lf.bevel
MWANZO CHAMA SERA KATIBA TUUNGE MKONO UCHAGUZI TUWASILIANE
banner

29 Aprili 2007

CHADEMA yaanza maandalizi ya kuchukua dola

Mwandishi wa habari wa Tanzania Daima, Ratifa Baranyikwa, anafanya mahojiano na mkufunzi wa ‘CHADEMA ni Msingi’, David Kafulila ambaye pamoja na mambo mengine, anazungumzia sababu za kuanzishwa mpango huo.

Swali: Nini maana ya CHADEMA ni Msingi?

Jibu: Huo ni mpango wa ujenzi mpya wa chama kuanzia ngazi ya nyumba kumi kwenda juu ili kuharakisha mabadiliko kwa Watanzania. Tunajenga mtandao wa chama wenye malengo ya kukitumikia chama na wananchi kwa kuwa serikali mbadala katika kipindi hiki cha mpito tukielekea kuchukua dola.

CHADEMA inaamini hiyo ndiyo njia pekee ya kuepuka machafuko nchini. Maana CCM imewakatisha tamaa Watanzania baada ya kuwa chama kilichokithiri kwa ufisadi. CCM inachukua dola kwa rushwa na inaongoza kwa rushwa. Sisi tumeona tuanze kuwaonyesha matumaini wananchi ya kuwapo kwa mabadiliko kwa kuanzia ngazi ya chini, tunataka kuwajengea matumaini kuwa muda si mrefu, ufisadi ulioota mapembe utakwisha tutakapoing’oa CCM madarakani.

Mwalimu Nyerere aliwahi kusema na namnukuu: ‘Nilisema awali kwamba kansa ya uongozi ndani ya Chama Cha Mapinduzi isingekuwa jambo la kutisha sana kama tungeanza kuwa tumeona chama kizuri cha upinzani kinachoweza kuiongoza nchi yetu badala ya CCM.

‘Ubovu wa uongozi ndani ya CCM ndio ulionifanya nikapendekeza tuanzishe mfumo wa vyama vingi, nilitumai kuwa tunaweza kupata chama kingine kizuri ambacho kingeweza kuiongoza nchi yetu badala ya CCM, au ambacho kingeilazimisha CCM kujisafisha kwa kuhofia kuwa bila kufanya hivyo itashindwa katika uchaguzi ujao’ - mwisho wa kunukuu.

Mwalimu alipotoa kauli hii CHADEMA ilikuwa bado changa lakini pia alikiri kuwa ndiyo chama chenye mwelekeo sahihi.

Swali: Mpango wa kukipeleka chama kwa wananchi unahitaji maandalizi ya kutosha. Je, umejiandaaje kwa hilo?

Jibu: Ni mpango mgumu, lakini chama kimejiandaa kuhakikisha kinawafikia Watanzania wote. Tunaamini Watanzania wamechoka, wamekata tamaa na CCM, jambo litakalotusaidia katika kuwaelimisha wananchi umuhimu wa kubadili utawala wa nchi.

Tumejipanga kufika kila sehemu ya Tanzania kwa wakati wake. Tutafanya mikutano ya hadhara katika mitaa yote ya nchi hii, tutawapa ujumbe wa tumaini jipya.

Tutafungua ofisi za chama, tunasimika mabalozi wetu, hatutawapa pilau wala kofia, bali tunawajengea ujasiri...mabadiliko yanawezekana, ni kazi ngumu lakini hakuna njia ya mkato ya kuiondoa CCM ambayo ndiyo mzizi wa ufisadi na umaskini wa Mtanzania.

Mwalimu Nyerere aliwahi kusema katika moja ya hotuba zake kuwa kama tukiacha utamaduni wa woga ukazagaa, tutakuwa tunakaribisha udikteta. Uhuru hauji wala haudumishwi bila kuwa tayari kulipa gharama zake, na vitu vyote vyenye thamani gharama zake ni kubwa.

Swali: Elimu mnayoitoa kwa Watanzania kupitia mpango huu inahusu nini?

Jibu: Yapo mambo matatu. La kwanza ni ukuaji wa chama katika muktadha wa historia, falsafa, itikadi na muundo wake. Tutafundisha mpango, mkakati na mwelekeo wa kisera wa CHADEMA itakaposhika dola na mafunzo ya uongozi na uanachama ili kuwafanya makada na wanachama wetu kuwa na viongozi mbadala katika maeneo yao.

Swali: Historia, falsafa, itikadi na muundo kwa maana gani? Hasa kwa Watanzania wa kawaida.

Jibu: CHADEMA inakua kifalsafa, itikadi na muundo wake na kadri miaka inavyokwenda ndivyo falsafa ya ‘nguvu ya umma’ kwa kiitikadi ya mrengo wa kati inavyozidi kuungwa mkono.

Hii inatokana na ukweli kuwa kadri miaka inavyopita ndivyo mamlaka ya uchumi na siasa za nchi yetu zinavyozidi kumilikishwa kwa kundi dogo kabisa la Watanzania na wageni ambao hata hivyo, uadilifu wao unatiliwa shaka.

Hayo ni madhara ya taifa kuongozwa na chama kisicho na itikadi wala dira. Hivyo tunafundisha namna ya kutumia falsafa ya nguvu ya umma kwa itikadi ya mrengo wa kati, tunazungumzia na kuhamasisha uchumi wa soko huria wenye taratibu na nidhamu na hasara za uchumi wa sasa wa soko holela chini ya CCM usio na taratibu wala nidhamu.

Tunafundisha uchumi wa soko wenye tija kwa wazawa kumiliki uchumi na madhara ya uchumi wa kizamani na ulioshindwa na serikali kumiliki uchumi. Tunafundisha umuhimu wa mabadiliko ya kimfumo, kama namna mfuno wa serikali za majimbo unavyorahisisha utekelezaji wa falsafa ya nguvu ya Umma.

Tunayafanya kulingana na historia ya chama chetu, ndiyo chama pekee katika kambi ya upinzani kinachoonyesha kukua. Mwaka 1994 kilipata madiwani 15 na wabunge wanne; 2000 kilipata madiwani 45 na wabunge 5 na kulifanikiwa kuiongoza Halmashauri ya Karatu, Kigoma mjini na Hai.

Halmashauri hizi katika kipindi hicho zilifanya vizuri katika kutekeleza miradi ya maendeleo. Tuliondoa tatizo la elimu ya sekondari ya Kigoma Mjini na kudhibiti tatizo la maji Wilaya ya Karatu. Mwaka 2005 Chadema kilipata madiwani 99 na wabunge 11.

Muundo wa sasa wa CHADEMA kama nilivyoeleza hapo awali unaanzia ngazi ya balozi, msingi, tawi, kata, jimbo la uchaguzi, mkoa, kanda hadi taifa.

Swali: Je, unakutana na changamoto zipi unapozungumzia itikadi ikilinganganishwa na zile za CCM.

Jibu: Kimsingi hakuna changamoto tunayopata kutoka CCM tunapozungumzia itikadi ya CHADEMA ya mrengo wa kati kwa falsafa ya nguvu ya Umma.

CCM hawana itikadi, wanaongoza nchi kwa matamko na maazimio, hawana sera kwa sababu hawana itikadi, hawana dira.

Swali: Unafahamu kuwa katiba ya nchi imeandikwa 'Ujamaa na Kujitegemea' ndiyo itakadi ya CCM?

Jibu: Naam, katiba imeandikwa hivyo na wao CCM wamekuwa wakiungama hivyo, lakini si kweli kuwa Tanzania tunafuata itikadi ya Ujamaa na Kujitegemea, ni uzushi tu.

Agrey Mwanri aliwahi kutamka kuwa nchi hii haina itikadi, kinachoendelea hapa ni shughuli tupu. Aliyasema haya alipokuwa akichangia katika Bunge la kwanza la bajeti la awamu ya nne mwaka 2006, alipokuwa hajateuliwa kuwa Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, inawezekana akakana sasa baada ya kuwa yeye ndiye katibu mwenyewe wa itikadi katika chama hicho kisicho na itikadi.

CCM ya Ujamaa na Kujitegemea iliondoka na Mwalimu Nyerere na ikazikwa rasmi mwaka 1991/1992 kupitia Azimio la Zanzibar lililofutilia mbali Azimio la Arusha ambalo ndiyo msingi wa Ujamaa na Kujitegemea. Ndio maana taifa linazidi kupotea.

Chama tawala kinapokosa itikadi maana yake kimekosa dira. Chama kinapokosa itikadi yake hakiwezi kuandaa sera. CHADEMA haishangai CCM wanapoamua kuiga MKUKUTA na kudai ndiyo sera zao, ni kwa sababu hawana msingi wa kutengeneza sera.

Mfano rahisi ni serikali ya CCM inaposema sera yake ya elimu ya juu ni 'cost-sharing' yaani kuchangia gharama kati ya serikali na mpata huduma. Hapo hapo inasema lipia asilimia 40 ya karo na serikali itakukopesha asilimia 60, ambayo utailipa. Wanaojua maana ya cost-sharing wanawacheka CCM, kwa tafsiri ya kinachofanyika hapo ni kwamba mzazi au mwanafunzi aliyelipia asilimia 40 na kukopwa asilimia 60 ni sawa na kujilipia asilimia 100, hayo ndio matatizo ya kukosa sera na kubaki tunadandia misamiati.

Mwalimu Nyerere kwenye kitabu chake cha 'Uongozi wetu na hatima ya Tanzania' amewaonya CCM wasiendelee kupitapita na kuwadanganya Watanzania kuwa CCM inafuata itikadi ya Ujamaa na Kujitegemea, aliandika kuwa ‘Halmashauri Kuu ya Taifa iliketi Unguja ikabadili Azimio la Arusha bila kwanza kutafuta maoni ya wananchi.

‘Na walikuwa na haki ya kufanya hivyo, maana sera ni yao, ubaya wao ni kwamba jambo lenyewe walilifanya kwa hila na hadi sasa wanaendelea kuwadanganya wananchi kwamba sera ya CCM bado ni Ujamaa na Kujitegemea.’ Haya ni maneno ya mwasisi wa CCM, mwasisi wa Ujamaa na Kujitegemea.

Swali: Katika mpango mkakati wa chama na mwelekeo wa kisera mnafundisha mambo gani, mnataka Watanzania wajue nini?

Jibu: Mpango mkakati wa chama na mwelekeo wa kisera unawasaidia wanachama na wafuasi kufahamu kanuni za msingi kwa chama chochote makini cha siasa chenye lengo la kuchukua dola. Chama chochote makini cha siasa huwa na mpango wake unaoeleza angalau nadharia, dhamira, malengo na matarajio ya namna ya kuyatumia madaraka hayo ya uchumi, siasa na kijamii. Mpango mkakati wa CHADEMA na mwelekeo wa kisera pamoja na kuelezea malengo na mwelekeo wa jumla na harakati za kuleta ustawi Tanzania, unachambua jamii ya Watanzania sanjari na chama chetu kimetoka wapi na kipo wapi, na hivyo wapi taifa letu linaelekea ukihusianisha na mwelekeo wa chama, hapa tunafundisha nafasi ya chama kwa mwelekeo wa nchi yetu.

Hata hivyo, funzo moja kubwa ni kwamba kadri tunavyozidi kujizatiti kwa kutumia hoja kujijenga, ukishindanisha hoja dhidi ya ubabe wa fedha na vyombo vya dola vinavyotumiwa na serikali ya chama tawala kwa faida ya chama tawala, ndivyo tunavyozidi kuungwa mkono na Watanzania. Tumeshinda katika nyoyo za Watanzania ingawa hatujafanya vizuri kwenye sanduku la kura. kwa hiyo changamoto pekee ni kuwajengea ujasiri Watanzania wazitii dhamira zao kwa kutuunga mkono.

Kwa hiyo, eneo hili tunafundisha mbinu za kujenga uchumi na siasa kwa itikadi na falsafa ya nguvu ya umma, tunasisitiza zaidi mabadiliko ya mfumo ili kuondoa uchumi wetu kutoka kuwa uchumi wa soko holela kwenda uchumi wa soko huria, wenye taratibu na nidhamu kwa falasafa ya nguvu ya umma ili kuhakikisha Watanzania wanafaidi matumizi ya rasilimali za nchi yao tofauti na ilivyo sasa.

Kwa upande wa uongozi na utawala, tunasisitiza serikali za majimbo kama njia pekee ya kuhakikisha itikadi yetu ya mrengo wa kati kwa falsafa ya nguvu ya umma, inapata fursa ya kuwatumikia wananchi, kwani inaongeza demokrasia ya kiuchumi kwa kuthibitisha ushiriki mpana wa umma katika ujenzi wa uchumi wa soko huria.

Swali: Mpango huu unawafundisha nini wana-CHADEMA?

Jibu: Kuna mambo makubwa mawili, kwanza ni namna viongozi wapya wa chama wanavyoweza kuisimamia serikali itekeleze ahadi zake katika ngazi husika. Katika hili tunawafundisha namna wanavyoweza kuwa viongozi mbadala na pili tunawafundisha majukumu yao kama viongozi katika mtazamo mpya baada ya kuchukua dola.

Tunawaweka tayari kiuongozi, wajue misingi ya uongozi wa chama, ndiyo sababu nasisitiza kuwa sisi kama serikali inayosubiri kuingia madarakani ni lazima tujipange jinsi tutakavyotumia mamlaka ya dola kiuongozi. Tunafanya kutokana na uzoefu tulioupata kutoka kwa chama kilichopo sasa madarakani CCM, kukosa kwake dira/itikadi inayotoa mwelekeo wa kisera kumesababisha mambo mengi kwenda kombo, mara kadhaa viongozi wa juu wa serikali wametofautina utadhani ni serikali mbili au tatu.

Mfano Rais anasema katika kuwasaidia Watanzania wa kipato cha chini mkopo ya wajasiriamali itatolewa kwa masharti, halafu anaibuka waziri mkuu anasema haina masharti, huu ni mgogoro kati ya mwelekeo wa kisera ambao kwa kawaida unatolewa na Rais dhidi ya mwelekeo wa kiutekelezaji wa sera ambao kwa kawaida unatolewa na waziri mkuu ambae ndio msimamizi Mkuu wa shughuli za serikali.

Mwalimu Nyerere aliwahi kuzungumzia mazingira ya namna hii ya uongozi, alisema serikali ya namna hii amnayo viongozi wake wakapingana katika maamuzi imepoteza uhalali wa kivitendo na mwenendo, imebaki na uhalali wa kisheria kwa sababu tu ilichaguliwa kwa mujibu wa katiba.

Nimnukuu katika kitabu cha 'Uongozi wetu na hatima ya Tanzania' uk 53, aliandika: ‘Kwa maana moja sasa hatuna serikali, tuna mawaziri tu, serikali ni timu, na timu halisi ina dira na rubani. Mkusanyiko wa mawaziri bila mwelekeo bila mwogozo, bila mshikamano na bila uongozi, kila waziri na la kwake hauwezi ukaitwa serikali.’

Swali: Mpango huu ni wa muda gani na umeanzia eneo gani?

Jibu: Mpango huu ni mchakato endelevu, sasa hivi tupo kwenye hatua ya kwanza, kujenga uongozi ngazi za misingi na mitaa kama nilivyoeleza hapo juu, baada ya hapo usimamizi na tathimini kila baada ya kipindi fulani. Tunachotoa sasa ni mafunzo ya awali, mafunzo yataendelea kwa namna katika ngazi mbalimbali, ni mchakato endelevu uliogawanyika kaktika hatua mbalimbali, ikiisha moja inafuata nyingine, mpaka kieleweke.

Kutakuwa na tathmini ya kiutekelezaji hivyo mpango huu unaweza kubadilika kimkakati kutegemea na tathmini iliyopatikana, hasa katika kipindi cha muda mrefu lakini malengo yake yatabaki kuwa yale yale. Tumenzia Ubungo, Tunduru na Karatu baada ya hapo tutakwenda katika majimbo mengine mpaka tuwafikie watanzania wote. Ni mapaka kieleweke.


 
lf.curl lf.curl2 rt.curl2 rt.curl