WATANZANIA wenzangu, naendelea kumshukuru na kumtanguliza Mwenyezi Mungu katika kila hatua ya maisha yetu, kwani bila yeye ndani ya “mji”, wote waulindao wafanya kazi bure.
Wiki iliyopita, nilimalizia tafakuri yangu kwa kusema, taifa letu liko njia panda. Maamuzi magumu sana yanastahili kufanywa kama kweli tunakusudia kuukubali ukweli wa mazingira ya dunia ya leo, ilhali, taifa likikubali kwa dhati na kwa dhamira kuwa sasa njia pekee kwenda mbele ni kwanza kubalisha fikra zetu na mazoea yetu.
Ndiyo, viongozi wa vyama vya siasa wote, wanaotawala na wasiotawala, wana kila sababu ya kubeba lawama kwa taifa letu kukwama na kukosa mwelekeo. Kila mwananchi ni mbia katika lawama hizi. Kila Mtanzania, kwa nafasi yake ana mchango kwa njia moja au nyingine kwa hali yetu kuwa hoi kama ilivyo leo, pamoja na kuwa tumepishana kwa viwango – lawama zaidi zikistahili kuelekezwa kwa wenye dhamana ya kutuonyesha njia.
Aidha, kila Mtanzania, bila kujali chama chake cha siasa, dini yake, jinsia, rangi, kabila na hata uwezo wake kiuchumi, ana uwezo wa kuwa wakala wa mabadiliko ya kwenda kwenye neema tunayostahili. Kila mmoja wetu ajiulize, kaifanyia nini nchi hii, hatua ya kwanza ikiwa ni kufikiri amewasaidiaje au amewalemaza vipi walioko madarakani kutekeleza wajibu wao?
Watanzania wenzangu, hakuna njia ya mkato. Maisha bora kwa kila Mtanzania yatabakia ndoto na vibwagizo vya uchaguzi kama wote kama taifa hatutaona tuna wajibu wa kujiondoa katika umasikini uliopo kuanzia kwenye kaya zetu.
Kwa wenye mamlaka ya juu, hatua ya kwanza ni kupata muafaka wa kitaifa, kisha kwa pamoja tukubali kusota juani ili tuchumie kivulini. Hii ndiyo changamoto kubwa inayomkabili Rais Kikwete na serikali yake, kwani wao ndiyo wenye dhamana ya kuongoza vita hii.
Kila siku tunatumia neno vita kama msamiati wa kudumu na wa masihara huku tukicheka! Vita dhidi ya umasikini! Vita dhidi ya rushwa! Vita dhidi ya dawa za kulevya! Vita dhidi ya ukimwi n.k. Vita haipiganwi milele. Huwa ni mkakati wa muda mfupi wenye kusudio la kuleta matokeo ya haraka.
Sasa naona msamiati unabadilishwa na kuwa “vita hii ni ya kudumu”. Hii ni ishara ya kukata tamaa na kutojua tuendako kama taifa. Huku ni kuwapa adui nafasi ya kudumu kunakoweza kutafsiriwa kama watawala kukosa dhamira, malengo mahsusi na mwelekeo na wengine wote kama taifa kubweteka kwa kudhani kweli kuna juhudi za dhati.
Kutangaza vita dhidi ya jambo lolote ni kutangaza mapambano na mapambano ni maumivu. Vita, kwa maana yeyote ile ni hali ya kutumia nguvu dhidi ya adui na penye matumizi ya nguvu siku zote kubembelezana hakupo!
Taifa letu leo limegeuka popo. Kwamba, taifa lolote linapokuwa na watawala wasioweza kusema bayana ni mfumo gani wa taifa wanakusudia kuujenga, na kisha wakaongoza azma hiyo, si kwa kauli na maandiko pekee, bali kwa vitendo, ni ishara ya taifa popo.
Katika makala zilizopita, nilieleza kinagaubaga kuwa msingi wa itikadi yoyote hatma yake ni jinsi inavyojielekeza kwenye mfumo wa uchumi na mahusiano ya kijamii.
Si dhambi kwa chama chochote kubadilisha itikadi yake. CCM ina haki hiyo. Kinachogomba ni usiri na ubabaishaji unaoandamana na azma hiyo. Hapa ndipo dhana ya upopo inapotamalaki.
Kama CCM imeona mapungufu katika mfumo wa kijamaa ilivyoshindwa kuujenga, isione haya, ikiri, itoke hadharani iliambie taifa. Haya ndiyo maamuzi magumu tunayostahili kuyakabili bila woga wala kuchekeana. Pungufu ya hili ni kuwa na utawala wa ghiliba, unaodanganya raia wake na unaokosa uhalali (legitimacy) wa kuongoza.
Nchi yetu leo inaelekea kuzama kwa kasi katika kinachoitwa katika siasa “itikadi ya sifa” (Populist Ideology). Chini ya itikadi hii, msingi mkuu wa ujenzi wa taifa huwa matakwa na kauli tamu (rhetorics) za kiongozi mkuu na wasaidizi wake wa karibu na kamwe si mifumo ya utawala iliyopo kwa misingi ya sera. Katika hali hii, umashuhuri wa kiongozi huonekana kama sifa ya taifa.
Itikadi hii isiyo rasmi, huibuliwa na kundi la tabaka la kati (middle class) linalowakilisha maslahi ya wafanyabiashara na watu wenye nafasi zaidi katika jamii, hasa wale wanaoishi katika maeneo ya miji (urban elites). Hawa hutumia nyenzo kadhaa, haramu na halali kujihalalishia nafasi za utawala kwa lengo kuu la kugeuza utawala chanzo chao cha sifa, utajiri na mamlaka.
Kundi hili hujisimika ndani ya chama cha siasa kinachotawala kupitia mtandao usio rasmi. Huu ndiyo mtandao tunaoshuhudia nchini mwetu leo. Hugeuza chama cha siasa kama chombo cha uchaguzi (electoral machinery) na hutegemea sana haiba binafsi ya kiongozi mkuu (personal charisma).
Ni rahisi kwa viongozi katika mazingira haya kulewa sifa zitokanazo na umashuhuri wao. Nao kwa upande wa pili huendeleza mfumo huu kwa kukumbatia kwa kiasi kikubwa yale mambo mepesi mepesi yenye kusudio la muda mfupi la kuongeza umashuhuri wao na washirika wao.
Taratibu kundi hili hujenga mikakati ya kunyonga demokrasia kwa kudhibiti fursa zote huku likijijengea uhalali wa kutawala kwa kukita mipango yote ya utawala kwenye malengo ya muda mfupi yaliyojikita katika chaguzi (electoral politics). Mipaka na mipango mingi ya utawala wa aina hii hulenga ushindi kwenye uchaguzi unaofuata na ni nadra kwa utawala wa aina hii kufikiria mipango ya muda mrefu nje ya kipindi cha utawala wao.
Kwa nia ya kutokutaka lawama, viongozi hufumbia macho usimamizi wa sheria na taratibu (law and order) huku wakiacha mambo yaserereke yenyewe. Hawako tayari kukiri na kuusimamia ukweli, kwani azma ya kudumu madarakani kwa wanamtandao ndiyo kielekezi cha utendaji wao wa kila siku. Hawako tayari kuchukua waziwazi “risk” ya kubadilisha mfumo na huachia mambo yajichukulie mkondo wake yenyewe.
Kauli nyingi za Rais Jakaya Kikwete kila akipata fursa, ni kuwakumbusha wana CCM wenzake kuhusu lengo lao la kushinda uchaguzi ujao – kwa udi na uvumba. Katika hali hii, agenda kuu ya utawala inakuwa ni kuwa madarakani kuliko kujenga taifa.
Ni rahisi wengine kusema Mbowe anamhukumu Rais na wenzake. Wengine wanaona makala zangu ni hasira za kushindwa uchaguzi. Ni haki yao. Aidha, yaweza kuwa ni wajibu na kazi yao kujenga taswira hiyo. Vyovyote watakavyosema, tayari nimeanza wajibu wangu wa kuwasaidia viongozi wetu.
Mpango wa kinachoitwa “Mabilioni ya Kikwete” kama mkakati wa kuondoa umasikini na mipango ya kuileta timu ya Real Madrid kama mkakati wa kuendeleza michezo na sifa za taifa, ni baadhi tu ya mipango isiyo endelevu inayoweza kughilibu raia na wakakosa kujikita katika mambo ya msingi yenye “serious impact” kwenye maisha na nchi yao.
Leo ni jambo la kawaida kusikia vilio vya wananchi: Kikwete tukomboe, Lowassa tusaidie. Ukweli ni kuwa tunawachosha viongozi wetu hawa. Wajibu wao si kusimamia kila kitu, bali kusimamia vyombo vilivyo chini yao kutekeleza majukumu yao. Hata hivyo, kinachowaponza ni azma yao ya kujijenga “kibinafsi” (personal institutionalization) badala ya kujenga mfumo mzima (system institutionalization).
Baadhi ya vyombo vya habari navyo kwa kujua au kutokujua, vinaendeleza utamaduni huu kwa kuona kuwa rais, makamu wa rais na waziri mkuu hawastahili lawama yoyote pale panapotokea udhaifu ndani ya serikali yao. Lawama nyingi zimekuwa kimkakati zinaelekezwa kwa mawaziri, wakuu wa mikoa, wilaya na watendaji wengine wa chini.
Hata hivyo, huwamiminia sifa viongozi hawa pale jema lolote linapotokea ndani ya nchi hata kama jema lenyewe limesabababishwa na chanzo kingine chochote nje ya serikali. Hali hii husababisha “kuwinda” ni nini cha kusema au kuwaeleza wananchi ambacho watasikia raha na hatimaye sifa za viongozi kuongezeka!
Mengi yanafanywa na serikali yetu leo, hususan katika kuimarisha huduma za jamii. Pamoja na huduma hizi kuwa muhimu, ni ukweli usiopingika kuwa, huu ni msukumo wa matumizi (consumption economy) ambao hauwezi kuwa endelevu (sustainable) kama kipaumbele chetu, kama taifa, hakitaelekezwa kwenye mikakati sahihi ya kuongeza pato la taifa kwa njia za uzalishaji na huduma (production and service economy).
Katika kufikia azma hii, ni vyema viongozi wetu wawe na uwezo wa kufikiria mbali zaidi ya uchaguzi. Uchaguzi ukiwa ndicho kigezo cha mipango yetu ya uchumi, karne ijayo itatukuta hapa hapa. Viongozi wetu wana woga usio sababu. Lazima wajipe ujasiri wa kuwa tayari kutawala hata kipindi kimoja, ili kuweza kufanya maamuzi magumu ya kulikwamua taifa hili.
Kinachohitajika ni kuthubutu. Tukitaka kwenda peponi, ni lazima tukubali kukabiliana na kifo. Ndiyo ukweli wenyewe. Matamanio ya maisha bora kwa kila Mtanzania, lazima yaandamane na viongozi wetu kukusanya kila nguvu ya taifa hili (ya akili na ya msuli) na kuitumia kwa azma hii bila kuoneana haya.
Katika makala zilizotangulia, nilisema uimara wa taifa lolote ni uimara wa uchumi wake. Uchumi wetu ni dhaifu ajabu na unategemea misaada toka nje kwa kiasi kikubwa. Leo hatuna jeuri ya kuwakatalia “wafadhili wetu” kwa chochote kwani hatuna ubavu wa kujitegemea.
Tafsiri yake ni kuwa, hatuna ubavu wa kujitawala. Cha kutisha zaidi, mbali na kauli za hapa na pale, sioni mkakati wowote wa makusudi wa kujitoa kwenye utegemezi huu kwa kushona suti yetu kwa kitambaa tulicho nacho.
Mara nyingi imenishangaza kuona kipimo cha ukuaji wa uchumi wetu kikipimwa na kuongezeka kwa mapato ya serikali kupitia kodi! Kila makusanyo yakiongezeka, serikali inajipongeza!
Nieleweke hapa! Maongezeko ya makusanyo ya kodi yanaweza yakatokana na kupanuka kwa uchumi wa taifa (economic base). Hata hivyo, maongezeko ya makusanyo yasiyoshabihiana na pato halisi la wananchi, ni ushuhuda wa kutosha kuwa umasikini unaongezeka ndani ya taifa. Wataalam wa uchumi wanasema hakuna kodi ndogo kwa mtu masikini. Kila kodi kwao ni mzigo.
Suala moja hapa ni wazi. Kwa uchumi kama wa kwetu ambao ni wa ndani (inward or import based economy) kuliko wa nje (outward or export based economy), makusanyo ya pato kubwa la taifa hutokana na kodi wanayolipa walaji wa ndani ya nchi (consumer based tax). Cha kusikitisha, wananchi wetu walio wengi hawajui kama wanalipa kodi.
Kampuni za simu, sigara, bia n.k zinaweza kuonekana zinalipa kodi kubwa kwa serikali. Ni sahihi, lakini kinachostahili kujulikana ni kuwa, kodi hii uhamishiwa kwa walaji na mwisho wa siku kampuni hizi kubwa (ambazo nyingi husamehewa kodi wanazostahili kulipa) hubakia kuwa mawakala wa kukusanya kodi (collection conduits) toka kwa watumiaji wa huduma au bidhaa zao, ambao wengi wao ni wananchi masikini.
Wakati hatuwezi kujitenga na mifumo na misukumo ya kimataifa, ni ukweli usiopingika kuwa, kila taifa lina wajibu wa kutambua nafasi yake katika jamii ya kimataifa na kisha kujiwekea mikakati yake ya kukabiliana na changamoto zake katika azma yake ya kufikia malengo yake.
Maendeleo kwa taifa ni jambo lenye sura mbili. Uimara wa uchumi unaofaidisha raia wake. Takwimu za kukua kwa uchumi bila vigezo vya kuboreka kwa maisha ya raia kamwe hakuwezi kuakisi maisha bora.
Ningependa kuhitimisha mchango wangu katika mjadala huu wa itikadi kwa kuzungumzia mtazamo mpya wa kiitikadi (contemporary thinking) wa “The Third Way”, ambao kimsingi unashabihiana na itikadi ya mrengo wa kati, ambao ninaamini ni suluhisho la ujenzi wa mfumo wa kiuchumi na kijamii unaojali na kutoa fursa kwa watu wote. Mtazamo huu ni mgeni hivyo kwa wale wataalam wetu wa enzi za Kivukoni wanaweza kuwa hawakuipitia enzi zao.
Ni dhahiri kila itikadi ina uzuri na ubaya wake. Ujamaa una sifa kubwa ya utu, kwamba kinadharia, ni mfumo unaojali watu wa tabaka la chini. Upande wa pili, uliberali una sifa kubwa ya mfumo wenye kuwezesha uchumi endelevu.
“The Third Way” ni mtazamo unaochukua yale yote mema ndani ya ujamaa na kuyaunganisha na yale yote mema ndani ya uliberali, huku ukikubali changamoto za mabadiliko ya kiuchumi na kiteknolojia.
Kwa mujibu wa Antony Giddens, mwanafalsafa wa kizazi kipya anayepigia sana chapuo mawazo haya, kupitia kitabu chake cha ‘The Global Third Way Debate’, anaainisha sifa kuu nne zinazostahili kuunda taifa la kisasa.
Kwanza, ni kukubali ukweli kuwa dunia sasa imeunganika kimfumo (interdependence) na hivyo kuwa na ulazima wa kujenga mifumo ya ushirikiano wa kimataifa ya kuwezesha kufanya kazi na kusaidiana pamoja.
Sifa ya pili ni uwajibikaji (responsibility). Kwamba kila mtu anastahili kupata haki zake za kijamii, lakini wakati huo huo akitambua haki hizo zinastahili kwenda sambamba na yeye kutimiza wajibu wake kwa jamii.
Sifa ya tatu ni fursa ya ushawishi (opportunity based incentives). Kwamba kutokana na mabadiliko ya kasi ya jamii, kila mtu ndani ya jamii anastahili kupewa fursa zilizopo zikiambatana na ushawishi unaoweza kusaidia watu kujiendeleza. Fursa hizi ni pamoja na elimu, afya nk.
Sifa ya mwisho, ni mamlaka kwa jamii (devolution). Kwamba enzi za serikali kujiamulia itakavyo zimekwisha. Jamii, kwa misingi ya kidemokrasia, zina haki ya kushirikishwa katika kuendeleza taifa lao.
Mawazo haya yanatambua na kuheshimu ukweli kuwa, uchumi imara ndiyo hujenga jamii imara na kuwa kwa hulka ya binadamu, matakwa ya pamoja (collective interests) hujengwa kupitia yale mambo yote ambayo binadamu wote wanayahitaji.
Taifa letu sasa linatakiwa litoke katika ndoto na likabiliane na changamoto za dunia. Zama za kubweteka na kujisifu kuwa maliasili nyingi tunazo zimepitwa na wakati. Mchango wa malighafi katika uchumi wote wa dunia (global economy) ni pungufu ya asilimia 20!
Mifumo mipya ya uchumi wa dunia inajikita kwa kasi katika uchumi wa huduma na teknolojia (service and information age economy). Mataifa yasiyo na maliasili kama Singapore na Hong Kong yameweza kutumia fursa hizi. Hata mataifa yaliyoendelea nayo sasa yanajielekeza kwenye sekta hizi za uchumi. Siri yake ni moja tu: ELIMU ELIMU ELIMU!
Tunahitaji kupaa na si kutembea au kukimbia. Wakati ilichukua mataifa ya Magharibi karne vizazi (generation) zaidi ya 10 kusimika mapinduzi ya viwanda (industrial revolution), dunia ya leo imeshuhudia mapinduzi ya teknolojia ya habari (information age revolution) ikijisimika na kutawala uchumi wa dunia katika kizazi kimoja.
Viongozi wetu wasipofanya maamuzi magumu leo na kupandikiza fikra na mikakati mipya ya kupambana katika dunia ya leo, hakika tutaendelea kulalamika na tutakaposhtuka, tutakuwa kwenye dunia yetu wenyewe!
Haya ndiyo maamuzi magumu, Kikwete na wenzake wanastahili kufikiria na si namna ya kugawa kadi za CCM na “vijembe”.
Nawashukuru kwa kunisoma!
Tuonane kwenye bajeti!