Huu ni mwaka wa uchaguzi. Hofu ni nyingi. Bila aibu Watanzania wengi wanaodai kuichukia rushwa wanajiandaa kuipokea. Wengine wanaandaa viwanja kwani wamepania kujenga!
Waganga wa kienyeji na hata wachawi wako kazini. Wateja wao nao wako kwenye nyumba za ibada wakijipendekeza kwa viongozi wa dini! Mavuno ya aibu ni mengi. Ilimradi, mambo ya fedheha ni lukuki.
Mazingira ya maandalizi ya uchaguzi yananitisha. Siyo kwa sababu naogopa uchaguzi. Ni kwa sababu naona tunda la uchaguzi. Ukipanda bangi lazima uvune bangi. Naona mkakati wa kupanda bangi kwa watu kugombania nafasi za uongozi kwa kila njia ya giza.
Mwananchi na umasikini wake alie, mkakati wa wengi ni watu kutafuta chanzo cha mapato na rushwa.
Watu wanawekeza kwenye siasa. Nchi ya ajabu hii! Mazingira na sheria zinaruhusu uharamia huu. Wenye kustahili kusimamia haki na maadili ndiyo kwanza wanaongoza mikakati ya kiharamia.
Unafiki Tanzania ni jadi. Unafiki ni mwingi. Unaniudhi. Sina hakika tuko wangapi tunaoudhiwa. Hata hivyo, unafiki una mipaka. Tena mifupi! Kwa bahati mbaya au pengine nzuri, mipaka ya unafiki huwekwa na wengine na siyo wanafiki wenyewe.
Nikitafakari unafiki wa nchi yetu, neno moja linanikera. Nalichambua kwa kina nashindwa kuelewa maana na mipaka ya neno AMANI.
Ghafla neno hili limekuwa gumzo. Najiuliza ni nani mwenye amani Tanzania? Nani mwenye hofu ya kuvunjika amani? Je ni kweli amani ina thamani mwaka wa uchaguzi tu? Je amani hupotezwa na wanasiasa pekee?
Nahudhuria misa maeneo mbalimbali! Mahubiri yote ghafla yametawaliwa na neno amani! Hotuba za viongozi wote wa Serikali, nazo zimejaa hofu ya kupotea kwa amani! Midahalo, semina, makongamano na kila mkusanyiko mazungumzo ni amani! Makala na maandiko mbalimbali nayo amani! Maneno matupu! Sina hakika kama yanaweza kuvunja mfupa!
Nafikiria umaskini wa nchi yetu! Inanilazimisha kukumbuka na kuamini kuwa kukosekana kwa amani Tanzania ni utamaduni wa maisha ya kila siku. Kikomo cha kukosekana amani ni mauti inayoweza kuepukika.
Najiuliza, ni Watanzania wangapi kila siku hupoteza maisha yao kwa sababu zinazozuilika? Kwao kukosekana amani ni utaratibu wa kila siku katika maisha yao. Mateso yao yana upana mkubwa!
Fikiri fedheha ya kutokujua familia yako itakula nini jioni mpaka kuona mwanao akikata roho sababu tu huna uwezo wa kipato cha kumhudumia matibabu. Jiweke katika hali hiyo. Kisha tafakari amani!
Fikiria walalahoi waliojaa magerezani kwa makosa ya kusingiziwa au kwa kukosa msaada wa sheria. Fikiria anasa za "watawala" kisha tafakari amani!
Nawaza wafanyabiashara wetu! Nakumbuka wasomi! Natafakari kauli za viongozi wa dini, nawawaza "watawala wetu" (siyo viongozi). Wengi wa hawa huishi mijini. Wana umeme, uhakika wa mlo, maji, nk. Wote hawa ndiyo majemedari wa kuhubiri amani.
Ni wepesi wa kukemea hisia za upotevu wa amani. Najiuliza kwa nini! Najipa ujasiri wa kuamini wana cha kupoteza. Wananikumbusha maneno ya wanafalsafa kuwa vita huleta usawa! (War brings equality). Inaweza kuwa tafsiri potofu! Naogopa! Si maneno mazuri lakini ni ukweli.
Dar es Salaam ikikumbwa na machafuko wote tutakuwa sawa! Wa kutoka Oysterbay, Masaki, Msasani, Mikocheni na Mbezi Beach na wale wa kutoka Manzese, Buguruni, Vingunguti na Kipawa tutaondoka mjini kwa miguu. Tutakutana Ubungo tayari kwa safari ya kuelekea "kambini". Huko mpango ni mahema tu!
Hakuna makasri wala mashangingi! Wenye nacho watakikimbia kwani kitageuka kitanzi! Wakati wa machafuko na mauaji ya halaiki ya Rwanda, wengi wa watawala waliungana na wananchi walalahoi kuwahi mahema ndani ya kambi za wakimbizi!
Tukumbushane enzi za Sokoine na wale watawala waliowaita "wahujumu uchumi". Wazee wanaelewa. Si rahisi vijana wa leo kujua kuwa baba zao walitupa fedha na mali kadhaa barabarani kuogopa kuitwa "mhujumu uchumi"!
Naipenda nchi yangu na WATU wake wote. CHADEMA imelia, wanademokrasia wamelia, maskini wamelalama. Maisha ni mzunguko.
Watawala wetu wanahubiri matokeo. Hawahubiri chimbuko. Ni vyema kujifunza kwa wenzetu wa nchi nyingine. Tusijione vijogoo vya amani na wapatanishi wa wenzetu ilhali tunafunika moto wa kuni na mapipa ya petroli ndani mwetu. Hakika mlipuko utatisha!
Tusione wenzetu wa nchi nyingine hawana akili! Ni wajinga kugombana wenyewe kwa wenyewe! Eti hawana uzalendo. Hawapendi nchi zao. Hawaijui amani.
Mimi nataka amani ya kweli na ya kudumu. Wengi wangependa hivyo. Ni unafiki kufikiria amani ya kudumu ilhali tuko tayari kujitajirisha kwa vyanzo vya haramu!
Mkakati wa amani uwe kukabiliana na chanzo na siyo matokeo. Tukihubiri bila kuchukua hatua za makusudi za kuzuia machafuko tutaumbuka. Jibu ni rahisi. HAKI itendeke na watu WAWAJIBIKE kwa wanaowaongoza katika ukamilifu wake! Amani haitahubiriwa tena kwani katika mazingira hayo itakuwepo bila hofu yeyote.
Sisi siyo kisiwa. Lolote laweza kutokea hata yale yasiyotegemewa kabisa. Ni nani aliamini kuwa Maaskofu wangeweza kutupiana masumbwi! Ndiyo dunia, ndiyo nchi yetu!