Hotuba ya John J. Mnyika akichukua fomu za kugombea Ubunge Jimbo la Ubungo
Wageni waalikwa, wapendwa wakazi wenzangu wa Jimbo la Ubungo,
Waheshimiwa viongozi na wanaCHADEMA wenzangu,
Marafiki zangu wanahabari,
Naomba ni wasalimu kwa heshima zote: Asalam Alyekum, Amani iwe kwenu,
CHADEMA - Vema! Tunajivunia nini - Nguvu ya Umma! People's-Power!
Ninayo furaha siku ya alhamisi hii ya upendo iliyoongezwa na ujio wenu wa kunisindikiza na kunisikiliza wakati wa zoezi hili muhimu kwa demokrasia na maendeleo ya Tanzania, jimbo la ubungo na yangu binafsi. Matabasamu yenu yananipa ishara ya taa ya kijani-Nasonga mbele!
Wengi najua mnasubiria niseme mengi hivi sasa lakini nawaombeni kwa ridhaa yenu niseme machache kwa kuwa huu si wakati wa kampeni na pia mengi nitayatoa kwenye ilani yangu kama mgombea nitakapopitishwa katika ngazi husika na mengine nitashawishi yaingizwe katika ilani za CHADEMA Taifa na wilaya ya Kinondoni. Naamini-haba na haba hujaza kibaba.
Wapendwa wakazi wenzangu wa Jimbo la Ubungo, WanaCHADEMA na wanahabari;
Uamuzi wangu wa kuwaza na kudhamiria kuwa mwakilishi wa wakazi wa Jimbo la Ubungo na watanzania umetokana na sababu mbili tatu, naombeni leo nitaje baadhi:
Mosi; Nimechoshwa kuyaishi matatizo ya wakazi wa Ubungo. Sikuhitaji utafiti wa kisayansi kuihisi hali hii. Kama mkazi wa kawaida wa Jimbo hili kuna mengi yananikera. Leo nitagusia machache:
Bado tunaendelea kupata tabu ya maji, wahanga wa tatizo hili wakiwa zaidi ni mama zetu ma dada zetu. Asilimia kubwa ya wakazi wa ubungo tunachota maji kwa foleni!
Bado tunaendelea kuona vijana wengi wakikosa nafasi za kielimu. Ni robo tu ya wahitimu wa shule ya msingi katika Jimbo la Ubungo ndio wanapata nafasi ya kwenda Sekondari. Asilimia 78 ya walimu hawana vitabu kamili vya kufundishia, nusu ya watoto hawapati nafasi ya kusoma shule ya chekechea, wanaenda shule ya msingi moja kwa moja!
Bado tunaendelea kupata tabu ya usafiri nyakati za asubuhi na usiku. Lakini wapo wakazi wa baadhi ya maeneo ambapo wanatembea umbali mrefu kila siku kwa kukosa kabisa mfumo wa usafiri. Asilimia 21 tu ya barabara ndio ziko barabara!
Bado tunaendelea kuona wakazi wengi wakiwa walalahoi na vijana wanne katika kila kumi wakiwa hawana ajira hata ya kujiajiri. Huku mitaji na mikopo hususani kwa wanawake na vijana ikiwa kiduchu na ikitolewa kinyemela.
Bado kuna hisia za vitendo vya rushwa katika upatikanaji wa huduma muhimu na dalili za ufisadi katika matumizi ya raslimali za walipa kodi. Lisemwalo lipo...!
Pili, sipendezwi na Bunge kuwa kibogoyo; Si utukutu, ni ukweli ulio wazi kwamba bunge letu limekuwa mchezo wa luninga. Hii ni tishio kwa demokrasia, maendeleo na mustakabali wa Taifa. Yapo mengi yaliyopitishwa yanatisha, yapo mengi yaliyofutikwa yamesahaulika. Lakini hii inachangiwa na kukosa wabunge makini sambamba na kuwa na bunge 'la chama kimoja'.
Tatu, kizazi kipya tumenyimwa wasaa wa kuleta maisha mapya; wengi ya waliopigania uhuru wa nchi hii walikuwa ni vijana, Tanzania ya miaka mwanzoni ya uhuru iliongozwa vijana, tena wengine vijana wabichi. Walianza kwa ari ya ujana chini ya visheni ya Azimio la Arusha. Walifanikiwa sana katika miaka ya awali lakini kadiri wakati ulipoanza kuwatupa walianza kugonga ukuta. Sipendi nichukue muda huu kukumbusha historia mnayoifahamu. Lakini ona hali inayoendelea-Uongozi katika na nyanja sekta zote umejaa tabaka la kizazi cha zamani-mfumo kongwe na ukiritimba.
Niishie hapo, sikuja hapa kunung'unika wala kuwaimbisha nyimbo za msiba.
Wapendwa wakazi wenzangu wa Jimbo la Ubungo, WanaCHADEMA na wanahabari;
Lakini hisia hizi ni za kila mtanzania na mkazi wa Ubungo! Sasa kwanini mimi nimekuwa kimbelembele leo kuchukua fomu za kuomba kuteuliwa kuwa mwakilishi? Kwa nini naamini CHADEMA inapaswa kupitisha jina langu? Nadokeza hoja kadhaa:
Mosi, nina visheni, mawazo na ubunifu ambao nataka kuchangia kama mwakilishi wa wakazi na Watanzania katika kutatua matatizo niliyoyagusia. Ahadi zangu, deni langu na mkataba wangu na wapiga kura utakuwa kwenye ilani nikipitishwa ngazi zote lakini ngoja nivujishe mawili matatu:
Nataka kuwa "mshinikizi na mweka wazi" wa serekali na wadau mbalimbali kutimiza wajibu wao wa kuhakikisha huduma zinapatikana na ustawi wa wananchi unaboreshwa. Mamlaka zinakiri kwamba zinauwezo kwa kuleta maji,hili lilidhihirika wakati wa uchaguzi wa serekali za mitaa, kuna maeneo ambayo yalipata maji baada ya kipindi kirefu cha 'ukame', maji hayo sasa yametoweka. Mamlaka zinatamba kuwa na uwezo wa kujenga barabara lakini hali ni tofauti. Naamini naweza kuwa Mbunge ambaye pia ni diwani mwenye kushinikiza utekelezaji na sio utelekezaji! Naamini wapo wakazi wanaokosa huduma kama umeme na haki zao nyingine kutokana na rushwa, urasimu na ukirimba-dawa ya uovu ni kuufichua. Nitashikia bango mambo kadhaa bungeni ikiwemo uundwaji wa Baraza la Vijana, Watanzania kunufaika na maliasili na raslimali zetu, Dira mpya ya Taifa na mambo mengine ambayo tulikuwa tukiyapigia debe kupitia mashirika yasiyo ya kiserekali.
Nataka kuwa "mtumwa, mtumishi na mwakilishi". Naamini uongozi ni kuwatumikia waongozwa, uongozi ni kutumwa. Hii ni hatua moja muhimu ya kuunganisha nguvu za wananchi katika kuleta demokrasia na maendeleo. Nitaendelea kuishi kawaida na wakazi wa kawaida na kuwa tayari kutumwa na kutumikia. Nitaanzisha kuwashirikisha wakazi na kupokea maoni yao kwa njia mbalimbali ikiwemo kuanzisha ofisi ya mbunge inayofikika, inayosikika na kufanya kazi. Pamoja na masurufu ambayo hotolewa kuendesha ofisi ambayo wengi huyatia kibindoni nitatoa asilimia kumi ya mshahara kuchangia ufanisi wa ofisi hii.
Nataka kuwa "Mwanamaendeleo"; pamoja na kuishinikiza serakali na washirika mbalimbali kutimiza wajibu, kwa nafasi yangu nami nitachangia katika kuleta maendeleo. Nitaanzisha Asasi wa Maendeleo Ubungo itakayotumia "ubunge" kuvuta raslimali za wakazi na wadau mbalimbali. Asilimia kumi ya mshahara wa mbunge itachangia mfuko huu. Vipaumbele vya mfuko huu vitakuwa mitaji na mikopo kwa wanawake na vijana; elimu hususani kwa wasio na uwezo; kuwapatia wakazi ujasiriamali ili kupanua kipato na ajira; huduma za afya ya msingi kwa mzunguko(mobile services); elimu ya uraia kwa wakazi kuchochea demokrasia, uwajibikaji na maendeleo; michezo, burudani na ukuzaji vipaji. Ni kwa kiasi gani haya yatafanyika? Nikipitishwa, ilani ya mgombea itasema.
Nataka kuwa "mwakilishi wa kizazi kipya"; naamini katika falsafa ya 'kizazi kipya, maisha mapya'. Mabadiliko ya kiuchumi, kisiasa na kijamii yanayoendelea duniani yanahitaji mabadiliko ya kiuongozi. Tukiendelea kuweka divai mpya kwenye viriba vya zamani nchi yetu itapasuka. Ningependa nipewe fursa ya kuonyesha kwa vitendo kwamba vijana tunaweza kuleta Tanzania yenye demokrasia na maendeleo. Naombeni nisichukue muda kueleza nini nadhani ni 'maisha mpya' tunayopaswa kuwa nayo. Sina nia ya kubagua, wachache wa kizazi cha 'zamani' wanapaswa kubaki wengi wafuate nyayo za Mwalimu ili tuwe na viongozi wengi zaidi wa kizazi kipya!
Pili, nina karama, uwezo, uzoefu na sifa za kuwa kiongozi, mwakilishi wa watu, kufanya harakati na kuchochea maendeleo.
Nimejitathmini na kubaini nina talanta ya uongozi ambayo nisipoitumia nitakuwa natenda dhambi. Vitabu vitakatifu vitakumbusha kwamba mengi yanatarajiwa kwa yule aliyepewa mengi. Baada ya kubaini niliweka bayana nia yangu mwanzoni mwa mwezi huu. Marafiki na watu mbalimbali hususani mama zangu na vijana wenzangu waliunga mkono tathmini yangu nakunihimiza nisonge mbele. Nimechukua fomu kama ishara ya kuomba fursa ya kusonga mbele!
Nisingependa kujipigia tarumbeta langu mwenyewe kuhusu uwezo na uzoefu wangu wa uongozi. Watu huamuliwa kwa matendo yao ya wakati uliopita lakini muhimu zaidi vile walivyo sasa! Yote niliyoyafanya kwa jamii ya Tanzania katika umri wangu huu mdogo wa miaka 24 mnayafahamu.
Naamini nina sifa za kiongozi bora ikiwemo utumishi, uadilifu, maadili, kujiamini, msimamo, visheni-nyinyi mnaweza zaidi kuwa kioo cha kunikosoa. Ila ninachofahamu ni kwamba mpaka sasa sijala rushwa wala kujichafua kwa ufisadi.
Wapendwa wakazi wenzangu wa Jimbo la Ubungo, WanaCHADEMA na wanahabari;
Naombeni nihitimishe kwa kutoa maoni na mawazo yangu kuhusu mambo kadhaa yaliyotokea ama yatakayotokea hivi karibuni.
Mosi, nachukua fursa hii kuwahamasisha wakazi wa Ubungo hususani wanawake na vijana kujotokeza kujiandikisha katika daftari la kudumu la wapiga kura kuanzia tarehe 29/3 mpaka tarehe 18/4. Kizazi kipya, maisha mapya-Tujiandikishe!
Pili, nimekerwa na kauli za viongozi waliopo madarakani kusema watatumia kila wawezalo ikiwemo 'dola' kuendelea kuwa madarakani. Huu ni uzalilishaji wa haki ya raia kuwa na viongozi wanaowataka na matusi kwa demokrasia. Rais Mkapa alirudia hoja hii na Makamba akaindeleza wiki hii kwa kuwataka maafisa watendaji wa kata (ambao ni watumishi wa serekali) kuhakikisha ushindi wa 'chama dola'. Napenda kuwakumbusha kwamba Mola akitaka dola itatoka 'hola'. Sauti ya watu ni sauti ya Mungu. "Nguvu ya Umma" itawahukumu.
Tatu, nashangazwa na uongozi wa Mkoa wa Dar es salaam kuwasahau wananchi muda wote na kukurupuka karibu na uchaguzi kuchangisha mamilioni ya shilingi. Sina nina ya kubeza michango ya kimaendeleo lakini zoezi hili lililoendeshwa kwa Jina la Mheshimiwa rais lina nia ya kuwaghilibu wananchi kipindi hiki cha uchaguzi. Lakini naamini wakazi wa Ubungo si wanyama, wakati ukifika watauliza maswali muafaka: Mbona hamkuchangisha milioni 500 kila mwaka toka uchaguzi wa 2000? Mbona hamkutujengea shule za sekondari siku zote? Mbona fedha za mikopo ya wanawake na vijana tayari ilishakuwepo kwenye mipango ya halmashauri lakini walengwa hawakupewa?
Nne, Mbunge wa sasa na viongozi wengine ambao mara baada ya uchaguzi walitoweka (wakazi wa Ubungo watakubaliana nami) wameibuka ghafla na kujinadi kama viongozi watu huku wakitumia takrima. Nachukua fursa hii kuwataka wakazi wa Ubungo na watanzania kwa ujumla kuwa macho na ulaghai wa manufaa ya siku moja!.
Katika moja ya vitabu vitakatifu tunasoma hadithi ya nabii mmoja aliyeombwa msaada na mtu mwenye ulemavu. Alimwambia sina fedha wala dhahabu ya kukupa lakini nakupa nilichonacho- "Inuka uende zako". Yule mtu aliinuka na naamini alikwenda kufanya shughuli za kujipatia kipato na kujitegemea. Nikipitishwa ngazi zote, nitawaambiwa wakazi wenzangu wa ubungo hususani wanawake na vijana kwamba sina fedha wala Takrima ya kuwapa, nawapa nilicho nacho- "Simameni, tushirikiane kuleta demokrasia na maendeleo".
Mungu awabariki kwa kunisikiliza.