Kwanza naomba nikupe pongezi kwa kuchaguliwa kwako kuwa Kiongozi wa nchi yetu. Inawezekana kuwa tayari nimeshakupa hongera
tulipokutana pale Dodoma siku uliyomwapisha Waziri Mkuu Ndg. Edward Lowassa au vile vile tayari umekwisha pongezwa na
Mwenyekiti wangu wa chama cha CHADEMA ndg. Freeman Mbowe pale Diamond Jubilee. Hata hivyo, kwa kuwa hii ni mara yangu ya
kwanza kuwasiliana na wewe kama Rais kwa barua, nimeona ni bora nikupe hongera zangu tena.
Vile vile nikutie moyo kwa kazi unayofanya. Umeanza kazi kwa kasi mpya, ari mpya na nguvu mpya ili kuleta Mabadiliko ya kweli
na Uhuru wa kweli kwa jamii ya Watanzania.
Kwamba timu yako nzima ya uongozi inafanya kama wewe ni suala la mjadala mwingine. Sina shaka hata kidogo kuwa Waziri Mkuu
na Spika wa Bunge letu tukufu wanaendana na ari yako. Ninaamini watakusaidia vya kutosha. Nina imani kubwa sana na viongozi hawa
licha ya changamoto kadhaa ambazo ninaamini ni matatizo ya kimfumo (systematic inherent problems) tu ambayo hata sisi
tungefanikiwa kupata ridhaa ya Watanzania na kuongoza taifa letu tungekutana na changamoto hizo. Nikisema sisi, ndugu Rais,
nina maana CHADEMA.
Ndugu Rais, barua hii ni yangu binafsi kama kijana mwenye kulipenda taifa langu na bara langu la Afrika. Kwa kuwa nina ofisi ya
kitaifa, kama Mbunge, nakuomba uchukulie barua hii kama inatoka kwa Mbunge kwenda Rais wa nchi ambae ni sehemu ya pili ya
Bunge.
Barua hii ina mawazo ya kujaribu kusaidia kutokana na changamoto iliyopo mbele yetu kufuatia hukumu ya Mahakama Kuu kuhusu
kuruhusu wagombea binafsi wa uongozi wa nchi yetu. Wagombea binafsi maana yake ni wagombea wasio na vyama vya siasa. Wanaweza
kuwa ni wanachama wa vyama, lakini hawana dhamana ya vyama vyao wanapogombea na kisha kuchaguliwa kuwa viongozi.
Ndugu Rais, kuwa na mgombea binafsi haina maana kuwa mgombea huyu hatakuwa na udhamini wa aina fulani. Mfano, Kikundi cha
Wafanya biashara wa zao fulani (mfano Tumbaku kule Urambo) wanaweza kudhamini watu kadhaa, wakagombea udiwani, wakashika
“majority” ya Halmashauri ya Wilaya. Maana yake ni kuwa maamuzi yote ya Halmashauri ya Wilaya Urambo yatakuwa chini ya
kundi hili. Hii inawezekana. Inawezekana pia hata kwa ngazi ya Ubunge. Sina uhakika katika ngazi ya Urais. Lakini sina haja
ya kukuhadithia alichofanya Rais Bingu wa Mutharika wa Malawi.
Ndugu Rais, Vyama vya siasa vimewekewa masharti ya kuandikishwa. Kuna sheria inayopelekea vyama kusajiliwa na kuna ofisi ya
Msajili wa vyama anaeratibu vyama vyote ikiwemo chama chako, CCM. Hata kama mmoja wa wajumbe wa secretariat ya chama chako
alinukuliwa akisema Msajili wa vyama ni karani tu, lakini ofisi hii ina majukumu makubwa sana ya kuhakikisha taifa halimeguki
kisiasa. Ingawa nina mawazo tofauti, kwamba ofisi hii ingeweza kuwekwa chini ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi badala ya muundo wa
sasa. Lakini hii sio hoja kwa sasa.
Kiufupi ni kwamba vyama vinaratibiwa. Katiba zao na hata kanuni zao za uteuzi wa wagombea wa nafasi zote zipo kwa Msajili.
Msajili aweza kufuatilia kuona kama chama kinafuata taratibu zake na anao uwezo wa kuonya.
Ndugu Rais, nchi haiwezi kuwa na ofisi ya kuratibu wagombea binafsi. Nidhamu yao Bungeni na hata katika Mabaraza ya madiwani
haitaweza kushughulikiwa na vyama. Hawa hawana vyama!
Ndugu Rais, sio nia yangu hata kidogo kushauri kuwa tusiruhusu wagombea binafsi. Hii itakuwa ni kuzuia uhuru wa Mtanzania
kushiriki katika uongozi wa nchi. Mahakama imesema ni kinyume na Katiba. Katiba ambayo sote tumeapa kuihifadhi, kuilinda na
kuitetea. Kiapo tulichokula ni kikubwa sana na lazima tuheshimu kiapo. Hata hivyo, suala hili ni lazima tuliangalie kwa mapana
yake.
Mara baada ya mahakama kutoa hukumu nilinukuliwa na magazeti ya hapa nyumbani na moja na Ghuba (Gulf Times) na lingine na
Marekani (The Herald Tribune). Nilisema kuwa maamuzi ya mahakama yanatutaka tufanye mabadiliko makubwa ya mfumo wetu wa siasa.
Maamuzi ya mahakama yanaweza kuudhoofisha mfumo wa vyama nchini kwetu.
Uzoefu wangu unaonesha kuwa Watanzania hawapendi vyama. Sio manazi wa vyama vya siasa. Hawaoni kama vyama vinawawakilisha.
Wanaona vyama kama vikundi tu vya watu wenye madhumuni ya kutawala. Hawaoni vyama kama Asasi muhimu za kujenga demokrasia na
kutoa sera mbadala. Ndio maana kati ya Watanzania milioni 16 waliojiandikisha kupiga kura mwaka 2005, ni Watanzania milioni
tano tu ndio wanachama wa vyama. Hata wewe ndugu Rais, umechaguliwa na Watanzania milioni 9 wakati chama chako kina wanachama
milioni tatu tu!
Kwa hali hii ya udhoofu wa vyama kutokukonga nyoyo za Watanzania, wagombea binafsi wanaweza kuvuruga kabisa mfumo wa vyama.
Hii ni hatari ninayoiona. Ni hatari kweli kweli. Ni hatari kwa sababu, nchi inaweza kukatika kwa matamshi tu ya mtu ambae hana
chombo cha kumdhibiti. Vyama vinadhibiti wanachama wake.
Ndugu Rais, mimi binafsi nina maoni yafuatayo ili kuimarisha Demokrasia katika nchi yetu kufuatia hukumu ya mahakama kuu.
Mapendekezo yangu haya yanaweza kuwa sehemu ya mjadala wa kitaifa uliouahidi wakati ulipolihutubia Bunge mwishoni mwa Disemba
2005.
- Wabunge wa kuchaguliwa moja kwa moja na wananchi watokane na Halmashauri za Wilaya za sasa. Mfano, badala ya Wilaya
ya Manispaa ya Kinondoni kuwa na Wabunge watatu, iwe na Mbunge mmoja tu. Halmashauri ya Wilaya/Mji/Manispaa/Jiji ndio iwe
Jimbo la Uchaguzi. Katika ngazi hii wagombea wasio na vyama waruhusiwe pamoja na wale wenye vyama.
Kwa hali ya sasa tutapata Wabunge 119 kutoka kundi hili. Idadi yao itaongezeka kutokana na kuongezeka kwa Halmashauri
zitakazoundwa pindi mahitaji yanapotokea. Haitakuwa tena kazi ya Tume za Uchaguzi kuunda Majimbo ya uchaguzi bali vile
vigezo vya kuunda Halmashauri (Baraza la Madiwani) vilivyopo kisheria (Local Government Authorities Acts) ndio vitatumika.
- Wabunge 231 watokane na kura za uwiano. Vyama vya siasa vitapata viti kutokana na uwiano wa kura ambao kila chama
kimepata katika Mkoa. Chama cha siasa ni lazima kiwe kimepata kwanza asilimia tano ya kura zote zilizopigwa katika Mkoa
husika ili kigawiwe viti. Kwa hiyo kila chama kitatengeneza orodha ya wagombea wake kwa kila Mkoa na kuipeleka Tume ya Taifa
ya Uchaguzi. Orodha hii iwe katika hali ambayo kama jina la kwanza ni Mwanaume la pili awe Mwanamke, hali kadhalika kama
jina la kwanza ni Mwanamke katika orodha la pili liwe la mwanaume. Mikoa itapata idadi ya Wabunge kutokana na vigezo maalumu,
mfano idadi ya watu n.k. Jambo la kuzingatia tu ni kwamba idadi ya sasa ya Wabunge katika mikoa isishuke baada ya mabadiliko
haya (no region shall be left worse off).
Mfano Mkoa wa Kigoma una Jumla ya Wabunge saba wa Majimbo. Iwapo tukibadili mfumo kama ninavyopendekeza hapa, kutakuwa na
wabunge wanne wa kuchaguliwa, kutoka Halmashauri za Wilaya Kasulu, Kibondo na Kigoma na Halmashauri ya Manispaa Kigoma
Ujiji. Hivyo wabunge watatu watagawiwa kwa vyama kutokana na uwiano wa kura ambao kila chama kitapata.
Kwa mapendekezo haya tuna uhakika wa kuwa na Wabunge wanawake zaidi ya theluthi moja katika Bunge. Lakini pia tutakuwa
na uhakika kwamba kila Mkoa utakuwa na Mbunge au Wabunge wanawake.
Ndugu Rais, mabadiliko haya ya mfumo wetu wa Uchaguzi yana faida nyingi sana. Moja ya faida ni kuvigeuza vyama vyetu vya siasa
kutoka katika kushindanisha watu tu, bali pia kushindanisha sera. Kwa sababu wananchi watakuwa wanapiga kura mbili. Kura moja
ya chama na kura nyingine ya ama diwani au Mbunge na Rais. Kura ya chama ndio itatufanya kupata wabunge wa uwiano. Wala
hatutatumia mfumo mmoja kuzalisha mfumo mwingine. Bali kila mfumo utazalisha Wabunge kuunda Bunge letu.
Vyama vikianza kushindanisha sera tutakuwa tumepiga hatua kubwa sana kama nchi katika kuimarisha mfumo wa demokrasia na kwa
kweli hatutokuwa na wasiwasi wa vyama kudhoofika kutokana na wagombea Binafsi kuruhusiwa.
Demokrasia ndani ya vyama itaimarika kwani Tume ya Taifa ya Uchaguzi itahakikisha vyama vinapata wawakilishi wake katika
Orodha ya Mikoa kidemokrasia. Pia pale Bungeni uliahidi kutengenezwa kwa “
code of conduct” ambazo zitakuwa binding kwa kila
chama ili kuimarisha demokrasia ndani ya vyama.
Ndugu Rais, najua una majukumu mengi ya Kitaifa. Sitaki nikuchoshe na barua yangu hii.
Hata hivyo, sisi hatutokuwa wa kwanza kufuata mfumo huu wa uwiano. Ndugu zetu wa Msumbiji wanafanya hivi. Pia Afrika ya
Kusini, Ujerumani, Uswidi na hata India.
Mfumo huu, pia unaweza kumaliza matatizo ya kisiasa ya Zanzibar kwani kila kura itakuwa na thamani. Wawakilishi wa Zanzibar
watatokana na kura za kila chama. Kura za Wapemba walio CCM na za Waunguja walio CUF zitahesabika. Hivyo, ile hali ya Pemba
yote kutoa Wawakilishi au Wabunge wa CUF tu au Unguja yote kutoa Wawakilishi au Wabunge wa CCM tu itaondoka. Hali hii pia
inaweza pelekea kupatikana kwa vyama vingine vyenye wawakilishi au Wabunge kutoka Zanzibar, kwani ushindani utakuwa ni wa sera
za vyama na sio watu.
Ndugu Rais, naomba utafakari mawazo yangu haya. Ninaamini kuwa ni muhimu kufanya mabadiliko ya mfumo wa siasa. Kesi ya
Mtikila sio sababu pekee ya mabadiliko, bali tunakokwenda hatuwezi kukwepa mabadiliko kwa faida ya demokrasia ya nchi yetu.
Kwa leo naomba niishie hapa. Nakutakia kila la kheri katika kazi.
Kwa ruhusa yako nina nakili barua hii kwa Spika wa Bunge letu Tukufu na pia kwa wasaidizi wako muhimu. Pia nina nakili barua
hii kwa Katibu Mkuu wa CHADEMA ambae pia ni Mjumbe wa Kamati ya Bunge ya Sheria, Katiba na Utawala.
Wako mtiifu,
Zitto Z. Kabwe (Mb)
Kigoma Kaskazini.
Nakala:
Ndg. Samuel Sitta (Mb)
Spika wa Bunge.
Ndg. Edward Lowassa (Mb)
Waziri Mkuu.
Ndg. Kingunge Ngombale Mwiru (Mb)
Waziri (OR) Siasa na Uhusiano wa Jamii.
Ndg. Mary Nagu (Mb)
Waziri wa Katiba na Sheria.
Ndg. Willibrod P. Slaa (Mb)
Katibu Mkuu, CHADEMA.