lf.bevel
MWANZO CHAMA SERA KATIBA TUUNGE MKONO UCHAGUZI TUWASILIANE
banner

7 Februari 2007

Shirikisho: Zanzibar wana hoja, Tanganyika tuna woga

na
Freeman Aikaeli Mbowe


LEO napenda kujadili fikra zangu binafsi kuhusu mchakato wa kukusanya maoni ya wananchi kuhusiana na kusudio la kuanzishwa kwa Shirikisho la Afrika ya Mashariki.

Nimefuatilia kwa karibu maoni mbalimbali ya wadau kuhusiana na mpango mzima wa shirikisho. Makala yangu itajikita zaidi katika hoja mbalimbali zilizoibuliwa na wadau kupitia vyombo vya habari vya nyumbani, mitandao mbalimbali ya tovuti na hata mazungumzo ya kawaida ya vijiweni.

Maoni mengi niliyoyapitia, yanabainisha jambo moja kubwa kwa mtazamo wangu. Kwamba Zanzibar kuna hoja na Tanganyika kuna woga tena wa kutisha. Nitafafanua.

Hofu na woga:

Hofu na woga unaowatawala Watanzania umejikita katika mambo yafuatayo miongoni mwa mengine:

  • Uchumi: Tanzania itamezwa kiuchumi - Kenya hapa ndiye victim mkuu. Kwamba wameimarika zaidi katika biashara, kilimo, viwanda, taasisi za fedha, sarafu na viashiria vingine vyote vitakavyoweza kufikirika ikiwemo uzoefu wa ujasiriamali na mitaji. Kwa nguvu hii, tunaogopa rasilimali zetu hususan maliasili - madini, misitu, mbuga za wanyama, nk. zitawaneemesha zaidi wao!

  • Kijamii: Ajira zitazibwa kwa Watanzania. Ukabila ni tatizo kubwa kwa washirika wetu. Kwa mara nyingine Kenya ni victim mkubwa zaidi kwenye hili. Hofu ya udini imejiokeza maeneo machache.

  • Siasa: Jirani zetu hawa hususan Rwanda, Burundi na Uganda watatuletea vita wakati sisi tuna amani! Ni wababe hawa! Sisi ni watu wapole! Kwa nini Yoweri Museveni wa Uganda anataka kutawala Shirikisho? Jirani zetu ni mabepari, sisi ni wajamaa!

  • Matayarisho: Wananchi hawajaelemishwa. Serikali inaburuza wananchi!

Hoja za Zanzibar

Kwa upande wa Tanzania Zanzibar, kuna hoja za msingi ambazo zimeibuliwa tena na viongozi wenzetu wa Visiwani. Nasema tena kwani mambo haya yamezungumzwa mara nyingi CCM na Serikali yake wakayapuuza!

Watanganyika wana somo moja la kujifunza kutoka Zanzibar, kuwa, linapokuja suala la maslahi ya Zanzibar (ndani na nje) dhidi ya nguvu nyingine yeyote ile, wenzetu hawa husahau itikadi zao na wote huwa kitu kimoja.

Nawapongeza sana kwa hili. Hoja za msingi zilizotoka Zanzibar - hadi tume ikakimbia - ni pamoja na:

  • Nafasi ya Zanzibar kama nchi katika Shirikisho iko wapi - Hii ni kuzingatia kuwa Shirikisho linakusudia kuunganisha nchi hizi katika ujumla wake kuwa moja na Zanzibar haijatambuliwa kama nchi.

  • Ni kwa nini tusimalize kwanza kero za Muungano pamoja na migongano yetu ya ndani kabla hatujafikia hatua ya Shirikisho?

    Rais Kikwete anasema cha msingi ni kuwasaidia Zanzibar waanzishe viwanda waweze kushindana! Hadithi ya kipofu kumwongoza kipofu! Rais wetu ni bingwa wa kutoa matumaini! Mtu apewe sifa zake!

    Naomba nieleweke. Bila kuathiri mtazamo wangu binafsi, naheshimu sana maoni mengi yaliyotolewa na Watanzania wenzangu.

    Kwa takwimu za haraka, Tanzania ndiyo nchi iliyobahatika kuwa na zaidi ya nusu ya eneo zima la Shirikisho lililokusudiwa. Nchi hizi nyingine nne kwa pamoja hazifikii eneo la Tanzania. Aidha, kama nchi tuna idadi kubwa ya watu kuliko wenzetu hawa.

    Kila nchi ina ukubwa kwa kilometa za mraba ni kama ifuatavyo. Idadi ya watu iko kwenye mabano: Jumla ya eneo la Afrika ya Mashariki ikiwemo Rwanda na Burundi 1.8 millioni km; Tanzania 945km (watu 38 milioni); Kenya 580km (watu 34 milioni); Uganda 236km (watu 27 milioni); Rwanda 26 km (watu 9 milioni) na Burundi 28km (watu 8 milioni).

    Kama Taifa, tuna mengi ya kujiuliza, na tuna kila sababu za kutafakari yaliyotusababishia Watanzania kujikuta na unyonge huu. Imeenda wapi jeuri tuliyoachiwa na Nyerere?

    Binafsi, mara nyingi nimeandika namna taifa letu limejawa na hofu na woga. Nina hakika wengi walifikiri ni lugha za ‘mfa maji’. Leo Taifa linatetemeka! Tumejitakia wenyewe na tuna wajibu wa kubeba msalaba wetu!

    Zamani Watanzania walikuwa na jeuri pamoja na umaskini wao. Watanzania walijisikia sana. Leo jeuri kwisha! Sasa tunahaha kutafuta mchawi toka nje wakati wachawi tunao humu humu ndani. Tunahitaji kutafakari chimbuko la aibu hii ya kufedhehesha.

    Tumeiogopa CCM na Serikali yake kwa muda mrefu, tumekuwa wepesi kukubali viongozi waipeleke nchi hii wanavyotaka na sasa tunalalamika wakati kimsingi maamuzi ya kuingia shirikisho yameshafanyika.

Programu ya Afrika ya Mashariki

Ningependa kuwatahadharisha Watanzania wenzangu kuwa leo tunakumbuka shuka wakati kumekucha. Uelewa wetu kuhusu mchakato mzima wa Afrika ya Mashariki ni mdogo sana.

Yapo maamuzi mengi ya msingi ambayo yameshafanyika nasi bado tumelala. Hapa nikumbushe machache.

  • Novemba 30. 1993 Marais Mwinyi, Museveni na Moi walikutana Arusha na kukubaliana kuunda tume ya pamoja ya ushirikiano wa Afrika ya Mashariki (East Africa Tri-Patriate Commision for Cooperation). Tume iweke mkakati wa kushirikiana katika nyanja za siasa, uchumi, mambo ya kijamii na utamaduni, utafiti na teknolojia, ulinzi na usalama pamoja na sheria na mambo ya usalama.

  • Novemba 30, 1999 makubaliano ya kuanzisha eneo huru la Biashara (East Africa Community Free Trade Agreement) yalisainiwa Arusha na Marais Mkapa, Museveni na Moi.

  • Januari 2001, sherehe rasmi za kuzindua Jumuia ya Afrika ya Mashariki ilifanyika Arusha uwanja wa Sheikh Amri Abeid na kuhudhuriwa na maelfu ya wawakilishi wa nchi hizi. Nilihudhuria kama mmojawapo wa wawakilishi wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Sherehe za vyakula na vinywaji zilifanyika maeneo mbalimbali ya Arusha. Kikwete, kama waziri wa mambo ya nchi za nje alikuwa muhusika mkuu.

  • Machi 2004, mkataba wa Umoja wa forodha (Custom Union ) ulisainiwa Arusha. Uhai wa mkataba huu ulipangwa na umeanza Januari 1, 2005. Kutokana na nguvu za kiuchumi za Kenya, mkataba unaitaka Kenya kulipa ushuru kwa bidhaa zake inazoingiza Tanzania na Uganda katika utaratibu wa kupunguza viwango vya ushuru kila mwaka (principal of asymmetry) kwa kipindi cha miaka mitano hadi 2010. Tanzania na Uganda zinaingiza bidhaa zake Kenya bila kulipia ushuru. Baada ya 2010, itakuwa huru kwa kila nchi kuingiza bidhaa zake katika eneo la ushirikiano bila kulipia ushuru.

  • Chini ya mkataba wa Afrika ya Mashariki, tayari kuna Mahakama ya Afrika ya Mashariki (East Africa Court of Justice) - ambapo Mhe, Joseph Warioba ni mmoja wa majaji

  • Tayari tangu mwaka 2001 tuna Bunge la Afrika ya Mashariki (East Africa Legislative Assembly) lenye wabunge 27 toka nchi wanachama.

  • Aprili 1, 1999 (sikukuu ya wajinga) pasipoti ya Afrika mashariki ilianza kutumika.

  • Mwaka 2010, imekusudiwa kuwa mwaka wa kuanza kwa soko la pamoja (Common Market) ambapo pamoja na mambo mengine, itakuwa huru kwa raia yeyote wa Afrika Mashariki kufanya kazi sehemu yeyote ya Muungano (Free movement of labour and services) pamoja na uhuru wa kuishi na kujistawisha (right of establishment).

  • Inakusudiwa pia kuwa na sarafu ya pamoja (Monetary Union).

  • Julai 1, 2007 viongozi wetu wamesharidhia Burundi na Rwanda kujiunga rasmi na Jumuia. Kelele za Watanzania kuzikataa nchi hizi ni sawa na kelele za mwewe!

  • Inakusudiwa vilevile tuwe na Muungano wa Kisiasa (East Africa Federation) ifikapo mwaka 2013

    Nimeonelea nitoe kwa kifupi hali halisi ilivyo kwa faida ya kuelewa tumeshajitumbukiza kiasi gani. Maamuzi mengi kati ya haya yametiwa saini Arusha na sisi tukiwa wenyeji na yanatekelezwa.

Tume ya Prof. Wangwe

Tume hii huenda inabebeshwa msalaba isioijua au imeamua kutumikia kafiri ipate mradi wake. Sisi kama wadau hatuna hakika ya undani wa hadidu zao za rejea.

Tume leo inatafuta maoni ya uharaka wa Muungano wa kisiasa au la! Haya yanafanyika wakati tayari maamuzi mengine mengi mazito yanayowagusa wananchi yakiwa yamekwishafanyika nyuma ya migongo yao.

Muungano wa kisiasa utaathiri ‘ulaji wa CCM’. Hiki ndiyo kilio cha viongozi wetu. Kwa mara ya kwanza wameona ulaji wao uko hatarini, wanataka Watanzania tuwakomboe! Wanataka kututumia kwa kisingizio cha ‘maslahi ya taifa.’

Kwa miaka 24 CCM na Serikali yake imekuwa kwenye mazungumzo na majirani zetu hawa. Gharama kubwa zimetumika. Wameridhia kichwa kichwa mambo mengi bila kuweka mikakati ya ndani.

CCM wametujazia wabunge katika bunge la Afrika ya Mashariki na hata bunge la Afrika. Hata siku moja hatujawahi kusikia wabunge wetu kule wanafanya nini au wanaridhia nini!

Hatujui mkakati wetu wa kutumia vyombo hivi! Tumebaki kujivunia Ooh, Tanzania bwana kiboko! Spika wa Afrika, Tanzania, Spika wa Afrika mashariki, Tanzania! Sasa babu Kubwa zaidi, naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Tanzania.

Kwamba wanakwenda kule kuwakilisha maoni yao au ya Tanzania hatujui, kwani hakuna utaratibu wa kupata taarifa hizo!

Museveni kutangaza azma yake ya kutawala Afrika ya Mashariki ndicho pengine kimewazindua! Kuna ubaya gani Museveni kutangaza azma yake? Mbona hawajishangai hao (CCM) ambao wanaendelea kutawala Tanzania kwa katiba ambayo hairidhiwi na wananchi wote? Hongera Museveni kwa hili huna kosa. Ni mkakati wenu wa ndani.

Uchaguzi ni kura. Tanzania tuna idadi kubwa zaidi ya wapiga kura! Hatuna mkakati ndiyo sababu tuna woga. Tumezoea vya kunyonga sasa tunahofu vya kuchinja. Kikwete na watu wake wanajua ndani ya ‘wanaume’ wa Afrika Mashariki, haibiwi kura mtu!

Woga na hofu zote za Watanzania (kwa wale wenye kuelewa) zilijulikana siku nyingi.

Rais wetu wa sasa Jakaya Kikwete ndiye alikuwa kinara wa makubaliano yote haya akiwa waziri wa mambo ya nje na leo anaonekana kutaka kukwepa lawama.

Hata tukitumia miaka mia moja, haitawezekana kuwaelimisha Watanzania wote umuhimu wa Shirikisho wakaelewa. Fikra zimejaa hofu na woga.

Kama tunaogopa watu waliotuletea umaskini huu na tunawarejesha madarakani kila mwaka, kwa nini tunawaonea Wakenya na Waganda kama vile wao ndiyo sababu ya unyonge, umasikini , udhaifu na hata ujinga wetu?

Maamuzi ya kuunganisha nchi ni maamuzi mazito. Ni shughuli ya kila Mtanzania na si viongozi wa serikali na vyama vya siasa pekee. Mjadala wa kitaifa unastahili kupewa nafasi na kisha utaratibu wa kura za maoni ufuate (referendum).

Tume ya Wangwe nina hakika haijahoji zaidi ya asilimia moja (1%) ya wakazi wa Dar es Salaam. Leo inatuambia imemaliza Dar!!

Sanduku la kura litumike kwa utaratibu wa kura ya maoni. Wananchi wote washirikishwe. Kila mtu ashiriki kujinyonya au kunyonga.

Kuna taarifa kuwa eti kura ya maoni itafanyika mbeleni! Lini, wakati tayari maamuzi yameshafikiwa?

Prof. Wangwe na wenzio, mna bajeti ya zaidi ya Sh bilioni 2. Najua mtadai muongezewe kwani kazi ni kubwa!

Nachokiamini, ni kuwa serikali tayari ina msimamo katika hili. Iko tayari kwa kila ushirikiano, lakini usiwe wa kisiasa! Siyo kwa sababu ya Tanzania ila ni kwa sababu ya CCM. Watanzania subirini mtaona kiini macho cha tume ya Prof. Wangwe.

Hali halisi

Tanzania ni lazima tumezwe. Hatuna ubavu kiuchumi, kijamii wala wa kisiasa wa kuzuia. Tumeathirika hata kisaikolojia. Kibaya zaidi tunalalamika na hatuna mkakati hata mmoja wa kutupa matumaini kuwa chini ya utawala wa CCM kuna kujinasua. Wengine watanihukumu kwa kauli hii, lakini maandishi hayafutiki.

Hofu zetu zote ni za ‘kujikinga na mashambulizi’ ya wenzetu. Hatujadili fursa zilizopo. Hatujadili kushambulia. Tumekiri unyonge. Tuko tayari kukimbia! Tunafikiria ndani tu (inward thinking).

Kenya tunayemkataa, leo ndiye mbia wetu mkubwa katika biashara katika nchi za Afrika ya Weusi. Pengine nitoe takwimu chache zitusaidie katika kutafakari.

Mwaka 2005, kwa mujibu wa taarifa za Benki Kuu, Tanzania iliuza nchi za nje (exports) za jumla ya shs za Kitanzania bilioni moja milioni mia nane na tisini na sita. (Tshs 1.896 bilion). Tuliagiza toka nje bidhaa za jumla ya shilingi bilioni tatu milioni mia saba ishirini na sita. (Tshs 3.726 bilioni).

Katika mauzo yetu nje, Kenya ilikuwa ya tano kwa kununua mali zetu baada ya Afrika Kusini (310 bilioni), Uingereza (301 bilioni), Switzerland (123 bilion), Uholanzi (102 bilioni), China (101 bilioni) Kenya (86 bilioni).

Nchi nyingine mashuhuri zilifuata kama ifuatavyo: Japan (77 bilioni) Ujerumani (76 bilioni), India (71 bilioni) Falme za Kiarabu Ð ikiwemo Dubai (38 bilioni), Marekani (bilioni 18).

Jirani zetu wengine walinunua bidhaa zetu kama ifuatavyo: Uganda (22 bilioni), Burundi (8 bilioni) na Rwanda (3 bilioni)

Tuliuza katika nchi 16 za COMESA jumla ya Shs 140.97 bilioni. Kati ya hizi shs 86.17 bilioni yalikuwa mauzo kwenda Kenya tu! Ukichangaya na Uganda, Burundi na Rwanda, tuliuza katika nchi hizi shs 120.6 bilioni.

Nchi nyingine zote zilizobakia za COMESA ambazo ni pamoja na Ethiopia, Eritrea, Somalia, Djibouti, Lesotho, Malawi, Zambia, Zimbabwe, Swaziland, Mauritius, Comoro na Congo zilinunua kwetu bidhaa za sh. 20 bilioni tu!!

Kwa upande wa nchi zilizotuuzia mali nyingi, Kenya nayo haikucheza mbali. Ni ya sita kutuuzia mali. Mtiririko wa kumi bora ni kama ufuatao: Afrika Kusini (440 bilioni), China (245 bilioni), Japan (225 bilioni), Falme za Kiarabu Ð ikiwemo Dubai (220 bilioni), India (211 bilioni), Kenya (175 bilioni), Uingereza (135 bilioni), Marekani (112 bilioni) na Ujerumani (99 bilioni).

Katika nchi za COMESA, tulinunua bidhaa za thamani ya shs. 220 bilioni ambamo Kenya na Uganda pekee zilituuzia mali za 181 bilioni. Nchi nyingine zote za COMESA zilizobakia zilituuzia bidhaa za 39 bilioni tu.

Nimeonelea niendelee kutoa takwimu hizi ili kusaidia wasomaji wangu kuelewa ni vipi jirani zetu walivyo muhimu kwa uchumi wetu pamoja na matatizo yao.

Hofu zetu ni suluhisho?

Tuna hofu ya kumezwa kiuchumi! Mbona tayari tumemezwa? Uchumi wetu tayari unamilikwa na wageni. Asilimia 80 ya bidhaa za viwandani kwenye maduka yetu ya rejareja zinatoka nje.

Kati ya hizi, nyingi zinatoka Kenya. Kenya ndiyo mwekezaji namba moja Tanzania leo akifuatiwa na Uingereza na kisha Afrika ya Kusini.

Kenya wana mikakati ya kiuchumi siyo na Tanzania pekee, bali katika Afrika nzima chini ya Sahara. Kenya ni mshindani wa Afrika ya kusini katika soko hili. Tanzania ni mteja.

Tumeshindwa kutumia soko letu la ndani, leo tunasaidiwa. Kama siyo Kenya, basi atakuwa China, India, Dubai, Afrika ya Kusini nk. Watanzania sasa tuko radhi tumezwe na Wachina na wengine kuliko jirani zetu wa Kenya, Uganda, Rwanda na Burundi.

Hapa tunawachukia weusi wenzetu bila sababu za msingi. Hawajatusababishia unyonge huu! Ukitawaliwa kiuchumi, utatawaliwa kisiasa.

Ukweli ni kuwa ni rahisi kufanya biashara na wenzetu wa Afrika mashariki kuliko China, Marekani na Ulaya. Hili ni soko rahisi zaidi kwetu. Kama nilivyosema, tatizo ni kukosa mkakati.

Tumelemaa kwenye siasa na propaganda. Nakumbusha, CCM wameshindwa hata kuendesha SUKITA ambalo ni shirika lao wenyewe, bado tuna wazimu wa kutegemea ukombozi wa kiuchumi kwa watu hawa!

Amani yetu inatuponza. Tumelala usingizi eti tunajisifia amani na utulivu. Amani inayotuingiza kwenye umaskini ni ya nini?

Kwamba tuko tayari kufa masikini badala ya kuibadilisha nchi hii kwa udi na uvumba ndiyo hoja nayostahili kupewa nafasi.

Tuna ogopa maliasili zetu zitachukuliwa! Mbona tayari zinagawiwa usiku na mchana? Hivi Watanzania hatuoni kila kukicha makampuni ya kigeni yakija kubeba maliasili zetu. Hapa hatuna ujanja. Hatuna mtaji wala hatuna teknolojia.

Mbona mbuga zetu zote leo tayari zimeshikwa na wageni! Mbona tayari ajira nzuri nzuri zimeshikwa na wageni? Tusilie, tuboreshe elimu yetu!

Cha muhimu hapa ni, Je? Tunafaidika inavyostahili na uwekezaji huu? Kama hapana nani alaumiwe?

Mustakabali wetu kama taifa

Tanzania si kisiwa. Hatuna uwezo wa kujitenga na jumuia ya Afrika ya Mashariki licha ya jumuia ya kimataifa.

Serikali yetu ni nyepesi sana kusaini mikataba ya kimataifa bila kwanza kutafakari maslahi ya Taifa. Hatuna mikakati ya kushindana. Ni watu wa kupokea fikra za wengine.

Ndani ya mipaka yetu Serikali ina ‘ngebe’ sana. Hatua moja nje ya nchi, tunakuwa wasindikizaji. Nimesema kumezwa ni lazima. Cha kutafakari hapa, ni kuwa tutamezwa mpaka lini?

Sera yetu ya mambo ya nje iliyoasisiwa na Benjamin Mkapa na waziri wake Jakaya Kikwete inazungumzia ‘diplomasia ya kiuchumi’ yaani Economic diplomacy. Hii imebaki nadharia kwani hatuna mkakati na malengo yanayotekelezeka.

Rais anajipongeza kwa kutembelea Soko la Hisa la New York ambapo hatuna ubavu wa kutia kichwa! Hizi ndizo ziara za kitalii. Si bora angeenda Soko la hisa la Nairobi? Tunawadharau Wakenya halafu tunawaogopa!

Balozi zetu sasa zimegeuzwa idara za mambo ya nje ya CCM. Bado mikakati haijaonekana. Tunagawiana fulana na kuimba mapambio!

Hata katika vyuo vyetu vikuu tumerudisha siasa kwa mlango wa nyuma ili kuzima kuibuka kwa fikra mpya za kuhoji! Mambo ya aibu!!

Hatuna historia ya kukataa maelekezo yoyote toka kwa wafadhili na wadau wengine wa kimataifa tangu kuondoka kwa Mwalimu Nyerere katika uongozi wa Taifa hili

Hitimisho

Sera yetu ya manbo ya nje inahitaji mjadala wa Kitaifa. Rais Kikwete ajue tuko wengi wenye uwezo na nia njema na nchi hii. Hatuombi kazi ila tuko tayari kushauri mkakati wa namna ya kuifaidi Afrika ya Mashariki.

Unyonge tunaouonyesha kwenye mchakato huu ni fedheha kubwa kwa Taifa hili. Ni fedheha kwa waasisi wa taifa hili na hata kwa vizazi vijavyo! Ni aibu kwa Rais Kikwete ambaye amekuwa kinara wa mazungumzo haya kwa muda mrefu.

Leo Kikwete anaogopa kivuli chake!

Tuna haja ya kujipanga nasi tushambulie. Tuna uwezo wa kuifaidi Kenya, Uganda, Rwanda na Burundi. Kujifungia ndani na kulia wakati hata chakula hatuna ni uwendawazimu na fikra potofu.

Tujitokeze, tupigwe ili nasi tujifunze kupiga. Kabla hatujatoka tuweke mkakati wa Kitaifa. CCM mmeshindwa hili, tuko tayari kusaidia kwa faida yetu sote.

Nchi isiyumbishwe katika kujadili Muungano wa Kisiasa na kusahau mjadala wa masuala ya kiuchumi ambayo tayari yanatekelezwa.



lf.curl lf.curl2 rt.curl2 rt.curl