lf.bevel
MWANZO CHAMA SERA KATIBA TUUNGE MKONO UCHAGUZI TUWASILIANE
banner

21 Februari 2007

Nchi imekwama; tayari Kikwete amelemewa (2)

na
Freeman Aikaeli Mbowe


WIKI iliyopita, nilianza kujadili hoja mpya iliyobeba kichwa cha habari kisemacho: “Nchi imekwama, tayari Kikwete amelemewa!”

Nilimalizia makala ile kwa kusema: “Sasa, hebu tuchambue bila woga ufisadi uliofanyika chini ya utawala wa Awamu ya Tatu, na ambao Serikali ya Rais Kikwete imeahidi kuuenzi na kuulinda, ikiupachika jina la wema! Mwanzo wa kulemewa kwake!”

Tafakuri yangu kuhusu hoja hii, itajadiliwa kwa makala kadhaa. Hivyo basi, ufisadi wa utawala wa CCM wa awamu zote (na si wa Awamu ya Tatu tu) baada ya kuondoka Baba wa Taifa kwenye uongozi, utajadiliwa katika mtiririko wa makala zangu kama jibu la kwa nini nchi imekwama na ni vipi Kikwete amelemewa litajibiwa.

Ningependa kuweka msimamo! Sifurahii nchi yetu kukwama. Sifurahii rais wetu kuelemewa. Nasikitika sana na ninamwonea huruma sana rais. Amebeba mzigo mkubwa na macho ya Watanzania milioni 38 yanamtazama yeye tu.

Pamoja na kuwa ni jukumu alilolitafuta kwa nguvu zote, kulemewa kwake kunaongezwa na kujikuta anakosa majibu mengi yatokanayo na majukumu kibao yanayomkabili. Ni matatizo ya kuwa na mfumo wa kumlimbikizia mtu mmoja ambaye ni rais na Serikali Kuu mamlaka ya kutisha.

Wengine tunaandika kwa sababu tunataka umma uelewe fikra zetu na uzihukumu au kuzitafakari kwa faida ya nchi yetu. Tunaandika ili watawala wetu waelewe watawaliwa wao tunawaza nini kuhusu muktadha wa nchi yetu!

Wiki iliyopita, niliandika na hata siku zilizopita nimepata kusema kuwa, mfumo wetu wa utawala umeshindwa kuutumia ukubwa wa nchi sambamba na utajiri wake wa asili na badala yake umekuwa sababu kuu ya kukwama kwa nchi yetu.

Serikali Kuu imejilimbikizia madaraka, sasa yanawalemea. Nchi ni kubwa mno, waziri mmoja na wizara yake hawezi kuongoza na kupata tija.

Mikoani na wilayani wanangojea fedha kutoka Serikali Kuu. Tumeua uwezo wa watu kufikiri na kujiendeleza. Lugha ni mfadhili na serikali ifanye hili na lile!

Mfumo wetu wa utawala kwa muda mrefu umejenga mlolongo wa viongozi wasio na ridhaa ya wananchi ‘kuwatawala.’

Wengi wa viongozi hawa wa kupachikwa, wamekuwa hawayaelewi maeneo yao ya kazi hadi siku wanapoteuliwa!

Wengi hutumia zaidi ya miaka miwili kujifunza utamaduni na mila za wanaowatawala! Wale wasio na uwezo wa kujifunza wanaendelea kuwa mzigo na kikwazo kwa wananchi wanaowatawala.

Hawa ni pamoja na wakuu wa mikoa, wakuu wa wilaya na makatibu tarafa. Wengi wao wanaishia kufanya kazi za uenezi wa chama chao kwani hana taaluma ya kumuongoza kufanya jingine! Utawala wa majimbo ungewataka waende kuomba ridhaa ya wananchi, hakuna dezo!

Hebu funga macho ufikirie na kutafakari: Mtu anateuliwa kuwa mkuu wa wilaya kuwaongoza watu zaidi ya laki nne. Kwa maana hii, anakuwa na mamlaka ya mwisho katika wilaya hiyo. Katika maisha yake yote, hajawahi kuishi au angalau kufika katika wilaya hiyo.

Mtu huyu katika maisha yake, hajawahi kuwa kiongozi katika ngazi yoyote. Pengine shuleni hakubahatika kuwa hata kiongozi wa darasa! Hana taaluma yoyote inayohusiana na utawala au uongozi wa watu. Anapikwa kwa ‘semina elekezi’ kwenye Hoteli ya kitalii ya Ngurdoto kwa wiki moja!

Ghafla anasimamia vyombo vya ulinzi na usalama! Anastahili kuwa na majibu ya mikakati ya eneo asilolijua! Ana mamlaka na roho za watu zaidi ya laki nne katika wilaya!

Ana bahati huyu! Anajuana na rais au waziri mkuu! Alipiga vigelegele sana wakati wa kampeni! Kapata zawadi! Nayo ni tuzo ya utawala asioujua, ambao kwa upande wa pili ni kukwama kwa wananchi wa wilaya hiyo kwa muda wote ambao rais ataamua kumbakisha hapo. Huku ni kufanya mzaha na maisha ya watu!

Ukuu wa wilaya sasa ghafla kila mtu anaona anaustahili. Hakuna vigezo wala sifa. Ni mapenzi ya ‘wazee’. Ukielezwa kundi la wapambe waliokuwa kwenye ‘waiting list’ baada ya Uchaguzi Mkuu utajua sasa uongozi si dhamana tena, bali ni vituko. Nakataa jambo lisilo na mipaka!

Wananchi wanahoji wabunge wao! Hawana uwezo wa kuwahoji wakuu wa wilaya. Wako pale kusimamia masilahi ya waliowateua na si wanaowatawala! Kwa mtaji huu tunategemea vipi miujiza ya maendeleo?

Wananchi nao kwa upande wa pili, hawawajui watawala wao wala historia yao, hadi pengine siku ya mazishi yao kwenye historia ya marehemu!

Mungu aepushe mbali! Siwatakii vifo ‘watawala wetu’ ila najenga hoja ya namna ilivyo vigumu wananchi kuwajua watawala wao wa kupachikwa!

Nikiri jambo moja. Wako wakuu wa mikoa, wilaya na hata tarafa ambao wamekuwa na uwezo na dhamira ya kweli ya kuwatumikia wananchi katika eneo walilopangiwa.

Wachache wamekuwa chachu ya maendeleo. Nawapongeza. Hata hivyo, hii haiondoi ukweli kuwa sasa muda umefika wa wananchi kutopachikiwa viongozi.

Hiki ni kionjo kimojawapo cha kusudio la sera ya majimbo, kwamba viongozi wetu wa kisiasa, wachaguliwe na wananchi na wawe na ridhaa ya kuwaongoza. Wale wa kuteuliwa na rais, wawe kwa mujibu wa taaluma na uadilifu wao.

Aidha, pawepo mipaka ya mwingiliano katika utendaji wa chama cha siasa na serikali, kwani tumeridhia siasa ya mfumo wa vyama vingi, hivyo tuna wajibu wa kucheza kwa mujibu wa sheria zake.

Tafakari nyingine muhimu ni kusudio la mkakati wa kutumia kwa faida ukubwa na utajiri wa nchi yetu. Kwa hali ilivyo leo, mamlaka yote ya rasilimali za asili za taifa hili yanamilikiwa na Serikali Kuu ikitokea Dar es Salaam.

Mayai yote tumeweka mikonnoni mwa kundi la watu wachache. Wanapokosa mwelekeo, Watanzania wote wanakwama. Tanzania leo ni Dar es Salaam. Ukichunguza takwimu utaona uchungu na kuwasikitikia Watanzania hasa wale waishio mikoani.

Makusanyo ya kodi za serikali, ni kigezo kizuri cha kupima uwezo wa watu wa kununua bidhaa na huduma katika eneo lolote.

Katika kujenga hoja yangu, nitatumia takwimu za msingi kuhusu Mkoa wa Dar es Salaam dhidi ya mikoa mingine hususan Kanda ya Ziwa, yaani Mwanza, Shinyanga, Mara na Kagera.

Nitajenga hoja kuwa, rasilimali ziko mikoani, takwimu za makusanyo sanjali na fedha kiasi zilizokusanywa ziko Dar es Salaam ilhali maisha bora na fedha za uhakika zikiwa katika nchi za wawekezaji.

Hebu linganisha mapato ya Mamlaka ya Kodi Tanzania kwa miaka ya fedha 2004/2005 na mwaka 2005/2006 kwa mujibu wa taarifa za TRA.

Mwaka wa fedha 2004/05, TRA walikusanya shilingi trilioni moja, bilioni 679 na milioni nane.

Kati ya hizi, shilingi trilioni moja, bilioni 71, milioni 442 zilikusanywa katika Mkoa wa Dar es Salaam. Hii ni sawa na asilimia 82 ya mapato yote ya serikali yatokanayo na kodi.

Mikoa mingine yote iliyobakia ilikusanya shilingi bilioni 299 milioni 802, ambazo ni sawa na asilimia 18 tu ya mapato ya serikali kupitia kodi.

Mkoa wa Mwanza ulikusanya shilingi bilioni 37, milioni 52 tu kwa mwaka, sawa na asilimia 2.2 ya makusanyo ya nchi nzima. Shinyanga ilikusanya bilioni 18, milioni 689, ambazo ni asilimia moja nukta moja (1.1%) ya mapato ya TRA kwa mwaka!Mkoa wa Kagera ulikusanya shilingi bilioni saba, milioni 252, sawa na asilimia sifuri nukta nne tatu (0.43%), na Mkoa wa Mara ulikusanya shilingi bilioni 34, milioni 548, sawa na asilimia 1.82 (1.82%) ya mapato ya TRA.

Kanda nzima ya Ziwa yenye wakazi zaidi ya milioni 10 ilikusanya kodi ya shilingi bilioni 93, milioni 683 sawa na asilimia tano nukta tano saba (5.57%) ya pato la taifa!

Mwaka 2005/06, TRA walikusanya shilingi trilioni 2, bilioni 40, milioni 393. Mkoa wa Dar es Salaam pekee, ulikusanya shilingi trilioni moja, bilioni 697, milioni 321. Hii ni sawa na asilimia themanini na tatu (83%) ya mapato yote ya serikali yatokanayo na kodi.

Mikoa mingine yote iliyobakia ilikusanya shilingi bilioni 343, milioni 75, ambazo ni asilimia 17 tu ya mapato yote ya TRA kwa mwaka.

Mkoa wa Mwanza ulikusanya shilingi bilioni 40, milioni 696, sawa na asilimia moja nukta tisa (1.9%). Shinyanga ilikusanya shilingi bilioni nne, milioni 889; sawa na asilimia sifuri nukta mbili tatu (0.23%) ya mapato ya nchi nzima.

Mkoa wa Kagera kwa mwaka huo wa 2005/06 ulikusanya shilingi bilioni sita, milioni 619, sawa na asilimia sifuri nukta tatu mbili (0.32%) ya pato lote la TRA kwa mwaka.

Mkoa wa Mara ulikusanya shilingi bilioni 34, milioni 548, ambazo ni sawa na asilimia moja nukta sita tisa (1.69%).

Kanda nzima ilikusanya shilingi bilioni 86, milioni 742 kwa mwaka, ambazo ni sawa na asilimia nne nukta 25 (4.25%) ya pato lote kwa mwaka.

Kanda ya Ziwa ina utajiri wa ajabu. Kuanzia idadi ya watu, ardhi safi, mvua za kutosha, ziwa, madini, pamba, mifugo n.k

Mauzo ya nchi kwenda nchi za nje (exports) yanategemea sana kanda hii. Katika mwaka 2006, kwa mujibu wa taarifa za uchunguzi, dhahabu ambayo hutoka kanda hiyo ilichangia asilimia 43.7% ya bidhaa zote zilizouzwa nje.

Samaki wa Ziwa Victoria walichangia asilimia 8.2 na pamba asilimia 3.3. Bidhaa hizi tatu za Kanda ya Ziwa pekee zimechangia asilimia 55.2 ya bidhaa zote zilizouzwa nje ya nchi.

Kwa ulinganisho wa makusanyo ya kodi na uuzaji bidhaa nje zilizotokana na kanda hii, ni dhahiri kuna mushkeli wa kutisha katika mikakati yetu ya kumiliki na kufaidisha wananchi na maliasili zao.

Aidha, ni ushuhuda tosha kuwa, maliasili nyingine kibao zilizozagaa nchi nzima hazijawekewa mkakati wowote. Wote wanasubiri Serikali Kuu na kituo kimoja cha uwekezaji kitafute wawekezaji! Tunajilundikia majukumu yanayotuelemea.

Je? Kama mauzo nchi za nje kutoka Kanda ya Ziwa ni makubwa kiasi hiki, inakuwaje kodi yake iwe ndogo mno? Huu ni ushuhuda kuwa ‘wajanja’ (wezi hawa) wanaivuna kanda hii na kuwaacha wananchi katika umaskini wa kutisha.

Najua watajitetea kuwa makampuni makubwa yanalipia kodi Dar es Salaam. Wanaweza hata kudai kodi inayokusanywa si kigezo cha kupima umaskini! Mimi nasema ni kigezo tosha!

Ni dhahiri basi, kanda hii itabaki kuambulia mapanki, mashimo ya migodi, vumbi la migodi na misaada midogo ya zahanati, barabara za vumbi pengine na madarasa.

Kodi inaondoa fedha mifukoni mwa wananchi. Ikikusanywa, ni uthibitisho wa mzunguko halali wa fedha unaoambatana na uwezo wa kununua bidhaa na huduma kwa wananchi. Ni uthibitisho wa uchumi kumilikiwa na wenyeji.

Nina hakika, pangekuwa na serikali ya Kanda ya Ziwa (Jimbo la Ziwa), yenye viongozi wa kuchaguliwa na wananchi wa kanda hii, yenye mamlaka na maliasili, nao wakahusishwa sambamba na Serikali Kuu, mapato ya maliasili hizi yasingefujwa na kuhamishwa kwa kiasi inavyofanyika sasa.

Serikali hii ya kanda yenye kuwajibika kwa wananchi wake ingesimamia maliasili ile. Ingekuwa na kituo chake cha uwekezaji kusaidia mikakati ya kanda. Ingelipa fungu kubwa la mgawo kwa Serikali Kuu. Serikali Kuu ingetumia fungu hilo kusaidia kikamilifu maeneo mengine.

Serikali Kuu imejikuta ina mamlaka na mali nyingi kiasi cha kushindwa kuzidhibiti.

Kwa kweli ya Mungu, ni laana kwa Kanda ya Ziwa kuwa maskini kiasi hiki. Hii ni kanda inayotoa wabunge wengi, tena wa CCM, na sijui ni kwa nini hawalioni tatizo la kanda yao. Sijui wanangoja nini CCM – labda uwaziri.

Nasisitiza, Kikwete amelemewa. Tunahitaji ku – overhaul nchi hii, ndiyo mwanzo wa salama yetu!

Tumekwama, tusione haya kukiri! Nimesema na ninarudia: “Tanzania, hata ukimleta malaika, kwa mfumo wetu wa utawala – kazi itamshinda!”

Inaendelea sehemu ya tatu



lf.curl lf.curl2 rt.curl2 rt.curl