lf.bevel
MWANZO CHAMA SERA KATIBA TUUNGE MKONO UCHAGUZI TUWASILIANE
banner

Hotuba ya Msemaji Mkuu Kambi ya Upinzani Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Mheshimiwa Susan A. Lyimo (Mb)

Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2008/2009

I. UTANGULIZI

  1. Mheshimiwa Spika,
    Kwa niaba ya Kambi ya Upinzani naomba nitoe maoni ya Kambi ya Upinzani kuhusu bajeti ya Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi kwa mwaka wa fedha 2008/2009 kwa mujibu wa Kanuni za Bunge Kanuni ya 99(7) toleo la Mwaka 2007.

  2. Mheshimiwa Spika,
    Itakumbukwa kuwa kwa takribani miaka miwili iliyopita nilikuwa Waziri Kivuli wa Elimu ya Juu Sayansi na Teknnolojia. Kufuatia mabadiliko ya Baraza la Mawaziri yaliyofanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania baada ya kujiuzulu kwa Waziri Mkuu, Kiongozi wa Upinzani Bungeni naye ilimbidi kupanga upya timu yake na akaniteua kuwa Waziri Kivuli wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi.

  3. Mheshimiwa Spika,
    Kwa kuwa hii ni mara yangu ya kwanza kusimama mbele ya Bunge lako tukufu kama Msemaji Mkuu wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi naomba nitoe shukrani zangu za dhati kwa Kiongozi wa Upinzani Bungeni Mhe. Hamad Rashid Mohamed (Mb) na Naibu wake Dr. Willibrod Peter Slaa (Mb) kwa kuniteua kushika nafasi hii. Vile vile napenda kuwashukuru kwa kunipatia msaidizi mahiri, Mheshimiwa Nuru Bafadhili (Mb) kama Naibu Waziri wangu. Hotuba hii imefika hapa kwa Msaada wake mkubwa sana. Nawashukuru pia Wabunge wote wa Kambi ya Upinzani walio katika Kamati ya Bunge ya Huduma za Jamii wakiwemo Mh. Mercy Mussa, Mh. Hemed Hemed, Mh. All Mzee na Mh. Dr. Taarab kwa mchango wao katika kukamilisha maoni haya ya Kambi ya Upinzani.

  4. Mheshimiwa Spika,
    Napenda kuishukuru kambi ya Upinzani, kambi makini kabisa chini ya Uongozi wa Mhe. Hamad Rashid, pamoja na Mhe. Dr. Slaa kwa uongozi wao madhubuti unoijenga kambi hii na kuifanya kuwa kambi imara na isiyotetereka, na hivyo kuweza kufanya kazi yake ya kuikosoa serikali bila woga wowote. Ninamhakikishia Mheshimiwa Kiongozi wa Upinzani Bungeni na Watanzania wote wazalendo kuwa nitafanya kazi hii, kwa kushirikiana na Naibu wangu kwa uwezo wetu wote kwa lengo la kusaidia maendeleo ya Taifa letu zuri la Tanzania.

  5. Mheshimiwa Spika,
    Pia kwa udhati kabisa napenda kutoa shukrani zangu za dhati kwa chama changu cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kwa kuendelea kunipa ushirikiano ndani na nje ya bunge, nami naendelea kuwaahidi kuitunza imani ya chama changu na kuendelea kuitangaza kwa watanzania wote. Baada ya kusema hayo, Mhe. Spika sasa naomba nitoe maoni ya kambi ya Upinzani katika Wizara ya elimu na mafunzo ya ufundi kama ifuatavyo:-
II.   ELIMU YA MSINGI
  1. Mheshimiwa Spika,
    Elimu ya msingi ni msingi kwa taifa lolote na ndiyo maana inaitwa msingi. Maendeleo yote ya elimu huanzia hapo. Na msingi wa elimu ukijengwa vizuri ngazi zote za elimu za juu zitaendelea vizuri.

  2. Mheshimiwa Spika,
    Pamoja na umuhimu huo, serikali kwa kushirikiana na nguvu za wananchi pia imefanikiwa kuongeza idadi ya shule za msingi, ambazo zimeongezeka kutoka 14,700 mwaka wa 2006 hadi 15,624 mwaka 2007. Hili ni suala la kujipongeza na kupongezana. Lakini tunashauriwa kutodanganyika na taswira ya takwimu tu. Na tujiulize je hivi kweli elimu inayotelewa inawiana na nguvu inayowekezwa na wananchi? Kwa sababu wananchi wanajitahidi kwa upande wao, waingereza wanasema “they have played their part” lakini je serikali inafanya nini? Has it played its part? Je walimu wako ? Vitendea kazi vipo? Teaching materials? Hili ni suala ambalo wizara ya elimu inatakiwa kulipatia majibu ambayo yanalandana na uzito wa jambo hili na sio vinginevyo.

  3. Mheshimiwa Spika,
    Sote tunafahamu kuwa ubora wa elimu haupimwi kwa uwingi wa shule wala idadi ya wanafunzi, la hasha! ingawaje mjadala wa kitaifa kuhusu uboreshaji wa elimu umejikita na kuelekezwa zaidi katika wingi wa vitendea kazi hii inashangaza ingawaje sote tunatambua kuwa “Quality is different from Quantity” yaani ubora ni tofauti na uwingi.

    Kambi ya upinzani inasikitika sana kuona ubora wa elimu katika shule zetu za msingi kutetereka. Tafiti nyingi zilizofanywa na taasisi tofauti zinadhihirisha hilo, lakini utafiti wa kisayansi uliofanywa na taasisi ya Hakielimu ndio haswa ulioweza kuweka bayana, ni kwa kiasi gani elimu ya msingi imeshuka ubora. Kwa mujibu wa utafiti huo, ubora wa elimu kwa shule za msingi umeshuka. Hii inatisha na kukatisha tamaa. Kwa sababu kama hatujengi msingi mzuri maana yake tunajenga taifa la wasomi wasio na uwezo kushindana katika ulimwengu huu wa utandawazi.

  4. Mheshimiwa Spika,
    Katika ngazi ya msingi suala la kifikika limefanikiwa kwa kiwango kikubwa. Tanzania imefanya vizuri sana na naona fahari kwamba mtandao wa shule za msingi unaofuata mtaala mmoja hata kama ni mzuri au mbovu kwa Maarifa ya kusoma na pia kutahiniwa darasa la IV na la VII. Umbali toka shule hadi nyumbani umepungua sana tangu 1978 na 2001, msukumo wa UPE, kwamba sasa wastani mtoto anatembea 1-4 Km. Kuondolewa kwa ada na michango mbali mbali kumeongeza sana watoto kwenda shule kwa wingi tatizo kubwa ni ukosefu wa waalimu, vifaa vya kufundishia na miundombinu ya staha. Shule nyingi ziko katika hali mbaya, shule nyingi hazina madarasa ya kutosha hivyo mlundikano wa zaidi ya watoto 100 kwa darasa ilhali linatakiwa kuwa na wanafunzi 45, watoto kukaa kwenye sakafu, mawe, magazeti na chini ya miti. Bado wanashirikiana vitabu katika uwiano wa 1:6, mwalimu mmoja akifundisha darasa zaidi ya mmoja kwa wakati.

    Huu ugawaji usio sawa wa rasilimali unapelekea matokeo mabaya katika usomaji. Hii pia itapelekea kutokuwa na usawa kati ya jamii. Ufutaji wa ada umepelekea gharama nyingine kuanzishwa kinyemela kama uchangiaji madawati na madarasa ambavyo pia inapelekea tofauti ya ubora wa elimu kwani jamii zinatofautiana sana kimapato. Hii ni lazima ibadilishwe kwani ni wazi kwamba kila mfumo wa elimu unategemea uwezo wa kifedha toka kwa jamii na familia ni wazi haitakuwa na usawa (inherently inequitable).

  5. Mheshimiwa Spika,
    kwa kuzingatia hilo, kambi ya upinzani inaitaka wizara kutoa majibu katika masuala yafuatayo:-

    1. Je nini hasa, kiini cha poromoko hili katika elimu?
    2. Je serikali inafanya nini ili kuweza kukabili tatizo hili ambalo limeikumba sekta ambayo inajenga taifa la kesho?

    A) Mtaala wa Shule ya Msingi

  6. Mheshimiwa Spika,
    Mtaala ni msingi wa elimu ya mahali popote kwani bila mtaala wanafunzi wasingekuwa na cha kusoma. Kwani mtaala ndio unaozaa masomo. Katika dunia ya sasa ya habari na mlipuko wa Maarifa, Nchi nyingi zinafikiria ni mambo gani yakamilishwe (covered) ili kutosheleza mahitaji muhimu ya wanaomaliza elimu ya msingi.

  7. Mheshimiwa Spika,
    Mtaala wa elimu ya msingi Tanzania umeparaganyika ukiwa na maeneo mengi mno (content areas). Wanafunzi wanachukua hadi masomo 11! Kiswahili, English, Hisabati, Sayansi, stadi za kazi, Haiba na michezo, Maarifa ya jamii, Teknohama, Dini, French, civics na kadhalika. Hili ni tatizo kubwa hasa katika mazingira ya kutokuwa na waalimu wa kutosha. Labda hii ndio sababu wanafunzi hawafanyi vizuri katika yale masomo muhimu ya lengo la elimu kwa wote, yaani kusoma na kuhesabu.

    Madhara ya mgawanyiko huu katika hatua za awali ni kutokuwa na umakini na uelewa mzuri wa masomo. Mjadala kuhusu kuunganisha masomo ya msingi yalifikiwa mwaka 1990’s. Ni wazi kuwa pamoja na kuongeza masomo haya, hakuna bajeti ya kufundisha na kujifunza kwa mfano fedha za kusomeshea walimu wa masomo haya mapya na wala vitabu vya kutosha kwa uwiano unaotakiwa. Matokeo yake vile vitabu vichakavu na uwiano wa mwalimu na vitabu imekuwa mbaya na bajeti ni finyu.

  8. Mheshimiwa Spika,
    Kama nilivyosema hapo awali, kuwa elimu ni chachu ya maendelo kwa taifa lolote lenye dhamira ya kufikia kilele cha ustawi wa jamii katika nyanja zote za kiuchumi, kiutamaduni na kisiasa. Lakini ili kufikia lengo hili, elimu inastahiki kutunzwa kwa sera endelevu na thabiti. Elimu ndio inayowawezesha ugunduzi wa kisayansi tena ni chimbuko la ustaarabu kote duniani.

  9. Mheshimiwa Spika,
    Pia katika suala la mitaala, itakuwa si busara kambi ya Upinzani kutokugusia suala zima la shule zinazofundisha kwa kutumia lugha ya kiingereza maarufu kwa jina “English Academy”. Hivi hii sera inayoruhusu shule hizi imeanza lini? Na ni kifungu gani cha sheria ambacho kinaruhusu hili? Kambi ya upinzani inapenda kujua kama sheria inaruhusu kuanzisha shule zinazotumia lugha ya kiingereza pekee au pia lugha nyingine pia zinaruhusiwa, kama vile kuanzisha “French Academy”, “Italian Academy” au hata “Hehe Academy”?

    B) Mpango wa chakula mashuleni

  10. Mheshimiwa Spika,
    Ukosefu wa chakula mashuleni ni tatizo kubwa nchini, na linaletelea adha kubwa kwa wanafunzi wetu. Kuwepo kwa chakula cha kutosha katika shule zetu itahakikisha kuwa watoto wetu wanapata elimu inayotakiwa, bila kuwa na fikra kuhusu chakula. Hii inatokana na ukweli kwamba watoto wanahitaji chakula kwa kiasi kikubwa kutokana na sababu nyingi zikiwemo za kibaiolojia ambazo zinahusiana na makuzi yao.

  11. Mheshimiwa Spika,
    Tatizo hili sio dogo na wala halihitaji kufanyiwa mzaha. Kwa sababu inasikitisha kuona kuwa shule nyingine hufikia hata hatua ya kufungwa kwa sababu ya ukosefu wa Chakula. Kwa mfano shule za sekondari za manispaa za Tabora zilizofungwa kwa sababu hiyo ni Shule ya Kazima, Milambo, Shule ya Wasichana Tabora na Shule ya Wavulana Tabora, Kilosa pamoja na na Shule ya Sekondari ya Wavulana Bwiru. Mkoa wa Mbeya na Rukwa nayo imeathirika sana. Inatia fedheha kuona kuwa sababu ya msingi ambayo ilipelekea shule hizi ni Serikali kushidwa kuwalipa wazabuni ambao wanasambaza Chakula Mashuleni kwa wakati. Hali hii inahitaji maelezo ya kina kunusuru elimu ya watoto wetu.

  12. Mheshimiwa Spika,
    Tafiti tofauti zinaonesha ya kuwa ukosefu wa Chakula Mashuleni husababisha wanafunzi wengi hasa katika shule za kawaida kuwa na uelewa mdogo darasani kutokana kutokuwa na lishe bora inayomwezesha kutulia darasani hadi mwisho wa masomo. Njaa imekuwa ni tishio kubwa mashuleni kwani ndio kimeonekana chanzo cha kushusha taaluma. Watoto wengi wamekuwa hawahudhurii madarasani kwa kushindwa kupata mlo utakaomwezesha awepo shule hadi mwisho wa vipindi hivyo na kuamua kushinda nyumbani au kutoroka.

  13. Mheshimiwa Spika,
    Mnamo tarehe 30 juni mwaka huu, Mheshimiwa waziri Mkuu aliwahimiza wananchi wachangie wenyewe chakula hicho cha wanafunzi Mashuleni. Hivi mtanzania anasaidiwa nini na Serikali yake kama kila kitu ajitahidi mwenyewe? Hivi kwa nini Serikali inahamisha majukumu yake kwa wananchi walio wanyonge na wasio na uwezo. Mwanachi achangie ujenzi wa shule, anunue mavazi ya shule, alipie mwenge, wanunue karatasi za mitihani, vitabu, madaftari, walipie majengo. Hivi faida ya kuwa na Serikali inayojali wananchi wake uko wapi? Hii kweli inamsaidia mwananchi au inamzidishia matatizo?

  14. Mheshimiwa Spika,
    Kwa kuzingatia umuhimu wa chakula kwa maendeleo ya afya na taaluma watoto wetu, kambi ya upinzani inahitaji ufafanuzi unojitosheleza ni kwanini wizara husika haikuwalipa wazabuni kwa wakati na hivyo kusababisha wanafunzi kurudishwa nyumbani bila ya kuzingatia watoto hao wako masomoni na mwisho wasiku wanapewa mitihani ya pamoja bila kujali usumbufu waliopata wakiwa shuleni? Pamoja na hilo kambi ya upinzani, inaitaka wizara kueleza ni mkakati gani ambao wamepanga ili kuhakikisha kuwa tatizo hilo halitajirudia tena.

  15. Mheshimiwa Spika,
    Katika nchi yetu wananchi wanatimu idadi ya milioni 34,569,232 kwa kutumia takwimu za sensa ya mwaka wa 2002. Kati ya hao wananchi wenye umri wa kati ya miaka 20 hadi 60 ni 13,657,215. Lakini kwa kuzingatia hilo tuchukue kata ndogo ya Mwampembele, wilayani Nkansi, Mkoani Rukwa, yenye jumla ya watu 10,064 tuseme kati yao wenye uwezo wa kuchangia kuwa ni 8500, na kama kila mmoja atachangia shillingi 10,000. Hii inamaanisha kuwa katika kata hiyo wananchi wameweza kuchangia shillingi 85,000,000. Na hapo bado hatuongeza mkono wa serikali wala wa wafadhili katika ujenzi huo huo wa shule.

    Hivi nani mwenye mamlaka ya kuhakikisha kuwa hizi pesa za wananchi zinatumika kama ilivyopangwa? Na pia ni nani mwenye jukumu la kuhakiki pesa hizo? Isije ikawa sisi tunahangaika na mafisadi wakubwa ilhali vifisadi vidogo vidogo vinaendelea kuzaliwa katika kata zetu.

  16. Mheshimiwa Spika,
    Kutofanya tathmini ya pesa za wananchi, madhara yake hayaishii tuu kwa wananchi bali hii inadhihirisha kwamba serikali iliyoko madarakani haijui hata thamani ya rasilimali zake wenyewe. Hii ni hatari, kwani watu wachache wasio na mapenzi na maendeleo ya watanzania wote kwa ujumla na waliojawa na tamaa watachulia nafasi hiyo na hivyo kujilimbikizia mali. Hii itazalisha ufisadi usioepukika kwa sababu, serikali haitaweza kumkamata mtu huyu kwa sababu haijui hata wananchi walichangia kiasi gani?

    Kwa kuzingatia hilo kambi ya upinzani inahitaji ufafanuzi wa kutosha ni kwanini hakuna tathmini ya nguvu za wananchi katika ujenzi wa shule. Na hivyo kuweza kuwahakikishia wananchi juu ya matumizi ya fedha zao?

    D) Kuhusu vitabu vya kiada Shuleni

    Wizara ya elimu mwaka 1992 ilitoa tamko kwamba Serikali itajitoa katika kuchapisha vitabu . Pia mwaka 2004 kamati ya kuthibitisha vifaa vya elimu iliundwa ili kuwezesha uwepo wa vitabu vya aina mbalimbali lengo likiwa ni wachapishaji waweze kuwa na ushindani wa kuchapisha na kusambaza vitabu Mashuleni ili mradi wapate vibali kutoka EMAC (Educational Materials Approval Committee), wanaoangalia ubora wa vifaa husika kwa ajili ya elimu.

    Mwaka 2005 wizara ikapeleka madaraka ya kununua vitabu Mashuleni.Tunaamini kuwa utaratibu wa kupeleka madaraka ya kununua vitabu Mashuleni ni mzuri na ni njia mojawapo ya kuboresha ubora wa elimu na kuboresha usomaji .Ni masikitiko makubwa kuona wizara ikilipia gharama za uchapishaji wa vitabu na kuvipeleka Mashuleni . Hii ni kinyume na sera ya mwaka 1992 . Kambi ya Upinzani inaitaka Serikali kutoa maelezo ya kina juu ya utaratibu huu ambao ni kinyume na sera ya elimu ya mwaka 1992 na Wizara inatueleza nini.

  17. Mheshimiwa Spika,
    Kuna maswali ya kujiuliza ni kwa nini Taasisi ya Elimu inachapisha vitabu vya shule za msingi na kwa nini Wizara imekuwa ikivinunua vitabu hivyo haswa ikizingatiwa kuwapo kwa ushindani wa kibiashara ? Pili ubora wa vitabu hivi unatia shaka sana kwani inaonekana kama havijaidhinishwa na wala kuhakikiwa na EMAC kitu ambacho ni kuwa vitabu vyote vya kiada vinapaswa kupita na ama kupitishwa (certified) na EMAC.

    Cha ajabu zaidi hapa ni kuwa Taasisi ya Elimu ni mjumbe wa EMAC kwa ajili ya kutathimini wachapishaji vitabu , wana wajibu wa kukuza na kuandika mitaala na kutoa mafunzo kwa waalimu. Ni kwa vipi tena wawe wachapishaji wa vitabu kwa mtaala huo huo huku wakishindana na wachapishaji wengine?

  18. Mheshimiwa Spika,
    Kambi ya Upinzani inajiuliza na kuiuliza serikali Ni kwanini Wizara na Taasisi wanataka kurudisha uchapishaji na urudufu (printing) wa vitabu kwa Taasisi ya Elimu?

    Kambi ya Upinzani inahoji pia ni kwa nini hakuna program za kujisomea Tanzania? Ukweli ni kwamba hakuna usomaji na haswa shule za msingi, na pia hakuna msingi wa kujijengea tabia ya kusoma katika jamii kwani msingi huu ulipaswa kujengwa kuanzia Mashuleni ,na cha ajabu zaidi ni kuwa hakuna maandalizi yeyote ambayo yamefanywa ili kuweza kulijengea taifa letu tabia hii kwani kila ukiuliza utaambiwa kuwa bajeti ni finyu na hairuhusu kununua vitabu na vifaa vingine muhimu kwa ajili ya kukuza tabia hii ya jamii kupenda kujisomea.

    Pamoja na kupongeza utaratibu mzuri wa shule kujinunulia vitabu, bado kunahitajika usimamizi mzuri zaidi kutoka wizarani na kwenye Halimashauri husika kwani zimeshindwa kuthibiti utaratibu wa shule kujinunulia vifaa vya elimu, utaratibu uliopo sasa hauko wazi sana ,matumizi mabovu ya fedha kama vile kupeleka sehemu nyingine fedha zilizokusudiwa kununulia vitabu na pia hakuna ufuatiliaji madhubuti ili kuhakikisha kuwa fedha zinatumika kwa ajili ya kazi ambazo zilikuwa zimekusudiwa na haswa kununulia vitabu.

  19. Mheshimiwa Spika,
    Tanzania inatumia karibia dola 20 milioni kwa mwaka kwa ajili ya ununuzi wa vitabu , ambapo kati ya hizo fedha 95% ni kwa program za elimu zinazogharimikiwa na Serikali au shule . Hivyo kwa mwaka kama Serikali inatumia 20 milioni katika vitabu ukilinganisha na dola 700 milioni katika simu na dola 200 milioni katika vinywaji (vileo) . Ni lazima sisi kama viongozi tuone umuhimu wa elimu na kuipa elimu kipaumbele . Sasa hivi kila kukicha ni kuwa Bar mpya zinafunguliwa na wengine wamefikia hatua ya kuwa na mini Bars majumbani mwao , sijui kwa hali hii watoto watapenda vipi kusoma , ni lazima pawepo na maotisha kwenye ujenzi wa maktaba na vituo vya elimu utolewe ili watu wetu waweze kujenga Utamaduni wa kujisomea.

III.   ELIMU YA WALIMU

  1. Mheshimiwa Spika,
    Moja kati ya wadau muhimu katika elimu ni walimu wenyewe. Uwekezaji katika walimu ni jambo muhimu sana. Tanzania tunashukurumu Mungu, vyuo vinavyofundisha fani hii ya ualimu katika mwaka wa fedha wa 2007/2008 umeongezeka kutoka 53 hadi 55 sawa na ongezeko la asilimia 3.6. Hili linaonyesha dhahiri kuwa sasa watanzania tunatambua umuhimu wa kuwekeza katika elimu.

  2. Mheshimiwa Spika,
    Lakini linalotupa shaka kambi ya Upinzani ni idadi ya wanfunzi katika vyuo hivyo. Kwa mfano idadi ya wanafunzi katika vyuo vya ualimu vya Serikali ilipungua kutoka 26,681 mwaka 2006 hadi 18,754 mwaka 2007. Wakati idadi ya wanafunzi wa ualimu kiwango cha diploma ilipungua kutoka 7,411 mwaka 2006 hadi 5,959. Idadi ya wanfunzi wa ualimu daraja “A” ilipungua kutoka 11,609 mwaka 2006 hadi 3,238 mwaka 2007.

  3. Mheshimiwa Spika,
    Katika taarifa ya serikali ya hali ya uchumi katika mwaka huo wa 2007/2008, sababu iliyotolewa na juu ya upungufu huo, ni kuongezeka kwa wigo wa masomo katika vyuo vikuu vya ndani. Kambi ya Upinzani inaona kuwa hoja hiyo ni dhaifu na haiwezi kukidhi katika kujibu hoja hii, kwa sababu zifuatazo:-

    1. Vyuo vya ualimu vinawezaje kuongezeka lakini vikaweza kuchukua kiwango kidogo cha wanafunzi kuliko kile cha mwaka jana?
    2. Wigo wa elimu ulipanuka tofauti na mwaka jana?
    3. Je ni nini hasa kilichopelekea kupungua kwa wanafunzi katika fani hii?
    4. Na baada ya kulitambua hilo je Serikali ilichukua hatua gani katika kutatua tatizo hilo hasa ukizingatia kuwa nchi inakabiliwa na tatizo la upungufu wa walimu? Kwa mfano wilaya ya Sengerema pekee yake ina upungufu wa walimu zaidi ya 1,000.

  4. Mheshimiwa Spika,
    Ubora wa elimu ni muhimu na unatokana na ubora wa ufundishaji. Kwa sasa shule za misingi zinafundishwa na walimu wa Grade A (70%) wengi wao hawajaweza kuinternalize na kufundisha mitaala vizuri kwani hata wao walikuwa na ufaulu mdogo kwa form IV. Bado wapo walimu wahitimu wa darasa la saba ambao ni walimu wa Grade B/C 26.9% wakati wa diploma ni 2.8 % na wenye digrii ni 0.2% tu. Hii ni hatari kwa ubora wa elimu.

  5. Mheshimiwa Spika,
    Katika nchi kama USA shule za msingi hufundishwa na wenye digrii wakiamini kuwa “huwezi kuacha kizazi cha vijana katika hali duni ya kiakili” ni wakati muafaka sasa Tanzania kufuta kabisa Grade B/C ya ualimu na pia wabadili Grade A kwenda kwenye Diploma katika elimu ya msingi. Ninaamini katika dunia ya sasa ambapo wimbo unaoimbwa ni Anga sio tena mwisho wa akili inayojengwa na uelewa thabiti na kuongozwa na wataalam waliobobea, mwanzo wa akili za vijana zinahitajika kilicho bora zaidi na sio walioshidwa.

  6. Mheshimiwa Spika,
    Panapokuwa na janga kubwa, ni lazima tupime na kulitatua kwa makini. Ni lazima tuwe na uwezo wa kuhakiki yale yote yanayotokea darasani. Tuna mtazamo hasi kwamba darasa ni mwalimu pekee. Ni mara chache sana walimu wakuu na walimu wakuu wa masomo kuingia darasani na wakaguzi ni mara chache na pengine kutoenda kabisa. Huku tukijua ufundishaji ni mbovu sana. Mbaya zaidi muda wanaotumia watoto shuleni unatosha lakini muda unaotumiwa kwa kufundishwa ni mdogo sana zaidi ya majaribio ya mwezi.

    Upungufu wa wanafunzi katika taaluma ya ualimu inafedhehesha nguvu za wananchi katika ujenzi wa shule, hivyo basi kambi ya upinzani inataarifu wizara husika kuchukua hatua za haraka katika kutatua tatizo hili ili kuweza kukidhi mahitaji ya walimu katika shule zetu.

    A) Chama cha Walimu Tanzania (CWT)

  7. Mheshimiwa Spika,
    Ni ukweli usiopingika kuwa walimu ndio watekelezaji wakuu na muhimu katika utoaji wa elimu bora na sio bora elimu. Kama walimu hawakuandaliwa vizuri kimaisha, katika mazingira yao ya kazi na pia mahali wanapoishi, hata kama serikali itajenga madarasa na mashule mengi kwa kutumia almasi na dhahabu bado elimu itakayo tolewa haitakidhi viwango vya kimataifa katika ulimwengu huu wa utandawazi. Kwa kuzingatia hilo, mhe Spika, leo kambi ya upinzani inataka matatizo ya walimu yatatuliwe haraka, kwa sababu taaluma ya ualimu inadharaulika na kuendelea kutovutia vijana wetu. Sikatai kuwa hii inawezekana kuchangiwa na sababu zingine lakini, kero za kudumu ndani ya wizara hii ambazo zinaendelea kurudisha maendeleo ya walimu nyuma ni moja ya sababu ya msingi kabisa.

  8. Mheshimiwa Spika,
    Mimi sijui sababu ya msingi ni nini hasa, lakini kila mwaka tunaongelea suala la kupunguza madeni ya walimu kwa wizara husika lakini ulimbikizaji wa madeni unendelea. Pamoja na kuwa serikali iliahidi kutolimbikiza madeni baada ya tume ya Waziri Mkuu ya 2004. lakini nasikitika kusema kuwa ndani ya mwaka huu pekee madeni yaliyokusanywa ndani ya mikoa mitano tuu, wilaya 30 tayari serikali inadaiwa wastani wa Shillingi 6.3 billioni. Hii itaisha lini? Hivi serikali ya awamu ya nne ina mpango gani na walimu wa nchi hii abao ni muhimu sana kwa maendeleo ya jamii zetu?

  9. Mheshimiwa Spika,
    Kero za walimu sio tuu katika upande wa malimbikizo, bali moja katika matatizo sugu ambayo huwapata walimu ni katika suala la kupandishwa madaraja. Kumekuwa na kero ya walimu wenye uzoefu tofauti kulimbikizwa katika cheo kimoja, lakini pamoja na serikali kuchukua hatua mwaka 2006, baada ya Mhe raisi kuagiza, hii ni sawa na mtu aliyechochea moto badala ya kumwagia maji ili chakula kisiendelee kuungua.

  10. Mheshimiwa Spika,
    Hii inakatisha tamaa na inasababisha walimu waendelee kuwa wanyonge kama vile raia wasio na haki na taaluma ya kujivunia. Kambi ya upinzani inamtaka mheshiwa waziri muhusika atueleze hasa sababu za msingi hasa ni zipi zinazosababisha kero hii iendelee kukomaa? Na je wizara inasubiri nini ili iweze kuchukua hatua?

    Kambi ya upinzani inaungana na walimu wote Tanzania, na inapenda kuwatanabaisha kuwa iko nao siku zote. Na kwa kutumia nafasi yake itaendelea kuikumbusha serikali juu ya matatizo yanayowakuta.

  11. Mheshimiwa Spika,
    Wataalamu wa elimu kwa muda mrefu wamekuwa na njia mbali mbali za kupima juhudi za nchi katika nyanja ya elimu. Kwa vyovyote vile, kiwango cha ushiriki (participation rate) ndicho kipimo kitumikacho. Kwa mfano uandikishaji wa udahili wa watoto unaonyesha Tanzania kufanya vizuri sana katika elimu ya msingi lakini kwingine haiendi vizuri kwani pyramid inakuwa nyembamba sana kadiri unavyoelekea juu. Kwa mfano, elimu ya msingi 97.3%, sekondari 11% na elimu ya juu ni 2.2% tu. Ukilinganisha na majirani zetu Kenya ni 23% elimu ya sekondari, na elimu ya juu ni 3%, uganda ni 12% elimu ya sekondari na elimu ya juu ni 3%. UNDP Human Report (2007).

  12. Mheshimiwa Spika,
    Kwa kawaida viwango vya ushiriki vinatokana na kiasi cha rasilimali kilichowekwa kwenye elimu na hivyo kila mara lazima tarakimu mbili ziwe sambamba nazo ni GDP (utajiri wa nchi na asilimia ya bajeti ya serikali). Ni ukweli kuwa bajeti ya elimu Tanzania bado si ya kuridhisha sana pamoja na kupewa kipau mbele ukilinganisha na jirani zetu. Kwa uchumi mdogo na idadi kubwa ya watu, rasilimali bado ni ndogo kwa kazi tulionayo siku za usoni.

    Ulinganishi wa fedha kwa ajili ya sekta ya elimu 2006/2007

    Nchi
    GDP % % Bajeti ya mwaka
    Tanzania
    4.5
    18.10
    Kenya
    6.4
    29.0
    Uganda
    4.2
    26.0
    Malawi
    5.3
    25.0

    Source: World Bank (2007) BEST (2007)

  13. Mheshimiwa Spika,
    Tanzania lazima ifikirie mara mbili kuhusu rasilimali inayoelekezwa kwa sekta ya elimu kama kweli tunataka malengo ya MKUKUTA na Dira ya Maendeleo ya 2025 yafikiwe. Kama kawaida suala muhimu ni uwezo dhidi ya utayari wa kugharamia huduma za elimu. Hali inayojionyesha katika jedwali, upanuzi wa mfumo wa kupata viwango shirikishi vya asilimia 100 kwa elimu ya msingi, 50% ya sekondari O-level na 25% A-level na 12.5. Elimu ya juu, itapima kwa uzito wa hali ya juu utayari(uhiari) wa serikali kugharamia badala ya uwezo kugharamia elimu. Hivyo ni ushauri wa kambi ya upinzani kwa serikali kujitahidi na kuwa na utayari wa kugharamia elimu kwani elimu ndio chimbuko la maendeleo na ni haki ya msingi ya binadamu kama ilivyo kwenye 1948 United Nation Declaration. Ni lazima kuwa na uwiano katika mfumo mzima wa elimu. Sasa hivi kuna msukumo wa kijamii kuliko wa kiuchumi katika elimu ya sekondari na ile ya juu na kidogo sana katika elimu ya ufundi na ile isiyo ya vyuo vya elimu ya juu yaani non-tertiary kama inavyojionyesha katika jedwali lifuatalo.

    Uandikishaji kwa jinsia, Aina na ngazi: 2007

    NGAZI ME KE Jumla %
    Awali
    387,868
    407,143
    795,001
    7%
    Msingi
    4,215,171
    4,107,754
    8,316,925
    81%
    O Level
    511,416
    455,671
    967,087
    9%
    A Level
    31,780
    21,643
    53,423
    1%
    Vyuo Vikuu-Umma
    27,937
    13,341
    41,278
    0.4%
    Vyuo Chini Ya Wizara Nyingine
    9,645
    7,227
    16,872
    0.2%
    Vyuo Vya Ualimu- Dip
    10,036
    8,718
    18,754
    0.2%
    Ufundi
    2,777
    767
    3,544
    0.05%
    Vyuo Vikuu Binafsi
    6,713
    4,033
    10,752
    0.01%
    Jumla
    10,223,606
    100%
    Chanzo: BEST (2007)

  14. Mheshimiwa Spika,
    Kuna tatizo kubwa katika elimu ya sekondari. Tukiwa na Gross Enrollment Ratio ya 5% (2004) na sasa kufikia 11% kwa nchi ya watu takribai milioni 40, ni vigumu kusema kwa uhakika kama tunaendelea vizuri.

    Nchi
    Viwango %
    Tanzania
    5
    Kenya
    23
    Uganda
    12
    Liberia
    23
    Lesotho
    20
    Tanzania
    5
    Namibia
    34

    Ongezeko la 50% kwa wanofaulu kuingia sekondari za serikali na wale wanaokwenda shule binafsi kutapelekea kuona mabadiliko makubwa. Pamoja na kwamba malipo yake ni kidogo mfano USD 20 kwa day Schools na karibia USD100 kwa boarding schools bado wazazi wengi zaidi 50% wanaishi chini ya mstari wa umasikini na wenye familia kubwa watashidwa kulipia watoto hao.

  15. Mheshimiwa Spika,
    shule nzuri za serikali zimetawanyika nchi nzima kwamba mtoto anaweza kusafiri kilometa 1000 na zaidi kwenda shule mfano Sumbawanga kwenda Ilboru na kadhalika. Hii inapelekea wengine washidwe kusafiri kutokana na nauli. Ujenzi wa shule za kata ni mzuri lakini zile jamii maskini zimeshidwa kutumia mwanya huu. Lakini inaonekana pamoja na wazo la kujenga shule hizi zitapelekea kutokuwa na usawa ambavyo inaweza ikaleta mashaka katika jamii ya kutokuwa na amani/upatanifu hapa baadaye. Kambi ya upinzani inaitaka serikali kutenga kiasi cha rasilimali kila mwaka kwa ajili ya jamii ambazo hazina uwezo wa kujijengea shule.

IV. UBORA WA ELIMU ITOLEWAYO

  1. Mheshimiwa Spika,
    Elimu bora hujenga uchumi bora. Lakini ubora wa elimu umeaangalia jambo moja la msingi nalo ni maarifa yatolewayo kuanzia kukumbuka (memorization) hadi kuainisha kufikiri na kutatua tatizo kwa kuweza kutathmini, kupanga, kusaini na kutumia kanuni kutatua matatizo ya maisha na maendeleo kwa ujumla.

  2. Mheshimiwa Spika,
    Ushahidi unaonyesha kwamba ubora wa elimu katika masomo yafundishwayo inatoa mchango mkubwa kwa jamii na pia kwa mtu binafsi kwa hivyo thamani ya fedha (value for money) na kwa mantiki hiyo shule nzuri zinakuwa na mdondoko mdogo, na pia wakariri wachache na hivyo zinachangia mafanikio ya kitaaluma na uzalishaji uchumi bora wa baadaye.

  3. Mheshimiwa Spika,
    Wote tunajua umuhumu wa masomo ya sayansi katika dunia ya leo. Hali ya Sayansi katika nchi yetu ni tishio na hatua zisipochukuliwa tutakuwa na madaktari na maprofesa wa tunguri. Hakuna maabara katika shule nyingi, na zilizopo hazitumiki kwa kukosa vifaa na mbaya zaidi ni kwenye shule za jumuiya. Ukweli ni kwamba uanzishwaji wa shule za jumuiya na sasa kata italeta mifumo miwili (mlinganisho) parallel moja wa matajiri na mwengine wa maskini.

    Bila kukusudia tunaua elimu kwa watoto masikini na wakulima kwa kuwa wataendelea kuwa kwenye mzunguko wa umasikini, usio na matumaini badala ya kuwa katika mzunguko ulio adilifu, bora na wa matumaini. Hii ni taaluma dhalimu (apartheid) ambavyo ni lazima iepukwe kwa gharama yoyote ile.

VI. MATATIZO YA KUJIFUNZA NA KUFUNDISHA SAYANSI NA HISABATI

  1. Mheshimiwa Spika,
    Kwa kawaida kunakuwa na mitihani ya darasa la 4, 7, kidato cha II, na IV na matokeo huwa yanakuwa kwenye daraja la “A, B, C, D, E”. Daraja D na E ni kufeli. Mtihani wa msingi (7) mwaka 2000 ulitoa viwango vya kufeli kwa 78% yaani kwa wale waliopata chini ya alama 60% kati ya 150. Katika shule za sekondari ukichukua alama ABC kama kufaulu kidato cha nne, viwango vya kufeli katika masomo ya Sayansi inatisha. Kwa hiyo ni vyema kukawa na mkakati wa makusudi kukazania masomo ya sayansi kwa kuwa sasa imefika pabaya/hatari vyovyote vile, Maarifa ya namba hasa katika hisabati na fizikia zimekuwa hatarini hapa nchini.

  2. Mheshimiwa Spika,
    Tanzania imeamua kwa makusudi kuweka mkazo kwa masomo ya Sayansi na teknologia kwa kuwa uchumi wetu unasukumwa na teknologia na ufahamu (knowledge based). Uwepo wa msukumo kidunia na kiutandawazi, huu ni mwelekeo chanya na unawakilisha mawazo mazuri ambayo yataletelea:-

    1. Kufundisha wanafunzi vizuri msingi wa sayansi
    2. Kufundisha hisabati na teknologia (basic) vizuri kwa wanafunzi
    3. Kufundisha lugha ya Kiingereza vizuri kwa wote kwani dunia lugha hii inatumika.
    4. Kuhakikisha tuantoa upendeleo kwa kuwaingiza shuleni wale wanaopenda hisabati, sayansii na teknologia.

  3. Mheshimiwa Spika,
    Takwimu zinaonyesha kuwa bado vyuo vya elimu ya juu vina wanafunzi wachache katika fani ya sayansi. Hili limepelekea kuwa na madaktari wachache sana, manesi wachache. Kambi ya Upinzani inaishauri Serikali iwekeze kwenye sayansi sasa kwa kutoa ufadhili (Grant) kwa wanafunzi wanaofanya vizuri kwenye masomo ya sayansi.

    Sasa hivi kuna tishio kubwa kwani wanafunzi waliochukua masomo kama kemia, fizikia, teknolojia, hisabati wameonyesha uwezo mkubwa wa kuchukua uhasibu, utawala, sheria, biashara na uchumi na hivyo kupata ajira haraka pindi wamalizapo. Hivyo mahitaji ya wanafunzi wa sayansi bado inaendelea kupanda kwa kasi na hivyo ni vigumu kwenda na kasi hii.

  4. Mheshimiwa Spika,
    Kambi ya Upinzani inashauri kuwa kama Tanzania inataka kufikia lengo la dira ya 2025 na MKUKUTA basi ni lazima hali hii ibadilishwe mara moja kwa:-
    Kuwa na Kamati ya Bunge itakayoanzisha mchakato wa mabadiliko. Changamoto sio ufundi au sayansi inayohitaji suluhisho bali maendeleo ya jamii katika kununua sura na hali (profile) ya sayansi na teknolojia ndani ya jamii na uchumi kwa ujumla . Kamati hii iwashirikishe katika utendaji wake wa kazi sekta kama sekta ya watu binafsi, viwanda , wanataaluma kwa lengo la kuwa ‘Think Tank’ ya Taifa katika masuala ya Elimu. Tunaamini kuwa tatizo la kijamii lazima lipatiwwe utatuzi wa kijamii , na huu utakuwa ni mkakati wa muda mrefu.

VII. ELIMU YA JUU

  1. Mheshimiwa Spika,
    Sina mashaka kwamba elimu ya juu inachangia sana uzalishaji kwa taifa katika nyanja zote za maisha, ambazo baadaye inabainisha kiwango cha ubora wa viwango vya maisha kwani siku zote pato huboreshwa na uzalishaji. Uwezo wa nchi yoyote kushindana kiuchumi katika ukanda na kimataifa utategemea sana katika elimu ya juu. Uchumi wote duniani unaongezeka kwa kutegemea teknologia na Maarifa ya hali ya juu ambapo bila elimu ya juu nani atashindana? Taasisi za teknologia (utafiti na Mafunzo) vinatoa msaada mkubwa kwa teknolojia na Maarifa yanayoendesha ukuaji wa uchumi na hivyo kupunguza umasikini. Na sio wa darasa la saba!

  2. Mheshimiwa Spika,
    Elimu ya juu ni muhimu sana kwani mbali na kutoa wafanyakazi kwa sekta mbali mbali nchini na nje, pia inajenga uwezo wa kushiriki katika dibwi linalokuwa la dunia ya Maarifa na kuweza kupokea na kutumia Maarifa hayo hapa nchini. Ni dhahiri kuwa elimu ya juu inaweza kuletelea ubunifu, uvumbuzi na kugundua wa mbinu ambazo zitasaidia maendeleo katika nyanja zote za maisha. Katika nchi maskini kama yetu elimu ni sharti ilete mabadiliko ya kudumu. Na kama tunataka kukuza uchumi wetu wote, hilo halitawezekana kama hatutajenga kujengwa uwezo katika mfumo wa elimu ya juu. Hivyo ni muhimu sana kutegemeana na kuimarisha mahusiano kati ya elimu katika ngazi zote za uchumi kwa maendeleo ya taifa.

  3. Mheshimiwa Spika,
    Ngazi za elimu ya juu, zinaonyesha ufinyu mkubwa kufikia, yaani kwa idadi yake na umbali wa kuvifikia (physical access). Uwezo wa kuchukuwa wanafunzi wengi pia ni mdogo kwa mfano vyuo vyote vya umma havijafikia wanafunzi 50,000. ukijumlisha idadi ya wanafunzi wote katika vyuo vya ufundi, Mbeya, Karume, Arusha na Dar es Salaam hata hawafiki 3500. na vyuo vingine 18 vinavyotoa Diploma kwenye wizara mbali mbali vinachukua wanafunzi 16,873 tu. Wanafunzi wengi wanaomaliza kidato cha 4 hawapati nafasi katika A-level na zaidi ya 50% wanaomaliza kidato cha 6 hawafaulu kujiunga na Elimu ya Juu. Hivyo viwango vya ushiriki (participation votes) vimeendelea kuwa chini sana kama jedwali no. 5 linavyoonyesha:-

    Na
    NCHI
    V/U
    1
    Tanzania
    2.2
    2
    Brazil
    18
    3
    Botswana
    4
    4
    Ivory Coast
    7
    5
    Misri
    38
    6
    Ghana
    5
    7
    Namibia
    7
    8
    Senegal
    5
    9
    Afrika Kusini
    15
    10
    India
    11
    11
    Malaysia
    27
    12
    Thailand
    37
    14
    Singapore
    45
    15
    Sri Lanka
    5
    16
    Mauritius
    21
    17
    Australia
    65
    18
    Korea Kusini
    82
    19
    Ufaransa
    54
    20
    Uingereza
    59
    21
    Canada
    59
    22
    Amerika
    81
    23
    Uganda
    3
    24
    Kenya
    3
    25
    Nigeria
    10
    26
    Rwanda
    3
    27
    Ethiopia
    3

    Chanzo: UNESCO (2006), World Bank (2007)

  4. Mheshimiwa Spika,
    Kwa upande wa uwezo, elimu ya juu bado inawezekana kwa wengi hasa baada ya serikali kutoa mikopo ya ada, malazi, chakula na vitabu. Lakini bado vyuo vikuu nyeti viko mashariki mwa nchi hivyo baadhi ya wanafunzi kutoka kaskazini, magharibi na kusini yawapasa kusafiri umbali mrefu sana 1000+ km hivyo kupelekea masuala ya usawa katika kupata elimu hiyo muhimu.

  5. Mheshimiwa Spika,
    takwimu, akili za kawaida, na tafiti zilizofanywa katika jamii mbalimbali zinaonyesha kwamba umuhimu wa elimu ya juu katika nyanja zote za uchumi na maendeleo ya watu kwani inasaidia (promote)

    1. Kukua kwa uchumi- inaboresha mapato na kipato, inaongeza uzalishaji, ujasiriamali, inaongeza pia kukua kwa jamii, ushiriki katika siasa na utawala wa kidemkrasia, kuondoa umasikini na uboreshaji wa umri wa kuishi na ubora wake.
    2. Uuongofu kwa viongozi: elimu inawapa ujasiri kuongoza kwa uadilifu, Maarifa na Maarifa ya teknologia na pia kutengeneza kada za walimu bingwa katika ngazi zote za elimu nchini

  6. Mheshimiwa Spika,
    Kuna mambo makubwa manne yanayohitajika katika mfumo wa elimu yaani kupata elimu hiyo kwa watoto wengi bila kujali rangi, dini, jinsia na utaifa, umuhimu wake kwa mahitaji ya watoto, familia na mahitaji ya uchumi; ubora wake kwa maana ya kupata Maarifa na mtazamo. Mfumo wetu wa elimu unahitaji uwazi/unyofu na uainisho wa uhakiki (intrinsical analysis) ili kuwa na elimu bora na si bora elimu.

    A) Mikopo kwa Wanafunzi

  7. Mheshimiwa Spika,
    Sera ya kuwakopesha wanafunzi asilimia 20, 40, 60 na wao kuchangia gharama za mafunzo yao kwa asilimia tofauti itaendelea kuwa chanzo cha migomo isiyokwisha katika vyuo vyetu vikuu, serikali inataka kuifanya elimu ya juu kuwa matakwa ya mtu binafsi badala ya mahitaji ya kijamii. Wakati mashirika haya dunia ya fedha yakitushauri sisi kuacha kuwekeza katika elimu ya juu,serikali za huko kwao zimejiwekea utaratibu wa kuhakikisha kuwa hakuna mtu anayeshindwa kusoma chuo kikuu kwa sababu ya kukosa pesa.

    Tamko la kuchangia asilimia 40 na zaidi ni gumu sana na litarudisha nyuma juhudi hizi za serikali za kuongeza namba ya wanafunzi katika elimu ya juu na kuongeza namba ya watanzania wenye elimu juu. Watanzania wengi hawaelewi maana ya asilimia 40 ya gharama za elimu ya juu.

  8. Mheshimiwa Spika,
    Gharama kubwa kabisa ni ada ambayo hutofautiana kufuatana na aina ya shahada. Kwa mujibu wa mwongozo huu, ada ya chini kabisa ni ile inayotozwa katika vitivo vya elimu, sanaa na sayansi ya jamii na uhandisi ambayo ni sh. 600,000 kwa mwaka, gharama nyingine na bila kujumlisha gharama ya malazi kwa mwanafunzi anayesoma shahada ya kwanza zilizotajwa hapo juu ni, 1,564,500. Asilimia arobaini ya hii ni sh 625,800.Kwa hiyo gharama ya chini kabisa ambayo serikali inataka mzazi wa mwanafunzi anayesoma chuo kikuu achangie ni sh 625,800 kwa mwaka.

  9. Mheshimiwa Spika,
    Hatua hii inagusa pia gharama za mafunzo kwa vitendo. Asilimia arobaini inapunguza gharama za mafunzo kutoka sh.6000 ambazo ukitoa asilimia 80 inabaki tshs 1200 kwa siku. Kwa hali ya uchumi ilivyo sasa kweli wanafunzi hawa watamudu kufanya mafunzo kwa vitendo katika sehemu walizopangiwa?

  10. Mheshimiwa Spika,
    Kwa mujibu wa ripoti ya serikali ya hali ya umasikini na maendeleo ya watu ya mwaka 2005, kipato cha wastani kwa mtanzania ni sh.9900 katika siku 28 (mwezi) kiwango ambacho inasemekana kimekuwa kwa asilimia chache sana mwaka jana.Kwa kiwango hiki na kwa mujibu wa viwango vya kimataifa vya kupima umasikini,asilimia 57.5 ya watanzania ni maskini wa kutupa. Hii ina maanisha kwamba, pato la wastani la mtanzania kwa mwaka ni sh.118,800. Sasa tujiulize, serikali inaposema wazazi walipie asilimia 40 ya gharama za kusoma chuo kikuu (zaidi ya sh. 625,800) inawalenga watanzania gani? Kwa takwimu hizi, zaidi ya asilimia 50 ya watanzania hata kama wangeamua kuacha kula, kutibiwa ambako wanachangia pia gharama na kuvaa kwa mwaka mmoja, wasingeweza kumudu hata asilimia 10 ya gharama za kumsomesha mtoto wao mmoja katika vyuo vetu vikuu vya umma? Kwa misingi hii hata vyuo vikifunguliwa vipya watasoma kina nani?

    Kambi ya upinzani inasisitiza kuwa watanzania kwa hali ya umasikini tuliyo nayo, wazazi wengi wa kitanzania hawawezi kumudu gharama za watoto wao kusoma chuo kikuu, hivyo serikali ina uwezo na wajibu wa kulipia gharama za elimu ya juu kupitia bodi ya mikopo bila kutetereka na kuwapatia wanafunzi mikopo.

  11. Mheshimiwa Spika,
    Pamoja na hayo kambi ya upinzani inaendelea kuhoji yafuatayo kuhusiana na mikopo. Hadi kufikia June 2008, ni kiasi gani cha fedha ambazo zilitolewa kama mkopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu nchini na kwa wastani wa shilingi ngapi kwa kila mwanafunzi?

  12. Mheshimiwa Spika,
    Kwanza, Jinsi mikopo inavyotolewa inapendelea vyuo vya binafsi. Kwa mfano, mwanafunzi mmoja wa chuo kikuu cha umma analipa ada kama Tshs. 600,000 na chuo cha binafsi mwanafunzi mmoja analipa kama Tshs. 2,500,000. Hivyo kwa mwanafunzi mmoja, chuo cha binafsi kitapata Tshs. 1,900,000 zaidi ya kile cha umma! Matokeo yake vyuo vya umma ambavyo ndiyo kimbilio la wanyonge na ambavyo ndiyo vinatoa elimu kwa idadi kubwa zaidi ya wanafunzi vinakosa pesa za kuboresha miundombinu ya utoaji elimu na vinashindwa kuwapa wanafunzi hawa elimu iliyo bora zaidi.

  13. Mheshimiwa Spika,
    Kuhusu vyuo vya elimu ya juu binafsi, tunaendelea kushauri serikali yetu kufanya yafuatayo:

    1. Kuvifuatilia kwa karibu vyuo hivi ili kuhakikisha vinaweka mbele umuhimu wa kukidhi viwango kuliko manufaa ya kibiashara.
    2. Serikali ihakikishe kuwa vyuo hivi vinatambua umuhimu wa kusaidia utoaji wa elimu hiyo kwa watanzania wote bila ya kuangalia tofauti za kimapato, kiitikadi, kidini na hata kijinsia.
    3. Serikali ihakikishe kuwa wenyeji wa maeneo ambayo vyuo vikuu hivi vinapatikana, haswa katika ile mikoa ambayo wenyeji wake wapo nyuma kielimu kama ilivyo kwa mkoa wa Morogoro, wanafaidika na kuwepo kwa vyuo katika maeneo yao.
    4. Serikali ihakikishe inalipitia upya suala la kulipia wanafunzi wa vyuo binafsi kupitia bodi ya mikopo ama ruzuku mbalimbali.

    B) Posho za Wanafunzi

  14. Mheshimiwa Spika,
    Kambi ya upinzani inaipongeza serikali kwa kuongeza kiasi cha posho za wanafunzi kutoka sh.3500 hadi sh. 5,000. Bado kiasi hiki hakitoshi. Kambi ya upinzani pia inapendekeza kuongezwa kwa posho ya mafunzo kwa vitendo na visifanyiwe mean testing, kuongezwa kwa viwango vya malipo wanayopewa wanafunzi kwa mahitaji yanayohusiana na masomo ya wanafunzi kama vile stationaries, study tours.

    C) Mapungufu ya Miundombinu muhimu

  15. Mheshimiwa Spika,
    Kuanzishwa kwa vyuo vikuu vipya na kuongeza idadi ya wanafunzi wanaojiunga katika vyuo vyetu ni lazima kuendane na juhudi kubwa za kuboresha mazingira ya kazi ya wahadhiri na wasomi watarajiwa. Vyuo vyetu vikuu hivi sasa, na vile vya kihistoria kama chuo kikuu Dar Es Salaam na vile vilivyozaliwa upya kama Chuo kikuu Cha Mzumbe, kwa miongo kadhaa sasa vimekumbwa na tatizo la kubwa la upungufu mahitaji muhimu. Mapungufu haya ni kama ifuatavyo:

    1. Upungufu, ufinyu na uduni wa vyumba vya mihadhara. Vyuo vyetu vimekuwa vikikumbwa na tatizo hili kwa miaka kadhaa sasa.
    2. Ukosefu wa maabara za utafiti na mawasiliano ya computer. Hali hii imepelekea wasomi wetu kuacha tabia za utafiti wa kisayansi na kulazimisha hata wanafunzi wetu kufanya mitihani inayopaswa kufanyiwa utafiti wa kimaabara kwa kutumia kifaa kimoja kwa watu zaidi ya kumi. Na wengine kutumia njia ya nadharia tu kukamilisha tafiti zao.
    3. Ukosefu wa wahadhiri wa kutosha na walio na sifa za kutosha.

    D) Mishahara ya Wafanyakazi waendeshaji

  16. Mheshimiwa Spika,
    Naipongeza sana serikali kwa kuona umuhimu wa wahadhiri wetu na kuwaongezea mishahara yao kwa asilimia mia. Hii sio tu itawafanya vijana wengi wafanye vizuri ili wabaki vyuoni kama wahadhiri bali pia itawafanya wahadhiri wengi kutokukimbilia nje ya nchi hivyo kujenga ile dhana ya uzalendo, tofauti na ilivyokuwa huko nyuma.

  17. Mheshimiwa Spika,
    Lakini pamoja na hayo serikali haikupandisha mishahara ya wafanyakazi katika taasisi hizi wasio wahadhiri (non teaching staff) ambao uzoefu unaonyesha kuwa wanafanya kazi zinazofanana na kuwiana pia makundi haya yanategemeana kiutendaji. Aidha sababu nyingine ambazo zinawafanya wastahili pia kuongezewa mishahara ni kama vile, ongezeko la idadi ya wanafunzi, kupanda kwa gharama za maisha, kuhama kwa wanataaluma na kushindwa kuajiri wanataaluma wa ngazi za juu kutokana na mishahara kuwa midogo. Kazi za watumishi hawa zinachangia sana katika ufundishaji na utafiti. Utekelezaji wa uboreshaji wa mishahara hiyo iliamuliwa ufanyike katika awamu mbili. Aidha, kutotekelezwa kwa maamuzi kwa upande wa waendeshaji kutaathiri ubora, viwango na thamani ya elimu inyotelewa katika vyuo vyetu.

  18. Mheshimiwa Spika,
    Serikali kuwaengua wafanyakazi waendeshaji katika utekelezaji wa maamuzi ya kamati kumeleta matatizo mengi, kama kuwepo kwa tofauti kubwa kati ya mfanyakazi mwanataaluma na mfanyakazi mwendeshaji. Tofauti hizi zimetokana na kutekelezwa kwa maamuzi ya kamati kwa upande mmoja (wanataaluma) na kuacha kundi lingine la wafanyakazi waendeshaji wakati maamuzi ya kamati yalizingatia kulinda uwiano uliyokuwepo kabla ya utekelezaji huu wa kibaguzi. Kambi ya upinzani inasisitiza kuwepo kwa uwiano na kuboresha mahusiano haya ya kipekee,jitihada za kuboresha mazingira ya kazi kwa wakati wote zililenga kuwakwamua waliomo katika mazingira ya kazi kwa kuzingatia uhalali na uwiano linganifu miongoni mwa watumishi wote. Tunaitaka serikali itoe tamko ni lini wafanyakazi hawa watatekelezewa maamuzi ya Kamati ya Raisi ya Oktoba 2005?

  19. Mheshimiwa Spika,
    Ikumbukwe kwamba katika kikao cha bajeti cha mwaka juzi na jana katika Bunge hili tukufu, mheshimiwa waziri akijibu hoja hii alisema suala hili linafanyiwa kazi. Kambi ya Upinzani inataka kujua ni kwa kiasi gani suala hili limetekelezwa katika bajeti hii!

  20. Mheshimiwa Spika,
    Ni jambo lisilopingika kwamba elimu katika ngazi ya juu ni gharama kubwa na sio jambo la kubishana ya kwamba elimu ya juu inahitaji kupanuliwa. Hili ni jambo muhimu na la haraka ambalo ni kipaumbele. Ni dhahiri kabisa pia kwamba uchumi wetu unaweza kulipia gharama zitakiwazo kwa elimu hiyo.Kusema tu hakuna fedha, hilo si jibu la kweli.Ukweli ni kwamba fedha zipo.Suala hapa ni namna gani tunagawa fedha kwa ajili ya matumizi mbalimbali, na kama kweli tunajali maendeleo ya wananchi wetu na ya nchi yetu. Jambo hasa ni katika namna tunavyochagua vipaumbele na kwa hiyo, ni lazima kujua kwamba ipo haja ya kuacha mengine kwa ajili hiyo. Kwa hiyo, kama tunajali na tunaamua kuwa elimu ni kipaumbele, basi bajeti itatengwa kwa ajili hiyo.

    Kambi ya Upinzani inamtaka waziri mwenye dhamana atoe tamko kuwa madai ya nyongeza ya mishahara kwa wafanyakazi waendeshaji ni halali na ni lini watalipwa. Kwa pamoja tuamue kweli na tuone nini kinaweza kufanyika katika kurekebisha hali hiyo na kupata ufumbuzi wa kudumu na endelevu.

MATUMIZI YA WIZARA KWA UJUMLA

  1. Mheshimiwa Spika,
    Sote tunafahamu ya kuwa wananchi wetu wanaishi katika mazingira magumu na yenye umasikini mkubwa. Na kwa kuzingatia hilo, bajeti yetu ya serikali imekua ikitafuta kila namna ili tu kuhakikisha kuwa tunamsaidia mtanzania huyu kuondokana na umasikini uliokithiri.tunapokuwa tunapanga kiasi gani cha pesa kiende wapi, pia huangalia kiasi gani cha pesa kilitumika vipi.

  2. Mheshimiwa Spika,
    Katika kuikumbusha tuu serikali, naomba kuwataarifu kuwa katika bajeti ya mwaka 2007/2008 kama yalivyochambuliwa katika kitabu cha Hali ya Uchumi wa Taifa Jedwali na. 26, Elimu imetumia Shilingi bilioni 552.7 sawa na asilimia 51 tu ya feha zilizotengwa.

    Kama pesa iliyotengewa mwaka jana sekta hii ilishidwa kumaliza je leo bajeti yetu inaipangia tena sekta hii kiasi cha shillngi trillioni 1.43 sawa na mara mbili na uchee ya zile za mwaka jana. Hivi katika hali ya kawaida tuu sekta hii itaweza kutumia pesa hizi? Kwanini sekta hii ilimbikiziwe pesa nyingi ilhali tunafahamu kuwa haitaweza kuzitumia? Kwanini basi hatakama kunahitajika ongezeko kubwa, kwanini basi katika mwaka wa fedha wa mwaka jana ilishidwa kutumia karibu ya asilimia 50 iliyopewa? Kwani kunaongezeko gani la mahitaji ambalo mwaka wa 2007/2008 halikuwapo?

HITIMISHO

  1. Mheshimiwa Spika,
    Kwa kumalizia Kambi ya Upinzani inapenda kuikumbusha serikali iliyoko madarakani maneno aliyosema baba wa taifa mwaka wa 1967 “Elimu itolewayo katika shule zetu za misingi inapaswa kuwa elimu iliyokamilika”. Mhe. Spika, inatia simazi kubwa kuona hata maneno haya ya baba yetu yanashidwa kuenziwa. Ni wazi kuwa marehemu hafurahii huko aliko, kwani aliacha msingi mzuri lakini leo hata kama mtoto wako anaenda shule, lakini mzazi hana imani na elimu yake.

  2. Mheshimiwa Spika,
    Ni muhimu basi serikali ifanye yafuatayo ili kurekebisha hali hii:-
    Kubadili mfumo wa Elimu toka 7:4:2:3 kwenda 10:4:3. mfumo huu haujagawanyika sana lakini ni comprehensive and less selective, lakini kubwa zaidi utaenda sambamba na mabadiliko ya kikanda (regions na kimataifa) mfano. Kenya ni 8:4:4, Uganda 12:2:3, Zanzibar 10:2:2:3 na nchi nyingi zilizoendelea ni 12:4. Nchi nyingine zinaendelea kwenye Universal tertiary Education

  3. Mheshimiwa Spika,
    Kuna kila sababu na haja ya kuwa na maboresho kwenye mfumo wetu wa elimu. Nguvu ya ufundishaji kuanzia waliomaliza darasa la 7 ,kidato cha nne na sita na wenye elimu ya shahada wachache ni lazima usukwe upya ili uwe uwiano wa 85% ya diploma na 15 ya shahada ya kwanza katika elimu ya sekondari idadi iwe reversed ili waalimu wengi wawe na shahada na haswa waalimu wa sekondari.

  4. Mheshimiwa Spika,
    Kwa kuzingatia Hilo, kambi ya Upinzani inawahakikishia wanachi wote kuwa haitathubutu kukaa kimya, pale mambo yanapokuwa yanaenda vinginevyo na matarajio yao. Tunaahidi kuendelea kushirikiana nao siku zote. Na Kwa upande WA serikali, ni matatrajio ya kambi kuwa wizara husika itatoa majibu yanayoshabihiana na maswali yaliyotolewa na kambi hii na si vinginevyo.

  5. Mheshimiwa Spika,
    nakushukuru wewe binafsi na waheshimiwa wabunge wote kwa kunisikiliza kwa makini na naomba kuwasilisha.

    Asanteni Sana.

    SUSAN ANSELM JEROME LYIMO (MB)
    MSEMAJI MKUU KAMBI YA UPINZANI WIZARA YA ELIMU NA MAFUNZO YA UFUNDI
    20.7.2007

 

lf.curl lf.curl2 rt.curl2 rt.curl