WATANZANIA wenzangu, amani iwe kwenu wote.
Nikiwa bado naendelea kupumzisha nyaraka zangu kwa Mheshimiwa Rais, naomba leo nijadili hoja kadhaa zilizoibuliwa na makala ya Prince Bagenda, iliyobeba kichwa cha habari: “Itikadi ya mrengo wa kati si jibu”, iliyochapishwa katika gazeti la Tanzania Daima Mei 9, 2007.
Prince Bagenda ni mwandishi mzoefu na msomi. Naamini bado ni mwanasiasa. Ameandika makala akisema anawatetea Watanzania, tena wale wa kipato cha chini. Ni dhahiri basi, itoshe kusema kuwa kwa sifa hizo, jambo analoibua linahitaji tafakuri ya kina.
Uandishi wa kisomi, ukitumiwa vizuri na kwa nia njema, waweza kuwa wa msaada mkubwa kwa jamii inayohusika.
Aidha, maandishi ya kisomi yanaweza kujengewa hoja yenye kusudio la kulinda masilahi binafsi kwa kuwatumia hao hao wanaodaiwa kutetewa kama daraja.
Maandishi hayo hayo, hata kwa kutokutamkwa bayana, yanaweza kutumiwa kusafisha wanaostahili lawama na hapo hapo kuhukumu wasiostahili.
Naam! Maandishi hayo yanaweza kuvishwa joho la hariri, na kisha yakajenga fikra au wazo ambalo linaweza kuangamiza jamii hiyo hiyo inayodaiwa kutetewa.
Kwa kuisoma katikati ya mistari, sehemu moja ya makala ya Bagenda ilidodosa vitu vingi vyenye kuashiria nia ya kubeza fikra, wajibu na hata visheni ya vyama vya upinzani nchini Tanzania sanjari na viongozi wake.
Mwandishi hata hivyo, aliiwekea makala yake kinga kwa kuandika kuwa hoja anazotoa hazina asili ya “kejeli za kujibizana na waandishi na wanasiasa,” - pamoja na kuwa alikaribisha mjadala wa kitaifa kujadili hoja zake.
Namshukuru Bagenda kwa changamoto zote alizoibua. Kwa msingi huo huo, makala yangu haina nia ya kukejeli dhamira ya mwandishi, kama vile isivyo kuwa na nia ya kusifu na hata kuhoji uelewa wake kuhusu changamoto za kisiasa, kijamii na kiuchumi alizotoa kwa muntaarifu wa dunia ya leo.
Upande wa pili wa makala ya Bagenda, unaibua mambo kadhaa muhimu na ya msingi. Nitashiriki mdahalo huu kwa kujadili hoja hizi za msingi.
Nia yangu ni kujaribu kushiriki kutoa mawazo yangu kwa lengo la kuweka misingi sahihi ya kifikra itakayowezesha Watanzania kuweza kujadili mustakabali wa changamoto za maendeleo nchini, sambamba na mantiki na dhana nzima ya uwepo wa vyama vingi popote duniani.
Bagenda, kwanza, anapendekeza kuwa Tanzania leo iwe na kile anachokiita “itikadi rejea”, akimaanisha itikadi ya ujamaa na kujitegemea ambayo yeye anaiona kama itikadi ya ukombozi dhidi ya mifumo gandamizi ya kibepari.
Pili, anaainisha kuwa leo Tanzania hakuna hata chama kimoja cha siasa chenye programu iliyo wazi ya kutetea na kutekeleza itikadi ya ujamaa na kujitegemea. Anaongeza kuwa CCM wana itikadi hii vitabuni lakini sera zake za serikali zinakinzana na itikadi yake.
Tatu, anapuuza itikadi za kiliberali zenye kukumbatia mifumo ya soko huria na hususan zile za mrengo wa kati katika mizania ya itikadi Tanzania na sehemu nyingine duniani.
Nne, anasema viongozi wa upinzani hawana hoja za kujenga uchumi mbadala wa mfumo tulio nao bali wameelekeza hoja zao kwenye malalamiko juu ya utendaji wa viongozi wa Awamu ya Nne na hoja zao zinaongozwa zaidi na mashambulizi ya lugha kuliko mantiki.
Sasa nijadili. Kwa lugha nyepesi, dhana ya msingi ya kuwepo kwa mfumo wa vyama vingi vya siasa katika taifa lolote, ni kutoa uhuru na fursa kwa wananchi wake, kwa ridhaa yao, kuungana na kujiendesha kama kundi lenye madhumuni na malengo ya kisiasa.
Kundi hili, kama chama, linastahili kuwa na uhuru wa kufuata itikadi yoyote wanayoiona inatimiza malengo yao ya kisiasa, kijamii na hata kiuchumi kwa mujibu wa sheria za nchi.
Tanzania kama taifa, tuliridhia mfumo huu mwaka 1992, na hivyo kufanya marekebisho kadhaa ndani ya katiba na kutunga sheria mpya iliyoainisha masharti na taratibu za kufuata ili chama kiweze kuwa na sifa ya kuitwa chama cha siasa.
Nipende kuainisha hapa kuwa, katiba yetu kama ilivyo leo, inakinzana yenyewe kwa yenyewe. Baadhi ya vifungu vinatoa uhuru wa kuwa na mfumo wa vyama vingi wakati huo huo katiba hiyo hiyo ikilazimisha kufuata siasa ya ujamaa na kujitegemea.
Ni dhahiri kuwa kwa hili, katiba yetu ina upungufu mkubwa ambao ukitafsiriwa kisheria, unatoa uhalali wa kufuta vyama vyote vya siasa ambavyo haviikubali itikadi hii kama msingi wa kuwapo kwake.
Aidha, baadhi ya vifungu vya katiba hii kama vilivyo leo, vinakinzana na sera za serikali ya CCM, kwani baadhi ya sera za serikali hazikidhi matakwa ya katiba. Labda turejee katiba yetu leo inasema nini kuhusu hoja hizi mbili.
Kuhusu vyama vya siasa, katiba yetu sura ya kwanza kifungu cha 3.-(1) inasema: “Jamhuri ya Muungano ni nchi ya kidemokrasia na ya kijamaa, yenye kufuata mfumo wa vyama vingi vya siasa.”
Kwa msingi huu, kifungu hiki cha katiba kinalazimisha vyama vyote kufuata itikadi ya kijamaa.
Katika katiba hiyo hiyo sehemu ya pili inayoainisha malengo muhimu na ya msingi ya mwelekeo wa shughuli za serikali ibara ya 9 na baadhi ya vifungu vidogo inasema:
“Lengo la Katiba hii ni kuwezesha ujenzi wa Jamhuri ya Muungano na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar au wa chochote kati ya vyombo vyake na udugu na amani kutokana na kufuata siasa ya Ujamaa na Kujitegemea, ambayo inasisitiza utekelezaji wa misingi ya kijamaa kwa kuzingatia mazingira yaliyomo katika Jamhuri ya Muungano.
Inaendelea: “ Kwa hiyo, mamlaka ya nchi na vyombo vyake vyote vinawajibika kuelekeza sera na shughuli zake zote katika lengo la kuhakikisha –
(b) kwamba sheria za nchi zinalindwa na kutekelezwa;
(f) kwamba heshima ya binadamu inahifadhiwa na kudumishwa kwa kufuata Kanuni za Tangazo la Dunia kuhusu Haki za Binadamu;
(h) kwamba aina zote za dhuluma, vitisho, ubaguzi, rushwa, uonevu au upendeleo zinaondolewa nchini;
(j) kwamba shughuli za uchumi haziendeshwi kwa njia zinazoweza kusababisha ulimbikizaji wa mali au njia kuu za uchumi katika mamlaka ya watu wachache binafsi;
(k) kwamba nchi inatawaliwa kwa kufuata misingi ya demokrasia na ujamaa.”
Naam! Mara kwa mara, umekuwapo utetezi wa kiujanja ujanja wa watawala kuhusu tafsiri halisi ya ujamaa na kujitegemea. Ni dhahiri, tafsiri muhimu kama hii ingestahili kuwa sehemu muhimu ya utangulizi ndani ya katiba.
Kwa kuangalia kwa kina mantiki ya vifungu hivi vya katiba, ni ushahidi ulio wazi kuwa, serikali ambayo inastahili kuendeshwa kwa mujibu wa katiba ambayo ndiyo sheria mama; kwa makusudi ndiye mvunjaji mkuu wa katiba hiyo hiyo, ambayo viongozi wake waliapa kuilinda.
Mara kadhaa nimeandika na kuhutubia kuwa taifa letu linahitaji sana maridhiano ya kitaifa. Hilo halitawezekana kwa kukumbatia itikadi moja, bali litawezekana kwa kwanza kuwa na katiba moja ambayo itaridhiwa na wote bila manung’uniko kama ilivyo leo.
Ni katika katiba ndipo tutakapoweza kuainisha pamoja na mambo mengine, maadili na miiko rasmi ya taifa hili ambayo si tu ibaki kwenye maandishi, bali wananchi wote wakiwemo viongozi waishi kwa ukamilifu wake, na asiwepo yeyote atakayekuwa juu ya sheria. Hapo, tutakuwa tumeweka msingi wa kujenga si taifa na watu wake pekee, bali upendo na amani ya kudumu.
Nikirejea kwenye hoja ya Bagenda, ya kuwa na itikadi moja iliyoridhiwa na vyama vyote, (anayoiita itikadi rejea), si tu kuwa inakinzana na maana halisi ya kuwa na uhuru wa kiitikadi, bali inalirejesha taifa katika mfumo wa chama kimoja.
Katika dunia ya leo, katika nchi yoyote yenye mfumo wa demokrasia ya vyama vingi, hapajawahi kutokea kulazimisha vyama kufuata itikadi fulani.
Itikadi za kisiasa ziko nyingi na kadiri maisha ya binadamu yanavyobadilika kutokana na misukumo mbalimbali, kunajitokeza vyama vya siasa vinavyowakilisha agenda tofauti tofauti.
Leo ni jambo la kawaida kusikia vyama vinavyotetea sera za mazingira vikishamiri kwenye nchi kadhaa.
Aidha, hakuna ubaya wowote vyama kufanana itikadi ndani ya nchi moja. Mnaweza kuwa na itikadi moja, mkatofautiana katika sera au mifumo ya utawala.
Itikadi ya siasa inakuwa na maana pale ambapo wale wanaoihubiri wanapokuwa kweli wanaitekeleza itikadi yao kisera na kiutendaji, hasa wanapokuwa madarakani. Pungufu ya hili ni utapeli wa kisiasa.
Ni upungufu mkubwa sera na mipango ya serikali iliyopo madarakani inapotofautiana bila kificho na itikadi ya chama tawala, tena katika mazingira ambayo viongozi wakuu wa chama ndio hao hao wa serikali.
Jambo hili mbali na kuwa ni ukiukwaji wa wazi wa katiba yetu ya leo, ni ushuhuda tosha wa jinsi watawala wetu wasivyokuwa wakweli katika fikra na dhamira zao dhidi ya kiapo chao cha utumishi kwa Mungu na umma wa Watanzania.
Vyama vinapokuwa vya upinzani, sera zake hubakia zaidi nadharia hadi pale vinapopata nafasi ya kuongoza dola.
Uwepo wa itikadi nyingi za kisiasa huwa hitaji la muda na mazingira. Hoja kuwa Ujamaa na Kujitegemea ndiyo itikadi anayoiita Bagenda ya “ukombozi” ni hoja tata yenye pia kuhitaji mjadala.
Nchi yetu haijawahi kujitegemea na binafsi sioni juhudi za dhati za kujitegemea kama taifa, bali kuendelea kuwa taifa tegemezi hata kwenye vitu vya aibu kama misaada ya ujenzi wa vyoo kwenye mashule yetu!
Nikubaliane na jambo moja kuwa; kwa nchi masikini kama Tanzania, ni muhimu kuwa na sera za kiuchumi zitakazoweza kusimika mfumo wa uchumi (economic system) ambao utaakisi hali halisi ya umasikini wa wananchi wetu.
Mfumo wa uchumi ninaouzungumzia hapa, unastahili kuweka bayana fursa za ndani na hata za nje za uzalishaji (production) za kuwawezesha na kuwashirikisha wananchi, sambamba na mgawanyo (distribution) wa kile kinachopatikana katika kukidhi mahitaji muhimu ya wananchi.
Sina hakika kama nadharia ya itikadi ya Ujamaa na Kujitegemea bila utashi wa kweli wa watawala inaweza kutoa nchi yetu katika lindi la umasikini unaolielemea.
Si siri kuwa nchi nyingi zinazoendelea ikiwamo Tanzania, ambazo zilikumbatia itikadi ya ujamaa na hata sasa katika mfumo wa soko huru, matabaka ya watawala na washirika wao ndio wenye kufaidi keki halisi ya taifa ilhali wananchi wengi wakiendelea kuwa maskini wa kutupa. Si siri tena kuwa siasa na vyama tawala vimegeuzwa miradi na vyanzo vya mapato kuliko dhana ya kutumikia umma.
Mfumo wa uchumi ni jambo pana na lina uhusiano wa karibu na itikadi za kisiasa. Katika mifumo mipya ya kisiasa na kiuchumi (contemporary political and economic systems) mbali na itikadi, kuna vigezo kadhaa muhimu vya kuangalia katika kupanga mustakabali wa nchi.
Wanasayansi wa siasa na wanafalsafa wa kizazi kipya kote duniani leo wanajadili kama kweli bado itikadi (ideology) ni dhana ya msingi katika kupanga mustakabali wa nchi yoyote.
Hali hii inasukumwa kwa kiasi kikubwa na kumomonyoka kwa nguzu za ndani za mataifa duniani (nation-state sovereignty) kunakosababishwa pamoja na mambo mengine, mabadiliko makubwa ya mahusiano mapya ya kiuchumi, kijamii na kiteknolojia. (global social, economic and political integration), mashuhuri kama utandawazi (globalization).
Baada ya kuanguka kwa dola ya Urusi katika miaka ya 1980 ambayo ilikuwa kinara wa itikadi za kikomunisti na kijamaa, na hivyo kuashiria mwisho wa vita baridi (cold war), mashindano ya kisiasa (political competition) ya kimataifa sasa yamerithiwa na mashindano ya kiuchumi (economic competition).
Lugha inayotawala dunia leo ni uchumi na demokrasia. Namna kila taifa litakavyoweza kutafsiri fursa zake katika wimbi hili ni changamoto kwa kila nchi.
Hapa ndipo watawala wetu wanastahili kutuaminisha kuwa wanajua wanakotupeleka.
Tanzania si kisiwa. Kwa udhaifu wetu kiuchumi na kiteknolojia hatuna ubavu wa kujitenga na wimbi linalounganisha dunia kupitia mifumo ya kiuchumi (economic globalization) na mpanuko wa technolojia (technological advancement).
Mataifa yaliyoasisi itikadi ya ujamaa, tena yenye nguvu kubwa za kiuchumi, kijeshi, kiteknolojia sambamba na utajiri wa kutisha wa maliasili kama vile Urusi na China, wametambua umuhimu wa uchumi wa soko dhidi ya uchumi hodhi.
Wamekumbatia sera za uchumi zenye kuheshimu uwezo binafsi (individual initiative) dhidi ya mikakati ya pamoja (communal initiative). Kasi yao ya maendeleo sasa ni ya kutisha.
Nchi zilizobaki ving’ang’anizi wa itikadi ya ujamaa ni Korea Kaskazini na Cuba, ambazo hali zao kiuchumi ni mbaya kupindukia.
Ni kweli duniani leo kuna mifumo mingi ya kijamii na kiuchumi inayonyonya nchi masikini zinazoendelea. Hata hivyo ni lazima tukiri kuwa watawala wa nchi nyingi za Afrika sambamba na mifumo yetu ya utawala ni sehemu kuu ya majanga yanayolisibu bara hili na Tanzania hatuna upekee.
Mifumo hii ya unyonyaji wa mataifa yanayoendelea, kwa kiasi kikubwa hupata baraka za watawala wetu pale masilahi yao binafsi yanapotangulizwa mbele kuliko yale ya taifa.
Wote tuna uzoefu jinsi nchi yetu ilivyoporomoka kiuchumi na hata kimaendeleo chini ya mfumo wa kijamaa.
Kinadharia, itikadi hii ni ya kuvutia hasa kwa nchi masikini, ilhali kwa hulka asilia ya binadamu walio wengi iliyojaa ubinafsi, itikadi hii haitekelezeki na muda umedhihirisha hili.
Kama nilivyosema awali, mada hii ni muhimu na ndefu! Niombe radhi kwa kutoimaliza na niahidi akipenda Mwenyezi Mungu nitaendelea wiki ijayo.
Nawashukuru kwa kunisoma.