lf.bevel
MWANZO CHAMA SERA KATIBA TUUNGE MKONO UCHAGUZI TUWASILIANE
banner

Waraka wa Nne wa Mbowe kwa Rais Mkapa

na
Freeman Aikaeli Mbowe


Mheshimiwa Rais,
AWALI ya yote naomba nimshukuru Mungu kwa kuwezesha nchi unayoiongoza angalau kusheherekea Sikukuu ya Krismasi kwa amani na utulivu wa kutosha. Hali hii haipingi ukweli kuwa wengi wa wananchi wako sikukuu hii haina tofauti sana na sulubu waliyoizoea katika siku nyingine za maisha yao.

Mheshimiwa Rais,
Mengi yamezungumzwa, kujadiliwa na hata kuandikwa kuhusiana na utawala wako. Pongezi, zikiwamo za kweli na za kinafiki zimekuwapo, lawama zimekuwapo na hata vilio vimejitokeza.

Naandika waraka huu nikijua ndiyo kwanza umesherehekea sikukuu yako ya mwisho ya Krismasi kama Rais wetu na nikijua kuwa sasa unajiandaa kuanza mkakati wa kuaga uliowaongoza na kuwatawala tangu 1995!

Wapo wanaokuna vichwa kwa hofu kila wakifikiria "mchezo mchafu" waliofanya chini ya utawala wako na pengine kinga ya mwavuli wa jina na uhusiano wako nao. Hawa wangependa uendelee kukalia kiti milele ili waendeleze uharamia wao kwa Taifa hili! Nakupongeza kuwa mapema kabisa ulikemea hili na sasa mshawasha wa kukutaka uongezewe kipingi haupo tena!

Fikra inayotawala wengi wa wasaidizi wako keo ni namna ya kutekeleza na kukamilisha sera ya CCM, yaani "Chukua Chako Mapema." Siku zimeisha na kuendelea kupora mali ya Taifa hili masikini hakuna uhakika kwa wengi wao!

Kwa nchi nyingi za Kiafrika, mwaka wa mwisho wa utawala ni mwaka wa "kubakwa kwa hazina ya nchi". Tunakusihi ujitahidi sana usimwachie mrithi wako hazina tupu.

Mheshimiwa Rais,
Wewe ni mwanahabari. Uchambuzi wa mambo ni msingi wa habari. Kwa kiwango kikubwa umeonyesha ujasiri wa kufumbia macho na kuziba masikio (angalau hadharani) kwa vilio mbalimbali, hususan vya wananchi wako. Umejitahidi kutoingilia masuala kadhaa yenye maslahi ya Taifa kana kwamba hayakuhusu, hata pale viongozi wako waandamizi wanapokuwa katikati ya kashfa nzito!

Mheshimiwa Rais,
Nimeandika mara nyingi kuhusiana na hatma ya nchi yetu, uongozi wake – ikiwamo Katiba na mustakabali wetu kama Taifa. Wengi wamesema na kundika kama mimi! Laiti Serikali yako ingekuwa kweli inasimamia haki na kutekeleza angalau kwa kiasi kidogo ushauri unaotolewa na wanaoitakia nchi hii mema, leo ungeng’atuka na kuiacha umeifikisha katika neema ya ajabu!

Tangu Uhuru, hakuna kipingi cha uongozi kilichopata ushauri wa "bure" kama chako! Awamu yako imevunja rekodi ya warsha, tume, semina, makongamano, mikutano, mafunzo na kila sampuli ya mikusanyiko ya kitaifa na hata kimataifa.

Pamoja na mingi ya mikusanyo hii kuwa chimbuko la utafunaji wa kodi za walalahoi kwa msingi ya posho na uwezeshaji, ushauri mkubwa na mzuri umetolewa kuhusu ubinafsishaji na uwekezaji sanjari na mikataba yake.

Aidha, mengi yameandikwa na kusemwa kuhusiana na rushwa sambamba na utawala bora; mahusiano yetu na asasi za fedha za kimataifa sambamba na wafadhili mbalimbali wa nje; Katiba sambamba na uboreshaji wa mfumo wa utawala wa vyama vingi vya siasa na hivyo misingi ya uchaguzi ulio huru na haki; haki za binadamu sambamba na utoaji haki ndani ya vyombo vya dola na mahakama; michezo sambamba na uongozi wa vyama vya michezo, hususan FAT na baadaye TFF. Ushauri ni mwingi!

Utawala wa awamu ya kwanza kwa kiwango kikubwa haukuruhusu wala kuvumilia ushauri. Wengi walibamizwa kwa kutoa ushauri! Haki za binadamu na uhuru wa vyombo vya habari vilidhibitiwa barabara.

Awamu ya pili ilijikuta ikiwa ya mpito! Ushauri ulikuwapo, lakini zaidi zilikuwa lawama! Vyombo vya habari navyo havikuwa vimeenea kama sasa! Awamu hii ilichanganyikiwa zaidi! Ilikosa rangi ikawa kinyonga!

Mheshimiwa Rais,
Wewe ni mmojawapo wa Watanzani ambao weonja uongozi ndani ya awamu zote hizi. Naamini Mungu amekujalia na ukweli ni kuwa jua halijakuwakia sawasawa kama wananchi unaowaongoza! Ni ukweli usiopingika kuwa maisha yako ya utu uzima yamekuwa ya neema kubwa kwa viwango vyovyote vile! Rais wetu hujakaa kijiweni kama wengi wa uliokuwa nao katika uongozi wa awamu ya kwanza na hata ya pili. Mkuu wetu, unajua kidogo mno kuhusu umaskini wa nchi unayoiongoza! Bahati yako hatuilalii mlango wazi, bali tunawajibika kuitumia kujenga hoja ya tulipotoka, tulipo na tunakokwenda!

Mheshimiwa Rais,
Una miezi michache sana ya kudhibiti Taifa hili. Nadiriki kusema kuwa umechelewa sana kuiweka nchi hii kwenye reli. Ghafla, inaonekana kama nchi hii sasa haina utawala ila watawala ni wagombea nafasi ya urais, wakuu wa vyombo vya usalama, hususan Polisi na Usalama wa Taifa!

Serikali yako sasa imegawanyika na kinachoendelea ni, ama mipango ya "Chukua Chako Mapema" au kuundwa kwa makundi na "Serikali" kadhaa zinazosubiri kuingia madarakani baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba, 2005.

Rais, umekaa kimya na makundi haya yanayotumia kodi za wananchi na gharama za Serikali kulazimisha ziara za kitoto zisozo lazima kwa ajili ya mikakati ya kampeni! Kazi za ujenzi wa Taifa sasa zimegeuka kazi za ujenzi wa wagombea urais wa CCM.

Hatari zaidi ni kuwa makundi haya sasa yanafanya kazi ya ziada kujipendekeza kwa vyombo vya usalama eti yaweze kupata baraka zao! Makundi haya kutegemea vyombo vya dola, hususan Usalama wa Taifa katika kuweka misingi ya ushindi badala ya wananchi ni ushuhuda tosha ya jinsi viongozi wa CCM na Serikali yake walivyozoea kupatikana kwa hila kwa kuitumia vibaya idara hii. Eti, leo Tanzania kiongozi hawezi kupita kwa ridhaa ya wananchi, bali kwa ridhaa ya Usalama wa Taifa! Aibu gani hii?

Mheshimiwa Rais,
Hebu angalia uchaguzi wa Serikali za Mitaa ulivofanyika kwa misingi ya kihuni. Jamii za Watanzania katika ngazi za vijiji sasa zimegawanyika kwa makundi ya itikadi na hii ni hatari sana kwa mshikamano wetu kama Taifa.

Mapambano kadhaa ya raia na polisi yamefanyika na hata watu kupoteza maisha yao! Vyama vya siasa na Serikali yako vimetupiana lawama na hata kufikishana mahakamani! Rais kimyaa!

Mheshimiwa Rais,
Mapenzi yako kwa chama chako cha CCM yanaweza kuhisiwa kuwa yamezidi busara za kawaida kiasi cha kuwa tayari kuona wananchi wako wasio wana CCM wakiwa daraja la tatu. Wa Serikali yako, wa CCM na wawekezaji ni wa daraja la kwanza, ilhali wafanyabiashara, wasomi na wasio na vyama ni daraja la pili.

Ukimya wako umechukuliwa kama kibali cha kudhalilisha wale wote wenye mtazamo tofauti na wa Serikali na chama chako. Ukimya huu umetumika kama kibali cha kupiga, kutesa, kunyima haki na hata kuua hao raia wako wa daraja la tatu; daraja la masikini wasio na haki na pengine ambao ni nuksi kwa taifa hili. Ukimya wako ni kibali cha mauti kwao! Ukimya wako mbali na kulea maafa haya, yanakuhalalisha kuwa sehemu ya kundi linalo ashiria maafa ya Taifa hili.

Mheshimiwa Rais,
Wengi wanaweze kusema sikutendei haki, kwani umekemea mara kadha vitendo viovu, ikiwamo rushwa na kauli zote zitakazoweza kusababisha uchaguzi ujao usiwe wa amani. Mfano, imeripotiwa kuwa umewasihi Watanzania kuomba uchaguzi mkuu ujao uwe wa amani na umekemea kauli za uchochezi toka kwa viongozi wa siasa tunapoelekea kwenye uchaguzi mkuu.

Kauli hizi nzuri umezitoa kama salamu zako za Krismasi katika ibada ya misa iliyofanyika katika Kanisa Katoliki mjini Masasi, mkoani Mtwara, ulikokwenda kwenye mapumziko ya Krismasi. Ni dhahiri kuwa umegundua kuna tatizo kubwa mbele yako na hivyo mbele yetu sote kama Taifa.

Hofu yako hii, kadhalika, imeonyeshwa maeneo mengi ya nchi yetu, hususan na viongozi wa dini, vyama vya siasa vya upinzani, vyama vya hiari, viongozi wastaafu, wahadhiri mbalimbali wa Watanzania wengine wengi walio nje ya uongozi wa Serikali na Chama chako. Wote hawa wamezungumza kwa nyakati tofauti.

Mara kadhaa, umeeleza "kusikitishwa" kwako na udhaifu wa vyama vya upinzani (hotuba katika Mkutano wa viongozi wa Maziwa Makuu, Dar es Salaam, Desemba 2004).

Mheshimiwa Rais,
Watanzania tunakufahamu kama mtu mahiri kwenye masuala ya fasihi na mnukuu mzuri wa falsafa mbalimbali. Naamini utakubaliana nami kwa msingi huo huo kuwa vitendo huzungumza vizuri zaidi ya maneno. Waingereza wanasema "action speaks louder than words."

Aidha, Waswahili nao wanasema maneno matamu yasiyofuatiwa na vitendo ni kichaka cha unafiki na uzandiki. Mkuu wetu una uwezo mpana na uzoefu wa uongozi kitaifa na kimataifa. Huna tatizo la ufahamu.

Kwa umri wako, elimu yako, uzoefu wako, uelewa wako, muono wako na sifa nyingine kemkem zilizokusheheni naamini kabisa kinachokosekana ni dhamira ya dhati na kweli sambamba na utashi wa kisiasa kutoka kwako binafsi ya kuona demokrasia ya kweli ikichukua mkondo wake.

Aidha, upande wa pili naamini kuwa unaelewa barabara msingi wa chimbuko la uvunjifu wa amani ni pale kundi moja linapoburuzwa na kuona na kuamini halitendewi haki. Kwa mantiki hii, dhana ya kuvunjika kwa amani hutokea tu pale wasio CCM wanaposimama kidete kudai haki! Hapo chama na Serikali yako huanza propaganda ya viashiria vya kuvunjika kwa amani!

Mheshimiwa Rais,
Chini ya utawala wako, kwenye ulingo wa utawala wa siasa za vyama vingi, maovu mengi, manyanyaso na hata mauaji yamefanywa dhidi ya wanachama na viongozi wa vyama vya upinzani. Viongozi wa chama chako na Serikali yako wamekuwa wepesi kutoa kauli za kibabe, majivuno na za kutisha dhidi ya vyama visivyo na mamlaka na dola na hivyo askari na silaha.

Tunashawishika kuamini kuwa yote haya yanapata baraka zako. Hata siku moja hatujasikia hatua kali zimechukuliwa na Serikali yako kwa kiongozi wake yeyote. Kadhalika, kada yeyote wa chama chako hupongezwa kwa kila hatua ya kudhalilisha upinzani! Si siri, wanaofanya udhalimu huu wanapongezwa kisirisiri na wengine hata hadharani kwa kupandishwa vyeo!

Rais wetu ukiishia kulaani tu na kuonya ilhali vingi ya vyombo vyako na wafuasi wa chama chako ndiyo kwanza vinaongeza kasi ya kunoa "mapanga", mafunzo ya kiharamia na kukusanya mabilioni ya fedha chafu kwa ajili ya uchaguzi, unatuambia nini Watanzania maskini? Haya hayatokei kama ajali! Yanafanyika kwa maelezo au baraka sawia toka ngazi za juu!

Utakubaliana nami kuwa Serikali yako ndiyo inayomiliki majeshi yote ya ulinzi na usalama. Wewe ni Amiri Jeshi Mkuu wa majeshi yote. Wewe ndiye sauti ya mwisho ya amani ya nchi hii. Unapofumbia macho haki ya wananchi wako "inapobakwa", naamini hutegemei maneno matamu yaweze kunusuru Taifa hili kuepuka machafuko.

Ni tegemeo letu sisi wananchi wako kuwa inapofikia hatua ya Rais wetu kukemea jambo, ni sahihi na lazima kabisa kemeo hilo liendane na hatua za uwajibishaji. Hatutegemei wasaidizi wako wachukue kauli zako kama porojo za kasuku! Kauli yako inastahili kuwa agizo lenye kuundiwa mkakati wa utekelezaji, tena haraka!

Kwa uelewa wako, (tofauti na walivyo viongozi wengi waandamizi ndani ya chama chako na ambao kwao siasa ni chanzo cha ajira yenye hadhi, potelea mbali hata kama hawana ufahamu wowote zaidi yakuzungumzia wapinzani) unajua fika kuwa kuna manung’uniko yaliyodumu kwa takribani muda wako wote wa utawala kutoka kwa wadau wenzako katika uongozi wa vyama vya siasa vya upinzani.

Unajua vyema kilio cha wananchi kuhusu Katiba itakayowezesha kuweka misingi imara ya utaifa na hivyo sauti ya pamoja katika kukabiliana na ujenzi imara wa demokrasia na maendeleo ndani ya nchi yetu!

Unajua vyema jinsi chama chako kilivyojikita leo kuwa chama dola. Rasilimali watu na fedha za Serikali yako leo vinatumika kunyonga vyama vingine na hivyo demokrasia katika nchi yetu.

Majeshi yote leo yanafanya kazi kwanza kwa manufaa ya CCM na kisha haki "baadaye."

Kama hayo hayatoshi, leo chama chako kinatoa mafunzo ya kiharamia kwa makada wake, hasa vijana yanasosimamiwa na wanajeshi wastaafu jinsi ya kutumia nguvu, vitisho, hila, ghiliba, fitna na kila aina ya uchafu kudhoofisha vyama vingine na hivyo demokrasia. Chama chako leo kimegeuka chama cha kijeshi. Haya yote yanafanyika kwenye kambi za vijana, tena mchana kweupe.

Unajua kabisa kuwa mbali na matumizi ya rasilimali za Serikali kwa matumizi haramu ya chama chako kinyume cha sheria, bado Serikali yako imejiwekea mpango wa kuchota kutoka Hazina zaidi ya milioni 700 kwa kila mwezi kwa kigezo cha "ruzuku" kwa vyama vya siasa ilhali chama kama CHADEMA kikiambulia shilingi milioni 5?

Bila aibu, katika mazingira haya yasiyo ya haki, wasaidizi wako wanaringa kuwa CCM ni chama dume! Vyama vingine vikalilie wapi? Vilindwe na nani? Vyama vingine vinalazimishwa kujifunza kuwa lugha pekee ya kuheshimiana ndani ya nchi yetu leo ni "upanga." Tunalazimika kukubaliana na maneno ya wahenga kuwa "amani haiji ila kwa ncha ya upanga!" na "dawa ya moto ni moto!" Rais hulioni hilo?

Kwa masikitiko CHADEMA tunalazimika kukubaliana na falsafa hii kama njia sahihi na mwafaka ya kupitia katika safari ya kutafuta ustawi wa haki ya uhakika kwa Watanzania, kwani kinyume chake ni kukubali kupigwa shavu moja kisha ugeuze la pili! Ujasiri huo wa chama cha amani tumelazimishwa kuuaga rasmi mwaka huu wa 2004. 2005 na mambo mapya! Muda utanena!

Mheshimiwa Rais,
Hakika muda wako umekwisha. Huna muujiza utakaoweza kuufanya kwa sasa, kwani wasaidizi wako wameshajua "Mzee ni mpole hataki noma na mtu". Sitaki kuamini kuwa yanayofanyika yote yana baraka zako. Napenda kuamini kuwa mengi yanafanyika kwa kupitia mgongoni mwako nawe kwa ukimya wako; kwa kujua au kutokujua, umeyabariki.

Si kusudio la waraka wangu leo kuzungumzia mazuri uliyoyafanya! Yapo mengi! Wapo wanaolipwa kuyasema. Aidha, wapo wanaojilipa kuyasema. Mimi nitayasema kwa heshima na unyenyekevu yote siku mwafaka ikiwadia.

Hata hivyo, si vibaya nikamalizia kwa kueleza kinachonichang’anya! Hivi Rais wetu wewe hulka yako ni ipi? Wako wanaosema wewe ni mpole! Wengine wanasema wewe ni mwenye mwoga! Wengine wanasema wewe ni mwenye huruma! Wachache wanasema pengine wewe kwa nafasi yako na waliokuzunguka huoni ukweli wa hali halisi! Wengine wanahisi kwa ukimya wako unawafanya waliokuzunguka washiriki "michezo michafu"! Ningependa nijipe ujasiri wa kutokubaliana na yote haya!

Huu ni mwaka wa mwisho wa utawala wako, na kwa muda wote huu ni kweli hakuna hata kiongozi mmoja wa Serikali yako na vyombo vyake aliyestahili kuwajibishwa, kufukuzwa hata kufungwa?

Mbona wizi na ufisadi ni utaratibu wa kila siku kwa wengi wa wasaidizi wako? Hakika hali hii ikiishia hivi, utatoka na rekodi ambayo kamwe si mfano wa kuigwa na rais ajaye!

Serikali yako imejaa madudu, wezi, maharamia, wala rushwa na mafisadi wa kila sampuli! Naam, wako wengine wazuri, wasafi, waliofanya na wanaofanya kazi nzuri. Uzuri wao unafunikwa na uchafu wa wengine.

Hivi kweli kazi ya vyombo vyako vyote vya dola ni kuhangaika na wapinzani tu? Hivi maharamia wote, majambazi wote wa kalamu na mikataba walioizunguka Serikali yako toka kwenye kundi la wafanyabiashara halali na haramu, na hata wawekezaji bandia hawaonekani mbele ya macho yako na vyombo vyako?

Mheshimiwa Rais,
Umeshakuta wapi duniani viongozi wa umma wanaotegemea mishahara midogo, lakini mamilionea? Nina hakika unajua kama wajuavyo Watanzania wote kuwa utawala wako unaongoza kwa mamilionea!

Tatizo la sisi Watanzania, wengi hatuna hulka ya kuwaambia wakubwa ukweli! Hata hivyo, kwa upande wa pili ni kielelezo tosha cha jinsi Taifa letu lilivyojengwa kwa misingi ya hofu, unafiki na uzandiki!

Rais wetu unamaliza muda wako! Ninakupongeza kwa utekelezaji wa ahadi yako ya Uwanja wa Kimataifa wa Mkapa! Lakini niruhusu kutoa dukuduku langu kwako kama Mwenyekiti wa CCM Taifa; Viwanja vyote mlivyotaifisha kwa Watanzania na kuvigeuza vya CCM nchi nzima leo vina hali gani?

Pamoja na kuchota mapato yake, chama chako kimetelekeza viwanja vyote vikuu vya mikoa kama Ilulu, Lindi; Majimaji, Songea; Jamhuri, Dodoma; Samora, Iringa; Mapinduzi, Mbeya; Tanganyika, Kigoma; Kirumba, Mwanza; Ali Hassan Mwinyi, Tabora na vingine vingi; unategemea vipaji vya kuchezea huo uwanja wa olimpiki vitatoka wapi?

Michezo kwenye wilaya ndiyo usiseme! Kila uwanja wa wazi ni wa CCM, kila maegesho ya magari nchi nzima ni ya CCM! Viongozi wa CCM ni maarufu kwa uuzaji wa viwanja! Mambo ni mengi!

Mheshimiwa Rais,
Hebu angalau zungumza kidogo kuhusu Serikali/wizara yako, TFF na hatima ya wananchi wako kwa mamilioni wanaopenda soka! Ni kweli Rais wetu umeonyesha kwa vitendo kuwa hupendi michezo. Ndiyo sababu inawezekana ukamaliza muda wako bila kuangalia hata mchezo mmoja wa kitaifa au kimataifa!

Pamoja na hayo, basi angalau mwaka huu wa mwisho tupe Watanzania zawadi ya kurejesha viwanja vyote vya michezo chini ya uangalizi wa uongozi mpya wa TFF au mamlaka maalumu ya Serikali (wakala) na vitengewe bajeti na Bunge ili visipotee kama mashirika ya umma, kwani mwelekeo ni huo! Chama chako hakina uwezo wala utaalamu wa kuendesha viwanja vya michezo.

Nakushukuru wa kusoma waraka huu na nitaomba usichoke kusoma nyaraka zangu, kwani ni sehemu ya mchango wangu kuwatayarisha wananchi kujua changamoto zinazomkabili Rais atakayekurithi!

Nakutakia wewe na familia mwaka mpya wenye fanaka na baraka tele!

lf.curl lf.curl2 rt.curl2 rt.curl