lf.bevel
MWANZO CHAMA SERA KATIBA TUUNGE MKONO UCHAGUZI TUWASILIANE
banner
Mabaraza
»Wanawake
»Vijana
»Wazee
b.part
Mengineyo
»Habari Mpya
»Makala mbalimbali
»Midahalo
»Blogu za wanachama
»Picha za matukio
»Maoni Yenu
b.part
Barua Pepe
jina la mtumiaji:
neno-siri
rt.bt.spc
bt.part2

Waraka wa kwanza kwa Wafanyakazi Vijana

2/2/2008

Salam za Mwaka Mpya:

Awali ya yote naomba kukupa salamu zangu za mwaka mpya nikikutakia mwaka wenye upendo, furaha, jitihada na mafanikio. Huu ni waraka wangu kwako wewe mfanyakazi kijana uliyemshirika wa Y4C na Mfuko wa Tumaini Jipya. Kama wewe hujawa bado wakala wa mabadiliko kupitia jumuia hii unaweza pia kusoma ujumbe huu, na nakukaribisha kujiunga nasi katika harakati za kizazi kipya.

Tumetoka wapi?

Mwaka 2007 ulikuwa ni mwaka mzuri katika harakati zetu za kuhamasisha na kusimamia mabadiliko nchini. Kwa upande wa chama kwa ujumla ulikuwa ni mwaka ambao tulikuwa mstari wa mbele katika kupambana na ufisadi na kutetea rasilimali za Taifa. Kuanzia Bajeti Mbadala ya Upinzani; hoja ya Zitto Kabwe kuhusu Buzwagi; Hoja na Dr Slaa kuhusu ufisadi Benki Kuu na hatimaye kutajwa kwa “Orodha ya Mafisadi”(list of shame); Ziara za Mwenyekiti Freeman Mbowe kuhamasisha wananchi vijijini nk- kwa ujumla moto wa mabadiliko umeanza kusambaa! Hatahivyo umekuwa ni mwaka ambao gharama za maisha zimezidi kupandishwa kwa kodi lukuki na matumizi makubwa ya serikali, huku suala la kuboreshwa kwa mishahara likiendelea kuwa kizungumkuti na ‘maisha bora kwa kila mtanzania’ ukiwa ni wimbo wa kebehi kwa wananchi wengi masikini. Kwa upande wa vijana, harakati zimeendelea vizuri- kuanzia utetezi wa maslahi ya wanafunzi mpaka utetezi wa maslahi ya ‘wamachinga’, huku matukio mbalimbali yakifanyika kuhamasisha harakati za kizazi kipya! Lakini fanikio kubwa kuliko yote kwa vijana katika mwaka uliopita ni uzinduzi wa Mfuko wa Tumaini Jipya kupitia jumuia ya Y4C.

Nachukua fursa hii kukumbusha tena dhamira ya mfuko wetu. Mfuko wa Vijana na Ubunge ni mfuko unaounganisha wafanyakazi wote wa Tanzania, waliodhamiria kwa dhati kuunganisha uzalendo wao kwa manufaa ya taifa lao, kwa kuchangia raslimali na ustadi wao wa kitaaluma ili kufanikisha azma ya kuongeza Wabunge Vijana kuanzia mwaka 2010 kupitia chama mbadala - CHADEMA. Mfuko huu ni wa jumuia ya siri ya vijana wafanyakazi inayojulikana kama Y4C (Youth for Change) ambayo iko chini ya kurugenzi ya vijana wa CHADEMA. Dira ya mfuko huu ni kuwa na; Bunge lenye uwakilishi mzuri wa vijana, lenye ushindani, na lenye kusimamia kikamilifu utendaji na uadilifu wa serikali kwa manufaa ya umma. Mfuko utatunisha angalau Tsh. Bilioni moja ndani ya kipindi cha miaka 3, kwa kuanzia mwaka 2008 - hadi Septemba Mosi 2010. Wazalendo 4,000 kama wewe watafikiwa nchi nzima na mfuko huu ambapo kila mmoja atachangia walau laki moja kwa mwaka ama elfu kumi kwa mwezi.

Tunakwenda wapi?

Mwaka 2008 umeanza kwa matumaini makubwa - katika mwezi Januari umefanyika upanuzi wa ofisi ya makao makuu ya chama katika awamu ya kwanza ili kupata nafasi kubwa zaidi ya kufanyia harakati; lakini pia ilikuwa ni kipindi cha kuweka sawa mipango yetu katika mwaka huu mpya. Kwa upande wa Mfuko wa Tumaini Jipya-Y4C tumedhamiria kuongeza idadi yetu na kufanya matukio katika mikoa mingine walau mine katika kipindi hiki. Sasa ni wakati wa kuendeleza safari ya pamoja kuyasaka mabadiliko.

Nakushukuru wewe kijana ambaye umeanza kuchangia mfuko huu tangu mwishoni mwa mwaka jana; na nikujulishe kwamba wapo vijana wa zamani ambao nao wameguswa na harakati hizi za kizazi kipya na kujitokeza kuchangia mfuko huu. Hivi karibuni, muasisi wa CHADEMA Mzee Edwin Mtei amejitokeza kuunga mkono harakati zetu kwa kuchangia shilingi milioni moja taslimu katika Mfuko wa Tumaini Jipya!

Ufanye nini tufike?

Leo nina maombi matatu kwako: Mosi, nakuomba uchangie harakati hizi kuanzia mwezi Januari na kuendelea. Na kama ahadi ama dhamira yako ilikutuma kuchangia kuanzia mwaka jana tulipofanya halfa basi unawajibika kufanya hivyo; kwani ahadi ni deni. Michango ya kifedha kwa ajili ya Y4C na Mfuko wa Vijana na Ubunge 2010 iwasilishwe kwenye akaunti ifuatayo:

Jina la Akaunti:TUMAINI JIPYA
Nambari ya Akaunti:018103010943
Benki:National Bank of Commerce (NBC)
Tawi la Benki:Mnazi Mmoja

Pamoja na FEDHA (treasure), unaweza kutoa michango mingine kama MUDA (time) na KIPAJI/UTAALAMU (Talent). Hivyo, unatarajiwa kutumia 3T ulizonazo katika kufanikisha harakati hizi.

Pili, nakuomba uunge mkono ujenzi wa oganizesheni ya chama mbadala kupitia uchaguzi wa CHADEMA. Hususani nakuomba uunge mkono uanzishwaji wa Baraza la Vijana wa CHADEMA (BAVICHA). Kama unataka kuona upinzani wenye nguvu Tanzania basi hii nayo ni hatua muhimu ya kuwa wakala wa mabadiliko unayotaka kuyaona. Ili kushinda uchaguzi na hatimaye kuweka uongozi mfumo mpya wa utawala ama kuepusha hodhi ya chama kimoja bungeni kunahitajika oganizesheni mahiri kuanzia ngazi ya chini mpaka taifa itakayoshiriki kufanya kampeni lakini pia kulinda kura. Huu ni wakati wa kujenga mfumo huo kupitia uchaguzi wa chama. Kama wewe ni mwanachama, ni wakati wa kutimiza wajibu wako kwa kushiriki katika mchakato huu. Kama wewe si mwanachama lakini unapenda mabadiliko ni wakati wa kuunga mkono harakati hizi kwa hali na mali. Maelezo na maelekezo kuhusu uchaguzi huu yanapatikana hapa: http://www.chadema.net/uchaguzi/2008/taratibu.php . Unaweza kufanikisha mchakato huu katika eneo lako au eneo lingine lolote utakaloona ni muhimu. Kuwa wakala wa mabadiliko unayotaka kuyaona.

Tatu, nakuomba ushiriki katika kuipanua jumuia yetu. Kumbuka lengo letu ni kuwa na wanaY4C elfu nne kutoka maeneo mbalimbali katika nchi yetu. Unaweza kuwasiliana na marafiki zako wengine ambao wanamuelekeo wa kuunga mkono harakati zetu ili niweze kuwasiliana nao kuwahamasisha kushirikiana nasi. Na pindi watakapokubali, ndipo unitumie majina na anuani zao ili niweze kuwasiliana nao kwa ajili ya hatua za ziada.

Hatuhitaji watu wote, tunahitaji watu walio bora- wenye imani, matumaini na mwelekeo wetu. “Better few, but better”. Mabadiliko ya kweli huanzia katika jumuia ya watu wachache na kuambukiza umma kwa ujumla. Lengo letu ni kuwa na watu elfu nne tu katika taifa la watu milioni karibu arobaini! Kufikia lengo hili ni suala rahisi kama wewe utachukua hatua. Vijana 200 kila mmoja akihamasisha vijana 5 kuchangia Mfuko wa Tumaini Jipya na kushiriki harakati za Y4C, tutakuwa na vijana 1000; vijana hawa elfu moja kila mmoja akitafuta wenzake watano tutakuwa na vijana 5000- tutakuwa tumevuka lengo letu la vijana elfu nne. Inawezekana, kama tu ukiamua kutimiza wajibu wako! Kwanini usiwahusishe marafiki zao watano katika jumuia hii?

Hayo ndiyo maombi yangu matatu; matatu tu. Lakini ukifanya hayo matatu, utakuwa umetoa mchango mkubwa katika taifa lako. Utakuwa umeingia katika kundi la waopambana na ufisadi na kutetea rasilimali za Taifa. Utakuwa umeingia katika jumuia ya wanaowezesha mabadiliko nchini. Na kwa wale watakotimiza wajibu huu mapema katika kipindi cha mwezi Januari na Februari, nitawapatia kalenda maalumu za chama mbadala.

Wajibu wetu

Mwisho narudia tena ahadi yetu ya kuendelea kuratibu harakati hizi na kuwapa taarifa za mara kwa mara. Tutawaeleza pia ratiba ya matukio ambayo yatafuata. “Dhana kuhusu Mfumo wa Tumaini Jipya” inayotoa picha pana zaidi ya harakati zetu inapatikana kwa wanachama pekee. Lakini pamoja na nia njema ya uwazi katika utendaji ikiwemo matumizi ya fedha suala la USIRI litatiliwa mkazo kwa nia ya kuhakikisha majina ya washirika wasiopenda majina yao kujulikana yanahifadhiwa lakini pia kwa nia ya kulinda siri za mikakati ya ndani ya utendaji wa mfuko mzima kwa ujumla wake. Hivyo taarifa za fedha na za utendaji zitawekwa katika mfumo ambao zitalinda majina na mikakati isiyopaswa kufahamika kwa umma. Kitu pekee cha kuhofia, ni hofu yenyewe. Uovu hushamiri Wema unapojificha. Tuko pamoja mpaka kitakapoeleweka!

Wako katika demokrasia na maendeleo,

John Mnyika
Mkurugenzi wa Vijana Taifa

CHADEMA: Mabadiliko ya Kweli; Uhuru wa Kweli
VIJANA; Nguvu ya Mabadiliko

Mawasiliano zaidi yafanyike kupitia:

Kurugenzi ya Vijana
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA)
Makao Makuu
Kinondoni, Mtaa wa Ufipa
P. O. Box 31191
Dar e salaam
Tanzania
Simu/Faksi: 2668866
A-pepe: vijana@chadema.net


Bw. John Mnyika (Mkurugenzi wa Vijana)- mnyika@chadema.net na 0754694553
Bi. Regia Mtema (Afisa wa Vijana)- chademav@yahoo.com na 0713760534


lf.curl lf.curl2 rt.curl2 rt.curl