lf.bevel
MWANZO CHAMA SERA KATIBA TUUNGE MKONO UCHAGUZI TUWASILIANE
banner

9 Mei 2007

Waraka wa sita wa Mbowe kwa Rais Kikwete

na
Freeman Aikaeli Mbowe

MHESHIMIWA rais,

Namshukuru Mwenyezi Mungu kutuwezesha tena leo kukutanisha mawazo yetu kupitia tafakuri hii tukiwa buheri wa afya japo katikati ya lindi la umaskini.

Pamoja na kupigwa marufuku kutokumtumia Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere kwa njia yoyote ile na ‘wapiga debe’ wako ambao sasa ni mawaziri wako waandamizi wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu uliopita; hatimiliki iliyosemekana inastahili kuwa kwako; kwani unamjua zaidi Baba wa Taifa; niruhusu nitii amri hiyo kwa kukumbusha yafuatayo:

Katika hotuba yako ya kulizindua Bunge jipya Desemba 30, 2005, ulisema maneno yafuatayo:

Mheshimiwa Spika:
Tangu tupate uhuru, kila awamu ya uongozi wa taifa imekuwa na majukumu yake ya msingi. Awamu ya Kwanza iliunda na kujenga taifa….. Mwalimu Nyerere hakurithishwa taifa na wakoloni…... Akatambua kuwa hata uchumi wa Tanzania ungekua kwa kasi kubwa kiasi gani, iwapo hakuna misingi imara na hisia za dhati za utaifa, baada ya muda tutasambaratika na uchumi huo utakuwa hauna maana…..

Mwalimu aliongoza vita dhidi ya ujinga, umaskini na maradhi. Mtandao mkubwa wa huduma za jamii tunaojivunia leo ulianza na falsafa ya maendeleo ya Baba wa Taifa. Wengi wetu tuliomo humu ndani, wa makamo yangu, tusingesoma na kufika hapa tulipo kama si kuona mbali na sera nzuri za Baba wa Taifa. Tutamshukuru yeye na mzee Karume daima.

Mheshimiwa rais,

Baada ya nukuu hii niruhusu nielekeze tafakuri yangu kwenye matumizi na anasa za serikali huku tukitafakari mantiki ndani ya maneno mazuri na yenye busara uliyoyasema.

Nianze kwa kukupongeza kuhusu jambo moja la msingi. Kuelekea kupungua kwa safari zako za nje. Sina hakika kama kupungua kwa safari zako ni kwisha au kupungua kwa sababu za safari hizo au mshituko uliotokana na kudhihirika kupitia taarifa ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Serikali juu ya matumizi makubwa ya serikali, tena nje ya bajeti.

Wewe binafsi umenukuliwa mara kadhaa ukitetea umuhimu wa safari zako. Wasaidizi wako nao wamekuwa wakitetea kwa nguvu zote umuhimu wa safari hizo.

Aidha, ni dhahiri pia kuwa, pamoja na sababu zilizotolewa kuwa bado ni hai, safari angalau kwa siku chache hizi zimepungua. Kwa vyovyote vile, ni jambo la heri na nina kila sababu ya kukupongeza.

Mheshimiwa rais,

Unapoendelea na misafara yako ndani ya nchi, nina hakika unaendelea kushuhudia nchi yetu ilivyo maskini. Ni dhahiri “umaskini, ujinga na maradhi” havitakwisha kama viongozi wa serikali wataendelea kuishi maisha ya gharama inayolipiwa na maskini hao hao viongozi wanaowakoga na maisha ya anasa.

Pamoja na wingi wa safari zako, ni vyema ukatafakari kwa kina risala ya wafanyakazi waliyokusomea Siku ya Mei Mosi jijini Mwanza, hususan kuhusu matumizi makubwa ya serikali yako. Ni dhahiri kuwa viongozi wetu na watendaji wa serikali wamejijengea utamaduni wa kujikweza pengine kwa lengo la kujilinganisha na yale yanayofanywa na serikali au mashirika ya nchi nyingine. Wewe kama kiongozi mkuu, uliyepewa sifa ya kumfanania Mwalimu, utuongoze kwa vitendo kumuenzi na ‘kumuishi’.

Ni kweli safari za viongozi ndani na nje ya nchi zinawachanganya wananchi. Kinachofadhaisha zaidi, ni kuwa, taarifa za gharama zake zimekuwa za usiri mkubwa, si kwa wanachi pekee, bali hata kwa wabunge ambao katika mazingira ya kawaida wana wajibu wa kuhoji. Wengi wa wabunge wetu, nao wamekuwa sehemu ya misafara hii kiasi kwamba nao ni sehemu ya watuhumiwa kwetu sisi raia.

Mheshimiwa rais,

Kama ninavyosema siku zote, pale penye usiri mkubwa, panajitokeza ombwe (vacuum) ambayo hujazwa na hisia. Ninajua una majukumu mengi na kwa vyovyote si wajibu wako kupanga misafara ya ziara zako, japo una mamlaka ya kutaka taarifa za kina ili pengine uelewe ni kwa nini hasa wananchi tunalalamika. Wasaidizi wako wana wajibu si wa kutetea ulazima wa safari zako tu, bali sasa watueleze na gharama zake halisi ili tutulie.

Kuna utetezi unaodai matumizi ya ikulu zikiwamo safari zenu viongozi wakuu ni masuala ya kiusalama na hayawezi kuwekwa wazi. Hili nalipinga, kwani gharama ya safari kujulikana hakuathiri usalama wako au wa nchi kwa njia yoyote ile.

Wananchi tunalazimika kuhisi kuwa huenda utetezi huu ukawa mkakati wa makusudi wa ufujaji fedha za walipa kodi na chanzo cha kinga ya upotevu wa mabilioni. Tusaidie kwa kututoa hofu hii.

Ni dhahiri lazima viongozi wetu wasafiri inapobidi. Hapa yanajitokeza mambo mawili. Moja, misafara ni mikubwa. Pili, misafara inafanywa kwa gharama kubwa zinazoweza kupunguzwa. Naelewa kila ukubwa wa msafara unategemea majukumu mliyojipangia, hata hivyo, ni ukweli usio wa siri kuwa wengi wa walio kwenye misafara yako na viongozi wengine waandamizi huwa zaidi wasindikizaji au watalii. Sina hakika kama wasaidizi wako wanakufahamisha gharama halisi za kila safari yako.

Mheshimiwa rais,

Misafara yako imekuwa ikisafiri daraja la kwanza (first class) au la pili (business class) na wachache daraja la tatu (economy class). Rais wetu na viongozi wakuu wengine wa nchi ni stahili yenu kusafiri daraja la kwanza.

Kisichoniingia akilini ni hii misururu ya mawaziri, wabunge na watendaji waandamizi wa serikali na hata wa mashirika ya umma nao kujikweza kusafiri daraja la kwanza ilhali watoto wetu wanashindwa kulipiwa chuo kikuu.

Gharama za madaraja haya ni ghali mno kwa uwezo wa nchi yetu. Kwa faida ya wananchi wetu pengine nitoe mfano. Wastani wa nauli ya safari moja ya ndege kutoka Dar es Salaam kwenda New York, Marekani na kupitia Washington DC huko huko Marekani na kurudi kwa daraja la kwanza ni wastani wa dola za Marekani 15,000 (fedha ya Tanzania sh 19,566,000) kwa mtu mmoja.

Daraja la pili (business class) ni wastani wa dola za Marekani 13,000 (fedha za Tanzania sh 16,957,200) kwa mtu mmoja. Safari hiyo hiyo daraja la tatu (upper economy class) ni wastani wa dola za Marekani 6,500 (fedha za Tanzania sh 8,478,600).

Daraja la mwisho kabisa (lower economy class) dola za Marekani 2,200 (sh 2,868,800).

Mheshimiwa rais,

Mawaziri na watendaji ndani ya serikali sasa wanajaa kiburi hadi kuanza kujiona wana hadhi ya gharama. Kama wanajiona wana hadhi, si wakajitegemee kama Watanzania wengine wanavyoishi? Mtumishi aliyepewa dhamana na watu anajipatia vipi hadhi kuliko waliompa? Hivi kweli kiburi hiki kinasababishwa na nini?

Nakuhakikishia, ni asilimia isiyozidi tano ya viongozi na watumishi wa umma wenye uwezo wa kusafiri daraja la pili (business class), achilia mbali la kwanza kwa kutumia fedha yao. Asilimia kubwa ni kuwa, hata wakitoka ofisini hata uwezo wa kupanda ndege hilo daraja la tatu hawana.

Hata wale wenye uwezo, inapokuwa ni lazima wasafiri kwa kujilipia binafsi hukumbuka busara zao na kusafiri kwa kubana matumizi. Sisi ni maskini na ni lazima tuishi kwa misingi ya umaskini wetu.

Mheshimiwa rais,

Pengine vilevile nizungumzie gharama za malazi za misafara ya viongozi wetu. Nikiri tena kwa heshima ya wadhifa wako, unastahili malazi yenye hadhi ya nyota tano.

Nikichukulia mfano wa hoteli uliyowahi kufikia New York ya New York Palace, Marekani, gharama ya malazi usiku mmoja bila kula ni wastani wa dola za Marekani 2,000, sawa na sh 2,600,000 kwa vyumba vyenye hadhi ya juu.

Vyumba vya kawaida kabisa katika hoteli hii ni wastani wa dola za Marekani 825, sawa na sh 1,075,800 kwa usiku mmoja bila kula. Hapa ndipo walipofikia wana msafara kutoka Tanzania, miongoni mwa nchi maskini zaidi duniani.

Wanamsafara ambao baada ya wiki mbili hivi wanarejea makwao kutumia maji ya visima, umeme wa mgawo na kusiko na mitaa wala mifumo ya maji taka.

Mheshimiwa rais,

Ni vyema tukikumbuka kuwa, madaraja haya ya ndege na hoteli yenye hadhi ya nyota tano wametengenezewa watu wenye uwezo, yaani kipato cha juu. Hizi ndizo hoteli za mamilionea wa dunia wakiwamo wachezaji wa kulipwa kama wa Real Madrid, wacheza sinema na wamiliki wa biashara za kimataifa.

Misafara yako imekuwa na watu wengi. Natambua unaposafiri na wafanyabiashara, huwa wanajilipia. Hebu serikali yako ijiulize ni mara ngapi watu wenye ‘fedha zao’ kwenye misafara yako wanasafiri daraja la kwanza?

Ni wachache mno. Sana sana wengi wao husafiri daraja la pili na la tatu. Wana uchungu na pesa yao. Wasio na uchungu ndio hao hulimbukia madaraja ya juu!

Hebu chukua mfano wa msafara wako wa wiki mbili kwenda Marekani wenye watu 40, unaweza kugharimu kiasi gani cha fedha. Nauli watu wanane daraja la kwanza, sh 19,566,000, kwa watu wanane ni sawa na sh 156,616,000. Wengine 15 daraja la pili, sh 16,959,200, jumla ya sh 254,388,000, na waliosalia saba daraja la tatu, sh 8,478,600, jumla ni sh 59,350,200.

Kwa mfano huu wa hesabu, nauli pekee ya msafara huu ni jumla ya sh 470,354,200, yaani shilingi milioni mia nne sabini, laki tatu, hamsini elfu na mia mbili tu!

Kwa hoteli ambayo ni sh 1,075,800 kwa mtu, kwa siku, ni kuwa kundi zima litagharimu sh 43,032,000, kwa siku. Siku 14 itakuwa sh 602,244,800. Yaani shilingi milioni mia sita na mbili laki nne na arobaini na nne na mia nane. Jumla ya hoteli na nauli pekee ni sh 1,072,599,000, yaani sh bilioni moja milioni sabini na mbili laki tano tisini na tisa tu!

Mheshimiwa rais,

Ukiongezea hapa gharama nyingine za chakula, posho, usafiri wa ndani wa magari, dharura, kusafirisha mizigo, vikao na visherehe vya hapa na pale sambamba na ufunguzi wa matawi ya CCM ni dhahiri gharama hizi zitafikia fedha za kutisha!

Nikumbushe historia kidogo. Wakati wa utawala wa Benjamin Mkapa na wewe ukiwa Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Waziri Mkuu wa wakati huo, Frederick Sumaye, aliandamwa sana kwa kile kilichoitwa matumizi makubwa ya safari yake moja kwenda Marekani. Alidaiwa kutumia sh milioni 500 yeye na msafara wake. Jambo hili lilitumika na kusukumwa sana na “mtandao”.

Pamoja na ukweli kuwa, matumizi yale hayakuwahi kupata maelezo ya kuridhisha, wengi hawakuliona kama mkakati wa kumshusha mbele ya jamii ya Watanzania.

Aidha, Watanzania wa kawaida hawakutegemea jambo hili lijirudie, tena kwa nguvu mpya, kasi mpya na ari mpya!

Mbona huko New York kuna hoteli nzuri tu za dola mia zinazolingana na hadhi ya umaskini wetu! Mbona tukienda wilayani tuko tayari kulala kwenye ‘guest’ za sh 10,000?

Ni dhahiri usiri na ufujaji wa fedha za wananchi hauko ikulu pekee. Maeneo mengi yana matatizo, tena yanayojengeka pale ofisi yako na ya Waziri Mkuu zinaposhindwa kuwa mfano wa kuigwa. Ofisi ya Waziri Mkuu kupata hati chafu ya ukaguzi ni kitendo cha aibu. Nani amfunge paka kengele sasa?

Ulivyolichukulia kwa wepesi suala la Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali ni jambo la kusikitisha. Watoto wetu wanaposhindwa sasa kusoma, hakika una kila sababu ya kumkumbuka Mwalimu na kutafakari!

Siku zote wanasiasa wa upinzani wanahoji, wanapuuzwa! Wanafunzi nao wamejaribu, wakapozwa na fulana, kofia na kadi za chama!

Walipoendelea wakatimuliwa kama vile waliowatimua wao walilipia chuo kikuu! Sasa wanahoji wafanyakazi hadharani kwa mara ya kwanza katika nchi hii! Kweli bubu akizidiwa husema!

Mheshimiwa rais,

Ni kweli! Hakika, Mwalimu na mzee Karume na serikali zao ‘waliona mbali’ wakaishi maisha ya kawaida yaliyofafanana na umaskini wetu, wakathamini wananchi kwa kauli na matendo, viongozi wetu wa leo ‘wakasoma bure na kufika hapa walipo.’

Mheshimiwa rais, tafakari!


lf.curl lf.curl2 rt.curl2 rt.curl