lf.bevel
MWANZO CHAMA SERA KATIBA TUUNGE MKONO UCHAGUZI TUWASILIANE
banner

21 Machi 2007

Leo ni raia…, kesho ni askari!

na
Freeman Aikaeli Mbowe

MAHABUSU wamegoma. Wamekubali kuendelea kusota ndani kufikisha ujumbe. Wamekubali kuteseka ili kuweka akilini mwa viongozi wetu kuwa, kama hawakubali kutoa haki, kuna siku watalazimishwa kutoa haki. Wanahitaji pongezi. Wameandika historia ambayo haitafutika. Kwa bahati mbaya, jamii haielewi kiongozi wa harakati hizi ni nani.

Angestahili kuwa na nafasi katika kumbukumbu za wanaharakati wa taifa letu. Tafakuri yangu ya Sera ya Majimbo itaendelezwa siku za usoni. Haijaisha, bali nimeihairisha kidogo ili kutoa nafasi ya kuchangia matukio muhimu yaliyojitokeza katika jamii.

Tafakuri yangu ya leo inakusudia kutanabaisha mambo ya msingi mawili. La kwanza, ni somo walilotoa mahabusu wetu kwa sisi wananchi wa Tanzania. La pili, ni somo walilotoa mahabusu kwa viongozi wa serikali na vyombo vingine vya umma vyenye wajibu wa kutoa haki.

Kile ambacho kilikusudiwa kuwa upendeleo wa kimkakati kwa “mwenzao” aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Tabora na kada wa muda mrefu ndani ya CCM, Ukiwaona Ditopile Mzuzuri, dhidi ya kesi ya mauaji inayomkabili, kimegeuka kuwa somo muhimu la kiharakati, ambalo Watanzania wanapaswa kulitafakari.

Ditopile anatuhumiwa kumpiga mtu risasi, tena inasemekana ni mbili. Kaua. Hakuna ubishi ingawa mahakama ndiyo itakayoamua. Kawekwa rumande. Kashtakiwa kwa kosa la kuua, hivyo hastahili dhamana. Uchunguzi kama upo unafanyika kwa kasi ya ajabu. Mashitaka yanabadilishwa. Kaua, ndiyo, lakini hakukusudia. Anastahili dhamana na anapewa dhamana. Kwa vipi hakukusudia? Ni swali ambalo pengine litajibiwa siku moja!

Watanzania wengi wanaungana na familia ya marehemu wakitaka haki itendeke. Wanawalilia ndugu za marehemu kwa mikono mitupu. Ndugu nao wanachachamaa wakidai hawakubali mpaka “kieleweke”. Vyombo vya habari na taasisi za kutetea haki za binadamu nao wanatoa matamko mengi.

Yote kwa wenye dhamana ya kusimamia haki, ni maneno tu ambayo hayavunji mfupa. Upande wa pili, serikali na “wenzake” wanahaha. Wanatafakari namna ya kumlinda mwenzao.

Mkakati makini wa kisanii unapangwa maeneo mbalimbali. Vyombo vya dola vinapewa jukumu, si la kutumia sheria kusimamia haki bali la kutumia udhaifu wa sheria kumlinda mwenzao. Katika hatua za awali kabisa, ndugu wa marehemu wanatembelewa na viongozi wa juu wa serikali.

Wao wanaamini wanapendwa na kuthaminiwa sana. Nina hakika hawakujua kuwa ni sehemu ya mkakati wa kuwafunga midomo. Kwani wao wakiridhika, “udhia utapungua.” Waliobaki wanaweza kuulizwa, pilipili wasizokula zinawawashia nini?
Wamepewa rambirambi na serikali! Sina hakika kama si kodi za wananchi. Misaada mbalimbali imetolewa kwa ndugu na jamaa wa marehemu. Mingine imetangazwa, mingine…!?

Viongozi wetu na wasaidizi wao ni wazoefu wa takrima. Penye udhia tia rupia. Ghafla ndugu wa marehemu waonekana kusimama upande wa mbaya wao! Ama kweli...! Kauli za “tunaishukuru serikali” zinapata nafasi. Kazi inaanza kuwa rahisi.
Penye kesi za mauaji, wadau wakuu ni wawili. Ndugu wa marehemu na jamhuri. Mashtaka huendeshwa na jamhuri. Msukumo wa ndugu husaidia kusukuma kesi. Wakitulizwa hawa, kazi ni rahisi kwani “jamhuri ni yetu!” Wanaofikiri ni yao waendelee kusubiri!

Tangu hatua za awali kabisa, polisi wanaonekana wakiwa na kila nia ya kumlinda Ditopile. Sikuwepo gerezani kujua alipohifadhiwa Dito. Hata hivyo, nitakuwa mwendawazimu nikidhani eti kweli Dito alikuwa rumande kwa misingi ya ukawaida wa rumande zetu, akila na kulala kama mahabusu wenzake.

Ndani ya mahabusu zetu, yako madaraja. Tupende tusipende, ndiyo hali halisi ilivyo. Inanikumbusha maandiko ndani ya kitabu cha George Orwell, cha Shamba la Wanyama (Animal Farm).

Katika kitabu hiki kilichoandikwa kabla ya vita kuu ya pili ya dunia, mwandishi anaandika; “all animals are equal, but some are equal than others.” Kwa Kiswahili chepesi, ni kuwa wanyama wote ni sawa lakini wengine ni sawa kuliko wengine!

Busara za kawaida zinaonyesha kuwa tahadhari kubwa ilitumika kuionyesha jamii kuwa, pamoja na kasi iliyotumika, sheria inafuata mkondo wake. Kila jambo lilienda kama lilivyopangwa. Hatimaye, Dito alipata dhamana.

Katika mkakati wa kumsaidia Dito, ni dhahiri kuwa jambo moja lilisahaulika. Awali halikuonekana madhara yake. Hili, ni namna ya kudhibiti kauli chafu za maringo za ndugu zake Dito ili waweze kula na “vipofu” bila kuwagusa mikono!

Wakilewa ukaribu wao na Rais Jakaya Kikwete, na wakijua fika kuwa mkakati wa nguvu umeandaliwa kumuokoa Dito, waliona wote wengine ni wajinga. Wakasahau ndugu yao amekuwa kiongozi wa ngazi mbalimbali za nchi hii na mashitaka yake yana nafasi kubwa kijamii.

Wakaonyesha tabia ya ajabu kabisa, ambayo haijawahi kuonyeshwa na ndugu wa rais yeyote katika historia ya Tanzania. Mambo ya ndugu na marafiki wa rais kuwa juu ya vyombo vya dola yakajitokeza kwa kiwango cha kutisha.

Kama vile kauli hazikutosha, sasa wakajipa wajibu wa kulinda mahabusu! Wakazuia na hata kuwapiga waandishi wa habari. Polisi wakaona na kubariki. Hii ni aibu si kwa Dito, bali kwa Rais Kikwete. Rais amejaribu sana kukaa kimya katika kesi hii.

Ni vyema ndugu zake wamefanya vioja. Ni busara atoe kauli ya kukemea hadharani, ili wengine tena wasiibuke na kudhani Watanzania walipomchagua Kikwete, walichagua marafiki na ukoo wake wote!

Hawa walifikiri wanamsaidia ndugu yao kwa jeuri ya ndimi na vitendo vyao. Wakati ni haki yao kumtetea na kumsaidia ndugu yao, ni vyema hata hivyo, ndugu hawa wakikumbuka kuwa wana wajibu muhimu.

Kwamba siku zote wanaposhangilia ndugu yao yeyote kuwa kiongozi pengine na kuonja utamu wake, wawe tayari kukubali na kukabiliana na changamoto hasi zinazoambatana na dhamana hiyo. Mimi si mpelelezi. Aidha, si hakimu. Sipendi kuingilia haki ya Dito. Hayo nawaachia wahusika. Muda utasema!

Hoja yangu leo inahusu utaratibu na fursa waliyotumia mahabusu kufikisha ujumbe wa kudai haki. Kwa kifupi, mahabusu wamedai kwa kukumbusha mambo ya msingi yafuatayo: Watanzania wengi wanabambikiziwa kesi, mfumo wetu wa utoaji haki (Polisi, Magereza na hata Mahakama) una tatizo la rushwa inayozaa uonevu na upendeleo.

Aidha, haki za binadamu hazithaminiwi magerezani. Mambo haya si mageni. Yamesemwa na yameandikwa sana. Mara zote serikali imejifanya kiziwi. Inapochukua hatua, basi huchukua bila haraka yeyote, ilhali mahabusu kwa maelfu wakisota jela kwa kesi za kubambikiwa sambamba na adha nyingine kadha wa kadha zitokanazo na mfumo wetu wa utoaji haki kuwa dhaifu.

Familia za mahabusu nazo huingizwa katika majaribu na kadhia nyingi kwa wanafamilia wao kujikuta katika matatizo wasiojua hatma na mwisho wake. Hata hivyo, udhaifu huu umekuwa neema kwa baadhi ya watendaji. Rushwa imeshamirishwa na kubarikiwa.

Katika sakata la Dito, serikali imejikuta uchi na hivyo kuwa katikati ya aibu. Kwa vigezo vyote, imeonyesha utendaji usio na uwiano na wenye misingi ya madaraja na upendeleo. Mahabusu wakaona mwanya, wakafanya kweli kufikisha kilio chao.

Yale ambayo yamezungumzwa kwa miaka nenda rudi bila serikali kujali, leo yanashughulikiwa wima wima. Serikali katika kujaribu kuficha aibu yake, inatumia kila silaha kujaribu kupooza mahabusu. Kumbe yanawezekana, lakini shurti kwa NGUVU!

Mara nyingi nimeandika na kuhubiri kuwa, utawala wetu hauongozwi na dira bali matukio ya shari (Management by crisis). Kwamba leo serikali yote (jopo la mawaziri), jeshi la polisi, mahakama, wizara ya sheria na taasisi nyingine kadhaa za serikali, zinafanya kazi kukidhi shinikizo la mahabusu.

Mahabusu wametoa somo. Serikali hii ya CCM haisikii bila ya nguvu kutumika. Kwamba mahabusu wamegundua “amani” kwao haisaidii kama wanaendelea kusota rumande. Walichokifanya mahabusu leo si kigeni katika harakati za kudai haki. Lakini ni kigeni kwa nchi yetu.

Hiki kinaitwa “civil disobedience”. Kwamba, wananchi wanaamua kuvunja sheria ili kushinikiza marekebisho ya sheria na taratibu za utawala. Katika civil disobedience, wananchi wanaamua kuvunja sheria. Wanakuwa tayari kwa kuadhibiwa na utawala wakijua ujumbe umefika. Walichokifanya mahabusu kuamua wao waendelee kusota jela ili kulazimisha mfumo wetu wa utendaji haki ubadilishwe, kimesababisha serikali kuchukua hatua.

Viongozi wetu mara nyingi wamekuwa viziwi wa matatizo ya wananchi kwa makusudi. Kama jambo haliwagusi moja kwa moja hawalishughulikii. Kama jambo linawaneemesha wao kwa gharama ya wananchi walio wengi, wanajifanya “hamnazo”!

Mahabusu hawa wamedhihirisha kuwa, viongozi wetu wanastahili kulazimishwa kusikiliza. Lazima walazimishwe kutenda. Busara za kawaida haziko kwao aidha kwa makusudi au kwa kukosa uwezo!

Ni hivi majuzi tu, wanafunzi wa vyuo vikuu waligoma, kudai nyongeza ya udhamini wa serikali. Serikali iliyoonyesha kuwadharau na kuwapuuza katika kilio chao, ghafla ikaanza kuona “umuhimu wa vijana wetu kupata elimu ya juu” baada ya maandamano. Cha kufedhehesha, wasomi wetu hawa tunaowategemea “wakanunuliwa” kwa bei nafuu, tena sana. Wakapewa maneno matamu, kisha wakavikwa fulana za kijani, biashara ikaisha!!

Hebu leo fikiria tatizo la usafiri wa watoto wetu wa shule. Limezungumzwa miaka nenda miaka rudi. Wananchi wanakosa maji, kimya, wanakosa umeme, kimya, bado wanaendelea kuiomba serikali iwafikirie na kuwaonea huruma! Hakika, Watanzania wataendelea kuumia hadi shida zitakapowaamsha na kugundua kuwa, “mahubiri ya amani ni kinga ya wajanja!”

Mambo kadhaa ni dhahiri. Watanzania walio wengi wana hali ngumu ya maisha. Wanashawishika. Wanadanganyika. Rushwa wanaichukia wanapotoa wao. Wakipata nafasi ya kupokea, wako tayari na kila msamiati utatumika kuonyesha uhalali wake. Rushwa ni rushwa. Haina mazingira.

Aidha, Watanzania wengi ni wasahaulifu. Watanung’unika, lakini hawatachukua hatua zozote kudhihirisha kwa vitendo kuwa, wanachukia dhuluma, maonevu au kukosekana haki! Kauli tu ya viongozi wa serikali inawatosha kuamini kuwa, viongozi wao wanawajali. Ni jamii nyepesi kusahau wingi wa ahadi za uongo kwa miaka nenda rudi.

Watanzania wengi vilevile ni waoga. Wanaiogopa sana serikali hata kama wanaona dhahiri haki yao na fursa vinapokwa. Wanatamani haki, lakini hawataki kuipigania! Hawataki msuguano, hawataki kuumia kwa lolote. Hawataki kukubaliana na falsafa rahisi kuwa, hakuna haki isiyopiganiwa na hakuna jema lisilotanguliwa na kuumia! Wanasahau haki hailetwi na vyama vya siasa pekee. Kwamba pale jamii nzima inapoona ina jukumu la kudai haki, tena kwa vitendo na ikibidi kwa nguvu, ndipo haki inapatikana.

Watanzania wataendelea kuhukumu sana vyama vya siasa hadi pale watakapogundua mapambano ya kudai haki na neema hayana mipaka ya kisiasa. Mahabusu wamefungua mlango. Raia wote wa nchi hii wana la kujifunza hapa. Wanajeshi na askari wote nao ni sehemu ya taifa hili, nao wanateseka vilivyo!

Hapa nitaambiwa Mbowe mchochezi. Anachochea wanajeshi wafanye mgomo! Wengine watatafsiri kuwa mgomo wa askari (wakiwamo wanajeshi) ni mapinduzi! Hata ikiwa hivyo, cha ajabu nini? Mbona Zanzibar wana serikali ya mapinduzi? Mbona hata chama kinachotawala kinajiita cha mapinduzi?

Tunaambiwa kila siku, askari hawapaswi kuingia kwenye siasa! Lakini kila siku tunashuhudia askari wakitumika na wakifanya kazi za kuhujumu haki kwa ajili ya CCM! Mkuki kwa nguruwe.

Ni aibu sana kuona askari waliokula kiapo wanakubali kugeuzwa makada wa CCM, kinyume cha kiapo chao! Taifa letu na watu wake wote, sasa tunastahili kuamka na kusimama kidete kudai haki. Rafiki yetu awe yeyote yule anayesimamia kwa vitendo kutoa haki sambamba na fursa za maisha bora kwa wote.

Adui yetu awe yeyote yule anayezuia haki na neema ya wengi kwa msingi wowote ule! Shida hukomaza. Mahabusu wa nchi hii kwa kweli hawana tofauti na wafungwa.

Wameteseka sana na sasa tayari wamekomaa! Leo ni wao, kesho ni wewe na mimi! Shime, wengine sasa tuendeleze harakati, kila mmoja kwa nafasi yake na wote kwa pamoja!

Kama hatutaki, basi ni haki yetu kuendelea kuumia, hadi hapo tutakapokubali kujitetea kwa njia yoyote dhidi ya yeyote anayetuumiza.

Siasa za Tanzania zimegeuzwa uongo na usanii. Ugumu wa maisha muda si mrefu utageuza utani historia.

Kwa nini tuweke mazingira ya kuruhusu fikra za mapinduzi ya kweli? Watawala makini husoma alama za nyakati!

 

lf.curl lf.curl2 rt.curl2 rt.curl