|
Afya kwa Wote
Hali Halisi ya Afya Ikoje Tanzania?
Mazingira duni ya wahudumu wa afya. Madaktari na manesi wanapata maslahi duni, vitendea kazi haba na chakavu
na hospitali ni chafu. Hali hii imewajengea wahudumu wa afya mazingira ya rushwa.
-
Gharama za afya ni mzigo kwa wananchi. Serikali imekwepa jukumu la kutoa huduma za afya kwa wananchi.
Huduma za afya zimekuwa za kibiashara.
- Huduma ya afya haziridhishi. Licha ya kuchangia gharama huduma ni mbaya na zinatolewa kwa misingi
ya rushwa. Wakati wananchi wanapoteza maisha yao kwa magonjwa yanayotibika kama malaria viongozi wanafuja fedha nyingi za
umma kutibiwa nje ya nchi. Wagonjwa zaidi ya mmoja kulala kitanda kimoja limekuwa jambo la kawaida. Inasikitisha zaidi
kuona kina mama wajawazito wakilazimishwa kwenda kujifungua bila vifaa kama vile pamba, gloves na hata nyembe!
Hii imefanya kina mama waendelee kujifungulia majumbani au hata kwa wakunga wa jadi kwa kukosa vifaa husika.
Kujifungua ni jambo linalostahili staha na faragha.
Serikali ya CHADEMA itafanya nini?
- CHADEMA inaamini kuwa afya bora ndio msingi wa maendeleo. Wananchi wasio na afya bora hawataweza kujishughulisha
katika ujenzi wa Taifa lao na katika kujipatia kipato cha kuendesha maisha yao ya kila siku. Tunatambua kuwa mataifa mengi
yaliyoendelea yamefanikiwa kwa kuwekeza katika afya. Kwa CHADEMA sekta ya afya itaboreshwa zaidi ili wananchi wote waweze kupata
huduma hii muhimu ili waweze kuchangia vyema katika maendeleo ya nchi yao.
- Gharama nafuu za huduma ya afya. Itapanua mpango wa bima ya afya kwa kumshirikisha kila Mtanzania. Huduma
zote zinazohusu afya ya mama na mtoto zitaondolewa kodi na kutengewa fedha za kutosha. Itatoa tiba ya malaria bure.
- Huduma kwa wanaoishi na VVU. Serikali za mitaa zitawahudumia watu wanaoishi na VVU kwa kuwapatia dawa za
kurefusha maisha na matunzo ikiwemo lishe bora.
- Bajeti ya afya kuongezwa. Maslahi na vitendea kazi vya madaktari na manesi kuboreshwa. Itatoa motisha kwa
hospitali safi.
|