lf.bevel
MWANZO CHAMA SERA KATIBA TUUNGE MKONO UCHAGUZI TUWASILIANE
banner


Hotuba ya msemaji mkuu wa kambi ya Upinzani Dr. Willibrod Peter Slaa (Mb)

Kuhusu makadirio ya matumizi ya fedha ya ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za mitaa kwa mwaka wa fedha 2008/2009


I.  Utangulizi

Mheshimiwa Spika,
Napenda kuchukua nafasi hii, kwa niaba ya Kambi ya Upinzani kuwasilisha Maoni ya Kambi ya Upinzani kuhusu Hotuba ya Mapitio na Mwelekeo wa Kazi za Serikali na Makadirio ya Matumizi ya Fedha, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa kwa Mwaka wa Fedha, 2008/2009 kwa mujibu wa Kanuni za Bunge Kifungu cha 96(6) Toleo la Mwaka 2007.

Mheshimiwa Spika,
Kwa namna ya pekee namshukuru Mwenyezi Mungu kunifikisha Kwenye Haki na Ukweli, baada ya kuishinda tena CCM kwenye Kesi ya Uchaguzi namba 20/2005 ambapo Mahakama Kuu Kanda ya Arusha ilinitangaza kama Mbunge halali wa Karatu na kutupilia mbali malalamiko yaliyowasilishwa na waliojiita wakereketwa wa CCM. Nawashukuru sana wananchi wa Karatu ambao waliendelea kuniunga mkono wakati wote wa kesi hiyo ya Uchaguzi. Nawapa pole kwa usumbufu wote waliopata kipindi chote cha kesi. Nachukua fursa hii kuwahakikishia kuwa nitawatumika kwa akili, moyo na uwezo wangu wote katika kufanya yale yote tuliyocheleweshewa kwa kipindi chote cha kesi. Nachukua fursa hii pia kuwashukuru Watanzania wote kutoka kona zote za Tanzania wenye mapenzi mema ambao kwa maelfu waliniletea salamu za pongezi baada ya Mahakama Kuu kutangaza ushindi huo tarehe 15 May, 2005. Asanteni sana Salamu zenu zilinifariji sana. Mwenyezi Mungu awarudishie mara mia kwa upendo wenu.

Mheshimiwa Spika,
Nitakuwa nimekosa fadhila iwapo sitatoa shukrani kwa Chama changu CHADEMA , vyama vya CUF, TLP, NCCR-Mageuzi , pamoja na Waheshimiwa Wabunge wenzangu wa Kambi ya Upinzani wakiongozwa na Mhe. Hamad Rashid Mohamed, (Mb) Mbunge wa Wawi na Kiongozi wa Upinzani Bungeni, na wengi wa Wabunge wenzangu wa Chama Tawala ambao wote kwa ujumla wao wakati wote wa Kesi walikuwa wakinitakia heri na ushindi. Ni kweli haki inaweza kucheleweshwa tu, lakini haiwezi kamwe kupotea na wala Ukweli hauwezi kufunikwa kwa mbinu na hila. Ninamshukuru sana Wakili wangu Tundu Lissu kwa kufanya kazi yake kwa umakini mkubwa.

Mhe. Spika, kwa mara ya kwanza katika historia ya nchi yetu, tumepata ushahidi wa dhahiri kwani kila tulipokuwa tukisema kuwa baadhi ya watu wa CCM huwa wanaiba kura watu wengi walikuwa hawaamini na wengine hutuzomea. Kwa uamuzi wa Mahakama Kuu katika kesi na 20/2005 hasa kwa wakereketwa husika kuingiza nyaraka za “kugushi”, na za “udanganyifu” Mahakamani ushahidi wa wazi umepatikana na mbinu moja ya wazi ya wizi wa kura nayo imebainika hadharani. Ninawashukuru sana wahusika wakereketwa waliotufungua macho kwa njia ya kesi hiyo kwani itatusaidia sana katika kupanga mikakati bora zaidi katika kuthibiti wizi wa kura katika chaguzi zijazo. Ni kweli kesi si jambo jema, lakini ‘hakuna baya lisilo na jema’, kwani bila kesi hiyo tusingeliweza kufahamu siri kubwa inayotumika katika kuiba kura.

Mheshimiwa Spika,
Napenda kumpongeza kwa dhati kabisa Mhe. Mizengo K.P.Pinda (Mb) Waziri Mkuu kwa kuteuliwa na Rais kuwa Waziri Mkuu na hatimaye kuthibitishwa na Bunge lako Tukufu. Ninampongeza pia Mhe. Celina O.Kombani (Mb) kwa kuteuliwa kuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa pia Mhe.Aggrey Mwandri kwa uteuzi huo, lakini pia kwa kuandaa Bajeti yao hii ya kwanza, wakisaidiana na Makatibu wao Wakuu na Wataalam wao wote.

Mheshimiwa Spika,
Nitakuwa mtovu wa shukrani iwapo sitakushukuru wewe binafsi, Naibu Spika na Wenyeviti wa Bunge kwa kazi nzuri mnayofanya ya kuliongoza Bunge letu Tukufu. Ninamwomba Mwenyezi Mungu awajalie hekima na busara na kuwapatia nguvu na afya mnazohitaji katika kuliendesha vizuri Bunge letu hasa katika kipindi hiki kigumu katika historia ya nchi na Bunge letu.

Mheshimiwa Spika,
Hii ni bajeti ya Tatu tangu Serikali ya Awamu ya Nne iliposhika uongozi wa nchi yetu. Kambi ya Upinzani inatoa maoni yake kwa kufanya tathmini ya Malengo na Mwelekeo wa kazi za Serikali katika vipindi mbalimbali vya nyuma ikiwa ni pamoja na utekelezaji wa malengo ya Serikali ya Awamu ya Nne kwa kipindi cha tangu waliposhika madaraka.

Mheshimiwa Spika,
Kwa vile Waziri Mkuu ni msimamizi wa Shughuli za Serikali Bungeni, na mjadala wa Waziri Mkuu unaihusu serikali yote, tunapenda Mheshimiwa Waziri Mkuu atoe majibu ya kuridhisha katika maeno yote ambayo Waziri wa Fedha hakutoa majibu ya Kuridhisha, hasa kwa vile Waziri Mkuu ndiye mwenye kauli kuhusu shughuli za Serikali Bungeni. Mheshimiwa Spika, kwa vile kupanga bajeti ni hatua moja muhimu, lakini usimamizi wa fedha hizo ni muhimu zaidi, Mchango wa Kambi ya Upinzani safari hii utajikita zaidi kwenye maeneo mengi yenye utata ili Bunge na Wananchi kwa ujumla wapate majibu ya kuridhisha.

Aidha, Mheshimiwa Spika,
kwa muda mrefu sasa Taifa letu, ndani ya Bunge hili Tukufu, kwenye mikutano ya hadhara na kwenye vyombo vya Habari limegubikwa na Taarifa za kusikitisha kuhusu Tuhuma za uvunjifu wa Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma namba 13 ya mwaka 1995, zinazomhusisha Mhe. Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu, Mhe. Benjamin William Mkapa kuhusiana au kupitia makampuni anayomiliki ya Tanpower Resources Ltd na ANBEM. Tuhuma hizo pia zimemhusisha aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini wa kipindi hicho hicho. Kambi ya Upinzani inaona si vema kujadili maswala ya Bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu, bila kupata ufafanuzi wa kina wa maswala haya muhimu kwani imani ya Watanzania wengi imeguswa na Tuhuma hizi na hivyo kuwa na mashaka na fedha nyingi zinazoidhinishwa na Bunge kama kweli zinatumika kwa malengo yaliyokusudiwa.

Kwa niaba ya Kambi ya Upinzani na wananchi wote wanaopenda kujua ukweli, Mchango wetu unajikita katika maeneo yafuatayo:

II.  Ubadhirifu/Rushwa na Ufisadi

Mheshimiwa Spika,
Bajeti inatumika na Serikali kupanga matumizi ya fedha kidogo zilizopo katika maeneo na Sekta muhimu zinazohitaji kipaumbele katika kuleta maendeleo kwa Taifa na Wananchi wote kwa ujumla. Hivyo ni kweli kuwa Bajeti ni silaha na chombo muhimu sana katika kutoa dira ya utendaji kazi katika Taifa. Hata hivyo, Kambi ya Upinzani, ina maoni kuwa kupanga ni kitu kimoja na kutumia kilichoidhinishwa na Bunge ni kitu kingine. Tatizo kubwa zaidi ni katika nidhamu ya Matumizi na Uadilifu wa kutumia kilichoidhinishwa na Bunge kwa malengo yaliyopitishwa katika Bajeti. Ni kwa msingi huu, haiwezekani kutenganisha masuala ya Bajeti na masuala ya udhibiti wa matumizi, nidhamu ya matumizi na uadilifu wa wanaopewa majukumu ya kusimamia utekelezaji wa Bajeti husika .

Mheshimiwa Spika,
kwa mujibu wa Katiba yetu, Ibara ya 63(2) Bunge ndiyo “chombo kikuu” katika Jamhuri ya Muungano na majukumu yake ya kikatiba, tukiacha ya kutunga Sheria ni “kuisimamia na kuishauri” Serikali. Kambi ya Upinzani ina maoni kuwa kwa vile viko vyombo vingi na watu wenye sifa mbalimbali wanaofanya kazi ya “kuishauri Serikali, Bunge ni chombo pekee cha “kuisimamia”. Hivyo ni lazima Bunge nalo lifanye kazi hii kwa uadilifu mkubwa Mhe. Spika, Bunge lisipotimiza vizuri wajibu wake huu, na mambo yakaharibika katika nchi, Bunge halitakuwa na maelezo yeyote kwani hakuna chombo kingine chochote kwa mujibu wa Katiba yetu chenye uwezo wa “kuisimamia Serikali”. Tunaposema Serikali ni pamoja na kusimamia Matendo na Maamuzi ya Rais, jambo ambalo watu wengi hawalielewi kwa kudhani kuwa Rais yuko juu ya Sheria ya Nchi. Kambi ya Upinzani imependa kuweka hili wazi kutokana na mawazo mbalimbali yanayojitokeza mara kwa mara katika mijadala mbalimbali kama yalivyoripotiwa na vyombo mbalimbali vya Habari. Huu ni msingi mkubwa katika nchi ya kidemokrasia na hasa inayofuata mfumo wa ‘mgawanyo wa Madaraka’ yaani Separation of Powers. Bunge basi linajukumu pekee la kuisimamia Serikali na vyombo vyake vyote bila kuingilia utendaji wao.

Mheshimiwa Spika,
jukumu la kusimamia ni pamoja na kupata Taarifa zote zinazohitajika kutekeleza jukumu la Usimamizi, kufanya maamuzi na kusimamia maamuzi hayo muhimu pale inapohitajika kama chombo cha Usimamizi.

  1. UBADHIRIFU KUPITIA EPA NA RICHMOND
  2. Mheshimiwa Spika,
    Mwaka uliopita, wakati nawasilisha Hoja ya Kambi ya Upinzani kuhusu Ofisi ya Waziri Mkuu nilitoa hoja mbalimbali kuhusu Ubadhirifu mkubwa ndani ya Benki Kuu ya Tanzania, (BoT) kama ilivyonukuliwa na Kumbukumbu za Bunge “Hansard” ya Kikao cha Tisa, Tarehe 25 June, 2007. Pamoja na kwamba hoja hiyo ilipingwa sana na baadhi ya Wabunge wenzangu. Nashukuru kuwa sasa suala la Ubadhirifu katika vyombo vyetu mbalimbali na ndani ya Serikali siyo tena suala la mjadala kwani mengi zaidi yamejitokeza. Jamii nayo sasa imezoea neno Ufisadi, na Ufisadi unajadiliwa kwa uwazi bila woga tofauti na ilivyokuwa hapo awali.

    Vyombo vya Habari navyo vimefanya kazi nzuri sana kufanya uchunguzi wa kina na kuwapa habari Watanzania kuhusu hali ya ufisadi katika nchi yetu. Kambi ya Upinzani inavipongeza sana vyombo vyote vya habari kwa kazi nzuri waliyoifanya na waendelee na moyo huo huo wa kuwaelimisha Watanzania.

    Mheshimiwa Spika,
    Kambi ya Upinzani imefarijika sana kwamba sasa pazia kubwa lililofunika masuala ya Ubadhirifu limeondoka na masuala haya yanajadiliwa siyo tu ndani ya Bunge lako Tukufu bali na Watanzania ambao kimsingi ndiyo wadau wakubwa na wamiliki wa mali na Rasilimali za Taifa hili.

    Mheshimiwa Spika,
    mjadala wa ubadhirifu na Ufisadi ndani ya BOT kuhusu Kasma ya EPA ulishafika ndani ya Bunge kama chombo cha Usimamizi. Bunge kama wawakilishi wa Wananchi wamestushwa na kiwango kikubwa cha Ubadhirifu huu, tena wakati wananchi wanajifunga mikanda, wanakabiliwa na hali ngumu ya maisha kutokana na gharama ya maisha ambayo imepanda sana. Maelezo kuwa gharama ya maisha imepanda kutokana na sababu zilizo nje ya uwezo wetu hazikubaliki kwa sababu haiwezekani hali hiyo iwe kwa wananchi wa kawaida tu, wakati kundi dogo la watu, kama ilivyoainishwa kwenye Ufisadi wa EPA linaneemeka na limeachiwa tu.

    Mheshimiwa Spika,
    Wananchi wengi wa Tanzania wameacha kunywa chai kwa vile Sukari sasa imekuwa bidhaa ya anasa, mikate iliyokuwa kimbilio la walala hoi hasa mijini imekuwa haishikiki tena kwa vile bei ya mkate unakimbilia shs 1,000. Nyama inazidi kuwa hadithi ya kusadikika kwa Watanzania wengi kwani bei ya kilo inakimbilia zaidi ya shs 2,500 kwa kilo katika maeneo mengi. Mchele ambao ukiacha mahindi unakuwa chakula cha Watanzania wengi unakimbilia Tshs 1,500/ kwa kilo. Mhe. Spika, lazima Bunge kama mwakilishi wa Wananchi lichukue nafasi yake kusimamia maslahi ya Watanzania na kulinda haki zao.

    Mheshimiwa Spika,
    Kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Ibara ya 8, na ninanukuu;

    “8(1)(a) Wananchi ndio msingi wa mamlaka yote, na Serikali itapata madaraka yake yote kutoka kwa wananchi...”
    “8(1)(b) lengo kuu la Serikali kwa Wananchi ni ustawi wa wananchi...
    “8(1)c) Serikali itawajibika kwa Wananchi...”
    “8(1)(d)Wananchi watashiriki katika shughuli za Serikali yao kwa masharti ya Katiba...

    Mheshimiwa Spika,
    hali ilivyo haielekei kabisa kama Serikali inawajibika kwa Wananchi. Wananchi wamebaki kuwa watazamaji katika shughuli za Serikali tofauti na matakwa ya Katiba kwani kama Bunge hili ambalo linawawakilisha Wananchi linashindwa kushirikishwa hata kwa mambo ya msingi ni kwa namna gani Serikali itajitetea kuwa Wananchi wanashirikishwa? Maoni haya yanatokana na mambo yafuatayo:-

    1. Hadi sasa, Takriban miezi sita, tangu Taarifa ya Ukaguzi wa EPA kuwasilishwa kwa Mheshimiwa Rais, Taarifa hiyo imebaki kuwa Siri. Usiri huu ndio unaosababisha minong’ono mingi na mashaka kuwa Serikali haiko makini na vita dhidi ya Ufisadi. Ufisadi uliohojiwa ndani ya Bunge na ilikuwa muhimu kwa Serikali kutoa Taarifa ya kina kwa Bunge na kwa umma wa Watanzania.

    2. Kambi ya Upinzani imestushwa sana na Taarifa ya Mhe. Mkullo Waziri wa Fedha alizotoa Bungeni ijumaa wakati anahitimisha hoja yake kuwa “Fedha za EPA si za Serikali bali za wafanyibiashara walizolipa kwa ajili ya kununua bidhaa nje” Mhe. Spika kutokana na Taarifa hiyo ambayo dhahiri ni ya kupotosha, Kambi ya Upinzani imefanya utafiti wa kina na kugundua kuwa Fedha hizo kimsingi zinatokana na programu inayoitwa “Debt Buy Back Program”. EPA imefanyiwa kazi sana na Timu ya Lazard na baadaye ukaguzi wa PricewaterhouseCoopers (France) tarehe 25 November, 2004. Hata hivyo ukaguzi uliofanywa na Deloitte and Touche 2006 na baadaye kuthibitishwa na Ernst and Young, 2007 ulithibitisha kuwa Kampuni 22 zilifanya biashara na Makampuni yanayodhaniwa “hewa”. Hivyo wafanyibiashara hao, wala “principles “ wao nchi za nje hawakuweka fedha zozote BOT kwa lengo kutumiza masharti ya Debt Buy Back Program kama alivyotaka kueleza Waziri wa Fedha. Kwa msingi huo fedha zilizoibiwa ni za Serikali ya Tanzania.

    3. Kwa Taarifa tuliyonayo, Ripoti ya Ukaguzi wa EPA katika kifungu cha 3.20, 3.23, na 3.24, kinatamka wazi uwepo wa “fraudulent supporting documents submitted in to support claims” Yaani ufisadi uliotumika ni pamoja na kutumia hati za kugushi katika kutoa fedha kutoka BOT; malipo ya viwango visivyo sahihi au kutumia viwango visivyo sahihi vya kubadilisha fedha (yaani incorrect amounts and incorrect exchange rate). Ukaguzi ulionyesha kuwa kati ya Tshs 133 Billioni malipo ya zaidi ya 90.3 Billioni yalifanyika kwa kutumia Hati za kugushi (invalid and fraudulent supporting documents), nyaraka hizi zimeonyeshwa katika kiambatanisho C ikionyesha na majina ya Makampuni husika.

    4. Katika kifungu cha 3.25 Ukaguzi huo ulishauri kuwa kwa malipo ya zaidi ya 42.6 Billioni uchunguzi wa kina unahitaji kufanyika. Taarifa hii haikutolewa wazi kwa Bunge wala kwa Watanzania ambao ndio wenye mali hiyo na Serikali ni mdhamini kwa niaba yao tu.

    5. Ufisadi unaotisha zaidi ni ule uliofanyika kupitia Kampuni ya Kagoda Agriculture Ltd iliyosajiliwa nchini chini ya Sheria ya Makampuni Sura ya 212 tarehe 29 September, 2005 na kupata Hati na 54040. Wakurugenzi waliosajiliwa wa Kagoda ni watu wawili wenye anuani za Kipawa Industrial area, Plot no 87 Temeke Dar-Es-Salaam, na P.O.Box 80154 Dar-Es-Salaam, kinyume na utaratibu wa usajili Brella ambao unahitaji wakurugenzi wa Makampuni kujisajili kwa kuonyesha anuani ya mahali anapoishi na siyo Sanduku la Posta.

      Isitoshe, kwenye Fomu za usajili, ambapo John Kyomuhendo amejionyesha kuwa “Promoter” hawakuonyesha kama ni wakurugenzi mahali pengine kwenye kampuni nyingine yeyote. Cha kushangaza ni kuwa Kampuni hiyo ambayo wakurugenzi wake dhahiri wanaonekana wapya kabisa katika uwanja wa biashara ndani ya wiki 8 walikuwa wamekwisha kuchotewa zaidi ya Dolla za Marekani 30.8 Millioni yaani karibu zaidi ya shs Billioni 40 kwa kinachoelezwa na ukaguzi wa EPA kuwa hati bandia ambazo dalili za wazi ni kuwa Hati hizo karibu zote zimesainiwa na watu wasiohusika na Makampuni zinazodhaniwa zimefanya biashara na Kampuni ya Kagoda (Kif.cha 3.27); baadhi ya Makampuni yaliyodhaniwa kufanya Biashara na Kagoda au hayako kabisa au yamekwisha kubadilisha majina yao (Kif.3.27), Makampuni hayo ambayo yako Marekani, Japan, Ujerumani, Italia, Ufaransa mengine hata anuani zake hazikujulikana kabisa. Katika hali hii inayoonyesha wazi kuwa kulikuwa na kugushi. Mhe. Waziri Mkullo alipokuwa akijibu alitetea kuwa fedha za EPA si za za Serikali. Kinachotisha zaidi, Mhe. Spika, hata Kampuni ya Ukaguzi ya Deloitte kwa Barua yao kwa Gavana wa Benki Kuu ya tarehe 6 September 2006 na kwa Wakurugenzi wote wa BOT ya tarehe 10 October, 2006 walipomjulisha Gavana, pamoja na wajumbe wote wa Bodi, kati yao akiwemo Katibu Mkuu wa Hazina Bwana Gray Mgonja, kuwa kuna utata kuhusu Kampuni ya Kagoda, ambayo japo ilisajiliwa 29 September,2005 tarehe 10 September 2005 ilikuwa tayari na Mkataba wa kiasi cha fedha za Japan (Japan Yen) JPY 956,110.986 na Kampuni ya Nishizawa Ltd na Mkataba mwingine wa Dola za Marekani 9,057,463.90 wa Tarehe 12 September, 2005 na Kampuni ya Textima Ltd na mikataba hii yote inatamka kuwa “Kampuni hii imesajiliwa Tanzania kwa mujibu wa Sheria” jambo ambalo dhahiri ni udanganyifu na ni uvunjifu wa Sheria.

    6. Isitoshe Mheshimiwa Spika,
      Kampuni ya Deloitte ilionyesha katika Barua walizomwandikia Gavana na Wajumbe wa Bodi dosari zifuatazo kuwa Mikataba (Deeds of Assignments) yana maneno na mfumo unaofanana jambo linaloashiria kuna kugushi, kwani makampuni kwa kawaida yanapenda kuwa na vipengele visivyofanana. Kati ya hati zote hizo hakuna hata moja iliyowekwa kwenye “Letter Head” ya Kampuni zao, mikataba yote imesainiwa ukurasa wa mwisho tu tofauti na kawaida ya kusaini mikataba, Makampuni 12 yana muhuri (seal) unaofanana na ule wa Kampuni ya Kagoda, Mikataba ya Makampuni ya Fiat Veicoli Industriali ya Italia, Valmet (USA) Adriano Gardella S.P.A (Italy) yote haikuwa na mihuri japo Mkataba unaonyesha kuwa muhuri umewekwa, Kampuni ya Valmet yenye Mkataba wa Dolla za Marekani 2,398,439.96 umewekewa saini na mtu anayeitwa Patrick Kevin, Mhasibu (accountant) jambo ambalo si kawaida kwa mkataba wa kiwango kikubwa kiasi hicho. Mambo haya yote yalipaswa kutoa ishara kwa Benki Kuu kuwa mikataba yote imegushiwa lakini wala siyo Benki Kuu wala Wakurugenzi waliostuka na kuchukua hatua pamoja na barua hiyo ya Deloitte.

    7. Mheshimiwa Spika,
      fedha hizi zililipwa kupitia Benki zetu wenyewe yaani Benki ya Kitanzania ambayo ni CRDB Benki. Hii ni Benki ambayo ilipaswa kuonyesha uzalendo kwani pamoja na ukweli kuwa mabenki ya kigeni kama vile Kenya Commercial Bank na Barclays Bank walikataa kulipa fedha hizo baada ya kuona kuwa zina harufu ya kifisadi na hata ikafikia mahali wakafunga Account za mteja mmojawapo baada ya kutilia shaka malipo hayo na kuwaandikia BOT pamoja na kuwarudishia hundi zao ,ila Benki yetu wenyewe ya CRDB haionekani ikichukua hatua zozote zile hata pale ambapo malipo hayo yalipofanyika kwa mkupuo kwa siku moja kwenye matawi tofauti ya Benki hiyo Jijini Dar es salaam kama vile matawi ya Kijitonyama, Azikiwe,Vijana , Lumumba, na Holland.

    8. Badala ya Gavana au Wakurugenzi ambao walijulishwa rasmi kuchukua hatua yeyote ya kisheria, badala yake Gavana wa Benki Kuu alimjulisha bwana Samuel Sithole Mkurugenzi wa Kampuni ya Deloitte ambaye alisafiri toka Afrika Kusini kuokoa hali hiyo, kuwa Waziri wa Fedha (wa wakati huo) anafahamu malipo (Transactions) hayo na angeliweza kuwapatia wakaguzi nyaraka zote husika kuthibitisha uhalali wa malipo hayo. Wakaguzi walikutana na Waziri wa Fedha wa wakati huo wiki ya 11 September 2006 na kuelezwa kuwa Malipo hayo yanahusu “ masuala ya Usalama wa Taifa” (State Secrets) na kwamba wakaguzi hawatapewa nyaraka zozote kuthibitisha uhalali wa Malipo hayo. Tarehe 14 September, 2006 Wakaguzi wa Deloitte walipewa ‘Draft Confirmation Letters” lakini bila Nyaraka zozote (supporting documents). Ndipo wakaguzi walipomweleza Governor tarehe 14 kuwa kutokana na hali hiyo wanatoa kwa BOT “Hati ya Mashaka (qualified Opinion) ya Ukaguzi. Sababu ya msingi ni kuwa wakaguzi waliamini kuwa nyaraka zilizotumika katika malipo hayo ‘ni za kugushi’ na kuwa kulikuwepo na uwezekano mkubwa wa Ufisadi mkubwa katika Malipo hayo. Badala ya kuchukua hatua, kwa mshangao mkubwa tarehe 21 September 2006 Wakaguzi wa Deloitte walifukuzwa kazi kwa kusema ukweli kwa Barua kutoka BOT. Mhe. Spika hii ni hali ya kutisha. Ni dhahiri kabisa kuwa Uongozi wa Benki Kuu, Wakurugenzi wa Benki Kuu akiwemo Gray Mgonja Katibu Mkuu wa Wizara ya fedha, na Waziri wa Fedha wote walihusika au kuficha au kwa uzembe katika njama za kuficha au kutaka kuficha ukweli huu uliowekwa bayana na Wakaguzi wa Kampuni ya Kimataifa ya Deloitte ambayo kwa hakika walionekana wazi kufanya kazi nzuri sana. Isitoshe kitendo hicho cha kufuta mkataba wa wakaguzi wakati kazi ya ukaguzi imekamilika na wakaguzi wameonyesha dosari kubwa katika mahesabu (irregularity) ni kukiukwa kwa taratibu za Kimataifa za ukaguzi (Taz. Barua ya Deloitte ya 10 October, 2006 iliyopelekwa kwa Mhe. Zakia Meghji).

    9. Utekelezaji wa maazimio ya Bunge kuhusu Kampuni ya Richmond iliyoingiza nchini majenereta kwa ajili ya Umeme wa dharura haujatolewa Taarifa. Kimsingi Kambi ya Upinzani inashangazwa na hali ilivyo, kwani tulitegemea Serikali itatoa Taarifa ya utekelezaji wa Maazimio ya Bunge na si majibu ya kisiasa. Maazimio kuhusu watu waliotakiwa kuchukuliwa hatua za kinidhamu hayajatekelezwa. Watu hao bado wako kazini kama desturi; mikataba iliyotakiwa kusitishwa haikusitishwa miezi kadhaa tangu maazimio hayo kupita. Kambi ya Upinzani, inashangazwa na hali hii, na haitegemei kuwa maazimio ya Bunge, ambayo ndio msimamizi wa shughuli za Serikali hayatekelezwi bali yanatafutiwa “maelezo”. Hii ni hali ya hatari katika mustakabali wa uendeshaji wa nchi.

    10. Pamoja na Taarifa ya Ufisadi ndani ya BOT pia hakuna hatua yeyote iliyochukuliwa kuhusu maeneo mengine tuliyoyaibua mathalan Ufisadi kupitia Kampuni ya Meremeta na Tangold. Waziri wa Fedha ambaye ndiye mwenye dhamana na makampuni hayo katika majibu yake siku ya ijumaa amerusha maswala hayo kwa Mawaziri wa Kisekta. Inawezekana Serikali inasubiri Bunge liunde tena Kamati Teule nyingine kwa lengo la kupitia makampuni haya ambayo umiliki wake umegubikwa na utata mkubwa kutokana na Meremeta kuandikishwa Uingereza ikiwa na Hati ya Usajili na 3424504 ya Tarehe 19 August,1997 na kupata Hati ya Kutimiza Masharti (Certificate of Compliance) nchini Tanzania kama Tawi la Kampuni ya Kigeni yenye na 32755 ya tarehe 3 Oktoba, 1997. Kinachoshangaza katika Kampuni hii ni kuwa wenye hisa wake tofauti na Bunge lilivyoelezwa mara nyingi, ni Triennex (PTY) Ltd ya Afrika Kusini yenye hisa asilimia 50%, Msajili wa Hazina mwenye hisa asilimia 50% kwa niaba ya Serikali ya Tanzania na Kampuni mbili za London Law Services Ltd wa Temple Avenue, wenye hisa 1% na London Law Secretarial Services Ltd ambao anuani yao ni sawa na hao wenzao, nao pia wana hisa 1%. Hii Meremeta hasa ni ya nani, na hawa London Law Services na London Secretarial Services ni akina nani hasa. Kampuni ya Meremeta ina hisa asilimia ngapi? Haya ni mambo yanatufanya tuwe na mashaka makubwa sana. Hivi Serikali inaogopa nini kuweka mambo haya wazi hadharani, angalau kwa Kamati husika ya Bunge basi ili kama kuna sababu ya msingi wawakilishi wa Wananchi waweze kufahamu.

    11. Vivyo hivyo kwa Kampuni ya Tangold ambayo ilisajiliwa katika kisiwa cha Mauritius tarehe 05 April,2005 Ikiwa na Hati ya Usajili na 553334 na kupata Global Business Licence (C2/GBL) tarehe 08 April, 2005. na kupata Hati ya Kutimiza Masharti hapa nchini tarehe 20 February 2006. Hata hivyo Mhe. Spika, Taarifa zilizoko ni kuwa Tangold imekuwa na akaunti NBC Corporate Branch, no. 0lll03024840 iliyofunguliwa Tarehe 1 January, 2003, yaani miaka miwili kabla Kampuni hiyo haiijasajiliwa Mauritius na takriban miaka 4 tangu imepata Hati ya ‘Kutimiza Masharti’ Tanzania. Ni kwa vipi, kampuni hii kufanya kazi wakati Bunge lilijulishwa na Mhe. Waziri Karamagi kuwa ndiyo iliyorithi Meremeta baada ya Meremeta kufilisika? Mhe. Spika haya maswali yanahitaji kujibiwa kinagaubaga ili kuwarudishia Watanzania imani kuhusu kinachojiri na usalama wa Rasilimali na fedha zao. Waziri Mkuu ndiye mtu stahiki wa kurudisha imani hii kama Kiongozi wa Shughuli za Serikali Bungeni, baada ya Waziri wa Fedha kushindwa kutoa majibu ya kuridhisha jana. Isitoshe, Makampuni haya tangu yaliposajiliwa nchi za nje na hata hapa Tanzania japo yamekuwa na akaunti katika Benki za nje na za Ndani Hesabu zao hazijakaguliwa na chombo chochote hadi leo (hatujui kama itakuwa imekaguliwa na CAG katika Taarifa ya BOT ya 2007/2008 ambayo haijawasilishwa Bungeni bado). Wahusika wa Tangold ni Bodi ya Wakurugenzi ambayo ni viongozi au waliokuwa viongozi waandamizi katika Serikali. Wakurugenzi hao ni pamoja na hayati Daudi Balali aliyekuwa Governor wa Benki Kuu (BOT), Andrew Chenge aliyekuwa Waziri wa Miundombinu, Gray Mgonja, Katibu Mkuu-Wizara ya Fedha, Patrick Rutabanzibwa- Katibu Mkuu-Maji na Vincent Mrisho-Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu.

    Mheshimiwa Spika,
    Ni muhimu sana kupata majibu ya maswali haya kwa mustakabali wa nchi yetu. Kupitisha bajet ni kitu kimoja na kuziba mianya ya ubadhirifu ni kitu kingine. Mheshimiwa Spika, kutokana na hayo yote yanayohusu Ufisadi ndani ya BOT, Kambi ya Upinzani, inastushwa kuwa wajumbe wa Bodi ya BOT waliokuwepo wakati wote wa sakata hilo bado wamebaki katika Bodi mpya akiwemo Katibu Mkuu wa Hazina Gray Mgonja. Hivyo basi:-

    1. Kambi ya Upinzani inamtaka Mhe. Rais, amwondoe haraka iwezekanavyo Gray Mgonja katika nafasi yake ya Ukatibu Mkuu wa Hazina. Gray Mgonja amekuwa mjumbe kwa kofia yake ya Katibu Mkuu wa Hazina. Vivyo hivyo, Rais wa Zanzibar naye amwondoe ndugu K.M.Omar, Katibu Mkuu wa Hazina (Z) ambaye naye anaingia kwa kofia yake. Hatua hii itaruhusu utekelezaji wa mapendekezo ya Wakaguzi (kif.4.3) kuwa Wakurugenzi wote wa BOT waliokuwepo kati ya September 2005 na Oktoba 2006 waondolewe wote na wengine wapya kuteuliwa. Ni kwa njia hii tu Serikali itarudisha imani ya Watanzania kwa chombo hicho kikubwa katika nchi kusimamia hazina, mali na rasilimali zao.

    2. Serikali iliambie Bunge hili, ni lini uchunguzi wa kina utafanyika kuhusu ubadhirifu katika maeneo mengine yanayohusu Meremeta, Tangold, Mwananchi Gold Co. ltd na Deep Green Finance Company Ltd. Kambi ya Upinzani haikuona uchunguzi wowote katika Taarifa ya Uchunguzi wa EPA kuhusu makampuni haya, na Kamati ya Bomani nayo kwa Taarifa tuliyonayo imependekeza uchunguzi wa haraka ufanyike kunusuru rasilimali za Taifa. Kambi ya Upinzani inahitaji maelezo ya kina siyo tu jinsi fedha zilivyokuwa zinahamishwa, bali pia nani wamiliki wa makampuni hayo binafsi yaliyolipwa fedha za walipa kodi wa Tanzania, kwanini Kampuni kama ya Deep Green Finance ilikuwa inafanya kazi wakati haikuandikishwa hata BOT kama financial institution kama utaratibu unavyotaka, kwanini Tangold imefanya kazi nchini miaka 4 kabla haijasajiliwa na kwanini Msajili wa Hazina ambaye ndiye mmiliki wa mali za Taifa kwa niaba ya Serikali hajaorodheshwa mahali popote katika Hati ya Usajili ya Tangold?

    3. Serikali iwasilishe mara moja mswada wa Sheria Bungeni kuondoa utata unaosababishwa na mgongano wa nafasi za Mwenyekiti wa Bodi na Governor wa Benki Kuu, nafasi ambazo kwa sasa zote zimeshikiliwa na mtu mmoja, kuweka kisheria nafasi ya Independent Audit Committee ambapo kwa sasa kamati hii inatoka ndani ya Bodi yenyewe na kupitia upya sheria nzima kama ilivyopendekezwa na wakaguzi (Kif.4.4).

    4. Kambi ya Upinzani inaitaka Serikali, bila kuchelewa kuwachukulia hatua za kinidhamu na za kisheria maofisa wote waliotajwa katika Taarifa ya Ukaguzi ya Ernst and Young, mathalan, Mkurugenzi wa Fedha wa BOT, Katibu wa Benki Kuu (SB), Mkurugenzi wa Sera za Uchumi (DEP), Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Madeni (DDDD), Kaimu Mkurugenzi wa Ukaguzi wa Ndani (IA), Mkurugenzi wa Ukaguzi wa Shughuli za Benki (Director of Bank Supervision). Kama hatua zimekwisha kuchukuliwa basi Waziri Mkuu alijulishe Bunge hili na Taifa kwa ujumla juu ya hatua zilizochokuliwa ili Bunge liweze kutimiza wajibu wake wa kuisimamia Serikali.

    5. Kama wakaguzi walivyopendekeza Kifungu cha 4.1 Serikali ilieleze Bunge lako Tukufu ni kwanini Serikali hadi sasa imeshindwa kutekeleza pendekezo la kufungua Upelelezi rasmi wa kijinai (formal criminal investigation) na badala yake kumekuwa na utata wa kinachoendelea kwani kumetolewa taarifa zinazogongana mara kwa mara na Kamati ya Mwanyika, Waziri wa Fedha na wakati mwingine hata na Wasemaji wa CCM. Taarifa hizo zimedai kurudisha au kukusanya mapato zaidi. Watanzania wamechanganyikiwa na kinachoendelea. Wanataka kujua mapendekezo ya Wakaguzi yanatekelezwa vipi, hatua gani imefikiwa, fedha ngapi zimerejeshwa, akaunti ngapi za wahusika zimefungwa (freeze) na wahusika wangapi wamekwisha kufikishwa mahakamani kati ya makampuni 13 yanayohusika na tuhuma za ufisadi wa zaidi ya shs 90,359,078,804.13. Kama kuna fedha zimerejeshwa ni kiasi gani kimerejeshwa, na nani, na zimewekwa wapi. Haya ni maswali muhimu, ni vema Serikali ikayajibu, na kama kwa sababu yoyote itakuwa si vema kuyajibu ndani ya Ukumbi wa Bunge zima, basi majibu yatolewe kwa Kamati ya Bunge ya Kudumu inayohusika na maswala hayo. Bunge kama msimamizi kwa niaba ya Wananchi itafanya makosa kuachia majukumu yake ya “kusimamia” kwa Serikali ambayo katika hatua ya awali ndiyo imetufikisha hapa.

    6. Mheshimiwa Spika,
      Serikali inafanya utani katika kutotoa Tamko kuhusu kifo cha Dr.Ballali aliyekuwa Governor wa Benki Kuu. Watanzania tunashindwa kuielewa Serikali kwa kukaa kimya. Ballali siyo mtu wa kawaida tu, bali alikuwa msimamizi wa Taasisi kubwa na Nyeti sana katika nchi yetu. Balali anahusishwa na Tuhuma zote zinazohusiana na Ufisadi Mkubwa ndani ya BOT. Ballali ndiye mtu pekee aliyekuwa na ufahamu wa kina kuhusu kilichojiri katika hayo yote yanayotuhumiwa. Serikali haikumhoji japo ilifahamu Ballali alikuwa mgonjwa jambo linalohitaji maelezo ya kina. Serikali ilikuwa na hofu gani kumhoji Ballali? Serikali ilitengua uteuzi wa Ballali bila hata kumpa haki yake ya kusikilizwa, jambo linalotia utata mkubwa sana, hasa baada ya Ballali kutoa Barua yake ya kujiuzulu mwezi December, 2007. Hatimaye kitendo cha Ballali Mtanzania kuweka wosia wa kuzikwa Marekani nayo imeacha utata na maswali mengi sana vichwani mwa Watanzania.

      Mheshimiwa Spika,
      huu ni wakati mwafaka Serikali isiachie majungu na umbea kutembea kwa usalama na uhai wa Taifa letu. Itoe mara moja Taarifa ya kina kuhusu kifo cha Ballali, ikiwa ni pamoja na alivyohusika na Tuhuma hizi zote. Isitoshe Kambi ya Upinzani inataka uanzishwe mara moja mchakato wa Uchunguzi ili Taifa liweze kufahamu kinagaubaga ni nini nafasi hasa ya Ballali katika Tuhuma zote zilizomkabili, ikiwemo ya EPA. Tunajua Ballali amefariki, Mwenyezi Mungu aiweke Roho yake mahali pema peponi, lakini kwa vile kuna Taarifa kuwa Ballali ameacha wosia kuhusu nafasi yake katika Tuhuma hizi ukweli hautapatikana isipokuwa kwa Tume/Kamati maalum ya Uchunguzi.Kambi ya Upinzani haiamini kuwa Serikali kwa kila kitu itatufikisha mahali pa kuunda Select Committee ya Bunge. Tamko la Waziri Mkuu, kuwa Serikali isipotenda vizuri na kwa Uwazi Bunge litaunda Kamati Teule nyingi. Tunamtaka sasa Waziri Mkuu kusimamia kauli yake hiyo aliyotoa ndani ya Bunge lako Tukufu. Iundwe Kamati huru ya Serikali na Taarifa yake iwasilishwe Bungeni.

 

  inaendelea...

 

lf.curl lf.curl2 rt.curl2 rt.curl