lf.bevel
MWANZO CHAMA SERA KATIBA TUUNGE MKONO UCHAGUZI TUWASILIANE


Hotuba ya msemaji mkuu wa kambi ya upinzani Mheshimiwa Grace Sindato Kiwelu Ofisi ya Rais,menejiment ya utumishi wa umma na tume ya utumishi wa Umma

Kuhusu makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka wa fedha 2008/2009


I.  Utangulizi

Mheshimiwa Spika,
kwa niaba ya Kambi ya Upinzani naomba upokee shukrani zangu za dhati kwa kunipa fursa hii ili nitoe maoni ya Kambi ya Upinzani kuhusu hotuba ya bajeti ya Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa umma, Secretarieti ya maadili ya viongozi pamoja na Tume ya Utumishi wa umma kwa mwaka wa fedha 2008/2009 kwa mujibu wa Kanuni za Bunge Kanuni ya 99(7) toleo la Mwaka 2007.

Mheshimiwa Spika,
awali ya yote napenda kumshukuru mwenyezi mungu kwa kutuwezesha kuwepo hapa leo kujadili mambo muhimu kwa maslahi ya umma wa watanzania, na kwa mema yote amabayo amekuwa akitujaalia. ni matumaini yangu kwamba majadiliano yetu yataweka mbele maslahi ya umma. Mwenyezi Mungu atusaidie.

Mheshimiwa Spika,
napenda kwa nafasi ya kipekee kabisa kutoa shukurani zangu za dhati kwa Mheshimiwa Shoka Khamis Juma (MB), Msemaji Mkuu wa upinzani - Utawala Bora kwa mchango wake mkubwa katika kufanikisha uandaaji wa hotuba hii, kwani ni msemaji mkuu katika wizara zinazojumuishwa katika hotuba hii. Vile vile, natoa pongezi za dhati kwa viongozi wetu wa Kambi ya Upinzani Mhe. Hamad Rashid Mohammed (MB) na naibu wake Mhe. Dr. Wilbrod Slaa (MB) kwa kutoa miongozo sahihi kwa mujibu wa kanuni za Bunge.

II. Menejimenti ya utumishi wa umma.

Mheshimiwa Spika,
Kambi ya Upinzani inatambua kuwa Utumishi wa Umma ni nguzo muhimu ya ukuaji wa taifa lolote lile duniani. Watumishi wa umma hutoa mchango mkubwa katika kulinda na kujenga heshima ya nchi, kudumisha usalama na kuiwezesha Serikali kufanya shughuli zake kwa njia nzuri na kukuza kipato cha Taifa na hatimaye kwa mwananchi mmoja mmoja .

Mheshimiwa Spika,
Kambi ya Upinzani inatambua umuhimu wa Ofisi ya Menejimenti ya Utumishi wa Umma kama sehemu muhimu sana katika kuimarisha utawala bora kwa uendeshaji wa shughuli za serikali, kuweka mfumo wa uendeshaji wa Serikali unaoleta tija na ufanisi, kujenga uwezo wa watumishi wa umma, na kuboresha maslahi ya Watumishi wa Umma.

Mheshimiwa Spika,
kwa kuelewa hilo ni muhimu sana idara hii iangaliwe kwa umakini kwa sababu Watumishi wa Umma ni moja ya kiini cha maendeleo ya Taifa.

Mheshimiwa Spika,
Kambi ya Upinzani inayaona mengi ambayo kimsingi yamekuwa yakidhoofisha swala zima la utendaji na uwajibikaji wa Watumishi wa Umma. Mambo haya yanatokana na kutokuwepo kwa umakini na ufuatiliaji thabiti ambao umepelekea kuporomoka kwa maadili na uwajibikaji wa Watumishi wa Umma, maisha duni yanayotokana na vipato duni, ubinafsi, Ufisadi na urasimu, na hivyo kurudisha nyuma maendeleo ya taifa hili.

Mheshimiwa Spika,
taratibu za ajira ya wataalamu wa kigeni kwenye utumishi wa umma limeendelea kuwa tatizo kwani hakuna mpango madhubuti wa kuhakikisha kuwa pale ambapo wataalamu hao wanaajiriwa panakuwa na mpango madhubuti wa kuwaendeleza wataalamu wazalendo kama njia ya kupunguza utegemezi wa wataalamu kutoka nje. kambi ya upinzani inaamini kuwa kama pangelikuwa na mpango mathubuti wa kuhakikisha kuwa wataalamu wetu wanaendelezwa na baada ya kuendelezwa pawepo na mpango mkakati wa kuhakikisha kuwa serikali inajenga mazingira bora ili wataalamu hao waweze kuja na kuendelea kufanya kazi hapa nchini badala ya kwenda kufanya kazi nje ya nchi.

III. Ongezeko la mishahara kwa watumishi wa umma

Mheshimiwa Spika,
maboresho ya maslahi ya Watumishi wa Umma ni jukumu muhimu sana la Ofisi ya Menejimenti ya Utumishi wa Umma. Kwa kutambua hilo, Serikali ya Awamu ya nne haikubaki nyuma na ndio maana ikaahidi ‘Maisha bora kwa kila Mtanzania’. Tumaini la kila mtumishi lilikuwa ni nyongeza ya mshahara kulingana na kiwango cha kupanda kwa hali ya maisha kiujumla.

Mheshimiwa Spika,
kwa tathmini ya Kambi ya Upinzani, Kima cha chini cha Mshahara kimepanda na kuwa Shillingi 100,000 tu kwa watumishi wa Serikali. Kutokana na kupanda kwa hali ya maisha, mkate sasa ni karibu shs 1,000/=, kilo ya mchele ni zaidi ya shs 1,200, kilo ya nyama ni zaidi ya shs 2,500/= maeneo mengi na kilo ya sukari ni zaidi ya shs 1,200 vile vile. Hali hii ya maisha haijajumlisha nauli zilizopanda, gharama za matibabu katika hospitali na zahanati nyingi zikiwemo za Serikali. Kwa hali hii Kima cha chini cha Shs 100,000 kwa hakika ni dhihaka kwa Watumishi na Wafanyi kazi wetu wa sekta ya Umma. Isitoshe Serikali haijasema chochote kuhusu kima cha chini katika Sekta binafsi. Mheshimiwa Spika,
Kambi ya Upinzani, kupitia kwa Hotuba ya Msemaji wake Mkuu kwa Wizara ya Fedha ambaye pia ni Kiongozi wa Kambi ya Upinzani ilipendekeza kwa mara ya pili mfululizo kuwa Kima cha chini kiwe shs 250,000. Kiwango hiki kinawezekana kabisa kama ilivyoonyeshwa katika Bajeti mbadala ya fedha mwaka 2007/2008 kama ilivyowasilishwa na Msemaji Mkuu wa Kambi ya Upinzani wakati alipowasilisha Bajet Maoni ya Kambi ya Upinzani.

mheshimiwa spika, kutokana na kuongezeka kwa mapato ya ndani na ukuaji wa makusanyo ya ndani , kambi ya upinzani inapendekeza kuwa kiwango cha chini cha mshahara wa wafanyakazi wa umma kiwe tshs 250,000/ kwa mwezi, kwa ngazi nyingine mshahara ungepanda kwa asilimia ambayo italeta uwiano baina ya kipato cha chini na cha juu. kiwango hiki hakitatozwa kodi ili kuweza kumfanya mtumishi wa ngazi ya chini aweze kumudu gharama za maisha ambazo zinapanda kila siku. ni dhahiri kabisa kuwa serikali kwa kulipa wafanyakazi wake kima hiki, kitajiweka katika hali ya kukwepa rushwa na ubadhirifu, kitawawezesha watumishi hao kujiwekea akiba wakati wa kustaafu.

Mheshimiwa Spika,
hatua hii inalenga kumwezesha mtumishi wa umma kuweza kuhimili hali ya ugumu wa maisha na haswa kutokana na na kasi ya kupanda kwa bei ya bidhaa mbalimbali . Wastani wa kasi ya upandaji bei ulikuwa asilimia 7.0 mwaka 2007 ikilinganishwa na asilimia 7.3 mwaka 2006. Hata hivyo hadi kufikia mwezi April 2008, kasi ya upandaji bei ilikuwa asilimia 9.7, upandaji huu umemuadhiri sana mtumishi wa umma kama ilivyo kwa wananchi wengine kwa ujumla wake, na ndio maana tunaitaka serikali ipandishe kima cha chini cha mshahara hadi kufikia shilingi 250,000.kwa mwezi ili kuweza kuwanusuru watumishi wetu na hali ngumu za maisha wanayokumbana nayo.

Mheshimiwa Spika,
mwaka 2007/2008 Kambi ya Upinzani iliitaka Serikali kuiweka hadharani ripoti ya Tume ya kurekebisha mishahara ya watumishi wa umma ambayo ilikuwa chini ya uenyekiti wa Ndg. Deogratias Ntukamazima, ili wabunge na wawakilishi wa wafanyakazi waweze kuona kama yaliyopendekezwa yanalingana na mapendekezo ya maoni ya vyama vyao vya wafanyakazi. Hadi sasa ripoti hiyo haijaweka hadharani na hata wabunge hatujapatiwa taarifa ya aina yeyote ile ama kupewa nakala ya taarifa hiyo. Hivi Bunge linategemewa vipi litimize majukumu yake ya Kusimamia Serikali kama kila mwaka tutakuwa tunaendelea kupata taarifa kwa kuichokonoa Serikali? Fedha za watanzania zilitumika katika mchakato mzima wa utendaji wa Tume hiyo, na hivyo ni lazima Wabunge na Watanzania wajulishwe matokeo ya kazi iliyofanywa na fedha zao. Taarifa hiyo siyo ya Serikali ni ya Taifa na hivyo haina sababu ya kuwa Taarifa ya Siri kwa Wabunge.

Mheshimiwa Spika,
Kambi ya Upinzani inauliza kuwa huu ndio uwazi na uwajibikaji ambao Ofisi hii inauonyesha na kuwa ndio mfano wa kuigwa na Wizara nyingine?

Mheshimiwa Spika,
Kambi ya Upinzani inaitaka Serikali kuhakikisha kuwa zinachukuliwa hatua madhubuti ili kukabiliana na janga la maambukizo ya UKIMWI kwa watumishi wa umma ili kuhakikisha kuwa watumishi hawa wanapata mafunzo mbalimbali ya jinsi ya kuweza kujikinga na maambukizi hayo. Hili tunalisema hapa kwani ukisoma kwenye kitabu cha mpango wa maendeleo wa Serikali mwaka 2008/2009, Serikali haikuweka mpango maalumu wa kukabiliana na janga hili haswa kwa watumishi wa umma . Kuna haja ya Serikali kuweka mkakati bayana kukabiliana na janga hili kwani likiachwa bila kutiliwa mkazo hata kama kiwango cha maambukizi kinaonekana kupungua bado litaweza kufanya jitihada mbalimbali zilizopo kutokuweza kuzaa matunda yanayotegemewa.

IV. Menejimenti ya Utumishi wa Ummma

Mheshimiwa Spika,
Menejimenti ya utumishi wa umma ni pamoja na kusimamia na kuweka miongozo ambayo itasaidia kuinua kiwango cha utendaji katika taasisi za utumishi wa umma na kuifanya kuwa kila huduma itakayotolewa kufananishwa na bidhaa bora katika soko.

Mheshimiwa Spika,
Kwa dhana hii basi, kila shughuli itakayofanywa na taasisi ya kutoa huduma kwa umma ambayo haitamlenga moja kwa moja mteja ambaye ni mwananchi basi ihesabike kama upotevu wa raslimali ya nchi “waste of resources”. Aidha hii ihesabike kuwa ni moja ya ufisadi unaofanyika kwa nchi yetu.

Mheshimiwa Spika,
Kambi ya Upinzani inaamini kabisa kuwa pale ambapo sekta ya utumishi wa umma itaanza kuelewa dhana ya biashara isemayo kuwa mteja ni mfalme na katika kadhia nzima ya utumishi wa umma mteja si mwingine bali ni mwananchi anayetakiwa kupata huduma, basi hapo tutakuwa tumefanikiwa kubadili ‘mindset’ kwa watumishi hao na yale matatizo yote na malalamiko ya huduma mbovu, kuchelewesha majibu, kuwapiga danadana ya ‘njoo kesho’ yatakuwa yamepatiwa suluhisho.

Mheshimiwa Spika,
Utumishi wa umma uliosahihi na unamchukulia mteja ambaye ni mwananchi kama ni mfalme, ni ule ambao utatoa taarifa sahihi na kwa wakati kwa umma. kutoa majibu kwa wakati kulingana na masuala yanayoulizwa na muulizaji.

Mheshimiwa Spika,
Katika kipindi hiki cha uongozi, Serikali imeshindwa na inaendelea kushindwa kuwapatia majibu wananchi (wateja) ambao wanaandika barua zao kwa misingi ya kupata ufafanuzi kulingana na masuala mbali mbali. Na jambo hili kwa ujumla wake linadhalilisha nchi inayojiita kuwa inafuata sheria na utawala bora. Mfano mzuri ni Mheshimiwa Waziri kivuli wa Utawala Bora alipoandika barua kwa Mkuu wa Mkoa wa Pwani kuhusu malalamiko ya wavuvi katika wilaya ya MAFIA, lakini hadi leo hii hajapata majibu ya barua hiyo.

Mheshimiwa Spika,
Kambi ya Upinzani inauliza, Kama Waziri Kivuli wa Utawala Bora anashindwa kujibiwa barua zake. Je, Hali ikoje kwa wananchi wa kawaida?

V. Tume ya Utumishi wa Umma

Mheshimiwa Spika,
Moja ya kazi za tume hii ni kumshauri Rais kupitia Menejimenti ya Utumishi wa Umma kuhusu utekelezaji wa Mamlaka ya Rais kikatiba mintarafu Ibara ya 36 ya Katiba na kuhusu ujazaji wa nafasi zilizowazi katika utumishi wa Umma, kadri Rais atakavyoona inafaa. Pia kuwezesha uteuzi na nafasi mbali mbali kutoka mamlaka mbali mbali za Ajira.

Mheshimiwa Spika,
Nafasi za uteuzi zinazoongelewa hapa ni zile za kada ya juu katika utumishi wa umma. Nafasi hizi ndizo zile zinazotakiwa kutoa maamuzi ya mwelekeo wa nchi yetu katika sekta mbalimbali.

Mheshimiwa Spika,
Udhaifu mkubwa katika utumishi wa umma wa kutokutaka kubadilika na kuwa na mtazamo wa kuongeza tija na kuweka mbele maslahi ya nchi, chanzo chake ni uteuzi usioangalia ‘records’ na Sifa (vetting) za utendaji wakati wa ujazaji wa nafasi mbalimbali za utumishi. Mwisho wa siku ndio hayo yanayosabisha watendaji kushindwa kutoa maamuzi yaliyo katika wigo wao wa kazi.

Mheshimiwa Spika,
Kambi ya Upinzani inaamini sasa kuwa uteuzi mwingi anaoufanya Rais unatokana na ushauri mbaya na upendeleo ambao hautilii maanani maslahi ya nchi anaopewa Rais na Tume hii katika kujaza nafasi zilizowazi katika utumishi wa umma.

Mheshimiwa Spika,
ukisoma maelezo kuhusu makadirio ya mapato na matumizi ya mwaka 2008/2009 katika taarifa ya kamati ya Bunge ya sheria , katiba na utawala , ukurasa wa saba (7) wa taarifa hiyo kwenye makadirio yaliyoidhinishwa kwa mwaka wa fedha 2007/2008 kiasi cha shilingi 4,183,205,000.00 ziliidhinishwa , ila mpaka kufikia mwezi April 2008 kwenye fungu la mishahara fedha zilizotolewa zilikuwa kiasi cha shilingi 2,019,527,454. hiki ni kiasi cha 48.3% tu.

Hii maana yake ni kuwa wizara iliomba pesa nyingi kupita kiasi, na sababu kubwa ni kuwa idara hii haijui idadi ya watumishi wake, kama hali ni hii kwa wizara hii, je, hali itakuwaje kwa wizara nyingine? Nini kilitokea kiasi kwamba mishahara iliyotumika ilikuwa ni kiasi cha 48.3% tu. Isitoshe kumekuwa na taarifa za Watumishi hewa katika Wizara mbalimbali hasa Wizara ya Elimu, kinyume na Naibu Waziri wa Fedha alivyojibu ndani ya Bunge hili” kuwa Watumishi wote wamesajiliwa kupitia Waajiri wao, na hivyo hakuna haja ya TIN number kwa Watumishi walipa Kodi”Jee si kweli kuwa serikali bado haijakuwa na majibu sahihi juu ya wafanyakazi hewa?Kambi ya Upinzani inamtaka Waziri atupe majibu ya kina juu ya jambo hili.

Ukiangalia bajeti ya Serikali 2008/2009 Serikali inaomba kupewa fedha kwenye fungu la matumizi maalum imeomba kiasi cha fedha kwa ajili ya kulipia mishahara ya nyuma (arrears), hizi ni fedha za kulipia nini kama kipindi cha mwaka 2007/2008 wizara haikutumia kiasi kilichoidhinishwa? Tunamtaka waziri atupe maelezo ya kina juu ya jambo hili . Kambi ya Upinzani pia inataka kufahamu Kima cha chini kwa mishahara ya Serikali hasa ni kiasi gani, au ndiyo hiyo 100,000 tuliyoisema?

VI. Ofisi ya Rais Utawala Bora

Mheshimiwa Spika,
Nguzo ya tatu ya MKUKUTA ni kuhakisha kuwa nchi yetu ina utawala bora unaofuata sheria. Vita dhidi ya rushwa ni msingi muhimu wa kujenga utawala bora.Pia ni msingi muhimu kwa Wahisani kuendelea kutupatia misaada yao. Tuhuma nzito za rushwa ikiwemo ile ya Richmond na malipo ya akaunti ya EPA Benki Kuu (BOT) hazijachukuliwa hatua za kuwafikisha wahusika mahakamani si kipimo kizuri kwamba nchi yetu inautawala bora.Pamoja na majibu wa Waziri Mkuu juzi, watanzania wanataka kuona sheria zinafuatwa bila ubaguzi, ambapo walalahoi, mara wanapotuhumiwa hukamatwa, hupelekwa Rumande, na kupelekwa mahakani. Lakini kwa vigogo wenye kutuhumiwa kwa Mabilioni mambo ni tofauti kabisa

Mheshimiwa Spika,
kwenye wizi wa fedha za umma uliofanyika kupitia account ya EPA umeifanya nchi yetu kujikuta inajenga matabaka mawili kwenye kuwafikisha wahalifu mahakamani na au kuwachukulia sheria vigogo waliohusika, kwani Serikali imejikuta ikikaa na wahalifu na kuwabembeleza kurudisha fedha walizoibia Taifa huku wezi wa kuku wakipelekwa mahakamani na sheria kutumika juu yao, huu sio mfano wa utawala bora hata kidogo kwani nchi inagawanywa kati ya walionacho na wasiokuwa nacho na hii ni hatari kwa ustawi wa Taifa na dhana nzima ya utawala bora kwa ujumla wake. Hata kama hoja ni kurudisha fedha kabla ya kuwafunga, lakini watuhumiwa hao wote wana mali zinazoweza kuchukuliwa na Serikali. Hivyo hakuna maelezo yeyote ya kwanini taratibu za kawaida za Sheria za nchi zisifuatwe hasa baada ya hatua hizo kupendekezwa na Wakaguzi wa Ernst and Young, kama ilivyoelezwa kwa vielelezo katika hotuba ya Msemaji Mkuu wa Kambi ya Upinzani, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tamisemi Dr. Slaa (Mb).

Mheshimiwa Spika,
Pamoja na maelezo ya Waziri Mkuu juzi, lazima tukubali kuwa kifo cha Gavana wa zamani wa Benki Kuu kimegubikwa na usiri hasa baada ya msemaji wa Ikulu kueleza kuwa Serikali haimtafuti Gavana wa zamani Daud Balali lakini ikimtaka itampata kwani Serikali ina mkono mrefu.

Mheshimiwa Spika,
haikupita muda baada ya kauli hii ya msemaji wa Ikulu kwani muda mfupi vyombo vya habari viliripoti kuwa Gavana Balali amefariki. Taarifa rasmi ya Serikali kuhusu kufariki kwake imechelewa kutolewa kiasi ambacho wananchi wengi hawaamini kama kweli Gavana Balali amefariki. Kwa serikali kutokuwa wazi kuhusu kuumwa, kutibiwa na kufariki kwa Gavana Balali kumejenga hisia kuwa kuna mambo yanayohusiana na ufisadi ndani ya Benki Kuu yanafichwa ili kuwalinda viongozi wa awamu ya tatu na ya nne waliyohusika kuidhinisha na kufaidi matunda ya ufisadi huu.

Mheshimiwa Spika,
Kambi ya upinzani inataka kupata maelezo ya kina juu ya ni wapi na hospitali gani alikokuwa anaugulia marehemu Gavana Balali, na je? Ni serikali ama ni nani alikuwa anagharamia gharama za hosipitali wakati wote wa uhai wake hasa ikitiliwa maanani kuwa alikwenda kwenye matibabu bado akiwa mtumishi wa umma, nivyema tukajua pia gharam za matibabu hayo. Balali ni kiongozi wa juu sana, na Watanzania wanahitaji kujua yaliyojiri na kwa kiwango gani alihusika na tuhuma zote zinazohusiana na EPA na kasma mbalimbali zinazohojiwa ndani ya BOT. Kambi ya Upinzani, kwa niaba ya wote wenye nia ya kutaka kufahamu ukweli itaendelea kuhoji hadi tutakapopata majibu ya kuridhisha.

Mheshimiwa Spika,
wakati waziri akiwasilisha hotuba yake ya bajeti ya mwaka 2007/2008 alisema ninanukuu “kuratibu utekelezaji wa awamu ya pili ya mpango wa Taifa wa kuthibiti na kupambana na Rushwa” Mwaka huu serikali inakuja na hoja kuwa sasa ni mwaka wa kuwahusisha wadau ,hivi kama kuratibu tu iliochukua mwaka mzima je? Hili la kuhusisha wadau litatumia miaka mingapi? Na je? tutaweza kufikia lengo la kupambana na Rushwa na Ufisadi?

Mheshimiwa Spika,
Kuendesha nchi kwa kufuata misingi ya sheria na demokrasia ndio nguzo kuu ya utawala bora. Utawala unaofuata sheria maana yake ni kupinga aina zote za ufisadi zinazoihujumu nchi na kuwanyima haki wananchi katika umiliki wa raslimali zao. Aidha uwepo wa demokrasia maana yake ni uwepo wa haki za msingi za binadamu pamoja na zile za kisiasa zitaweza kulindwa na kusimamiwa kwa ukamilifu wake. Swali la kujiuliza ni kuwa kweli Tanzania inaendeshwa kwa kuzingatia matakwa ya utawala bora?

Mheshimiwa Spika,
Kambi ya Upinzani katika kujibu swali hilo ni kuwa Tanzania haina utawala bora, kwa vigezo vichache vilivyoainisha hapo juu ni kweli utawala bora bado. Ufisadi ndio umeota mizizi, sheria haziheshimiwa mfano tumetunga sheria kwamba muekezaji aende Tanzania Investiment Centre (TIC) mambo yake yote yatamalizwa,bado wawekezaji wanatangatanga,TIC haina ubavu mradi hakuna tafauti yeyote,huku tunatumia fedha nyingi kuwaita wawekezaji.Siasa zimefuata mtindo wa kifisadi (fedha ndio inaongoza siasa). Matumizi mabaya ya vyombo vya ulinzi wa raia hasa nyakati za uchaguzi, badala ya vyombo hivyo kulinda maslahi ya nchi na wananchi ili mwananchi achague kiongozi amtakae na kura yake iheshimiwe, baadhi ya watumishi wa vyombo wanalinda maslahi ya watu binafsi,baadhi ya watendaji wa vyombo hivyo vinashirikiana na mafisadi kuficha ukweli wa upotevu na wizi wa raslimali za nchi.

Kambi ya Upinzani inauliza ni nani anatakiwa awe msatari wa mbele alinde (national interest) maslahi ya Taifa?

Mheshimiwa Spika,
mfano mzuri kuhusu kuvunjwa kwa kanuni na misingi ya utawala bora ni pale viongozi wa Serikali walipo waalika viongozi wa vyama vya Upinzani kwa barua, lakini wakafukuzwa katika kikao wakati wa ziara za Mhe. Rais mkoani Mwanza. Je hapa ndio tunajenga umoja wa kitaifa kama alivyosema Rais katika hotuba yake ya ufunguzi wa Bunge hili?

Aidha sambamba na hilo ni pale aliyekuwa Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es salaam kutumia ofisi za umma kutangaza hadharani kabla hajaachia rasmi ofisi yake kuwa akistaafu rasmi atajiunga na Chama Cha Mapinduzi. Je, watu wenye madaraka Serikalini/ katika utumishi wa umma walio kama Kamanda huyo mstaafu ni wangapi? pia inaonyesha kuwa Jeshi la Polisi lililokuwa chini yake lilikuwa linaongozwa kwa kufuata itikadi za chama tawala. Hii ni dhahiri kuwa Demokrasia ya kweli katika siasa za nchi hii bado. Serikali inatakiwa kuwabadili watumishi wake ki-mtazamo ili waendane na mabadiliko ya Dunia na mfumo uliopo sasa.

VII. Usalama wa Taifa

Mheshimiwa Spika,
Idara ya Usalama wa Taifa majukumu yake yameainishwa katika fungu 30. Kambi ya Upinzani inaomba kuwe na value for money inayopatikana kutokana na kuwekeza katika idara hii kwa kuhakikisha kuwa inasimamia kweli maslahi ya Taifa na ya watu wanyonge hasa kule vijijini, na hasa kwa kusimamia sheria na taratibu mbalimbali za kuhakikisha uchaguzi wa huru na haki.

VIII. TAKUKURU

Mheshimiwa Spika,
TAKUKURU ni taasisi ya kuzuia na kupambana na rushwa, katika taarifa yake ya utekelezaji inaonyesha kuwa pamoja na mambo mengine wamefanya tafiti 28 ili kubaini mianya ya rushwa na hatimaye kutoa mapendekezo ya namna ya kuziba mianya hiyo.

Mheshimiwa Spika,
Kambi ya Upinzani inaona kuwa taasisi hii bado ipo nyuma ya dunia ya sasa kwani haionekani ikilishughulikia suala la rushwa kwa stahiki yake na haswa rushwa kubwa zinazofanywa na vigogo mbalimbali kwani wao wamejikita kufuatilia dagaa wa rushwa huku mapapa yakiachwa na kujitengenezea himaya zao bila hofu .

Mheshimiwa Spika,
Kambi ya Upinzani inaamini kabisa kuwa dawa ya kuzuia rushwa ni uwazi katika utendaji wa kazi huku kila mmoja akiongozwa na uzalendo juu ya nchi yao. kila mtu akielewa nini kinafanyika na kwa maslahi ya nani ndio njia pekee.

Mfano, Tume ya Jaji Warioba ilikwishafanya kazi hii, na wao wanarudia tena na huo kama si ufisadi ni nini? Hili ni tatizo la msingi katika nchi yetu, kufanya kazi moja mara mbili au tatu. Sambamba na hilo ni Serikali kuunda tume za madini sita tofauti kwa muda wa miaka mitano, na zote zinatumia fedha za walipa kodi. Na baada ya hapo Serikali inaunda tume ya kuangalia jinsi ya kutekeleza maagizo ya tume ambazo zimewasilisha mapendekezo ya Tume.Kambi ya upinzani inamtaka waziri atupe tathimini ya fedha na utekelezaji wa Tume angalau ya majaji Nyalali,Kisanga na Warioba.

Mheshimiwa Spika,
Tunaomba TAKUKURU watusaidie hali hii tunaiweka katika fungu gani la upotevu wa raslimali ya nchi?

Kambi ya Upinzani inaamini kabisa kama kutakuwa na mabadiliko ya kimtazamo kwa watendaji wa sekta ya umma ( mindset change) katika utoaji huduma kwa wananchi na wananchi kuelewa haki zao katika upatikanaji wa huduma husika ni dhahiri rushwa itakwisha.

Mheshimiwa Spika,
TAKUKURU haikuchukua hatua yeyote bali inasubiri uchunguzi wa SFO ya Uingereza ambayo kimsingi inapeleleza kampuni ya BAE ya kwao kuhusiana na Tuhuma za rushwa inayoikabili Kampuni hiyo. Watanzania waliohojiwa na SFO ni mashahidi tu wa Uingereza katika upelelezi huo. Kambi ya Upinzani inaitaka Serikali ieleze Bunge hili ni kwanini Serikali/ Takukuru inapata kigugumizi kuwapeleka mahakamani wahusika hao kwa tuhuma ya Rushwa ya katika ununuzi wa Rada baada ya mtuhumiwa aliyepokea dola milioni 12 kuruhusiwa kukiri kuweka fedha hizi katika akaunti yake Uswisi? Isitoshe Serikali ilimwachia huyo baada ya kutoa kiapo mbele ya Mahakama ya Kisutu na hata Hati zake za kusafiri hazikuchukuliwa! Wananchi wengi wamepoteza imani na TAKUKURU kama chombo cha kupambana na rushwa kwani kinaonekana kuwa chombo cha kuwalinda mafisadi. Kuna baadhi ya viongozi wenye fedha nyingi katika akaunti za nje na ndani ya nchi ambazo hazielezeki kwa vipato vyao halali, hata hivyo hawajachukuliwa hatua yeyote amgalau ya kiuchunguzi wa kijinai, ama sivyo Bunge lielezwe tofauti.

Mheshimiwa Spika,
kunyamaza huku kwa taasisi hii katika kuwachukulia hatua wale wote wanatuhumiwa kuwa wameliingizia Taifa hasara kubwa kwa maslahi yao binafsi kunasababisha wananchi wakose imani na taasisi hii muhimu. Kambi ya Upinzani inaitaka Serikali ianzishe mchakato wa kuichunguza TAKUKURU yenyewe kwa lengo la kujisafisha, kuona kama yenyewe ni safi, jambo ambalo kimsingi linaashiria kuwa haiko safi ndiyo maana linashindwa kuchukua hatua kwa watuhumiwa mbalimbali.

Mheshimiwa Spika,
miongoni mwa maelezo aliyotoa waziri wakati akiwasilisha hotuba yake ya bajeti kwa mwaka 2007/2008 alisema kuwa, ninanukuu “kuendelea na uchunguzi wa tuhuma 2,037 zilizopo na nyingine zitakazowasilishwa. Kipaumbele kitawekwa katika tuhuma zinazohusu mikataba mikubwa ,manunuzi Serikalini ,matumizi ya fedha za Serikali katika miradi mikubwa” Kambi ya Upinzani inataka kupata maelezo ya kina juu ya hatua ambazo zimefikiwa kwenye uchunguzi huu na haswa wa mikataba mikubwa na manunuzi serikalini. Ni hatua gani zimechukuliwa hadi sasa? Kama kwa kipindi cha mwaka mzima TAKUKURU imefanya uchunguzi wa tuhuma kubwa za Rushwa zipatazo kumi(10) na ni tuhuma tano (5) tuu kati ya hizo ndio ziko katika hatua za mwisho za uchunguzi ,kwa mwendo huu je? tutaweza kweli kukabiliana na rushwa kubwa? Kama kwa mwaka mzima hatuwezi kupeleka kesi hata moja ya rushwa kubwa mahakamani TAKUKURU wana haja kweli ya kuwepo? Kuna haja ya wao kuendelea kutumia rasilimali za nchi kama hawawezi kulisaidia taifa ? Tena siku hizi kazi yao kubwa imekuwa Semina yenye sura ya posho tu, isiyo na fanaka, kwani kwenye wilaya nyingi maofisa wa TAKUKURU ndio wanaosemekana kuhusiana na wahalifu kuhujumu nchi kwa njia ya Rushwa.

Tunamtaka Waziri atupe majibu ya kina kwa mwendo huu tunahitaji muda wa miaka mingapi ili kuweza kukabiliana na rushwa hizi kubwa?.

IX. Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma

Mheshimiwa Spika,
Katika kutekeleza utawala bora katika nchi, ni kuwa na Serikali inayowajibika kwa wananchi, viongozi wanatakiwa wawe walio na maadili mema na kuwa mfano wa kuigwa kwa watanzania wote kama alivyokuwa Hayati baba wa Taifa. Mheshimiwa Spika,
misingi ya maadili ya viongozi wa umma kwa mujibu wa Ibara 132(5) ya katiba ya Jamhuri ya Muungano ni pamoja na kuwataka viongozi wa umma kutoa mara kwa mara maelezo rasmi kuhusu mapato,raslimali na madeni na kupiga marufuku mienendo na tabia inayofanya viongozi kuonekana hawana uaminifu au uadilifu au kuonekana kuwa kichocheo cha rushwa katika shughuli za umma na kuhatarisha maslahi au ustawi wa jamii.

Mheshimiwa Spika,
Waziri wakati anawasilisha hotuba yake ya bajeti ya 2007/2008 , alisema na ninanukuu “kuendelea na zoezi la kuhakiki mali za viongozi wapatao 400 walizotaja katika Tamko la Rasilimali na Madeni kwa madhumuni ya kuhakikisha kuwa mali zilizotajwa katika Tamko ndizo walizonazo . Aidha ,ulinganisho utafanywa kati ya mali zilizotajwa kwenye Tamko na maelezo ya kipato cha viongozi husika” mwisho wa kunukuu. Kambi ya Upinzani inamtaka waziri kutoa maelezo ya kina juu ya hatua ambayo imefikiwa hadi sasa kwani ni mwaka mzima sasa tangu Waziri atoe ahadi hiyo ndani ya Bunge . Pili tunamtaka waziri atoe Maelezo ya kina juu ya hatua ambazo zimechukuliwa kwa mujibu wa sheria ya maadili ya viongozi.

Mheshimiwa Spika,
hadi kufikia tarehe 28 April 2008 ni viongozi wa umma 4,261 sawa na asilimia 57.22% tu ndio wamerejesha fomu za tamko la mali na madeni kati ya viongozi 7,447 waliokuwa wametumiwa fomu hizo. Na kati ya hao viongozi wa siasa waliowasilisha fomu zao ni 2,130 kati ya 3,983, sawa na 53.5% tuu ,huku viongozi wa utumishi wa umma ni 2,734 kati ya 3,464 , sawa na 80%. Kambi ya Upinzani inataka kupata maelezo ya kina ni viongozi gani hao wa kisiasa ambao hawajawasilisha Fomu zao kwa madaraja yao kama ni mawaziri ,wabunge na madiwani ni wangapi kwa kila kundi, na kwa kuwa mengine ni ya kikatiba, ni hatua gani imechukuliwa dhidi ya viongozi hao wanaodiriki kuvunja katiba na kutekeleza sheria za Nchi .

Mheshimiwa Spika,
kwa mujibu wa sheria ya maadili ya viongozi wa umma kutokana na ibara 132(6) ya katiba ,imeweka masharti ya kiongozi wa umma kufukuzwa au kuondolewa kazini kutokana na kuvunja maadili ya viongozi ,bila kujali kama kazi hiyo ni ya kuchaguliwa au kuteuliwa.

Mheshimiwa Spika,
Kambi ya Upinzani inataka kupata maelezo ya kina juu ya viongozi na watumishi wa umma ambao wamechukuliwa hatua hii kwani kila mwaka tunaletewa taarifa hapa Bungeni kila wakati kuwa kuna viongozi ambao hawatekelezi sheria hii ,kwa nini hatua hazichukuliwi? Ama hao viongozi na watumishi wako juu ya sheria za nchi? Tunataka maelezo ya kina .

X. Mpango wa Shughuli za Mwaka 2008/2009

Mheshimiwa Spika,
Tume ya Utumishi wa Umma imepanga kutumia takribani 150 milioni kwa ajili ya kulipia gharama za kuendesha vikao vya Tume kujadili rufaa na malalamiko yatakayowasilishwa kwa Tume. Aidha Tume itatumia kiasi cha shilingi 360.134 milioni kwa ajili ya kujadili mashauri ya nidhamu na masuala ya ajira. Kambi ya Upinzani inaona kwa kweli hii ni kutokutenda haki kwa watanzania walipa kodi wa nchi hii. Kwa sababu mtumishi anapopata ajira anapewa masharti ya ajira mojawapo likiwemo nidhamu yake mahali pa kazi. Kinyume na hapo kanuni ziko wazi, hivyo kuna sababu gani za kutenga fedha nyingi namna hiyo kwa ajili ya kujadili nidhamu ya watumishi?

Kambi ya Upinzani inaitaka Serikali itoe ufafanuzi kuhusu suala hili.

Mheshimiwa Spika,
Baada ya kuyasema hayo kwa niaba ya Kambi ya Upinzani, Naomba kuwasilisha.

Grace Sindato Kiwelu (Mb)

Msemaji Mkuu wa Kambi ya Upinzani
Ofisi ya Rais, Menejiment ya Utumishi wa Umma

 

lf.curl lf.curl2 rt.curl2 rt.curl