lf.bevel
MWANZO CHAMA SERA KATIBA TUUNGE MKONO UCHAGUZI TUWASILIANE
banner

6 Juni 2007

Waraka kwa Watanzania (3)

na
Freeman Aikaeli Mbowe

WATANZANIA wenzangu,

Kwanza nimshukuru sana Mwenyezi Mungu kutupa wengi wetu fursa ya kuonana tena wiki hii kupitia tafakuri yangu. Wako wengi ambao bahati hii hawakuipata na hivyo tuna kila sababu ya kupiga goti kushukuru.

Wiki hii, tafakuri yangu itaendeleza somo nililoanza wiki iliyopita, lililotokana na mjadala wa makala ya mwandishi, msomi na mwanasiasa, Prince Bagenda.

Dhana ya itikadi, vyama vingi na mahusiano yake na mifumo ya kiuchumi na utawala, ni somo pana. Magwiji wa sayansi ya siasa na uchumi wameandika maelfu na maelfu ya vitabu kuhusu somo hili. Hii ni kutokana na ukweli kuwa, sayansi ya siasa ni mada ya kudumu yenye umbo la kubadilika (politics is a game of dynamics).

Neno itikadi (ideology), ni zao la fikra za mwanafalsafa Mfaransa, Antoine Destutt de Tracy, aliyezaliwa mwaka 1754 na kufariki mwaka 1836, katika utafiti na maandiko yake ya “Elements d’Ideologie” wakati wa utawala wa Mfalme Napoleon nchini Ufaransa.

Alikuwa akijaribu kuoanisha mawazo, namna fikra zinavyoweza kuwekwa pamoja kwa njia ya busara na kujengewa utaratibu wa utawala unaoweza kuzaa jamii yenye kuishi kwa utaratibu fulani wa haki na ustawi.

Hii ilifuatia bara la Ulaya kwa karne kadhaa kuwa katika utawala wa ki-imla (anarchy). Mfumo huu uliweka utawala na miliki ya jamii mikononi mwa makundi madogo ya watu kwa misingi ya kidini na hata kifamilia, hali iliyosababisha machafuko na mapigano mara kwa mara katika sehemu nyingi za Ulaya.

Mijadala kuhusu itikadi za kisiasa kwetu Afrika, laweza kuonekana jambo geni. Itikadi zote tunazojaribu kuziishi Afrika leo, sambamba na mifumo yake ya kiuchumi, ni za kuiga.

Iwe ya kiliberali (liberalism) au kijamaa (socialism), ya kikomunisti (communism) au ya kifashisti (fascism), ya kihafidhina (conservatism) au ya ki-utaifa (nationalism).

Kutokana na mahitaji ya wakati na misukumo ya kijamii katika dunia ya sasa, itikadi kadhaa zinazowakilisha makundi ndani ya jamii nazo zimechukua nafasi yake.

Hizi itikadi za “kisasa” (contemporary ideologies) ni pamoja na “jinsia” (feminism) na “mazingira” (ecologism). Itikadi hizi zilizopamba moto kuanzia miaka ya 1970, zimeweza kushika kasi pote duniani na kujipenyeza katikati ya itikadi nyingine.

Itikadi ya “jinsia” kwa mfano, imekuwa ikitetea haki za wanawake, watoto, wazee na makundi mengine yote yanayoonekana “dhaifu” ndani ya jamii. Nafasi ya makundi haya ndani ya siasa za Tanzania leo, ni uthibitisho tosha kuwa itikadi yoyote si umbo la kudumu.

Itikadi zote zimeanza kama fikra na hivyo nadharia (theory) za mtu na si kundi kama Bagenda alivyojaribu kutuaminisha. Fikra hizi hulenga kusudio la mwasisi wake kwa misingi ya jamii ya namna gani anakusudia kuishawishi na kisha kuijenga katika misingi hiyo ya ki-fikra.

Katika historia ya binadamu, siku zote jamii hulishwa na kuaminishwa fikra zilizoibuliwa na mtu mmoja mmoja. Hata kwenye dini, ukweli ndiyo huu. Uenezi wa itikadi nao hutegemea ushawishi wa muasisi kwa jamii anayokusudia kuijenga. Hapa ndipo mahitaji ya jamii yanapojikita na kujisimika katika misingi ya itikadi iliyojengwa.

Itikadi huzaliwa na kwisha kutokana na namna inavyoweza kukidhi matumaini ya jamii husika. Muda umekuwa jibu la kutosha la ni itikadi zipi zimeweza kuhimili misukumo ya mahitaji ya jamii.

Ulazimishaji wa mwendelezo wa itikadi yoyote katika jamii huzaa machafuko, kwani hubaki kuwa hitaji la watawala na si la watawaliwa. Hapa ndiyo dhana ya demokrasia inaposhika mizizi.

Ni kwa misingi hii, leo itikadi kama za kifashisti na kikomunisti zimekufa kifo cha asili bila vita yoyote kupiganwa. Msuguano wa vita baridi kati ya mataifa ya magharibi na mashariki ulikuwa mkali na wenye misingi ya chuki kubwa.

Tafiti za wanazuoni wengi zilihofu kuwa, mvutano huu ungeweza kuzaa vita kuu ya tatu ya dunia. Hili halikutokea na badala yake mabadiliko ya kiasilia (natural evolution) yamechukua mkondo wake.

Baada ya vita kuu ya pili ya dunia mwaka 1945, dunia ilishuhudia itikadi mbili za ukoministi na ujamaa kwa upande mmoja na uliberali na ubepari kwa upande wa pili zikishika kasi, hususan katika bara la Ulaya, Amerika ya Kaskazini (Marekani na Canada) na Asia.

Afrika, maeneo mengi yalikuwa makoloni ya mataifa ya Ulaya na suala la itikadi halikuwepo kwenye fikra za viongozi wetu wa wakati huo. Kilichotamalaki ni namna ya kupambana na ukoloni na kujitawala.

Ni jambo la msingi kukumbuka kuwa pamoja na maingiliano yote, itikadi zote kuu katika zama zote zina misingi yake. Misingi hii huwekwa na mifumo ya kiuchumi, kisiasa na kijamii.

Ikiepukwa, haiwezi kuwa yenyewe tena. Hapa ndipo tunapopata uhalali wa kuihoji CCM, serikali yake na Bagenda kuhusu nini haswa wanakusudia wanapodai Tanzania ni nchi ya ujamaa na kujitegemea.

Nifafanue kidogo. Fikra za misingi ya kijamaa kwa kiasi kikubwa zinafanana na zile za kikomunisti. Waasisi wake ni wanafalsafa Wajerumani, Karl Marx (1818 – 1883) na Friedrich Engels (1820 – 1895). Misingi yake ilikusudia kuweka njia zote kuu za uchumi kwenye miliki ya umma chini ya usimamizi wa serikali; si miliki ya serikali kama kwa sehemu kubwa ilivyokuwa hapa kwetu Tanzania.

Ni itikadi inayokumbatia mfumo wa soko hodhi ambapo maamuzi yote ya kiuchumi hayaendeshwi na nguvu za soko bali mapenzi ya walio madarakani.

Kijamii na kisiasa, japo kinadharia, ujamaa ni mfumo unaopaswa kujenga mahusiano ya kijamii yasiyo na matabaka (classless society). Ni mfumo usioamini katika uhuru wa mtu binafsi kupata na kumiliki mali na ukisisitiza mgawanyo wa pato kwa misingi ya usawa.

Upande wa pili, fikra za kiliberali, ziliasisiwa karne ya 16 na kuboreshwa na wanafalsafa kadhaa kama John Locke (1632 – 1704), Immanuel Kant (1724 – 1804), John Stuart Mill (1806 – 1873) na wengineo. Hata hivyo, itikadi hii ilipata msimamo wake wa kiuchumi (uhuru wa soko) toka kwa mwanafalsafa na mchumi kutoka Scotland, Prof. Adam Smith (1723 - 1790).

Ni itikadi ambayo inatoa fursa kwa soko kutawala uchumi, japo haizuii serikali za nchi husika kuweka mikakati yake ya kuhakikisha fursa zinatolewa kwa haki kwa makundi dhaifu ndani ya jamii, ikiwemo huduma za jamii kama elimu, afya, maji, chakula na makazi (welfare states). Aidha, ni mfumo unaosisitiza na kuheshimu uhuru wa kila mtu (individual freedom) katika kupata na kumiliki mali kwa misingi ya halali.

Pamoja na kuwa itikadi kongwe iliyopitia majaribu mengi ya wakati, ni itikadi iliyoendelea kurekebishwa (dynamic transformation) kwa kuzingatia hulka halisi za tabia za mwanadamu na mahitaji ya wakati.

Kisiasa na kijamii, ni mfumo unaoshabikia kikamilifu utekelezwaji wa tamko la dunia la haki za binadamu (Universal Declaration of Human Rights). Tanzania ni mdau wa tamko hili, japo baadhi ya matakwa ya tamko hili hayajazingatiwa katika sheria na Katiba ya Tanzania.

Tamko hili, lenye vifungu 30, lililobuniwa na gwiji la sheria kutoka Canada, Profesa John Peters Humphrey, mwaka 1948 na kisha kuridhiwa na Umoja wa Mataifa, Desemba 10, 1948, linatambua na kuheshimu haki zote za msingi za binadamu.

Itikadi hii ndiyo leo inatawala zaidi ya asilimia 80 kati ya mataifa 197 yaliyo wanachama wa Umoja wa Mataifa, yakiwemo mataifa yaliyoasisi ujamaa.

Ukweli unabakia kuwa, baada ya ushindani wa karne nzima, kutokana na hulka mbalimbali za binadamu na mazingira yake, itikadi ya ujamaa, pamoja na kuonekana kama tamu na safi, imeshindwa kutimiza yale yaliyokusudiwa na waasisi wake. Mfano rahisi ni Tanzania.

Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, ndiye aliyekuwa muasisi wa itikadi hii nchini mwetu. Pamoja na unyofu wa Mwalimu na dhamira nzuri sana aliyokuwa nayo juu ya nchi yake, alijikuta akishindwa kupata mafanikio ya kiuchumi, japo aliweza kwa kiasi kikubwa kupata mafanikio makubwa ya kijamii.

Sasa imedhihirika kuwa, siasa ni uchumi; kwamba uchumi ndiyo nguzo kuu ya utawala wowote. Mipango thabiti ya kijamii ya taifa lolote, haiwezi kusimamiwa na uchumi legelege. Hali hii huzaa utegemezi wa hali ya juu, kama ilivyo kwa nchi yetu leo.

Imedhihirika bila shaka kuwa, watawala wetu leo wameshindwa kuliweka taifa hili kwenye mserereko wa uchumi wenye kutoa matumaini ya kuweza kujitegemea angalau kwa miaka kadhaa ijayo.

Nimalizie hoja kuhusu itikadi kwa kumweleza ndugu yangu Bagenda kuwa, hatuna sababu ya kubeza hali halisi ya dunia. Itikadi zote (iwe ujamaa au uliberali), zimeasisiwa na mataifa ya Ulaya. Changamoto yetu, iwe ni tutumiaje uzoefu wao (empirical experience) na tuijengee mazingira ya kwetu, tujenge dhamira safi tulijenge taifa letu!

Mataifa yao yamedumu katika harakati hizi za fikra kwa karne kadhaa, tangu enzi za wanafalsafa mahiri kama Socrates na Plato waliozaliwa na kuishi miaka zaidi ya 300 kabla ya kuzaliwa Yesu Kristo.

Katika mifumo ya dunia ya leo (New International political order), dhana ya kulazimishwa itikadi imepitwa na wakati. Ni jukumu la kila chama cha siasa kuwa na itikadi yake ambapo raia hupewa fursa ya kuchagua kupitia chaguzi zilizo huru na za haki, ni itikadi na kisha ni sera zipi wanazoona zinakidhi mahitaji yake sambamba na uhalisia wa mazingira yake, kwani kila nchi ina upekee wake (nation-state peculiarity).

Ni dhahiri, makala chache ndani ya gazeti haziwezi kutoa elimu ya kutosha kwa jamii yetu kuweza kupata ufahamu wa kina wa ni nini itikadi, asili yake wapi na tafsiri zake zikoje sambamba na dunia ya leo inakwenda kwa kasi gani!

Tukubaliane jambo moja! Elimu ya uraia itakayojumuisha elimu ya siasa ya itikadi zote (comparative political studies), ni muhimu sana katika nchi yetu. Lazima tufike mahali tutoe elimu hii kuanzia hatua za kwanza kabisa za elimu ya watoto wetu, ili tujenge taifa lenye kujielewa na wakati huo huo lenye kuelewa nchi nyingine zinaishi vipi, na hivyo changamoto inayolikabili.

Miaka kadhaa iliyopita, Watanzania tulifundishana siasa ya upande mmoja. Kila mtu alifundishwa mazuri ya ujamaa sanjari na utukufu wake na madhila ya itikadi nyingine sanjari na “unyama” wake. Hizi zilikuwa, kinachoitwa kwenye siasa, propaganda ambapo fikra za upande mmoja hupandikizwa kwa kila fursa ipatikanayo (indoctrination).

Leo sehemu kubwa ya kizazi chetu imechanganyikiwa. Wanajiuliza bila majibu kutoka kwa watawala: Iweje itikadi tuliyoaminishwa kuwa ndiyo sahihi, leo tunaikana kisiri siri? Iweje wale wote tuliowabeza na kuwatukana leo ndio kimbilio letu?

Naam, Bagenda analalamika kuwa vyama vya upinzani leo vimejikita katika kukosoa utendaji wa serikali ya awamu ya nne, tena kwa lugha ambayo yeye haipendi. Huko nyuma tulikuwa naye wakati tukikosoa utawala wa awamu ya pili na tatu! Sijui mwenzetu kimemkumba nini ghafla! Mbona CCM ni ile ile na watu wake ni wale wale, tena sasa ikiwa na mtandao hatari zaidi?

Kumbe vyama vya siasa baada ya uchaguzi vifanye nini? Mbona huu ni utaratibu wa kawaida dunia nzima? Nina hakika Bagenda anajua wajibu wa vyama vya siasa visivyo madarakani, ni pamoja na kuwa “watch-dog” wa serikali iliyoko madarakani katika kuhakikisha “checks and balances”.

Pengine Bagenda angetusaidia zaidi kama angetushauri kuwa jukumu hili litekelezwe vipi.

Taifa hili chini ya Mwalimu, lilijengwa likajiamini sana kwani kiongozi wetu naye alijiamini. Alisimamia kile alichokiamini, potelea mbali kama ni sahihi au hapana. Alitenda alichohubiri na alihubiri alichoamini!

Taifa halizuki. Hujengwa na viongozi. Viongozi wenye inda, waso-kauli, waso-misimamo, waso-dhamira ya kweli na waso-fikra huru, nao hujenga taifa legelege, tegemezi na lenye hofu.

Ghafla leo, kujiamini kwa Tanzania kumekwisha! Utawala wetu si kisima cha fikra tena, bali ni kisima cha kumeza fikra za wengine. Uimara wa taifa huonekana kwa ulinganisho na nchi nyingine. Tunaweza kujidai ndani ya mipaka yetu, lakini tukipambanishwa na nchi nyingine tunanyong’onyea kwa woga na hofu!

Mfano rahisi, angalia jinsi tulivyokumbwa na hofu ya Shirikisho la Afrika Mashariki. Sasa hatuogopi tena mataifa makubwa, bali tunaogopa mataifa madogo madogo, tena majirani zetu. Bila aibu, tunajifungia ndani ya sanduku. Tunahofia Kenya, Uganda na hata Burundi na Rwanda! Hapa ndipo tulipofikishwa na CCM.

Vyama vingi ni fursa ya kuwepo utajiri wa fikra. Bagenda anapaswa kufahamu kuwa, mazingira ya Tanzania hayatoi fursa ya utajiri huu wa fikra kulijenga taifa kama inavyostahili kutokana na mikakati ya makusudi ya ukandamizaji na unyongaji wa wazi wa demokrasia inayofanywa na serikali.

Ni fursa tunayoshindwa kuitumia na badala yake imegeuzwa chimbuko la chuki ya watawala na washirika wao dhidi ya viongozi na wanachama wa vyama vya siasa.

Huko nyuma, niliwahi kuandika sana kuhusu fursa na athari za mfumo wa siasa ya vyama vyingi. Ni mfumo mzuri ambao ukiwekewa misingi mibaya, unaweza kuwa wa maafa makubwa kwa nchi na watu wake.

Maafa ya mfumo huu hutokea pale ambapo waliopo kwenye madaraka ni viongozi dhaifu, wenye madhambi na hivyo waoga wa kuondolewa kwenye utawala. Hofu ya kupoteza madaraka hutamalaki.

Hali hii ikishajengeka, watawala hujiona salama zaidi ndani ya chama chao. Hutumia vibaya mamlaka ya serikali kujijengea uzio utakaofunika maovu yao. Hutumia fursa hii ya tofauti za kisiasa baina ya vyama kuhalalisha misingi ya kujenga chuki za kiitikadi, ambazo humomonyoa umoja wa kitaifa.

Muda si mrefu, chuki hii husambaa na kuwa chuki taasisi, yaani chuki iliyojisimika katika ngazi zote za uongozi wa kisiasa na kushuka kuanzia taifa hadi kwenye kaya.

Kumepandikizwa chuki za kushangaza na kutisha katika nchi hii. Chuki hizi si rahisi kuziona katika mazingira ya kawaida, kwani taifa letu limejengwa na linaendeshwa katika misingi ya kinafiki na hofu. Bagenda anajua kuwa kukabiliana nazo tu, ni jambo lisilo masihara.

Inahitaji watu wenye busara, fikra pana na subira kweli kweli kusimamia jitihada za kusimika mfumo wa vyama vingi ndani ya jamii yoyote. Tanzania ni mwathirika mkubwa wa mfumo wa vyama vingi. Madhara yake kwa nchi hii ni makubwa na mapana sana. Inahitaji ujasiri kutanabaisha madhara yake.

Viongozi makini wanapokuwa madarakani, huelekeza nguvu kubwa katika ujenzi wa taifa na si chama cha siasa. Hutoa nafasi kwa vyama vyote kukua, kwani huongozwa na matamanio ya ujenzi wa taifa lote, vikiwemo vyama vya upinzani.

Waliotutangulia katika ujenzi wa demokrasia ya vyama vingi, waliliona hili na kujiwekea utaratibu wa kutenganisha utendaji wa serikali na ule wa chama tawala. Sisi tunakazana kuunganisha!

Taifa letu liko njia panda. Linahitaji maamuzi magumu sana. Tunaweza tukaendelea kudanganyana, kupongezana, kusifiana, kuchekeana na hata kuoneana haya, lakini tujue kwa kuendeleza hulka hizi, tunakaribisha maangamizi ya taifa letu, na si ya Mbowe, Lipumba, Mbatia au Mrema!

Nawashukuru kwa kunisoma!


lf.curl lf.curl2 rt.curl2 rt.curl