lf.bevel
MWANZO CHAMA SERA KATIBA TUUNGE MKONO UCHAGUZI TUWASILIANE
banner

2 Mei 2007

Waraka wa tano wa Mbowe kwa Rais Kikwete

na
Freeman Aikaeli Mbowe

MHESHIMIWA rais,

naendelea kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuniwezesha kuendeleza utii wangu kwa taifa langu na kwako kupitia tafakuri hii. Niruhusu japo kwa kifupi kufafanua msingi wa dhamira ya waraka wangu kwako na uhusiano wake na utata wa tafsiri ulioibuliwa na baadhi ya wasaidizi wako kufuatia nyaraka zangu kwako.

Mheshimiwa rais,

natambua na naheshimu sana, tena sana, mamlaka uliyopewa na katiba ya nchi yetu - licha ya mapungufu yake – ya kuwa rais na mkuu wa nchi yetu.

Aidha, natambua na kuheshimu majukumu mengi mazito uliyonayo ya kuongoza serikali. Hakika wewe binafsi na ofisi yako kama taasisi, unastahili utii kutoka kwa wote unaowaongoza kwani mbali ya kuwa ni ustaarabu na uungwana, ni wajibu wa sisi wananchi wako kutii mamlaka.

Naomba nikiri kuwa, sina chuki yoyote binafsi kwako, kwa viongozi wengine wakuu wa nchi na serikali yako, akiwamo makamu wako na waziri mkuu kama ilivyojaribu kuelezewa na tahariri ya gazeti la kila siku la serikali la Daily News toleo la Aprili 30, 2007.

Mheshimiwa rais,

kwa kuheshimu katiba hiyo hiyo, naamini utakubaliana nami kuwa, kama raia huru ndani ya nchi yako, nina uhuru wa kutoa mawazo kupitia fursa mbalimbali zilizoruhusiwa na katiba ambayo wote tuna jukumu la kuilinda.

Ni siri iliyo wazi vilevile kuwa, kwa nafasi yangu ndogo ndani ya jamii, nikiwa kiongozi wa chama cha siasa, ni wajibu wangu kuibua fikra, kuchochea mijadala na hata kukosoa pale serikali yako inapokuwa inatenda ndivyo sivyo. Nidhamu ya woga naikataa, kwani hata wewe binafsi umenukuliwa ukiwataka Watanzania waache kukupamba pasipo na sababu.

Nina hakika utaendelea kunivumilia, wakati nikiendelea kuwakilisha hofu halisi inayojengeka kutokana na kile ninachokiona kuwa ni usiri wa serikali kwenye mambo kadhaa yanayogusa maslahi ya umma. Nivumilie vilevile, ninapojaribu kukumbusha yale yote uliyotuahidi wananchi wako. Naamini kuwa mkweli ni sehemu ya utii wangu kwako na nchi yetu na kamwe si dharau.

Mheshimiwa rais,

kama kuna jambo moja linaloangamiza taifa hili ni nidhamu ya woga. Hili nimelizungumza mara nyingi. Kadhalika nimetambua mara kadhaa, mamlaka makubwa ya mimi kuhukumiwa na sheria - kama ni sheria za haki au hapana - sina nia ya kuingia kwenye mjadala huo. Mwenye nia mbaya na nchi yetu, kamwe hawezi kujitokeza hadharani na akawa tayari kuhesabiwa kwa kauli yake na kalamu yake.

Mheshimiwa rais,

natambua kuwa, ninapoandika waraka kwako, tena kupitia gazetini, siandiki barua binafsi, kwani wadhifa wako ni taasisi. Bali nawasilisha mbele ya umma wa Watanzania kupitia kwako, kama taasisi ya kiongozi mkuu wa nchi, nikilenga kukujulisha ni kitu gani kitutaabishacho sisi raia.

Ni dhahiri wasaidizi wako wana wajibu wa kuchukua hatua, kwa kutupa majibu yale yote halali yaliyostahiki tunayohoji kupitia waraka huu na majukwaa mengine halali.

Wasaidizi wako hata hivyo watatusaidia zaidi kama watajenga utamaduni wa kujibu hoja mbalimbali zinazojadiliwa na kuibuliwa na wadau tofauti kupitia vyombo vya habari, ili kuondoa dhana mbaya inayoweza kujengeka pale lugha kali inapotumika kuweka msisitizo na kuomba “attention” ya serikali yako.

Nina hakika utaendelea kuuona umuhimu wa vyombo vya habari vinapoandika habari za upande wa pili.

Inawezekana kabisa kwa sababu za kibinadamu, maneno mengine yakaonekana makali na yasiyopendeza; mengine yakapewa tafsiri ya matusi, dharau na hata uchochezi. Kama hilo limejitokeza, niwie radhi, kwani halikuwa kusudio na halitakuwa kusudio la tafakuri yangu.

Mheshimiwa rais,

naomba sasa niendelee na hoja yangu ya msingi ya kuchambua hotuba yako ya Desemba 30 mwaka 2005, wakati ukilizindua bunge jipya, ambayo kwetu ni dira yako kuhusu mustakabali wa taifa letu.

Chini ya kifungu cha siasa, ulizungumza yafuatayo:

“Mheshimiwa Spika; ni kweli nchi yetu sasa ni ya demokrasia ya vyama vingi. Lakini ni wazi bado utamaduni wa mfumo huu wa siasa ni mchanga na kwa ujumla haujaimarika vya kutosha. Tutajitahidi kujenga utaratibu na misingi ya mahusiano mema zaidi baina ya vyama vya siasa nchini Tanzania. Mimi naamini wakati umefika, kama alivyowahi kusema Rais Mkapa, kuwa tuwe na maadili yatakayotawala shughuli za kisiasa, ambayo hayategemei hiari ya viongozi wa kisiasa waliopo madarakani. Yanakuwa ni maadili na miiko ya lazima, yanayobana kila chama cha siasa, wanachama na viongozi wake, ikiwemo wale wa chama tawala.

“Tusipofanya hivyo — na dalili zimeanza kuonekana — wanaweza kujitokeza watu wakavuruga nchi yetu kwa kisingizio cha uhuru wa kisiasa. Uhuru bila mipaka ni fujo, na siwezi kukubali nchi mliyonikabidhi kuiongoza itawaliwe na fujo.

“Mheshimiwa Spika; Yameanza kujitokeza mawazo kuwa uongozi unaweza kununuliwa kwa fedha. Kama ni kweli, tusipokuwa waangalifu, nchi yetu inaweza kuwekwa rehani kwa watu wenye fedha za kununua uongozi au wanaoweza kupata fedha za kufanya hivyo. Ni kweli kwamba fedha ni nyenzo mojawapo muhimu katika kufanikisha uchaguzi. Lakini, fedha kutumika kununua ushindi si halali. Ni vema sasa tuanzishe mjadala wa kitaifa na hatimaye kuelewana kuhusu utaratibu halali, ulio wazi, wa chama au mgombea kutafuta fedha za uchaguzi; na utaratibu halali, ulio wazi, wa chama au mgombea kutumia fedha hizo. Na utaratibu tutakaokubaliana uwe ni sehemu ya maadili ya uchaguzi katika uchaguzi wa kiserikali na ndani ya vyama vya siasa. Katika mjadala huo suala la takrima nalo tuliangalie.”

Mheshimiwa rais,

hakika maneno haya machache kama yakitekelezwa, yanabeba jibu na suluhisho la mitafaruku mingi isiyo ya lazima ya hali ya kisiasa na kijamii nchini mwetu.

Sehemu hii ya hotuba yako, inatanabaisha mambo kadhaa. Kwamba unauona kuwa, mfumo wetu wa vyama vingi kuwa ni mchanga na kuna umuhimu wa kuwa na maadili ya kisiasa yatakayosimamia maridhiano na uendeshaji wa shughuli za kisiasa. Wananchi wako walifarijika zaidi waliposikia umeunda wizara nzima yenye jukumu la kusimamia na kutekeleza jambo hili.

Mimi naamini, hata hivyo suluhisho la kudumu si maridhiano ya kisiasa pekee, bali maridhiano ya kitaifa, yanayounganishwa na kusimamiwa kwanza kabisa na katiba, kisha sheria, kanuni na hatimaye taratibu.

Wanasiasa na vyama vya siasa ni sehemu tu ya wadau wa taifa hili, na hivyo ushirikishwaji wa wadau wote katika mchakato wa kuridhia na hatimaye kuiheshimu, kuilinda na kuitetea katiba ni jambo la msingi.

Mheshimiwa rais,

kwa umuhimu na uzito wa jambo hili, bado wananchi wako tunangojea kwa hamu utekelezaji wake, kwani ni miezi 16 sasa bado hatujaanza kuona dalili za utekelezaji wa dhamira hii.

Wapo baadhi ya watu wamekuwa wakitaka tukupe miaka mitano ndipo tujitokeze na kuanza eti kupima ahadi zako. Yapo yenye kuhitaji subira hiyo, kwani pengine yanahitaji kwanza kutafuta nyenzo za utekelezaji. Hili linahitaji dhamira ya kweli tu na si fedha.

Tunapokumbusha mambo haya, hatuna nia mbaya, la hasha isipokuwa tu, tunalenga kuweka msisitizo tukikumbusha kile tunachokiona kuwa cha msingi kufanywa kwa haraka.

Mheshimiwa rais,

jambo jingine lililojitokeza kwenye hotuba yako ni hili la ununuzi wa uongozi. Wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu, nikiwa mmoja wa wagombea urais, nilisema mara kadhaa kuwa, ule haukuwa uchaguzi, bali mnada wa kura.

Nilishtushwa na sehemu ya kauli kwenye hotuba yako iliyosema: “Yameanza kujitokeza mawazo kuwa uongozi unaweza kununuliwa kwa fedha. Kama ni kweli...”

Napata wakati mgumu kuamini kuwa mheshimiwa wakati ukitoa maneno hayo ulikuwa hauna taarifa kuwa rushwa, tena ya kutisha, ilikuwa imeshaanza kuwa mtindo wa kupata uongozi katika taifa letu.

Ushahidi wa hili ni rahisi kabisa; Jaji Joseph Warioba, aliyepata kuwa Mwenyekiti wa Tume ya Rais iliyokuwa ikichunguza mianya ya rushwa, amekuwa akilizungumzia tatizo hili la rushwa katika siasa, mara kadhaa sasa.

Mheshimiwa rais,

siku zote, panapokosekana taarifa sahihi - aidha kwa kutojua, kwa makusudi kwa nia ya kuficha ukweli au kwa udhaifu wa uwajibikaji - ni rahisi hisia kutawala.

Uchaguzi mkuu uliopita, ulitia aibu taifa letu. Naamini kwamba CCM bado haijapania kutokomeza rushwa ya uchaguzi, kwani kwa muda mrefu imekuwa ni moja ya silaha zake kubwa, kila mara wagombea wake wanapochuana na wapinzani ambao kwa kawaida ni “wachovu” wa kiuchumi.

Mheshimiwa rais,

matumizi makubwa ya fedha yasiyo na mipaka, limekuwa ni jambo la kawaida kabisa kwa wagombea wa CCM wanaochuana ndani ya chama hicho chenyewe na dhidi ya wapinzani kuanzia katika udiwani hadi urais.

Hadi leo hii, bado tunajiuliza hivi ni mabilioni mangapi yaliyotumika kwenye kampeni za udiwani, ubunge na urais za chama chako na nini kilikuwa chanzo cha fedha hizo?

Kwa bahati mbaya, CCM wala zile kamati zake za ushindi hazijapata kutueleza ni kiasi gani hasa cha fedha kilitumika. Kwa kweli hali hii imekuwa ikihalalisha hisia mbaya kushamiri.

Pasipo kuwa na maelezo yatakayosaidia kufuta hisia za namna hiyo, bado hofu kuwa baadhi ya wagombea walitumia fedha haramu zitaendelea kujitokeza.

Pamoja na yote, nakupongeza kwa ujasiri wa kuliona hili ni tatizo. Tayari miezi 16 imepita, tunasubiri kwa hamu mchakato wa marekebisho ya sheria yatakayoweka mipaka na ukomo wa matumizi ya fedha kama ulivyoahidi wewe mwenyewe, kwani jambo hili sasa linatuweka katika hatari ya kuwa na viongozi waliopatikana kwa misingi ya rushwa na hata fedha haramu ndani ya taifa letu.

Pamoja na kutambua tatizo hili, bado CCM iliendeleza utamaduni huu katika uchaguzi mdogo wa Tunduru. Aidha, mchakato wa kugombea uongozi ulioanza ndani ya chama chako, unaweza kuingia katika hatari hiyo hiyo hivi karibuni. Kwa sababu ya sheria kutokuwa tayari ni dhahiri, viongozi wengi watapatikana katika mazingira yale yale yaliyozingirwa na wingu la rushwa ile ile iliyokutia hofu wakati ulipotoa hotuba yako.

Kwa mtaji huu, hakika vita dhidi ya ufisadi, pamoja na kuundiwa sheria mpya, bado itakuwa tatizo, kwani watakaoisimamia, nao wanaweza kuwa wamepatikana kwa rushwa hiyo hiyo. Hakika, tatizo hili ni sugu ndani ya ya taifa hili na unahitaji “msuli wa ziada” kukabiliana nalo.

Mheshimiwa rais,

nakushukuru kwa kuendelea kunisoma, na kama kawaida, naahidi kuendeleza utii wangu wiki ijayo.

Mheshimiwa rais,

naomba kutoa hoja!

 

lf.curl lf.curl2 rt.curl2 rt.curl