lf.bevel
MWANZO CHAMA SERA KATIBA TUUNGE MKONO UCHAGUZI TUWASILIANE
banner

Viongozi wetu si Wala Rushwa, ni Wauza Nchi

na
Freeman Aikaeli Mbowe


Nlichanganyikiwa. Bado nachanganyikiwa na huenda nikaendelea kuchanganyikiwa. Kila nijiuilizapo ni nini kinanichangaya, sipati jibu. Ndiyo. Niko katikati ya giza nene hasa niwazapo Tanzania yetu ilipotoka; ilipo; na inapoelekea kuishia na kujikita.

Kwa makusudi kabisa, nasema inapoelekea kuishia kwani sasa naamini zaidi ya siku zote kuwa nchi yetu katika ujumla wake, yaani watawala na watawaliwa, tumekubali rasmi kuwa nchi hii ibinafsishwe kwa wawekezaji wa nje kiitikadi, kiuchumi, kimaadili na kibaya zaidi kifikra.

Mara chache ninapochanganyikiwa kuhusu nchi yangu napenda kuandika makala. Naandika makala si kwa nia nyingine, ila kwa lengo la kuchangia mawazo na muono wangu na jamii nzima ya Watanzani wenye kupenda kusumbua vichwa vyao katika kufikiria mustakabali wa nchi yetu. Ni kipindi cha takriban miezi mitatu sasa sijaandika makala. Wapenzi wengi wa makala zangu wameniuliza kulikoni? Wengine wamehisi labda "nimeshashughulikiwa." Nawahakikishia kuwa niko salama salimini lakini, bado nachanganyikiwa.

Hivi karibuni, jirani zetu wa Kenya walifanya uchaguzi wao mkuu. Yaliyotokeza wakati wa uchaguzi huo na baada, ndiyo hasa yamenifanya nichanganyikiwe zaidi.

Mazingira ya uchaguzi huo yamenitia hofu na simanzi kuu kwani sasa nimethibitisha yale niliyohisi siku zote kuwa Tanzania ni nchi iliyokosa fikra za ndani. Ni nchi ambayo sasa imejikita katika fikra za kuiga na kulinganisha kwa "asilimia mia moja".

Balaa kubwa ni pale kuiga huku kwa kiasi kikubwa hufanyika bila ya kufanya upembuzi yakinifu kuhusu athari zinazoweza kusababishwa na kuiga huko.

Yaliyotokea Kenya yamewatia kizunguzungu viongozi wote wa nchi hii kwa njia tofauti. Wote kwa maana ya CCM na Serikali yake na hata kambi nzima ya upinzani. Wasomi wetu, wafanyabiashara na hata viongozi wa dini nao sasa wanaona dira ya nchi yetu kama isiyozumgumzika bila kutafakari yaliyotokea Kenya.

Kundi lote hilo linaangalia yaliyo na yanayotokea Kenya kwa upande mmoja kama jinamizi linaloashiria uporaji waulaji uliozoeleka kwa miongo kadhaa na kwa upande mwingine kama ishara ya ujio wa ulaji wa uhakika. Hawa wote, sema utakalo, ndio "wenye nchi".

Aidha, liko kundi kubwa la Watanzania walala njaa (wananchi) linalojifariji kuwa yaliyotokea Kenya sasa yako mbioni kuingia Tanzania kwa dhana ya "kama wapinzani wakiungana!"

Ukiwauliza wao wanajiweka wapi katika mizani ya siasa za Tanzania wanakuambia kuwa wao si wanasiasa, hawataki kujishughulisha na siasa lakini wanataka mabadikiko na neema. Balaa kubwa hii. Maadikiko gani hayo ya kijamii yasiyowahusisha wanajamii kisiasa?

Upande wa pili wa wananchi kuna kundi la "watelekezwa" aah samahani; "wakereketwa". Hawa wamelewa harufu ya utawala pamoja na kuwa hawajawahi kuonja matunda ya utawala.

Ulevi wa harufu ya utawala umewalevya kiasi kuwa hawaoni, hawasikii pamoja na kuwa wana njaa, umaskini na dhiki ya "kishindo". Kila siku wanasikia mapambio ya "CCM ina wenyewe" lakini kwa ulevi wa harufu ya utawala wanashindwa kupambanua tafsiri.

Hawa nao kwa upofu wao hawaishi kujipa matumaini kuwa ya Kenya, KANU na Moi siyo ya Tanzania, CCM na Mkapa.

Kenya ni jirani zetu. Ni nchi ambayo nadiriki kusema kuwa ina hulka tofauti sana na Tanzania. Ukiondoa rangi inayotuunganisha, ni nchi yenye watu wenye ujasiri na fikra kali zilizo endelevu zenye kujua walikotoka, waliko na wanakokwenda.

Kwa jirani zetu hawa, kwa historia yao, kila mwananchi anajua fika faida na utamu wa utawala mzuri na machungu na athari za utawala mbaya. Wenzetu hawa wanaunganishwa na malengo yenye maslahi kwa nchi yao na si upuuzi wa itikadi na sera zenye maneno matupu na zisizotekelezeka bila huruma ya wafadhili. Kikomo cha fikra zao ni ule utayari wa wenzetu kudai kwanza haki zao za msingi bila woga wala ajizi tangu enzi za MAUMAU.

Uchaguzi wao umedhihirisha kuwa wamekomaa kiasi cha kuweza kuweka mdudu wa ukabila pembeni na kusimamia maslahi ya nchi yao.

Tunachohitaji kujifunza kutoka Kenya ni jinsi Wakenya walivyounganisha nguvu zao kudai mabadiliko yenye muono wa maendeleo yao na si tu utawala wa NARC. Wakenya katika ujumla wao walijumuika kudai maslahi yao.

Haukuwa muungano wa vyama vya upinzani tu bali muungano wa jamii nzima ya Kenya. Taasisi zote za dini Kenya (Wakristo na Waislamu) walidai kwa nguvu zote mabadiliko ya utawala waziwazi bila kificho.

Makanisa na misikiti yalihuribi waziwazi uovu, uoza na ufisadi wa Serikali na kuwaamsha waumini wao waung'oe utawala wa KANU wa Moi. Vyama vya hiari navyo kamwe havikubali nyuma vikijumisha wafanyakazi, wakulima, wafugaji, wafanyabiashara, watetezi wa haki za binadamu, wanasheria, wanamazingira, walimu na wanafunzi.

Vyombo vya habari navyo vilifanya kazi ya ziada kuelimisha umma hatua za kuelekea uchaguzi na maendeleo ya zoezi zima la uchaguzi. Safu zao za wahariri na hata makala mbalimbali zilijaa uchambuzi wa kina na zilitoa uelewa mkubwa kwa wananchi bila hofu, woga wala upendeleo.

Bila kujali miliki ya chombo cha habari, kila kimoja kilijaribu kujenga nguvu ya hoja ni kwa nini upande kinaosimamia unafaa kuchaguliwa. Mauzo ya magazeti yalipanda mara tano ya kawaida. Wote hawa walionyesha upevu mkubwa wa kutaka mabadikiko kwa amani.

Kwa kifupi wenzetu hawa waliamua kuachana na UNAFIKI na kuamua kufanya kweli.

Vyombo vya habari ni kielelezo cha jamii. Jamii iliyo makini ina vyombo vya habari makini na ndivyo ilivyo kwa waandishi wake wa habari. Vyombo vya habari ni mhimili mkubwa wa jamii katika masuala ya maendeleo ya kiuchumi, kijamii na hata kimaadili.

Pamoja na Kenya kututangulia kwenye uhuru wa vyombo vya habari, wenzetu wamekuwa makini kujenga sekta ya habari iliyo na misingi ya kuelimisha kuliko kupotosha.

Kwa tunachokiita uhuru wa vyombo vya habari, leo tunakubali Watanzania wazamishwe kwenye habari za umbeya, ngono na majungu. Tanzania leo tuna magazeti na majarida ya umbeya kuliko nchi nyingine yeyote Afrika.

Wakati nchi hii ikihitaji kila rasilimali iliyopo ya kiakili na kihali kuelimisha umma namna ya kujitoa kwenye umaskini wa fikra na hatimaye uchumi, taarifa za ngono, umbeya na fitna ndiyo malikitu.

Utasiki ...oh! ...fulani kapata buzi! ... oh fulani kafumaniwa Magomeni! ...oh! Kigogo akutwa gesti... n.k.

Nakiri kuna vyombo vinavyojitahidi na navipongeza. Lakini hao wanaoruhusu Watanzania wajazwe habari zisizo habari wanatengenezea kizazi cha leo na kesho ufahamu gani? Au ndiyo usemi wa "Ukimwamsha aliyelala utalala wewe?"

Kwa tafsiri sahihi, jambo la kwanza na la msingi la kujifunza ni kuwa mabadiliko ya Kenya yaliletwa na UMMA wa Wakenya tena wengine wao wakiwa wanachama wa KANU.

Kwa mlinganisho; nchi zetu mbili hizi zilipopata Uhuru miaka ya 1961 na 1963, viwango vyake vya maendeleo vilipishana kidogo sana. Leo miaka zaidi ya 40 inaonyesha tofauti kubwa ya maendeleo ya kijamii, kiuchumi na hata kisiasa.

Lakini cha msingi zaidi ni ukomavu wao wa fikra za ndani unaoipa Kenya jeuri ya hata kupambana na mataifa makubwa katika nyanja za uwekezaji, biashara, michezo na hata utafiti. Wakati Tanzania leo tumekubali kumezwa kiuchumi na kifikra na Afrika Kusini, Kenya leo ni mshindani mkubwa wa Afrika Kusini katika nyanja za uwekezaji, biashara na michezo.

Jambo moja ambalo ni dhahiri ni kuwa Wakenya walipiga hatua kubwa sana chini ya utawala wa Kenyatta na hata Moi. Wametuzidi kwa mbali Watanzania na nchi nyingine zote za Afrika zilizo kusini mwa jangwa la Sahara, ukiondoa Afrika kusini katika nyanja nyingi.

Kenya leo ni mwekezaji mkubwa Tanzania kuliko nchi nyingine yoyote ya Afrika. Asilimi 60% ya bidhaa za nyumbani kwenye maduka ya Tanzania zinatoka Kenya. Watoto wetu kwa maelfu wanasoma Kenya. Kenya leo haiko katika kundi la nchi maskini zaidi duniani.

Kenya leo inatoa wahitimu wa vyuo vikuu zaidi ya 45,000 kila mwaka wakati Tanzania, pamoja na wingi wetu na ukubwa wa nchi yetu, hata hatufiki 10,000. Tanzania tunazalisha chai tani 25,000 wakati Kenya wanazalisha tani zaidi ya 130,000 kwa mwaka!

Kenya leo ina medali za dhahabu, shaba na fedha kwa maelfu kutokana na mafanikio makubwa katika michezo mbalimbali ya kimataifa hususan riadha. Leo wenzetu wanashiriki Criket World Cup na wako sita bora. Dunia nzima inawaangalia wanavyofanya kweli. Sisi zaidi ya asilimia 99 hatujui huu ni mchezo gani.

Hayo yote si ajali, ni watu walikaa, wamekaa na wanaendelea kukaa na kupanga mikakati, si blah, blah. Ukilinganishaa utapata wazimu na kuichukia Serikali yako. Je tunalo cha kwetu? Je, ni kipi tunamiliki? Na, huenda wasomaji wangu wapenzi mtachanganyikiwa kama nilivyochanganyikiwa mimi.

Ndiyo, kuna uozo wa KANU, lakini uozo wa KANU na Serikali yake ni utani ukilinganishwa na uozo, uzembe, ubutu wa upeo, na kikubwa zaidi unafiki uliokithiri ndani ya CCM na wengi wa viongozi wake.

Kwa msingi waliyojiwekea wenyewe, Kenya leo ingekuwa mbali sana, na hilo Wakenya wameliona na hawakuwa na muda wa kucheleweshwa na kuendelea kufanywa mazezeta. Unashangaa na kujiuliza: Iweje pamoja na mafanikio yote Moi na KANU wang'olewe?

Hilo ni swali ambalo jibu lake ni kuwa Kenya hawana "njaa ya akili" ila wana njaa ya maendeleo na kwa hilo wanajua haki zao za msingi na hawana masihara! Sisi tuna njaa zote - akili, tumbo na maendeleo. Na kwa hakika, hakuna asilani mtu yeyote anayeweza kufikiria maendeleo kama kwanza hana akili (fikra) za kimaendeleo na hajala.

Viongozi wa iliyokuwa Serikali ya KANU na Moi mwenyewe walituhumiwa kwa rushwa kama ilivyo kwa viongozi wa CCM na Serikali yake. Tofauti kubwa ya rushwa ya viongozi wa Kenya na Tanzania ni kuwa ya Kenya mara nyingi ililiwa na Wakenya wenyewe na kiwango kikubwa katika mipaka ya nchi yao na wamewekeza kwa nguvu katika sekta mbalimbali za uchumi wao ikiwemo kilimo, utalii, viwanda, "real estate", usafirishaji na mawasiliano na hata biashara.

Pamoja na madhara ya rushwa hiyo, imechangia uwekezaji wa ndani wa Kenya.

Tusidanganyane, dunia ya leo siasa ni uchumi. Kama uchumi wa nchi yako unayumba, kila kitu hata Serikali yako, itakuwa ya ubabaishaji tu. Huu ndio ukweli kuhusu Serikali ya Tanzania.

lf.curl lf.curl2 rt.curl2 rt.curl