Mheshimiwa Spika,
Naomba kutoa hoja kwamba Bunge lako Tukufu liunde Kamati Teule kwa madhumuni ya kuzifanyia uchunguzi tuhuma za ubadhirifu, ufisadi na uvunjaji wa sheria za nchi zinazoihusu Benki Kuu ya Tanzania (BOT) ambacho ndicho chombo kikuu cha usimamizi wa fedha nchini pamoja na watendaji wake wakuu.
Mheshimiwa Spika,
Mnamo tarehe 25 Juni, 2007 wakati wa kujadili hoja ya Mheshimiwa Waziri Mkuu nilitoa taarifa ya mdomo ya kutaka iundwe Kamati Teule ya Bunge ili ichunguze tuhuma mbali mbali zinazoihusu Benki Kuu ya Tanzania.
Napenda kukushukuru Mheshimiwa Spika kwa kuikubali hoja hii na kuipangia ratiba katika Mpangilio wa Shughuli za Bunge lako Tukufu.
Mheshimiwa Spika,
Natoa maelezo yangu kwa kuzingatia mamlaka ya kikatiba ya Bunge lako Tukufu ya kusimamia Serikali kama yalivyoainishwa na Ibara ya 63(2)(3)(e) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, 1977.
Mheshimiwa Spika,
Wakati nikichangia hoja ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, nilielezea taarifa ya kuwepo ubadhirifu mkubwa wa fedha za umma ndani ya Benki Kuu kama zilivyotolewa katika waraka uliosambazwa kwenye ‘Mtandao’ na kunakiliwa kwa watu mbalimbali wakiwemo wafadhili na wahisani wetu mbalimbali. Leo, baada ya utafiti wa kina, sihitaji kutumia tena taarifa hiyo iliyopatikana kwa njia ya ‘Mtandao’-Internet kwani taarifa nilizonazo zinajitosheleza kabisa kujenga hoja nzito ya kuliomba Bunge lako Tukufu likubali kuunda Kamati Teule ya Bunge. Taarifa hizi ni pamoja na Taarifa za uhakika kutoka vianzio rasmi kama vile BRELA, Federal Trust (MAURITIUS) Ltd ambayo ni Msajili wa Makampuni ya Offshore, ‘Registrar of Companies –Companies House, London’, Taarifa za uhakika kutoka ndani ya BOT, zikiwemo taarifa za Ukaguzi za Delloite and Touche, CAG pamoja na nyaraka nyingine mbalimbali ambazo zote zitakabidhiwa ofisini kwako kwa wakati mwafaka ili kuiwezesha Kamati Teule, iwapo itakubaliwa na Bunge lako Tukufu liweze kufanya kazi zake kikamilifu. Mhe.Spika, kwa mujibu wa nyaraka zilizoko maeneo muhimu na ambayo Watanzania wengi tunataka kupata maelezo ya kina kupitia Bunge lako Tukufu, na hivyo kunifanya mimi kuliomba Bunge lako Tukufu kuunda Kamati Teule ni haya yafuatayo:-
- Taarifa zilizoko kwenye Magazeti, na hasa Gazeti la Serikali ‘Daily News’ Issue no. 0856-3812 na 9315 la 22 June, 2007, Taarifa ambayo haijakanushwa na Serikali wala na BOT kuhusu Fedha kiasi cha Shillingi Bilioni 30.8 zilizolipwa kwa Kampuni ya Kagoda Agricultural Ltd. Kwa mujibu wa Taarifa hiyo, mikataba 9 ilisainiwa tarehe 18 na 19 Octoba, 2005 na Makampuni 12 ya Nje chini ya mkataba na kampuni ya Kagoda Agricultural Ltd. Hii ni majuma machache tu tangu Kampuni hiyo iliposajiliwa tarehe 29 Septemba, 2005 na ndani ya majuma yasiyozidi manane Kampuni hiyo imekwisha kujipatia zaidi ya Shillingi Bilioni 30. Isitoshe, Taarifa hiyo inaonyesha majina ya wakopaji hayajulikani hata yalipotafutwa katika Kampuni mama zilizoko Ujerumani, Italia, Uingereza, Japan, Yugoslavia, Ufaransa, na Marekani. Vivyo hivyo, Taarifa hizo zimebebwa pia na Gazeti la ‘Kulikoni’ toleo na 67 la Jumatatu, 21-1 Julai, 2007, Ukurasa 1. Mheshimiwa Spika, hadi leo ninapowasilisha hoja hii, ‘Taarifa’ zote hizo hazijakanushwa na wahusika wala na Serikali. Mhe. Spika, hizi ni taarifa nzito zinazohitaji maelezo ya kina kutoka kwa Serikali na Benki Kuu ili kuondoa mashaka yeyote yanayotokana na tuhuma hizo za ubadhirifu. Serikali pia kupitia Waraka wake kwa IMF ulioandikwa na Mhe. Zakia Meghji, Waziri wa Fedha, 27, June, 2007 imekubali kuwepo kwa tatizo katika eneo hilo na kuiarifu IMF na hata Bunge lako Tukufu kuwa ukaguzi maalum utafanyika. Nitalieleza suala hili baadaye kidogo.
- Maelezo ya Serikali kuwa imeanzisha mchakato wa kumteua Mkaguzi Maalum (Hansard, tarehe 28 June, 2007) kwa kukubaliana na Shirika la Mfuko wa Fedha wa Dunia (IMF) ili kushirikiana na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ni maelezo yasiyoridhisha kwa vile jukumu la Usimamizi wa Mali na Rasilimali ya Tanzania ipo mikononi mwa chombo cha Wananchi ambacho ni Bunge, na jukumu hili kamwe haliwezi kuachiwa chombo cha nje ya nchi kama IMF, World Bank au chombo kingine chochote cha Nje. Aidha, Chombo cha Serikali ndicho kinachotuhumiwa, na kwa mantiki ya kawaida, Serikali haiwezi kujisimamia, na wala kujichunguza, jambo ambalo ni kinyume kabisa na dhana ya ‘utawala Bora’ na Uwazi yaani ‘Transparency’. Jukumu la kuisimamia Serikali ni la Kikatiba na Bunge hili kamwe haliwezi kujivua jukumu hili na wala Serikali haiwezi kuweka vikwazo kwa Bunge kutimiza wajibu wake wa Kikatiba. Iwapo Serikali inapenda kuendelea na njia yake ya ‘Uchunguzi’ inaweza kuendelea, na Bunge nalo likaendelea na jukumu lake lililokabidhiwa na Wananchi kwa mujibu wa Katiba ya Nchi yetu. Bunge (Mbunge) linapohoji jambo linafanya hivyo kwa niaba ya wananchi, ambao ndio wamewachagua wawe wawakilishi na wasimamizi wa mali yao kwa niaba yao.