lf.bevel
MWANZO CHAMA SERA KATIBA TUUNGE MKONO UCHAGUZI TUWASILIANE
banner

28 Februari 2007

Nchi imekwama; tayari Kikwete amelemewa (3)

na
Freeman Aikaeli Mbowe


WIKI iliyopita nilimalizia makala yangu kwa kusema, Tanzania hata ukimleta malaika, kwa mfumo wetu wa utawala kazi itamshinda.

Hii ni kauli nzito. Inatia woga na inahitaji ujasiri kuitafakari na kuikabili.

Wanasiasa ni watu wa ajabu kidogo. Wanasiasa, watawala wa Tanzania ni watu wa ajabu sana! Hata wanapoona chembe ya ukweli, wengi hukataa kuukiri hadharani. Hapa ndipo dhana ya kukwama inapoota mizizi.

Bila kujali ni chama gani cha siasa kiko madarakani, nchi yetu inahitaji mabadiliko makubwa ya kifikra, kimtazamo na hivyo kimkakati. Ni muda muafaka sasa kuachana na mazoea.

Tufanye maamuzi magumu kwa ujasiri, tena bila woga, kama kweli tunakusudia kuiweka nchi yetu katika njia ya maendeleo endelevu. Lazima kama taifa, tukubali kutembea kwenye njia ya mabonde, vilima na miiba ili tufikie azima ya kujenga taifa lenye uhuru wa kweli, amani ya kweli na ya kudumu.

Maamuzi ya kuikwamua nchi iliyokwama kamwe hayawezi kuwa mepesi. Hayawezi kufikiwa kwa kukumbatia yaleyale na pengine walewale waliotukwamisha.

Hayawezi kufikiwa kwa kuchekeana wala kuoneana haya. Hayaji penye misingi ya kuleana na kulindana. Hayawezekani penye mwelekeo wa utawala wa kutaka sifa na mbwembwe (populist and pompous politics).

Hayawezi kufikiwa kwa viongozi wetu wakuu hususan rais kucha kutwa akitembeza bakuli la kuomba misaada nje ya nchi kwa wahisani na wafadhili bila kwanza kuweka misingi sahihi ya ndani ya kujikwamua.

Wawekezaji makini hawaendi kwenye nchi iliyojaa rushwa, isiyo na nishati na miundombinu ya uhakika, eti kwa sababu wameombwa na rais.

Nchi iliyoshindwa hata kuweka majina ya mitaa mipya maeneo kadhaa mapya yaliyopimwa ilhali meya anashinda uwanja wa ndege kupokea na kusindikiza kila kukicha.

Misaada tumepewa na tunapewa sana! Mikopo tumepewa na tunapewa sana! Madeni tumefutiwa na tunafutiwa sana! Bado tumekwama! Bado tunaomba! Tukipata kidogo cha ndani, tunakifuja kisha tunaendelea kukinga bakuli! Hivi hatuoni aibu?

Kwa kipindi cha miaka thelathini iliyopita, Tanzania ni nchi ya kwanza katika Afrika chini ya Jangwa la Sahara isiyokuwa na vita, kwa kupewa misaada ya kimaendeleo. Hili nalo ni ulemavu wa kutisha na chimbuko jingine la kukwama kwetu! Nitalijadili siku yake!

Wenye dhamana ya kuongoza taifa wanahitaji kuchagua kati ya mawili:

Mosi, utawala wa haki (justice) ambapo sheria na taratibu (law and order) zinasimamia fikra pana na mikakati endelevu (long term vision and sustainable strategies) zenye kwanza kulenga masilahi ya taifa na watu wake, Au, pili, kuendeleza utawala wa mazoea (business as usual) na wenye kutaka sifa ambao hutegemea zaidi kauli za viongozi sambamba na matukio ya dharura (management by crisis) bila kujali sheria na taratibu za nchi.

Katika makala zilizopita, nilijaribu kuainisha jinsi mfumo wetu wa utawala ulivyo hodhi. Mfumo unaorundika maamuzi yote nyeti yakiwamo yanayohusu miliki ya rasilimali zote kuu za taifa mikononi mwa kundi dogo linaloitwa Serikali Kuu.

Aidha, nilijaribu kuainisha jinsi Serikali Kuu, hususan rais alivyolundikiwa na kutwishwa majukumu makubwa ya kimaamuzi bila kujali ukubwa na upana wa mtandao wa nchi yetu na bila hata mifumo ya kumdhibiti!

Nilitoa mifano rahisi ya kufikirisha kuhusiana na hali ya kiuchumi ya Kanda (Jimbo) la Ziwa.

Leo nitaendeleza mjadala zaidi katika uchumi na nitajenga hoja kuhusu tija za kiuchumi zitakazoweza kutokana na mfumo wa utawala wa majimbo. Mfumo unaokusudia kutoweka mayai yote kwenye kapu moja.

Hizi ni fikra zangu binafsi zinazojengwa na uelewa pamoja na hisia zangu. Naziamini. Fikra zangu hizi zinatokana na uchambuzi binafsi wa mazingira yetu, uzoefu wa nchi nyingine mbalimbali sambamba na vionjo mbalimbali kutoka kwenye tafiti za wachumi mbalimbali wa zaidi ya karne tano zilizopita.

Si mawazo ya Benki ya Dunia (World Bank) au Shirika la Fedha Duniani (IMF). Si sharti, ni fikra mbadala zilizo wazi kwa mjadala.

Kwa ukubwa wa nchi, rasilimali zetu za asili na idadi ya watu, nchi yetu inaweza kugawanywa katika majimbo nane. Majimbo haya yatajitegemea kiuendeshaji (semi autonomous) isipokuwa kwa yale maeneo yatakayosimamiwa na sera kuu za taifa kwa mujibu wa maridhiano ya kikatiba.

Rasilimali za kila jimbo zikitumiwa ipasavyo kwa mikakati endelevu sambamba na ushindani unaoambatana na uhuru wa ushirikiano wa moja kwa moja kati ya jimbo na jimbo (inter province economic cooperation), kila jimbo katika kipindi cha miaka isiyozidi kumi ijayo, linaweza kuwa na uchumi unaolingana na uchumi wa taifa zima la Tanzania kwa sasa.

Kwa kuanzia, kila jimbo linaweza kuchagua vipaumbele vyake katika masuala ya kiuchumi na kuweka mkakati wa ndani wa kuviendeleza kutokana na mazingira yake. (specialization).

Mara nyingi, mitazamo yetu imelenga kuangalia kilichopo leo na kutoona fursa zilizopo. Tunakuwa wepesi wa kufikiria kuvuna bila kujua tuna wajibu mkubwa wa kupanda, kupalilia na kisha ndiyo hatimaye tuvune.

Kwa hali ilivyo leo, jimbo la Ziwa (mikoa minne ya Kagera, Mwanza, Shinyanga na Mara) linatoa zaidi ya nusu ya mauzo yetu nchi za nje.

Kanda ya Ziwa ingekuwa na uhuru wa kujiendeleza bila kuomba kila kitu sambamba na maelekezo kutoka Serikali Kuu, leo jimbo hili pekee lina uwezo (economic potential) wa kuwa na uchumi unaolingana na Tanzania nzima katika kipindi cha miaka isiyozidi kumi.

Kwa kuwa na uhuru wa kiuchumi bila kubughudhiwa na Serikali Kuu, sanjali na fursa za ziada (comparative advantage), serikali ya jimbo hili inaweza kujiwekea mipango yake endelevu na kuweza kuzalisha na kulisha bidhaa na vyakula si Tanzania pekee, bali pia nchi nyingine za Maziwa Makuu.

Aidha, inaweza kuweka taratibu zake za kisera za kiuchumi kulingana na msukumo wa soko katika eneo la Maziwa Makuu (market forces) kuliko kukwazwa na kifungo cha sera za biashara zinazotawala Tanzania nzima.

Nikiwa bungeni, nakumbuka mvutano mkubwa baina ya baadhi ya wabunge wa Mkoa wa Kagera waliokuwa wanailalamikia Serikali Kuu kuwanyima ruhusa wakulima wa kahawa wa mkoa huo kuuza kahawa yao Uganda.

Kwenye soko la Uganda ambalo halikuwa na urasimu, wakulima hawa waliweza kulipwa mara moja, tena bei zaidi ya mara tatu ya ambayo wangeipata kwa kuuza kahawa yao katika mfumo wa Tanzania .

Kwa mfumo wetu, kahawa yote huuzwa kupitia soko la kimataifa la kahawa la Moshi.

Leo hakuna hata mkoa mmoja umeweza kuweka mkakati wake wa ndani wa kuweza kuuza moja kwa moja bidhaa zake nje ya nchi. Makampuni yapo, lakini si katika mkakati wa kisera wa kimkoa.

Kuna Watanzania wengi tu ambao mfumo wetu ungeruhusu, wangeweza kuleta ufanisi wa kutisha katika majimbo mbalimbali.

Majimbo yote hayawezi kulingana katika rasilimali na hivyo nguvu za kiuchumi. Hii ni hali halisi ya maisha duniani katika nyanja yoyote. Kamwe, binadamu hawalingani.

Hata mikoa yetu leo ina tofauti kubwa za kirasilimali na kimaendeleo. Cha msingi hapa, ni lazima kuweka mfumo ambao utaweza kuendeleza majimbo yenye upungufu (na si uhaba) wa rasilimali, bila kuathiri au kukwamisha majimbo yenye rasilimali nyingi?

Mfumo wetu wa utawala, bila kujua umeendelea kuipokonya baadhi ya mikoa rasilimali watu wake (systematic internal brain drain) na kuwaamishia kwenye baadhi ya mikoa hususan Dar es Salaam panapoonekana kitovu cha kila kitu. Ukweli Dar es Salaam ni kitovu cha biashara tu.

Hali hii imesababisha baadhi ya mikoa kubaki duni kimaendeleo, na siri hapa ni utawala wa majimbo ambao sasa badala ya watu kukimbilia Dar es Salaam penye Serikali Kuu, watu watarudi kuendeleza kwao, na kikubwa zaidi kushiriki katika uongozi wa jimbo lao.

Ni vyema kukumbushana kuwa suala la uraia chini ya utawala huu ni suala la kitaifa. Hivyo kwenu si tu pale ulipozaliwa au kukulia, bali popote pale utakapoamua kuishi katika mipaka ya Tanzania.

Tujiulize, leo ni wasomi wangapi wakishapata shahada ya chuo kikuu au kufuzu elimu yoyote ya vyuo vya elimu ya juu mbali na wale walioko kwenye Serikali Kuu, Serikali za Mitaa na asasi zisizo za kiserikali hubaki mikoani, achilia mbali wilayani? Haya ni maswali magumu ya kujiuliza!

Juhudi za kujenga uchumi ni lazima sasa zipanuliwe na zisiwe suala la Dar es Salaam pekee.

Jimbo la kusini ambalo limependekezwa kushirikisha mikoa ya Lindi, Mtwara, Wilaya ya Tunduru na sehemu za kusini za Mkoa wa Pwani, ambalo leo huonekana mojawapo ya sehemu maskini ya nchi yetu, ni eneo lenye utajiri wa kutisha!

Gesi pekee, ingetosha kubadilisha uchumi na maisha ya Watanzania waishio eneo hili, achilia mbali, mabonde yenye rutuba, pwani ndefu na nzuri, korosho na hata madini ya vito! Lakini wapi!

Kila kitu kinabebwa, kama si kwa malori, ni meli na mabomba na kupelekwa Dar es Salaam kufidiwa na wajanja. Wananchi hoi! Wabunge wao kucha ni kulalamika na kuendelea kuiomba serikali iwaonee huruma. Ndugu zangu wa kusini, hapendwi mtu hapa! Siri ya mafanikio yenu iko mikononi mwenu!

Tunahitaji usimamizi makini, sahihi na wenye kujali rasilimali zetu (sustainable and starategic utilization of our natural resources).

Tanzania leo hakuna mkoa hata mmoja usio na rasilimali, achilia mbali mikoa kadhaa ikiunganishwa kuwa jimbo. Ni kosa kufikiri kuwa rasilimali zetu ni lazima ziwe madini na vito!

Watu na ardhi bila hata kipande kimoja cha madini ni rasilimali tosha ikiwekewa mkakati sahihi. Tanzania hatuna jangwa popote.

Lazima leo tukumbuke kuwa kwa mfumo wetu, uzembe wa Serikali Kuu, ni janga kwa nchi nzima.

Tukumbuke mfano hai wa ufisadi, uzembe na tamaa ya wachache katika Serikali Kuu na sekta ya nishati na umeme ulivyoweza kuingiza zaidi ya asilimia 80 ya taifa kwenye adha ya mgawo wa umeme!

Serikali Kuu tuliyo nayo leo ni sawa na mtaka yote kwa pupa ambaye hatimaye hukosa yote.

Kwa kuwa halmashauri za wilaya hazina chanzo cha uhakika cha mapato, Serikali Kuu hushika mpini, na hali hii imeathiri kwa kiasi kikubwa ari ya utendaji na hata tija ya wataalamu wachache walioko katika ngazi za wilaya.

Hebu tena tuchukue mfano mwingine wa Wizara moja ya Kilimo.

Nimekuwa bungeni kama mbunge na nimekuwa diwani katika Halmashauri ya Wilaya ya Hai, hivyo ninayoyaandika nimeyashuhudia na si mambo ya kubuni. Nimeshuhudia jinsi nchi nzima inavyotegemea Serikali Kuu kama chanzo cha mapato na hata maelekezo.

Tunaye waziri mmoja wa Kilimo anayesimamia kilimo nchi nzima. Kila kitu kinachohusu kilimo katika nchi hii kiko chini yake.

Kuanzia mazao makuu ya biashara kama pamba, kahawa, korosho, katani, chai, tumbaku, maua na pareto hadi mazao ya chakula, zikiwamo nafaka, mboga na hata matunda!

Ni wazi kwa mzigo huu, ufanisi hauwezekani, kwani ni vigumu kwa waziri hata na wataalamu wote wa wizara kuweza kusimamia sekta hii nyeti kwa tija inayostahili. Kwa upana huu wa majukumu, specialization haiwezekani.

Najua wengine watahoji kuwa mbona kuna wataalamu wa kilimo mikoani na hususan wilayani?

Hawa ni tegemezi. Hawana mamlaka wala maamuzi bila kibali cha Serikali Kuu. Asilimia zaidi ya 95 ya mipango yao inategemea mafungu na kibaya zaidi maelekezo kutoka Serikali Kuu.

Kwamba nchi nzima wenye akili ya kuwaza kuhusu kilimo wako Dar es Salaam tu!

Hawa ni kundi kibao la wataalamu wa kilimo ambao wenyewe si wakulima na utaalamu wao wa kilimo umeishia kwenye nadharia, na wachache tafiti miaka kadhaa wakiwa vyuoni.

Kwa mazoea na utamaduni huu, tutaendelea kuua kilimo, kumnyonga mkulima na kuukumbatia umaskini. Tutaendelea kubadilisha mawaziri wa kilimo na kila mmoja atatoka na lawama kuwa wizara imemshinda.

Tungekuwa na utawala wa majimbo leo, kila jimbo lingekuwa na wizara yake ya kilimo. Juhudi (kama zipo) zinazofanywa na wizara moja ya kilimo iliyoko Dar es Salaam leo, zingerudufishwa (multiplied) mara nane.

Tusingekuwa tumeweka mayai yetu yote katika kapu moja. Upungufu wa sera au uzembe wa kundi dogo lililoko Dar es Salaam, kamwe lisingekuwa tatizo kwa nchi nzima.

Kila Jimbo lingekuwa na sera na mikakati yake ya kilimo inayojitosheleza na inayotokana na mazingira ya jimbo. Hii ni pamoja na hali ya hewa, ikiwamo misimu ya mvua.

Katika hali hii, ni rahisi kila jimbo kuwa na mazao machache yanayoweza kuwekewa mipango madhubuti ya ugani (extention services) itokanayo na matokeo ya tafiti sahihi za eneo. (research and development through appropriate technology).

Badala ya kupanua Serikali Kuu, tunastahili kuipunguza na kutoa madaraka ngazi za jimbo ili kurahisisha maamuzi na kuruhusu mikakati ya kila jimbo kusimamia rasilimali zake na kuziendeleza.

Nilieleza siku za nyuma, kuwa Serikali Kuu inastahili kubaki na wizara nyeti hususan za Ulinzi na Usalama, Mambo ya Ndani, ikiwamo Uhamiaji, Fedha na Mambo ya Nje.

Kwa utaratibu utakaoafikiwa, kila jimbo litachangia sehemu ya mapato yake kwa Serikali Kuu kwa ajili ya miradi au mipango ya kitaifa.

Narudia na nitarudia sana. Hoja ya kuutazama upya muundo wa utawala wa nchi yetu unahitaji mjadala wa kitaifa. Utakuwa ni upungufu mkubwa na ufinyu wa fikra kwa yeyote kuliona suala hili kwa jicho la ushindani wa vyama vya siasa.

Tunaogopa nini kukabiliana na fikra hii sambamba na changamoto zake?

Maendeleo ya Tanzania yataletwa kwa kuweka maridhiano na masilahi ya kitaifa mbele.

Vyama vya siasa, taasisi na asasi mbalimbali zenye kujadili mustakabali wa nchi yetu na hata watu binafsi visiwe kikwazo kwa maridhiano ya kitaifa, bali viwe chimbuko la fikra mbadala za kulikwamua taifa letu lilipokwama.

Inaendelea sehemu ya nne



lf.curl lf.curl2 rt.curl2 rt.curl