Mhe. Freeman Aikaeli Mbowe, Mwenyekiti wa chama Taifa,
Mhe. Dr. Wilbroad Peter Slaa (MB), Katibu Mkuu wa chama,
Mhe. Dr. Lilian Mbowe, Binti yetu mpendwa, Mke wa Mwenyekiti na Mshauri mkuu,
Waheshimiwa wabunge,
Watendaji wa Makao Makuu ya chama,
Viongozi mbalimbali,
Wazee wa CHADEMA mkoa wa Dar Es salaam,
Familia ya Mwenyekiti
Wanahabari,
Wageni waalikwa,
Mabibi na Mabwana,
Kwa niaba ya wazee wenzangu na kwa niaba yangu binafsi napenda kuchukua fursa hii kukushukuru Mwenyekiti na familia yako, kwa kukubali mwaliko wetu na kuweza kushiriki nasi katika tukio hili la kwanza la kihistoria katika historia ya uhai wa chama chetu. Pia nitumie fursa hii kuwakaribisha wageni wetu wote katika hafla hii na mjisikie mko mahali sahihi kwa wakati sahihi.
Mhe. Mwenyekiti naomba sasa nitoe maelezo mafupi juu ya sababu zilizotusuma kuandaa tukio hili katika eneo hili japo kuwa halina mandhali ya kuvutia kama kumbi za mahoteli mbalimbali hapa jijini. Katika shughuli zako za ujenzi chama na kupigania hali bora ya maisha ya watanzania wenzako umepita mikoa, wilaya na vijiji mbalimbali vya Tanzania na kujionea hali duni ya maisha ya watanzania huko vijijini.
Eneo hili la kijiji cha Makumbusho limekusanya mifano ya asili za maisha ya makabila mbalimbali ya Tanzania, kwahiyo tumeona ni eneo linaloweza kuvuta kwa karibu zaidi hisia zako juu ya maisha ya watanzania unaowapigania.
Kwahiyo tumekuleta hapa ili kukukumbusha safari yako ya mapambano ambayo bado yanaendelea, kwasababu hiyo tunaamini sasa utakuwa tayari kutuvumilia kwa hali yoyote iliyopo katika eneo hili. Mhe. Mwenyekiti, kabla sijaeleza sababu zilizotusukuma kuandaa hafla hii, naomba uniruhusu kurejea kwa ufupi historia ya chama chetu katika mapambano yake ya kutafuta mabadiliko ya kweli na uhuru wa kweli. Toka CHADEMA kilipoanzishwa na baada ya kupata usajili wa kudumu chini ya Mwenyekiti mstaafu ambaye pia ni muasisi wa chama Mhe. Mzee Edwin Mtei ambaye alizunguka maeneo mbalimbali ya Tanzania kwa lengo la kukitambulisha chama kwa watanzania.
Mwaka 1995 chama kilishiriki uchaguzi wa kwanza wa vyama vingi vya siasa kwa mafanikio ya kutia moyo ambapo chama kilipata viti 4 katika bunge la jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Baada ya hapo chama kiliendelea na harakati zake chini ya Mzee Mtei na baadaye chini ya Mhe. Mzee Bob Nyanga Makani hadi kilipoingia kwenye uchaguzi wa pili wa vyama vingi mwaka 2000, na kupata viti 5 katika bunge la Jamhuri ya Muungano na viti 49 vya udiwani.
Kwa wastani wa idadi ya viti na umri wa chama ilionekana chama kilikuwa kinashuka kiutendaji, lakini baada ya wewe kuchaguliwa kuwa Mwenyekiti wa chama mwaka 2003, ulianzisha kasi ya ujenzi wa chama ambayo ndani ya CHADEMA ilikuwa haijawahi kutokea katika kipindi chote cha uhai wake, uliacha jimbo lako la HAI ambalo ulikuwa ukiliwakilisha bungeni, ukaacha posho zako za vikao vya bunge na kubwa zaidi ukapunguza sana muda wa kukaa na familia yako na kuamua kuzunguka nchi nzima ili kuhamasisha watanzania kukiunga mkono chama ili kiimarike na kuwakomboa. Kwa hakika leo CHADEMA kinajulikana katika kila pembe ya nchi yetu.
Ni ukweli usiopingika kuwa katika ziara zote ulizofanya mikoani za kujenga na kuimarisha chama, sehemu kubwa ya fedha zilizotumika kugharamia shughuli mbalimbali zilitokana moja kwa moja au kwa njia nyingine na juhudi zako binafsi au familia yako kwa sababu ruzuku ya chama ambayo sisi sote tulikuwa tunaijua ya shilingi milioni 5 isingetosha hata kuchapa kadi peke yake kwa mwezi.
Ulibuni mipango mbalimbali ya kukijenga chama na kuwajengea uwezo viongozi mbalimbali kwa mfano mpango wa “CHADEMA NI TAWI”, falsafa ya NGUVU YA UMMA na kauli mbiu ya hakuna kulala mpaka kieleweke ni matunda ya ubunifu wako na ni mambo ambayo yanawajengea uwezo viongozi wa chama ngazi zote na kutujengea heshima mbele ya watanzania na kubainisha dhamira ya chama kwao.
Umeongeza kasi kutafuta marafiki wa chama ndani na nje ili kukijengea chama uwezo. Pia umeongoza mageuzi makubwa ndani ya chama na umeweza kuhimili mikikimikiki iliyotokana na mageuzi haya. Ulifungua milango kwa watu wote kujiunga na chama na ndiyo maana leo hii CHADEMA inajulikana kama “REAL MADRID” katika siasa za Tanzania.
Kwa ujumla umekuwa jemadari wa kutumainiwa katika chama na umerudisha imani ya watanzania kwa mageuzi. Wakati tunakaribia uchaguzi mkuu wa 2005, kwa imani kubwa ambayo wana CHADEMA na watanzania kwa ujumla walikuwa wamejenga kwako, uliombwa na vikao vya chama bila ridhaa yako mwenyewe kugombea urais wa jamhuri ya muungano kwa tiketi ya CHADEMA pamoja na kutwishwa jukumu hili zito na hatari.
Vikao vyote vyama chama vilipitisha jina lako kuwa mgombea wa nafasi hiyo bila kuanisha wapi utapata fedha na nyenzo zingine kwa ajili ya kampeni, ulipowauliuza kuwa nitapata wapi nyenzo zingine kwa ajili ya kampeni, vikao viliagiza kuwa fanya kila lililo ndani ya uwezo wako kuhakikisha kampeni zinafanywa kwa ufanisi na hadhi kubwa ili kukijenga chama na kuimarisha uwezo wake baada ya uchaguzi.
Sisi tuliposikia hayo tuliingiwa na wasiwasi mkubwa kwa vile tulijua chama chetu hakina fedha na kazi ameachiwa mtu mmoja tu kwa kuzingatia kuwa wasaidizi wako karibu wote walikuwa wagombea wa nafasi mbalimbali lakini tulifarijika sana baada ya kuona kampeni zimezinduliwa na kupanda kasi siku hadi siku.
Mhe. Mwenyekiti ulifanya kampeni ambazo wana CHADEMA wanaojua uwezo wa chama chao kifedha walifarijika na kujua kuwa tunaye kiongozi anayeweza kukipigania chama. Sisi tulilazimika kuamini kuwa fedha karibu zote zilizotumika katika kampeni kwa namna yoyote ile, zilitokana na juhudi zako wewe mwenyewe. Juhudi ulizofanya za kuhakikisha kampeni zinafanyika kwa ufanisi mkubwa ndizo zilizotusaidia kusogea kutoka tulipokuwa hadi hapa tulipo leo.
Juhudi hizo zimekitoa chama kutoka
- Wabunge 5 hadi wabunge 11
- Mbunge 1 viti maalumu hadi 6
- Asilimia 4.23 mwaka 2000 ya kura zote za wabunge hadi asilimia 8.2 mwaka 2005
- Madiwani 49 hadi 99.
- Ruzuku ya chama nayo imeongezeka kutoka milioni 5 kwa mwezi kipindi cha 2000-2005 mpaka milioni 35 kwa mwezi sasa.
Haya ni baadhi tu ya mafanikio yanayoonekana ambayo kwakweli wewe ni msingi mkuu wa mafanikio yake. Kwa kuzingatia ukweli huu wote na mengine ambayo hatukuyataja sisi wazee wa Dar Es salaam tuliona kama wanachama tunalo jukumu la kutambua juhudi unazofanya kujenga chama chetu. Tumeamua tukuite hapa leo ili tutoe shukrani zetu za dhati kwako binafsi na kwa familia yako kama washauri wako namba moja kwa kazi nzuri na kubwa ambayo familia imekuwezesha kukifanyia chama na watanzania wote.
Pamoja ana shukrani zetu za maneno, tumeandaa zawadi kidogo kama ishara ya shukrani zetu.
Mhe. Mwenyekiti, Tunakuomba upokee:-
- Vazi la mgolole na kilemba kama ishara ya busara na uongozi wa watu
- Mkuki kama silaha ya mapambano ili kuwarejeshea watanzania uhuru wa kweli na mabadiliko ya kweli.
- Ngao kama ishara ya ulinzi wako katika mapambano na ulinzi wa watu wako yaani watanzania.
Pia kwa kutambua mchango wa binti yetu yaani mkeo Dr.Lilian Mbowe tunaomba kumzawadia kinyago cha Twiga ambaye ni mnyama mwenye sifa kubwa mbili:-
- Ni mnyama mpole sana asiye na ugomvi na mnyama yeyote porini.
- Ni mnyama mwenye busara na upeo wa kuona mbali, na kwasababu ya upeo wake huwaokoa maelfu ya wanyama kule mwituni kwa kuwaona maadui zao wangali mbali na kuwapa ishara wanyama wengine ili wajiokoe kwahiyo wewe kama mshauri namba 1 wa mwenyekiti, tunakupa alama hii ili udumu kuwa na upole, busara na upeo wa kumshauri kwa kwa hekima na busara Mwenyekiti wakati yuko katika mapambano ya kuwakomboa watanzania
Mhe. Mwenyekiti hatuna cha zaidi cha kuwapa ili kufananisha na kazi yenu kama shukrani yetu kwenu bali tunaomba mtambue kuwa tunatambua juhudi, busara na dhamiri yenu ya dhati ya kuwakomboa watanzania na tunaomba Mungu awazidishie nguvu na hekima ili uongoze chama chetu na kukifikisha kwenye lengo lake kuu la kushika dola.
Ahsanteni sana Mungu awalinde wewe na familia yako