuwa mashamba yaani vitegauchumi; majukwaa sasa yamekuwa ndiyo majembe na vyombo vya habari pembejeo!

Nimefuatilia kwa karibu yanayotokea nchini mwetu hususan katika nyanja za kisiasa katika siku za karibuni! Sasa nina imani kuwa mimi siyo peke yangu ninayechanganyikiwa, bali kuna umma mkubwa wa Watanzania ambao wanachanganyikiwa pengine kuliko mimi!

Yaliyosibu uchaguzi wa marudio wa Pemba na chaguzi ndogo za Bukoba Vijijini, Kilombero, Kigoma Kusini na Mpanda ni ushuhuda tosha wa jinsi wanasiasa wa Tanzania walivyo na sifa za kuwa waigizaji wa filamu za "Charlie Chaplin" kuliko kuwa viongozi wa watu wenye uwezo na dhamira ya kuendeleza demokrasia ya nchi hii, hatimaye maendeleo ya wananchi wetu.

Huhitaji shahada ya juu kugundua kuwa njaa ya akili imetuzonga sisi wanasiasa kiasi cha kutokuthamini na kuheshimu mabilioni ya fedha zilizotolewa na walipa kodi wa nchi nyingine ili kuleta amani katika nchi yetu kupitia "muafaka"!

Kwamba mabilioni ya misaada toka kwa wafadhili ambayo yangeelekezwa kwenye mipango ya maendeleo yalibidi kugeuzwa njia kupelekwa kwenye "muafaka" si mali kitu! Kwamba hata kodi ya Watanzania hawa masikini inavyopotea kurudia uchaguzi wa Pemba si hoja!

Ni vyema ikaeleweka kuwa sheria ni kitu kimoja na haki ni kitu kingine. Sheria hutungwa na binadamu lakini haki hutolewa na Mungu.

Ni mwanasiasa gani wa Upinzani Tanzania asiyejua kuwa sheria nyingi zilizopo zenye kuweka mustakabali wa masuala ya kisiasa na hivyo uchaguzi katika nchi hii ni kiini macho?

"Wanamageuzi" wetu tena baadhi wakiwa wanasheria waliobobea wamesahau kuwa kabla ya uchaguzi mdogo wa Pemba wamewahi kulalamika sana kuhusu mapungufu mengi ya katiba na uwepo wa sheria nyingi zinazonyima haki?

Kumbe "wanamageuzi" sisi tunalia tu wakati tunaona "Wenzetu" wakifaidi kwa kutumia sheria hizi kandamizi?

Kilichotokea Pemba siyo mserereko wa kukomaa kwa demokrasia katika nchi yetu bali ni ushuhuda wa jinsi baadhi ya wanasiasa wetu walivyo mzigo kwa Watanzania; walivyo bei poa na wasivyostahili hata kuwa viranja wa shule za msingi.

Wakati kichefuchefu cha Pemba hakijaisha kutoa nyongo Watanzania makini, likaibuka sakata la kufukuzwa Wabunge wawili wa Upinzani, tena na Chama chao! Kisa? Wamesaliti "chama" chao!

Kwa mtaji huu kwa nini usichanganyikiwe? Zamani nikiamini kuwa mchezo wa kuigiza katika nchi yetu uko Bungeni tu! Sasa napanua wigo! Wanasiasa wengi wa Tanzania hususan "wanamageuzi" ni waigizaji ambao wao wanafanya mzaha na roho na maisha ya Watanzania wenzao kwa maslahi binafsi!

Hata kabla ya wajumbe wa kikao kilichowafukuza uanachama wabunge wa Kisesa na Bariadi hawajafika makwao, Spika wa Bunge anatoa maelezo yanayoweza kutafsiriwa kama "mwongozo" kuwa punde akipokea barua toka kwa Mwenyekiti au Katibu Mkuu wa chama chao atatangaza majimbo hayo kuwa wazi!!??

Naye Msajili wa vyama vya siasa bila hata kupepesa ukope, anahalalisha maamuzi ya kikao cha chama na matamshi ya Spika katika staili ya haraka ambayo pengine inaweza kutafsiriwa kuwa anasheherekea kumaliza kazi aliyotumwa!

Hapa sina lengo la kuhoji au kujadili uhalali wa kauli za viongozi hawa waandamizi wa vyombo vya kutunga sheria na kutoa haki. Ninacholenga hapa ni jinsi maslahi ya nchi na wananchi yanavyoweza kuwekwa rehani kwa kutumia sheria kandamizi kwa lengo la "kuondoa udhia mfalme apumzike"

Kuna mambo mengi ya ki-aina aina yanafanywa na chama tawala. Yanaudhi na tena yanakera. Hata hivyo ukitafakari kwa kina unaona wanajaribu kwa kila mbinu kulinda mkate wao ambao tayari wanao mkononi. Kutokana na ukali wa njaa, wanamageuzi wao wanagombania harufu ya mkate ambao bado unaokwa!

Kwa mara nyingine tena "wanamageuzi" wa Tanzania wanakomoana kwa kutumia sheria zilezile kandamizi wanazopigia kelele ziondolewe. Tena wanafanya madudu haya kisha wanajipongeza!

Bila aibu wala soni wanakimbilia kwenye vyombo vya Serikali ya CCM kuomba msaada wa kumaliza matatizo yao ya ndani wakitegemea watasaidika. Hali hii inaashiria kuwemo mamluki tele ndani ya kambi ya upinzani. Kama sio mamluki; na hawajaweza kujua somo rahisi kuwa kamwe CCM haiwezi na haina nia ya kusaidia kuimarisha upinzani sio Tanzania pekee bali hata ndani ya nchi yeyote ya Afrika: basi hakika hawana sifa za kuwa viongozi wa mageuzi na pengine hata klabu ya walevi.

Unaweza kulinganisha hali hii na ugomvi wa mbuzi na kondoo ambao walikwenda kwa chui mwenye njaa ili awasuluhishe!

Ningependa nieleweke kuwa sio kwamba sikubaliani na ushirikiano na Serikali ya CCM! Hasha! Ninachoamini ni kuwa ni upungufu mkubwa wa mbinu za kisiasa kuamini kuwa ugomvi ndani ya vyama vya mageuzi utamalizwa na vyombo vya Serikali ya CCM.

Laiti wanachama wa vyama vya mageuzi wangejua viongozi wao "wanavyojigonga" kwa viongozi wa Serikali!? Ukitafakari kwa kina ni nini hasa kinapelekea viongozi wetu hawa kujigonga kwa kujipendekeza unagundua kuwa lengo ni kujisogeza karibu na ulaji.

Kwa lengo la kuwa kwenye orodha ya kudumu ya kualikwa kwenye dhifa za Kitaifa Ikulu, Safari za ng'ambo hata ikiwa Afghanistan na Kosovo (Si atapanda ndege?), kushikwa mkono na kupiga picha na viongozi wa juu serikalini sambamba na "Vimshiko" vidogovidogo vya hapa na pale "wanamageuzi" hawa wako tayari kuuza wanachama wao bei poa na hivyo TAIFA letu.

Majimbo mawili ya Bariadi na Kisesa ambayo Wabunge wake wametimuliwa Bungeni yana Watanzania zaidi ya nusu milioni wakiwemo wanachama wa vyama mbalimbali vya siasa na hata wasio na vyama.

Wabunge hawa walichaguliwa na watu mchanganyiko na sio wanachama wa chama kimoja cha siasa. Tunawatendea haki gani wananchi hawa 500,000 kwa kuwanyima uwakilishi Bungeni na maeneo mengine kwa kuwafukuza Wabunge wao bila ridhaa yao?

Kwamba chama cha siasa hata kama kina wanachama HAI wasiozidi 50 kinapewa madaraka ya kisheria ya kuwanyima haki maelfu kwa maelfu ya Watanzania?

Watanzania wenzangu, pamoja na wenzetu wa Bariadi na Kishapu kukosa uwakilishi kwa kipindi kirefu, nchi yenu italazimika kutumia takriban shilingi bilioni moja kurudia chaguzi hizi! Ilhali wananchi wetu wanazama kwenye lindi la umaskini, wanasiasa wenu wako tayari kupoteza fedha zote hizi kufurahisha genge la wanasiasa!

Kwa bahati mbaya zaidi, ni "Wanamageuzi" hawa hawa tunategemea wasaidie kuondoa sheria hizi kandamizi! Kwa mtaji huu ni dhahiri kuwa Watanzania tunahitaji kutafakari upya mustakabali wa nchi yetu kwa kukataa sasa kuongozwa njia na wanasiasa vipofu!

Hebu fikiria, zamani chama kimoja kilishika hatamu nchi ikaenda mrama; leo vyama vyote 16 vikishika hatamu nchi hii itaacha kuvurugikiwa na watu wake kuendelea kuchanganyikiwa?

Mstakabali wa nchi uwe kwenye mikono ya wananchi wenyewe na sio wanasiasa wenye upofu wa fikra na tamaa ya fisi. Ni kwa nini tuwajengee viongozi wa vyama vya siasa "Umungu Mtu" kwa kuwapa uwezo wa kucheza na wawakilishi wa watu ambao wameshachaguliwa kihalali?

Upungufu huu sio tu kuwa unapinga dhamira nzima ya demokrasia bali pia unaweka mizizi ya kutukuza viongozi hata wanapokuwa mzigo kwa chama na hivyo wanachama na nchi kwa ujumla.

Napoandika makala hii, niko Kanda ya Ziwa nikifuatana na Wabunge wenzangu wa CHADEMA sambamba na viongozi wengine waandamizi wa Chama chetu. Hii ni mikoa ya Mara, Mwanza, Shinyanga na Kagera.

Pamoja na lengo kuu la kujenga chama chetu, kipekee nina hamu kubwa ya kujionea mwenyewe jinsi mikoa hii iliyoshehena utajiri wa asili ikiwamo watu zaidi ya milioni tisa ( Sensa ya 2002), madini ya sampuli mbalimbali ikiwamo dhahabu, almasi, Uranium,bati, mawe ya thamani; mifugo, ardhi kubwa ya kilimo cha biashara na chakula, uvuvi wa kimataifa, mbuga za wanyama nk

Pengine baada ya kujionea mwenyewe hali halisi nitaweza kujua kama ile sera ya "kujazana mapesa" imefanya kazi kiasi cha kutokuona tena umuhimu wa uwakilishi Bungeni; au pengine ilikuwa tamthilia ya "mpiga filimbi wa Hamelin".

Kisiasa, nchi yetu leo ina kazi ngumu ya ziada! Kwanza ya kujua ni nani hasa wanasiasa na wanastahili kufanya nini bila hata kujali wanatokea chama tawala au upinzani! Kwa jinsi mambo yanavyokwenda, Watanzania sisi tukitegemea baadhi ya masultani tulio nao, nchi hii inakwenda kombo.

Naandika makala hii nikijua kuwa itakuwa siki kali kwa wale wote waliokuwa na walio bado mamluki wa CCM. Mamluki hawa ni hatari na hawafai kwa dawa, chakula wala mbegu. Ni wasaliti wakubwa wanaostahili kubebeshwa lawama na laana duniani na ahera.

Ni heri mara milioni wale walio CCM na kujitambulisha hivyo kuliko wale waliojipandikiza au kupandikizwa upinzani huku wakijua fika kuwa lengo lao ni kuuwa. Waelewe kuua upinzani halisi ni kuangamiza Taifa hili (wakiwemo wana CCM).

Tunatembea Tanzania nzima na tutaendelea ili kutafuta mustakabali wa nchi yetu hususan vizazi vijavyo. Ikimpendeza Mungu tuwe kafara kwa ajili ya watoto na vizazi vijavyo vya mama Tanzania na iwe hivyo!

Katika kutembea huku, jambo moja la ajabu limejidhihirisha. Watanzania wako tayari kuungana kama Taifa kuleta mabadiliko yatakayotoa matumaini mapya ya maisha kwao. Hapa nasema Watanzania na sio Wanamageuzi! Cha kushangaza zaidi hata wana CCM sasa wanapitisha mfadhaiko wao kwetu wakituomba "Jamani unganisheni nguvu!?". Nakubaliana nao.

Ni ukweli usiopingika kuwa CHADEMA kwa muda mrefu imekuwa na lengo hili. Naamini lengo hili kamwe halitakufa bali sasa kwa "shule" tuliyoipata imetubidi kubadilisha mkakati. Vyama vya siasa sio mali ya viongozi (kama wao wanavyotaka viwe). Ni mali ya wanachama nao wako tayari kuunganisha nguvu.

Baada ya kujifunza (sio kupoteza) miaka zaidi ya kumi na kugundua kuwa "penye udhia pameshatiwa rupia" na hivyo tunapoteza muda kuunganisha "waigizaji" na hivyo kujaribu kuchanganya maji na mafuta.

Tuko tayari kuchukua jukumu la kuunganisha Watanzania wote wapendao nchi yao. Nasema WOTE wakiwamo wa CCM. Tumeamua kuanzia ngazi za chini kwani hawa ndiyo waliofanywa mashamba sio na CCM pekee bali hata na baadhi ya wanaojiita wanamageuzi.

Baada ya mimi na wenzangu wa CHADEMA kuanza mkakati huu, wengi wameniuliza: "Mbowe vipi, unataka Urais? Yaani Watanzania tumefikishwa mahali ambapo hamna mtu anaamini kuwa mtu anaweza kujitoa mhanga kwa ajili ya nchi yake na watu wake bila kuwa na lengo binafsi!

Aliyesema kwa kuwa Rais wa Tanzania ni ulaji ni nani? Hata Baba wa Taifa akihoji "Kwa nini watu wakimbilie Ikulu?"

Napenda kutamka leo kuwa ndoto yangu na naamini ya wengi wa Viongozi waandamizi wa chama chetu ni kuona falfasa na itikadi yetu mpya ya "Nguvu na mamlaka ya umma" inakomboa nchi hii.

Jukumu langu na wenzangu sasa ni kuwaamsha, kuwahamasisha, kuwaelimisha, kuwashawishi na kuwaandaa Watanzania wachukue hatua za kijasiri ya kuimiliki, kuitawala, kuilinda na kuifaidi nchi yao kwani miaka zaidi ya kumi ya utawala wa mfumo wa vyama vingi na mingine zaidi ya 30 ya chama kimoja umedhihirisha kutokuwepo kwa nia hiyo (na pengine uwezo) toka kwa wengi wa viongozi.

Tunahitaji Bunge Makini na sio Bunge lililo kamati ya Chama chochote cha siasa!? Tunahitaji Halmashauri za Wilaya zinazojua zinafanya nini na kwa vipi ndani ya maeneo yao! Hatuhitaji viongozi na watendaji wa Serikali ambao badala ya kusogeza huduma kwa Wananchi, kila siku "wanajichana" kwenye semina ndani ya mahoteli makubwa ya kitalii na kumaliza asilimia 75 ya fungu ambalo lingepelekwa kwa hao wanaowajadili kwenye hizo semina!?

Wingi wa vyama vya siasa Tanzania sio wingi na utajiri wa sera, bali ni wingi wa vinywa vyenye njaa kali na tamaa mithili ya fisi vinavyongojea "mkono" udondoke toka CCM, vile, vishibe bila hata kujali mkono uliodondoka unaweza kusababisha ulemavu kwa Watanzania!

Ni vyema na wanachama wa vyama vya siasa wajue tafakari ya viongozi wanapofika hatua ya kuwaita "mtaji". Kwa lugha nyepesi mtaji wa fedha au mali ni kitu kinachowezesha kumpatia mwenye nacho faida. Watanzania kataeni sasa kuwa mitaji ya wanasiasa.

Kataeni kuwa mitaji kwa kuwaacha hao viongozi wenu wakijitanua kwenye dhifa za kitaifa! Kataeni kuwa mashamba yao! Nafasi mnayo na msipoteze tena muda!

Jueni kuwa wengi wa viongozi wenu wameshafika bei (tena poa) na sasa ni chui waliovaa ngozi ya kondoo!

Vikao visivyoisha vya viongozi wa kambi ya upinzani visivyo na mafanikio yanayopimika jijini Dar es Salaam ni ishara kuwa mkakati huu hauna dhamira ya kweli bali ni muendelezo ule ule wa mikakati ya kudhoofisha upinzani.

Ni vyema Watanzania wakajua kuwa pengine ni heri na mapenzi yake Mungu kuwa ilishindikana (kwa makusudi au bahati mbaya) kwa Wanamageuzi wa nchi hii kuungana na kutwaa utawala wa Taifa letu huko nyuma!

Wanafalsafa wanasema hakuna kitu chenye tiba nzuri zaidi katika masuala ya kijamii kama MUDA. Kama si Mungu kuipenda sana Tanzania, si angetupa tulichokesha tukiomba mwaka 1995? Yaani nchi ingejikuta kwenye utawala wa kiinimacho na mamluki kibao!!

Leo wahesabu! Kila kukicha wanatimka kurudi "nyumbani" kwani kazi waliyotumwa wameikamilisha. Kama sivyo, basi mlo walioutaka umechelewa kuiva nao wana njaa! Balaa gani hii!!

Miaka kumi ya shida na dhiki aliyotupa Mungu imetuwezesha sio tu kukomaa kwenye matatizo bali vilevile kuwajua manabii wa uwongo waliojaa kambi ya upinzani.

Kama kawaida yangu napenda kukamilisha makala yangu kwa kuwarudia Watanzania. Inakuwaje wananchi wa Bariadi na Kisesa mnanyang'anywa wabunge wenu nanyi mnakaa kimya? Hata tamko la wazee, vijana na hata kinamama hakuna! Hata maandamano ya kuonyesha kutokubaliana na kukosa uwakilishi Bungeni?

Watanzania kwa woga huu mnajenga Taifa legelege na mnawajengea viongozi wenu jeuri isiyi na kifani.

lf.curl lf.curl2 rt.curl2 rt.curl