lf.bevel
MWANZO CHAMA SERA KATIBA TUUNGE MKONO UCHAGUZI TUWASILIANE
banner

11 Aprili 2007

Waraka wa tatu wa Mbowe kwa Rais Kikwete

na
Freeman Aikaeli Mbowe

Mheshimiwa rais,

NASHUKURU tena Mwenyezi Mungu kwamba wewe na taifa letu mko salama, kwa maana kuwa hatuna mapigano ukiachilia mbali yale yanayosababishwa na majambazi.

Aidha, leo nimshukuru Mungu sana kwa jinsi alivyowajalia Watanzania uvumilivu, subira na matumaini. Wananchi wako wana shida zisizo na mfano ambazo nyingi zikisababishwa na chama na serikali unayoiongoza.

Bila mkono wa Mungu kuwapa uvumilivu na subira, vyombo vyetu vya ulinzi na usalama vingekuwa na wakati mgumu kweli kweli. Hata hivyo, wengi wao bado wana matumaini yatokanayo na kauli yako kuwa “maisha bora kwa kila Mtanzania yanawezekana.”

Mheshimiwa rais,

Niruhusu leo niingie moja kwa moja kwenye sehemu ya pili ya hotuba yako.

Naomba kwa faida ya uchambuzi na kumbukumbu, ninukuu neno kwa neno yale yote uliyosema kama sehemu ya kifungu cha siasa katika hotuba yako ya Desemba 30 mwaka 2005, ukizindua Bunge kule Dodoma. Hapa nanukuu:

"Siasa

Mheshimiwa Spika:

Chama Cha Mapinduzi kimerejeshwa madarakani kwa kura halali za wananchi zilizotupa idhini ya kutawala, tena idhini kubwa isiyo na shaka hata kidogo. Hatutaona aibu kuitumia idhini hiyo, kupitia Bunge hili, kutekeleza Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya 2005.

Kama mwana-CCM, nafurahia sana ushindi wetu. Lakini, nikiwa rais, napenda niwahakikishie wapinzani kuwa hatuna nia au sera ya kuua vyama vya upinzani. Serikali ya Awamu ya Nne itaendeleza, kwa dhati, mfumo wa siasa wa demokrasia ya vyama vingi. Ushauri wangu kwa vyama vya upinzani kwa wapinzani ni kuwa wasiwe wepesi kutafuta mchawi kila wanaposhindwa uchaguzi. Badala yake nawaomba wajiulize kwa nini Watanzania wamewakataa kiasi hicho. Nina uhakika watapata jibu"...

 

Mheshimiwa rais,

Nilijadili kwa kirefu katika waraka uliopita uzito unaoambatana na kauli yako. Nilibainisha kuwa, roho za Watanzania zaidi ya milioni 35 pamoja na jamii nzima ya kimataifa, inaona na ndivyo ilivyo kuwa kauli yako ni dira ya nchi. Ni mamlaka.

Nina hakika maandalizi yako ya miaka kumi kuitafuta hiyo kauli yanakuweka katika historia ya pekee. Kwamba hata Mwalimu hakutumia miaka kumi kupigania uhuru wa nchi yetu.

Hii ikichanganywa na miaka yako karibu ishirini ya uwaziri, iliyochanganyika na ubunge bila kusahau uongozi ndani ya chama chako, kwa hakika u kipimo na taswira sahihi ya aina ya viongozi na mfumo tulionao. Ni kipimo cha neema au laana ya nchi yetu.

Mheshimiwa rais,

Nikirejea kwenye sehemu ya hotuba yako iliyo kwenye mjadala leo, ni dhahiri basi kilichowakilishwa na kauli hii, kikipimwa na uwepo wako ndani ya Baraza la Mawaziri na hivyo serikalini kama nilivyoeleza hapo juu na ndani ya Kamati Kuu ya CCM kwa muda mrefu, tafsiri ni kati ya mawili.

Aidha, unathibitisha u-kinyonga na unafiki wa watawala wetu, yaani hulka ya kuuma na kupuliza; hulka ya kujifanya “hamnazo”. Zote hizi zikiwa ni sifa, kila mtu akiwa na tafsiri yake kama ni sifa nzuri au mbaya.

Upande wa pili, unaweza kuwa unathibitisha jinsi watawala wetu mlivyo mbali na wanasiasa wenzenu wa upinzani kiasi cha kutokujua mazingira na suluba wanazopata katika kupigania demokrasia, haki na hatimaye neema katika nchi yetu.

Nina hakika moyoni unajua kuwa si kweli kuwa matokeo ya kura yalikuwa ya “halali tena bila shaka”. Najua ilivyo vigumu kwako kukiri shaka iliyopo.

Si vyema vilevile, mimi kusema rais wangu kasema uongo na hivyo ni mwongo kwani utakuwa ni utovu wa nidhamu kwa utamaduni wa Tanzania, lakini ni dhahiri rais hukusema ukweli.

Umetoa changamoto kwa wapinzani kujiuliza imekuwaje wananchi wawakatae kiasi hicho. Wananchi hawajawakataa wapinzani, bali mfumo wa kiimla na kiharamia wa utawala wa nchi yetu ndiyo uliowakataa.

Ni kweli kambi ya upinzani ina matatizo yake. Yaliyo ndani ya uwezo wake na nje. Yapo ya kujitakia. Yapo ya kubambikizwa, haya yakiwa ndiyo mengi.

Mheshimiwa rais,

Unajua kuwa wapinzani hawakupambana na CCM. Walipambana na mfumo mzima wa utawala, wakiwemo viongozi na watendaji wote wa serikali, majeshi yote yakiwemo ya ulinzi, polisi, usalama wa taifa, KMKM na hata mgambo, tume zisizo huru za uchaguzi n.k. Walipambana na ufisadi na uharamia.

Walipambana na chama kokoro kilichobeba waadilifu kiduchu ndani ya kundi kubwa lililotafuta hifadhi ndani ya chama kwa kukiteka na kujitwisha ilani ya uchaguzi wasiyoiandaa, kuiamini na hata kuijua.

Walipambana na kundi lenye fedha nyingi za halali na haramu, likijumuisha wafanyabiashara halali, wezi na hata majambazi. Walipambana na watu wenye hofu ya kila aina, waliojiandaa isivyo kawaida kwa mema na shari sababu ya udhaifu wenu, naam, sababu ya kinga ya ufisadi baada ya uchaguzi.

Wapinzani hawakuwa dhaifu. Wangekuwa dhaifu usingewakimbia kwenye mdahalo wa uchaguzi mkuu dakika za mwisho bila maelezo ya kuridhisha kwa wananchi. Wengi wanaopenda kusimamia kweli na haki wanajua ushindi ule una shaka.

Mheshimiwa rais,

Hata kwenye sehemu ya kwanza ya hotuba yako, ulikiri kuwa kugombea kupitia upinzani ni ujasiri. Kunahitaji kujitoa mhanga na kujituma kwani mmepandikiza hofu kubwa kwa raia wengi walio wema.

Mifumo yetu ya utawala, sheria na zaidi katiba; vyote vikibarikiwa na kusimamiwa na dhamira mbaya na za kinafiki za kisiasa tena kwa kuitumia dola; vimerasimisha vitisho, uonevu, udhalilishaji na upendeleo wa aina mbalimbali dhidi ya wapinzani.

Vyote hivi vimefanyika kama sehemu ya mkakati haramu wa kunyima upinzani vitu viwili muhimu; rasilimali watu (human resource) na rasilimali fedha (financial resource).

Hizi ni sababu tosha na za uhakika za mkakati wa kunyonga upinzani, hata kama hupendi kukiri.

Mheshimiwa rais,

Leo mfumo huu umekuwepo kwa miaka kumi na tano. Huu si muda mfupi. Ni wazi kuwa kumekuwepo nguvu za ziada za kuukandamiza mfumo huu, nawe, kwa nafasi za uongozi ulizoshika, umeshiriki kikamilifu kwa njia halali na zisizo halali.

Hujawa wa kwanza kutoa kauli za kinafiki na za kutatanisha za kukusudia kujenga mazingira ya kuimarisha demokrasia.

Rais mstaafu, Benjamin Mkapa alikutangulia. Wote wawili, kwa kutumia kofia zenu kama watawala wakuu wa nchi, mmejenga utamaduni wa kutoa kauli za matumaini kughilibu taifa na wananchi wake, na kisha mnajifungia ndani kuweka mikakati ya kunyonga upinzani na hata demokrasia.

Angalau Mkapa alijulikana mapema kuwa si mkweli kutokana na tabia yake ya ubabe. Hakuweza kuficha unafiki huu kwa muda mrefu. Rangi yake halisi ilidhihirika kuelekea mwishoni mwa utawala wake. Dhambi ile ya “kula nyama ya mtu” aliyosema Mwalimu, ilihamia hata ndani ya chama chenu.

Unajua! Mwulize Mzee John Malecela. Mkishanyonga upinzani, mjiandae na nyie kunyongana wenyewe kwa wenyewe kama mlivyoanza. Wewe bado tunasubiri kuthibitisha rangi zako, kwani tumeshaziona.

Naomba unielewe. Kunyonga kwenu upinzani kunatekelezwa kwa njia nyingi. Ziko za siri zinazofanywa na makachero ndani ya chama chako ambazo unazijua. Mmetoa na mnatoa mafunzo mbalimbali, tena mengine mkiwatumia wanajeshi wastaafu kufundisha mambo ya kiharamia, huku juhudi zikifanywa kuhadaa umma kuwa ni mafunzo ya kiitikadi.

Itikadi ya chama haifundishwi na wanajeshi. Haifundishwi kwa siri. Mmefundisha vikosi vyenu vya kuhujumu na kuvuruga uchaguzi, hasa pale mnapolemewa. Mmefundisha vikundi vya kueneza propaganda chafu za makusudi za kuchafua vyama vingine.

Mafunzo haya yameumiza wengi, yanaathiri demokrasia na maendeleo ya taifa na unajua. Kibaya zaidi, yanafanywa kwa msaada wa serikali, yaani dola kwa kutumia kodi ya wananchi na wahusika wako juu ya sheria.

Mheshimiwa rais,

Kauli yako uliyoitoa bungeni, imepimwa kwenye uchaguzi mdogo wa Tunduru. Kama uhuni na uharamia uliofanyika Tunduru ndiyo tafsiri ya kauli yako ya Desemba 30, 2005, na hivyo dhamira yako kama rais na Mwenyekiti wa CCM, bora utumie wingi wa wabunge wako kubadilisha katiba kurejesha taifa hili kwenye mfumo wa chama kimoja!

Sisi Waswahili tuna hulka moja kuu. Tunaamini, kauli ni mali. Inapotolewa na mtu wa uzito wako, haiwi mali tu, bali kama nilivyodokeza awali, inakuwa mamlaka.

Hatuna utamaduni wa kuhoji na wanaohoji ni rahisi kuonekana watovu wa nidhamu machoni pa wanaohojiwa. Ni hulka ya kondoo.

Kondoo ni mnyama wa ajabu. Wengine humwona mpole. Wengine humwona mtiifu. Wengine mjinga. Ana hulka moja, ni mnyama asiyefikiri nje ya uzio au upana wa malisho yake. Kondoo, hana maamuzi yaliyo yake popote anapokuwa na mchungaji wake.

Siku zote kondoo humfuata nyuma mchungaji wake. Mchungaji akitoweka ghafla, kondoo huweza kushinda pale alipoachwa, hata pengine kukesha.

Ukijenga taifa la makondoo, utaongoza makondoo. Umesema, tena huko huko Dodoma, Watanzania wasikujaze sifa usizostahili, wakuambie ukweli. Ni kweli, tuko kilioni. Kukusifu kunakostahili na kusikostahili ni mkakati wa mawakala wa mtandao. Ni tunda la kazi yako. Ni sehemu ya ajira ya watu. Wewe umefika, wao safari imeanza, hivyo ni lazima utumike kama daraja. Nakupongeza kama kauli yako safari hii ni ya kweli.

Naam, turuhusu tukusifu kila unapostahili. Una haki kwani wewe si shetani usiye na jema. Hakika nakataa kuwa kondoo, lakini natii rai yako kwamba nikusifu unapostahili. Kwamba tukuambie ukweli.

Kama kweli, haya yote niliyoyaeleza hapa ni uzushi, fitina na majungu, niko tayari kuubeba msalaba wangu japo najua, kwa kusema tu ukweli tena wazi, naweza kutwishwa msalaba usionistahili. Niko tayari kwani ni sehemu ya utii na mapenzi yangu kwa nchi yangu.

Nakushukuru na naendelea kukuahidi kuwa utii wangu utaendelea wiki ijayo!

Mheshimiwa rais,
Naomba kutoa hoja!

 

lf.curl lf.curl2 rt.curl2 rt.curl