lf.bevel
MWANZO CHAMA SERA KATIBA TUUNGE MKONO UCHAGUZI TUWASILIANE

28 Januari 2005

Hotuba ya John J. Mnyika, Mkurugenzi wa Vijana wa CHADEMA,
Mwenyekiti wa TYVA Taifa wa zamani

Ufunguzi wa Mkutano mkuu wa Tanzania Youth Vision Association (TYVA)

Kaka Daniel Benard, Katibu wa TYVA Taifa,
Viongozi na wajumbe wa kamati ya utendaji ya TYVA Taifa,
Viongozi na wawakilishi wa matawi ya TYVA kutoka mikoa mbalimbali,
Wawakilishi wa asasi washirika wa TYVA,
Wapendwa wanachama wenzangu,
Wageni waalikwa,
Makaka na madada,mabibi na mabwana,

Hakuna zawadi ndogo tena mara nyingi zawadi ndogo zaweza kuwa almasi na kuzidi maghala ya zawadi. Zawadi zisizouzwa mathalani upendo huleta faraja kuliko fedha. Nafasi ambayo uongozi wa TYVA umenipa na nyinyi wenzangu mkaridhia kunisikiliza ingawa tayari nimeshajiuzulu uenyekiti wa Taifa wa TYVA ni kigezo tosha cha upendo wenu, ni ishara ya kwamba mnanithamini-zawadi hii yazidi almasi.

Kujiuzulu uenyekiti wa Taifa TYVA

Pengine nianze na viporo ili tuanzapo masuala ya mkutano wetu wa leo tusinukiwe-amam harufu mbaya au nzuri na yaliyopita. Tugange yajayo! Baadhi waliniuliza maswali mengi kuhusu kujiuzulu kwangu baada ya vyombo vya habari kuweka mambo hadharani. Kwa kuwa huu ni Mkutano mkuu, nahisi nitumie fursa hii kufafanua kwa wanachama wenzagu kuhusu kujiuzulu kwangu.

Inafahamika kwamba TYVA imekuwa ikiwahamasisha vijana kushiriki katika mambo ya kijamii, kiuchumi, kisiasa na kimichezo. TYVA inaamini kwamba kila kizazi lazima nje ya uvunguvungu kiutambue utume wake ama kiutimize au kiusaliti. Hivyo kizazi kilichozaliwa baada ya uhuru wengi wao wakiwa ni vijana kinawajibu wa kuwa mstari wa mbele katika kutambua mustakabali nchi.

Kupitia programu na shughuli zake mbalimbali TYVA imegundua kwamba kuna ushiriki finyu wa vijana hususani katika siasa ambazo zimetawaliwa na wazee, vijana wanatumika zaidi katika siasa kama wahamasishaji tu! Niliamini na naamini umefika wakati wa kuonyesha na kusimamia kwa vitendo yale ambayo TYVA imekuwa ikiyahamasisha na kuyasimamia.

Hivyo nilitangaza kujiuzulu rasmi kuwa Mwenyekiti wa Taifa wa TYVA na kujiunga na siasa lengo langu kuu likiwa kuwa mstari wa mbele kujenga mifumo katika vyama na kuhamasisha ushiriki wa maana wa vijana katika siasa. Naamini hatua hii itachochea ushiriki wa kizazi kipya katika katika kuboresha mustakabali wa nchi yetu na kutetea maslahi ya vijana. Uamuzi huu niliufanya baada ya kutafakari pamoja na viongozi wenzangu na kwa pamoja tukaona - TYVA itabaki makini na imara.

Nimejiunga na CHADEMA na kuteuliwa kuwa Mkurugenzi wa Vijana Taifa na natarajia kugombea ubunge kupitia chama hiki cha kizazi kipya! Uamuzi wangu wa kujiuzulu ni sehemu ya kulinda maslahi ya TYVA. Si busara asasi yetu hii ikaoanishwa na chama chochote cha siasa. Lakini kama ilivyoada-muenda kwao si mtumwa-naahidi kuendelea kutoa roho, akili na mwili kwa TYVA kutimiza utume misheni yake-tuko pamoja katika harakati.

Mafanikio yetu 2004

Mwaka huu tumeutumia kuanza kutekeleza rasmi mkakati wetu wa miaka mitano. Sipendi kuwa mmbea na kusema pembeni masuala ambayo katibu mkuu atayawasilisha katika ripoti ya mwaka. Lakini niseme kwamba nafarijika tulipo na naamini tutakwenda mbali zaidi. TYVA sasa tunaheshimika kwa umma, serekali na asasi mbalimbali. Nachukua fursa hii kuwashukuru UNICEF na mshirika wetu wa muda mrefu-FNF kwa ushirikiano wao wa hali na mali tumefika tulipo na tutakwenda tunapotaka kwenda! Mradi wa kukusanya maoni ya vijana kuhusu MKUKUTA umetufanya tutoe mchango wa pekee kulinda maslahi ya vijana na kuchangia mustakabali wa Taifa. Programu ya kuwajengea uwezo wagombea vijana umetupa mwanya wa kuonyesha kwa vitendo vijana ni Taifa la leo-kama wao wanaweza wana nini hata sisi tushindwe tuna nini? Tumepanuka na kutanuka-uwepo wa matawi ni uthibitisho tosha. Lakini tafiti ama kwa lugha sahihi zaidi tathmini tulizozifanya kupitia programu hizi zinaonyesha safari bado ni ndefu!

Changomoto zilizotukabili

Ni nyingi! Si sababu ya kukata tama-ni sababu ya kujipanga vizuri zaidi. Mosi, Tumeendelea kuendesha TYVA kwa kujitolea zaidi na hivyo kukosa nguvu kazi ya aina zote wakati wote. Pili, tumekuwa peke yetu-asasi nyingine za vijana zipo kimya au zimezama katika uzalishaji mali, uelimishaji rika ama zimetosa katika kuburudisha. TYVA imekuwa sauti ya pekee jangwani-Tunaonekana vimbelembele. Pia, Baadhi ya shughuli zetu hazikuweza kufanyika kutokana na kutopata raslimali. Tunapaswa kuzichangamoto changamoto hizi kabla hazijatuchangamoto.

Ripoti kuhusu ushiriki wa vijana mwaka 2004

Tena si safari ya tambarare, kuna vilima, mabonde, kona kona na vikwazo mbalimbali. Hayo yatawekwa bayana na ripoti kuhusu ushiriki wa vijana katika mwaka 2004 ambayo ni sehemu ya ajenda zetu za leo. Lakini kwa ujumla vijana wanazidi kulala hoi-ama kwa kazi nzito ujira mdogo, wengine kwa kusumbuliwa kwenye sehemu zao za biashara zianazoitwa biashara zisizo rasmi na wengi wao kwa kusumbuka kutafuta kazi bila mafanikio.

Ni imani yangu mtajadili mambo haya baada ya ripoti hiyo kuwasilishwa. TYVA tusimame kidete kueleza serekali yetu, jamii na wadau mbalimbali wa maendeleo kwamba kama kuna tishio la amani Tanzania basi ni tatizo la ukosefu wa ajira! Kama tutaendelea kuwa na tabaka la wenye navyo-sio wenye nacho, na tabaka la wasio nacho-hawana hata ajira ambao wengi wao ni vijana waliopigika tutaendelea kukalia bomu la wakati.

Yapo mengi yamesemwa katika ripoti hii kuhusu ushiriki wa vijana kwenye maeneo mbalimbali lakini kama nilivyosema awali-sitaki kusutwa!

Michezo na muziki wa kizazi kipya

Nasikitika kwamba bado tumeendelea kushuhudia jasho la vijana wenzetu na vipaji vyao vikipotea katika sekta ya michezo. Faraja yetu imekuja hivi karibuni baada ya vijana wenzetu wa Serengeti boys kufanya yasiyotarajiwa. Nachukua fursa hii kuwapongeza vijana wenzetu. Mmelidhihirishia Taifa kwamba hata vijana tukibanwa vipi bado tunaweza kuhamasika-tukihamasishwa, tukabanana kiaina na kuleta kicheko. Bado narajea ahadi tuliyotoa na maandalizi bado yanaendelea lazima tuwakusanye vijana kwa ajili ya kuwachangia na kuwapongeza vijana wenzetu wa Serengeti boys-ndo ndo ndo si chururu!

Kwa upande mwingine, tulitumia mwaka huu kuhamasisha vijana wenzetu kujitokeza kuongoza sekta ya michezo hususani soka. Tulipata kigugumizi baada ya vijana kuchelea kujitokeza kugombea. Hata hivyo mabadiliko yaliyotokea TFF yametupa faraja kwamba shirikisho jipya, limepata viongozi wapya, tunategemea mambo mapya kwa manufaa ya kizazi kipya. Tenga na timu yako-Tuko pamoja!. Naamini TYVA itatumia mwaka huu kuhamasisha mabadiliko kama haya katika vyama vya riadha, mpira wa pete na maeneo mengine, ni wajibu wetu.

Maendeleo katika muziki wa kizazi kipya yanatupa matumaini, nawapongeza kwa kuleta mageuzi katika lugha,muziki wa hapa nyumbani. Muziki wa kizazi kipya waweza kuwa ukombozi wa tabaka la walalahoi hususani vijana. Sauti za vijana zimeburudisha, kukosoa na kuelimisha. Tupige hatua kuungana na vijana wenzetu kujilinda dhidi ya unyonyaji. TYVA itetee muziki wa kizazi kipya kwa ajira.

Uchaguzi TYVA

Leo tutachagua viongozi wa Taifa wa TYVA. Hatma ya asasi hii itakuwa kwenye roho na akili zenu wanachama. Kuna mambo kadhaa myatafakari. Kwanza uongozi uliopo umekaa muda mfupi lakini tayari imeonyesha muelekeo mzuri-Hivyo nashauri mbakishe sehemu kubwa ya uongozi huu ili tuwe na muendelezo. Pili, tunahitaji vijana wapya katika uongozi ili tuweze kuwa na timu itakayolisukuma gurudumu hili wakongwe wengine watakapong'atuka-hivyo nategemea wanachama wapya mtajitokeza kugombea. Tatu, mkumbuke kwamba uongozi unaomaliza muda wake uliona haja ya kuwazoesha wanachama wengi utendaji kabla ya uchaguzi-bahati nasibu si kitu kizuri katika suala nyeti kama uongozi. Hivyo wapo wanchama waliojitokeza kuonyesha vipaji vyao kwa kufanya kazi bega kwa bega na uongozi-hawa tuwatazame kwa jicho la mnastahili!Tukosoane uchaguzi usiwe dampo wala maabara.

Mambo ya msingi 2005

Mosi, ni uchaguzi mkuu-hapa ndipo mustakabali wetu wa miaka mitano na pengine zaidi ya hapo, utawekwa rehani. Vijana tusipoukomboa kwa kura zetu tutakuwa tunafanya uhaini dhidi ya umoja na uhuru wetu. TYVA isiache wajibu wake wa kutoa elimu kwa vijana kujiandikisha na kupiga kura. Isiache pia kuwahamasisha na kuwajengea uwezo vijana watakaojitokeza kugombea. Hivi tuko wapi vijana wakati bunge la watanzania 231 linakosa kijana wa chini ya miaka 27, lina vijana 17 tu wa kati ya miaka 28 na 35 wakati kati ya kila raia kumi, sita ni vijana? Hali haiko tofauti sana kwenye mabaraza ya madiwani. Huu ni udikteta wa mfumo zee!

Pili, tushikie mabango suala la kuundwa kwa Baraza huru la Vijana. Kuzungumzia suala hili, sina nia ya kunyanyasa jinsia yoyote, isiwe titi la mkwe! Sera ya vijana, ambayo pia tunapaswa kuipata ile mpya,inasema kutakuwa na baraza, Katiba ya nchi inatoa uhuru wa kukusanyika na mikataba ya haki za binadamu inasimamia haki hii.

Tatu, tunapaswa kuambiana ukweli na kukosoana. Vijana wengi wa Tanzania bado wamelelala ama wamelewa. TYVA iwawezeshe vijana kujitambua ikiwemo kujua haki zao. Vijana hususani wanachama wa TYVA tuwe makini zaidi jamii ipate kurudisha imani kwa morani wa utandawazi na mfumo wa soko. Hii itapunguza mamilioni ya shilingi yatodumbukia kwenye kuendelea kuwafanya vijana mradi kwa kigezo cha kuwa wahanga wa maambukizo,maangamizi na maambukizi.

Nne, tuguse ushiriki wa vijana katika nyanja zote. Ni kweli siasa ama niweke kwa lugha inayokubalika zaidi uongozi bora ndio msingi wa nyanja zote lakini hatima ya siku anachohitaji binadamu ni amani,maendeleo, ustawi, amani, upendo na furaha. Vyote hivi vinapatikana katika nyanja ana sekta mbalimbali. Tulenge ajira, tuhimize elimu, tushiriki michezo, tuboreshe afya na maeneo mengine. TYVA isiupe kisogo MKUKUTA, mikakati na michakato mingine!

La mwisho ingawa ni la muhimu zaidi: Tusimamie dira ya TYVA ya kuona jamii huru ya kidemokrasia yenye amani ambapo kuna ushiriki mwafaka wa vijana. Injini zisilale!

Natangaza mkutano mkuu wa TYVA umefunguliwa rasmi na nawatakia jihada, upendo, furaha na mafanikio.

 
lf.curl lf.curl2 rt.curl2 rt.curl