Naandika makala hii nikifikiri na kushukuru! Nashukuru kwa vile leo ni Januari 1, 2005. Nina
sababu zote za kumshukuru Mungu kwa kunichagua kuwa mmoja wa waliobahatika kuuona mwaka 2005.
Nafikiri, kwani ndiyo kwanza nimemaliza kusoma hotuba ya Rais wetu, Mheshimiwa Benjamin Mkapa,
ya kuaga mwaka 2004 na kukaribisha mwaka 2005.
Naendelea kufikiri nikiangalia luninga kuhusiana na maafa yanayoendelea kuwakumba binadamu
wenzetu sehemu mbalimbali za dunia. Maafa ya Kusini Mashariki mwa Asia yatakanayo na Tsunami
yananitisha.
Naumia zaidi kwani ni wiki chache zilizopita nilikuwa nchini Sri Lanka kikazi! Nilitembelea
maeneo kadhaa ambayo leo naona ni mahame na makaburi! Nabahatika kuwaona baadhi ya viongozi
waliokuwa wenyeji wangu wakihangaika! Nawaonea huruma wote! Ni watu wema! Munga awajaze ujasiri
wa kukabiliana na haya yote.
Hotuba ya Rais inazidi kunichanganya! Nashindwa kuelewa uchambuzi wake wa hali ya kisiasa ni
malalamiko, maagizo au majuto! Naamini halalamiki kwani Rais akilalamika, maana yake ni kasheshe
tupu! Mazingira yananilazimisha kuamini kuwa hotuba hii ni sehemu ya mkakati wa "Funika kombe
mwanaharamu apite."
Hotuba ya Rais kuhusu hali ya kisiasa naikubali. Kinadharia, imesheheni kila ukweli. Sina nia ya
kuchambua hotuba ya Rais, ila ni vyema tukakumbushana kuwa udhaifu wa vyama vya siasa leo ni
matunda ya "mchezo mchafu" wa Serikali ya Rais Mkapa. Namuomba Mungu amwezeshe kufanya miujiza
itakayosababisha kugeuza hotuba yake kuwa dhamira ya kweli ndani ya miezi 10.
Makala yangu leo ni sehemu ya mkakati wa kujadili mustakabali wa nchi yetu hasa tunapoelekea
kwenye Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani. Nitajaribu kuchambua nafasi ya asasi za
kijamii (civil society) ikijumuisha asasi zisizo za kiserikali (maarufu kama NGO) kwa upande
wa pili.
Umekuwa utamaduni wa kawaida sasa wa kusoma habari za kusulubu vyama vya siasa vya upinzani.
Wasomi wetu, waandishi wa habari na hata viongozi wa asasi kadhaa za kijamii wameongoza suluba
hii. Wengi hubeza kazi iliyofanywa na inayofanywa na wapinzani!
Sina hakika kama wengi wao wanaelewa kuwa udhaifu huu ni tunda la jamii dhaifu! Udhaifu huu wa
jamii ni wa njia nyingi na sio kusudio langu kuujadili leo. Wanadai haki fulani au mafanikio
fulani kutoka ndani ya vyama hivi bila kwanza kuangali wajibu wao katika kuviimarisha.
Sijitetei. Najadili. Ni sekta ipi katika jamii yetu leo iko safi kiasi cha kuthubutu kuhukumu
wengine? Ipi safi? Sekta ya Habari? Sekta ya Michezo? Taasisi ya Dini? Vyama vya Dini? Vyama
vya Hiari? Vyama vya Wafanyakazi? Sekta ya Elimu? Sekta ya Afya? Serikali?
Mwalimu Julius Nyerere aliwahi kusema - Ukiweka dodoki kwenye maji safi litanyonya maji safi!
Ukiliweka kwenye maji taka, kadhalika litanyonya maji taka! Hapo ndipo tulipo! Wote ni wadau wa
tatizo!
Ni Watanzania wangapi wa kundi hili wanaelewa ukweli wa siasa za Tanzania? Hebu fikikira! Jamii
nzima ya Chuo Kikuu eneo la Mlimani wako zaidi ya 12,000 ukijumuisha wanafunzi na wafanyakazi.
Wote hawa ni wapiga kura! Katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa 2004, waliopiga kura ni pungufu
ya 400! Unatarajia nini katika jamii kama hii?
Ni wangapi wa wasomi wetu wanajaribu hata kuvielewa vyama vya siasa? Ni wangapi
wanajishughulisha hata kusoma sera zao na mikakati? Ni wangapi huenda kwenye mikutano ya
hadhara? Nilikutana na mhadhiri mmoja wa chuo kikuu kimoja akaniuliza ni kwa nini tunahangaika
na "kauchaguzi haka ka mitaa? Kwani una faida gani kwenu?" Hawa ndio wasomi wetu! Na wako wengi
nchi nzima! Unatarajia nini?
Ni nadra sana kusikia Watanzania wa kundi hili wakikiri na kuheshimu sulubu na adha wanayopata
Wapinzani. Wengi wao bado hawataki kuheshimu ukweli kuwa kujitambulisha waziwazi katika siasa
za upinzani Tanzania ni kujitoa mhanga! Bado wanapenda kuamini kuwa wapinzani ni wabinafsi
wanaoangalia maslahi binafsi kuliko ya nchi.
Kadhalika, utamaduni wa kutotofautisha vyama katika kuvichambua hautendei haki vyama. Ni mara
chache sana kusikia wachambuzi hawa wakitofautisha vyama vya upinzani na hata viongozi wake.
Wanapokuwa na ujasiri wa kutofautisha, basi hufanya hivyo kwa kuangalia matokeo. Hawaangalii na
kuchambua msingi wa matokeo.
Nina imani kabisa kuwa kuna tofauti kubwa katika vyma vya upinzani. Utamaduni wa kulaani vyama
kiujumla kwa sababu tu haviungani dhidi ya CCM ni muono mfupi usiowapa Watanzania fursa ya
kujua ni vipi vyama hivi vinatafautiana kifikra, kimwelekeo, kinyenzo, kimtazamo, kisera na
hata kimaadili.
Ukweli kuwa upinzani bado ni dhaifu, hauuwi hoja kuwa vipo vyama vya upinzani ambavyo vinakua
pamoja na juhudi kubwa za Serikali na CCM kujaribu kuvidhoofisha. Sioni haya mahali popote
kusema CHADEMA inakua, pamoja na mazingira magumu sana ya utendaji kazi!
Wasomi na waandishi wa habari mara nyingi wamehoji udhaifu wetu. Tunaukubali na ni changamoto
kwetu viongozi wa upinzani. Tunawaomba ujasiri huo huo muutumie kulinganisha mazingira ya vyama
vyetu! Ni wangapi wamekwenda hatua moja mbele na kuangalia nyenzo za vyama vya siasa? Tuangalie
moja tu, ruzuku ambayo inatokana na kodi ya wananchi.
CHADEMA inapata ruzuku ya shilingi milioni 5 kwa mwezi. CUF milioni 90 kwa mwezi. CCM zaidi ya
shilingi milioni 700 kwa mwezi. Kwa hali hii ni dhahiri kuwa wanasiasa wa CHADEMA wanafanya kazi
ya "utume." Wanajitolea muda wao, mali zao na hata roho zao. Pengine wangestahili pongezi na
kupewa nishani kwa kujitoa mhanga kuwaamsha Watanzania na si kuwakatisha tamaa kwa kuwabeza!
Roma haikujengwa siku moja!
Dhana ya jumla ya kuwa adui ni CCM nina hakika imepitwa na wakati. Ni ukweli usiopingika kuwa
kuna watu wachache safi ndani ya CCM kama iivyo kwamba kuna watu wengi hatari na wachafu ndani
yake. Penye mlo siku zote "fisi" hawachezi mbali.
Hali kadhalika, hali ndani ya kambi ya upinzani kwa kiasi inashabihiana na ukweli huu. Kuna watu
safi na kuna watu hatari. Kwa mwamvuli wa kutetea wanyonge, siasa hugeuzwa chanzo cha mapato na
umashuhuri.
Wengi wa wasomi wetu wanajisikia kuwa wao ni wateule wachache ndani ya nchi hii. Pamoja na wengi
wao kusomeshwa na kodi za wananchi maskini, wengi wao wakiishi vijijini, wanaamini, wao wana
mchango mkubwa kwa nchi hii kwa kuwa ndani ya asasi za kijamii ama ajira zao nyingine!
Kuna hisia miongoni mwa jamii kuwa malengo ya asasi hizi za kijamii ni maslahi binafsi kwanza.
Yaani ni mkakati wa utafutaji kipato na ajira kupitia sekta mbalimbali ambazo asasi hizi
huwakilisha. Binafsi, naamini kabisa kuwa ziko NGO chache ambazo kwa kweli zimefanya na bado
zinaendelea kufanya kazi nzuri sana nchini.
Leo jamii ya Watanzania wenye ahueni ya maisha imejaa ubinafsi wa kutisha. Mtu akipata mafaniko
kidogo hasiti kujijengea uzio yeye na familia yake. Yanayotokea nje ya uzio hayamhusu! Watu hawa
hujitambulisha na watawala na hupata faraja kubwa. Wako juu ya sheria. Kauli za "nitakufunga,
usicheze na mimi" kwao ni utamaduni wa kawaida! Nakweli wamefunga watu!
Mbele ya watawala, watachanga mamilioni kwa kigezo cha kuleta maendeleo ya walalahoi hao hao
wanaosulubiwa na mfumo wa utawala. Hawapigi kura hawa, wala hawawajui viongozi wao wa mitaa na
vijiji! Wanawajua vigogo!
Hivi karibuni, kulikuwa na uchaguzi wa Serikali wa Mitaa. Mimi nauita utani wa demokrasia. Maeneo
mengine kama Hanang anakotoka Waziri Mkuu wetu, Mheshimiwa Frederick Sumaye, hadi leo uchaguzi
haujafanyika. Kulikoni?
Mambo mengi machafu yalijitokeza na bado yanajitokeza, kwani uchaguzi haujaisha! CCM wemejivunia
ushindi waliouita wa kimbunga! Sisi tunasema ni ushindi wa aibu! Majigambo haya yanatolewa na
kiongozi mmoja wa ngazi ya juu wa chama kilichong'ang'ania bila aibu kuwa mchezaji na mwamuzi!
Wasomi wetu na waandishi kimya!
Bahati mbaya zaidi kiongozi huyu kwenye siasa za uchaguzi aliishia kulamba patupu mapema kabisa
kwenye kura za maoni mwaka 1995. Hana historia ya kuchaguliwa katika siasa! Leo mwenyewe
anaogopa kugombea uchaguzi. Kajikata mapema na kudai "hagombanii Urais" ana jukumu maalumu!
Waziri "msimamizi" wa mchuano huu naye ana maneno ya karaha! Naye ni mtu wa kuzawadiwa nafasi.
Hajawahi kupigiwa kura na wananchi! Nafasi yake Kiserikali ni kwa fadhila ya Rais. Hajui uchungu
wa kuibiwa kura!
Haya, yupo mwingine, labda yeye aitwe MC (msema chochote). Naye kama mwenzie ni mtu wa kupewa
ubunge na uwaziri kwenye kisahani! Kubeza upinzani kwake ni utamaduni.
Wanasiasa wa kuteuliwa ni hatari, si kwa demokrasia tu bali hata kwa kauli zao. Wengi wa
wanasiasa wanaopewa nafasi za ubwete, ni wakandamizaji wa wazi wa demokrasia. Kama wamepata
bure, kwa nini waheshimu mfumo wa uchaguzi?
Wasomi na wanahabari wetu ambao tunataraji kwa nafasi yao ya usomi wangesaidia kuelemisha umma
namna uchaguzi huu usivyokuwa huru na wa haki, wanakazana kubeza matokeo ya vyama vya upinzani.
Kwamba uwanja haukuwa tambarare si hoja!
Duniani kumekuwapo mifuno mingi ya utawala. Kwa miaka mingi vyama vya siasa vilionekana kama
watoto wa demokrasia. Max Weber, mwanafalsafa Mjerumani katika masuala ya utawala, na mtunzi wa
kitabu mashuhuri cha "Principles of Management" katika karne ya 19 ndiye aliyetoa tafsiri hii.
Katika mifumo ya utawala wa miaka ya karibuni, kumejitokeza mkakati usio rasmi wa vyama vya hiari
kudhaniwa kuwa na uwezo wa kuchukua nafasi ya vyama vya siasa. Kama jinsi utitiri wa vyama vya
siasa unavyokua, utitiri wa NGO nao unapamba moto. Ni kawaida kusikia wahadhiri wa vyuo vikuu
wakilaani hali ya vyama vya siasa ilhali wao ni sehemu ya kuvidhoofisha!
Wengi wa wasomi mahiri nchini wanafanya kazi ndani ya NGO. Wamekuwa mahiri kuchambua nadharia
mbalimbali za mustakabali wa nchi. Sina hakika ni kwa kusudio la kweli la kuokoa nchi hii au ni
mkakati wa kujipatia chanzo cha uhakika cha mapato. Hawako tayari kuimarisha vyama vya siasa vya
upinzani kwani siasa hizi ni sulubu na njaa tupu!
Pale wengi wao wanapokuwa na ujasiri wa kuingi kwenye vyama vya siasa, basi itakuwa ni CCM.
Pengine ni kwa sababu ya maslahi binafsi. Wachache wenye kifua cha kuthubutu kujihusisha na
wapinzani honekana kama "mamluki" katika jamii yao!
Jumuia ya kimataifa imekuwa mstari wa mbele katika kulemaza wasomi wetu hawa. Mabilioni ya fedha
yametolewa kwa ajili ya kuanzisha, kupanua na hata kuendeleza asasi hizi za kijamii. Kazi hii
imefanyika juu ya mfumo dhaifu wa vyama vya siasa na hata asasi za kidemokrasia kama Bunge na
mabaraza ya madiwani. Asasi hizi za kidemokrasia zinanyongwa kwa kunyimwa rasilimali watu na
hata rasilimali fedha.
Wasomi kutimkia kwenye NGO imekuwa fasheni. Kuangalia upande mmoja tu wa jamii na kupuuza asasi
za kidemokrasia na vyama vya siasa kuna madhara makubwa kwa nchi zetu za dunia ya tatu hususan
Afrika.
Wasomi wengi siku hizi hupenda kuitwa "wanaharakati" lakini si wanasiasa. Kwao siasa ni aibu!!
Wanashiriki kudhoofisha vyama lakini wanakuwa wepesi kutokutafakari ni kwa nini vyama vya
upinzani vinakuwa dhaifu!
Rasilimali watu na fedha sasa inaelekezwa zaidi kwenye mipango ya kuimarisha asasi za kijamii
kwa kisingizio kuwa vyama ni dhaifu! Sijui ni nani aviimarishe na vipi! Wasomi wanangojea
vyama viimarike kwanza ndiyo waingie!
Asasi za kijamii ziko kwenye sekta nyingi. Haipingiki kuwa hatima ya asasi hizi huishia
kutegemea maamuzi yanayofanywa na asasi hizo hizo za kidemokrasia ambazo wao huziona dhaifu
na kuzibeza. Ni dhahiri kuwa asasi za kidemokrasia zikiwa dhaifu, maamuzi yake nayo yatakuwa
dhaifu.
Maendeleo ya nchi hayawezi kupata msingi mzuri kama mchakato mzima wa maendeleo hayo unaegemea
upande mmoja wa asasi za kijamii ambazo rasilimali nyingi hutumika kuziimarisha huku nguvu
kidogo sana ikielekezwa kwenye asasi za kidemokrasia.
Hatari ya hali kama hii ni kuwa mara nyingi huonekana kuna ombwe katika uongozi wa nchi. Udhaifu
wa asasi za kidemokrasia husababisha kuwa na Serikali legelege isiyowajibika kwa wananchi. Hali
hiyo hutoa nafasi kwa wanasiasa wenye kupenda umaarufu na madaraka (populist politicians)
kujaribu kuziba pengo.
Hii ndiyo hali tunayoiona kwenye nchi yetu leo ambapo kila mtu anataka kuwa Rais. Nafais hii
nyeti inaonekana kwa ni kitega uchumi na watu "wanuana." Wasomi wetu wanaishia kukusanya mafao
ya semina na tafiti, nchi inakwenda na maji.
Huu ni mwaka wa uchaguzi! Mabilioni ya pesa sasa yanamwagwa kwa asasi za kijamii eti kutoa elimu
ya uraia! Unafiki mtupu! Nina hakika kila NGO hata za sekta zisizohusiana na mbambo ya uraia
ziko kwenye mkakati wakuomba fedha kwa wafadhili ili "kutoa elimu ya uraia".
Wengi wa hawa wadau wasiotaka kujionyesha wazi wataelekeza "mafunzo" yao kwenye eneo walitakalo
na si mahitaji halisi yanayohusu uchaguzi.
Ni vyema ikakumbukwa kuwa kuibuka kwa asasi za kijamii duniani hasa kwenye miaka ya 1980 na 1990
kulichochewa kwa kiwango kikubwa na kukosekana kwa uhuru wa vyama vya siasa hasa katika nchi za
Ulaya ya Mashariki na Asia. Wimbi hili baadaye lilihamia Afrika.
Katika nchi hizi, vyama vya siasa ama vilikuwa haviruhusiwi au vilibanwa sana. Asasi hizi
zilitumika kuwa harakati za kweli za kudai demokrasia. Kadiri muda ulivyosogea, na vyama kupata
nafasi zaidi, wanaharakati wengi waligundua "utamu" ambao wengi wao hawakuwa tayari kuuacha na
kuingia moja kwa moja kwenye siasa.
Kwa upande wa pili, nchi nyingi za Magharibi na wafadhili kwao waliona ni fursa ya kuingia ndani
ya nchi hizi kwa mwamvuli usio wa kisiasa wa kutumia asasi za kijamii. Wengi wao walishachoshwa
na mfumo wa vyama vingi vya siasa kwenye nchi zao na wakataka sasa watafute mfumo mpya ambao
hautaingiliana na uhuru wa ndani wa nchi walizokusudia!
Ni ukweli usiopingikaa kuwa hata wafadhili hawa wengi wao wana nia za kitapeli. Hutumia matatizo
ya Afrika kuwaghilibu wananchi na serikali zao kutoa mamilioni ya fedha kusaidia demokrasia na
majanga mengine ya Afrika. Zaidi ya nusu ya fedha hizi hurudi kwao kwa vigezo ya malipo hususan
"consultancy" na hata zabuni mbalimbali.
Tumeshuhudia NGO nyingi zisizotaka siasa zikikwama kiutendaji shauri ya kukwaruzana na Serikali
kwa kuonekana zinaingilia mambo ya kisiasa. Nyingine hujihusisha na mambo mbalimbali ya huduma
za jamii, nyingine tafiti za kisiasa na kiuchumi,nyingine uangalizi wa uchaguzi.
Pamoja na kazi nzuri ambazo baadhi yao wanafanya, bado wanategemea kwa kiwango kikubwa wanasiasa
hao hao wanaowaona dhaifu kuwapa mwanya wa kutekeleza malengo yao!
Tatizo mojawapo kubwa la siasa za upinzani Tanzania ni nyenzo. Wanaharakati wetu wanajua kuwa
nyezo huweza kupatikana pale tu ambapo rasilimali watu sahihi inajihusisha na vyama vya siasa.
Hata watoe elimu ya uraia kwa miaka 100, kama vyama havitapata wagombea wazuri na nyenzo za kazi,
uwakilishi wa wananchi kwenye asasi za kidemokrasia utakuwa legelege. Serikali itaacha
kuwajibika na wanaharakati hawa watabaki pembeni hawana la kufanya ila kulalamika. Hali hii ipo
Tanzania leo na wasomi wetu wanaiona. Sijui wanangojea miujiza gani.
Si nia yangu kubeza kazi inayofanywa na vyama vya kijamii. Mchango wao katika jamii ni mkubwa.
Hoja yangu ni kuwa vyama vya kijamii leo vinadumaza demokrasia kwa kuvikaba pumzi vyama vya
siasa, hususan vya upinzani.
Naheshimu sana wengi wa viongozi wa NGO hizi! Wengi ni mashuhuri na wanaheshimika katika nyanja
mbalimbali. Naamini ni watu makini wanaoweza kutoa mchango mkubwa zaidi kwa nchi hii kama
wangeweka maslahi binafsi pembeni, wakaingia kwenye siasa bila hofu. Mara nyingi hupenda kusema
binadamu haishi kwa mkate tu!
Mwaka 2002 nilishuhudia mshikemshike kati ya "wanaharakati" na wanasiasa. Serikali ilileta
bungeni muswada wa sheria ambao pamoja na mambo mengine ilikusudia kudhibiti asasi zisizo za
kiserikali.
Ni dhahiri "wanaharakati" walitaharuki na kuhangaika kila kona ya eneo la Bunge. Walionekana
dhaifu. Wengi walihofu kupoteza ulaji pamoja na kutokuwa tayari kukiri hivyo. Wachache walikuwa
na sababu za msingi. Walisikitisha!
Siungi mkono udhibiti wa asasi zisizo za kiserikali, lakini si nia yangu kujadili mada hii leo.
Nia yangu ni kuwakubusha "wasomi na wanaharakati" wetu kuwa kupuuza siasa kunaweza kuwa na
madhara makubwa kwa maisha yao na kwa hakika hata kwa Watanzania wengine wanaowategemea
wawaonyeshe njia.
Nchi yetu inahitaji vyama vya siasa (si chama) vyenye nguvu na vyenye kuheshimu demokrasia, Bunge
lenye nguvu za hoja lisilitawaliwa na itikadi ya chama chochote! Tunahitaji mabaraza ya madiwani
yenye kujua wajibu wao! Yote haya hayaji kama ajali. Yanakuja pale jamii ya wasomi wanapokubali
changamoto ya kuitumikia jamii wanamoishi. Maprofesa, kazi kwenu! Nakaribisha mchango wa mawazo.